UKURASA WA 56 SEHEMU YA 1

UKURASA WA 56
SEHEMU YA 1.
KOREA KASKAZINI

Ni usiku ambao kwa pale Korea Kaskazini ulikuwa ni wa kipekee sana. Baridi kali iliendelea kuwachapa wakazi na waenyeji wa nchi ile. Tairi za ndege binafsi zilikita ardhini na baada ya dakika moja, Malocha akiwa na Masai walishuka toka kwenye ndege na kwenda kwenye gari moja la kifahari sana.

Mwendo wa dakika ishirini ulitosha kufika sehemu moja iliyokuwa na mgahawa mkubwa ambao watu mbalimbali walijumuika usiku ule na kupata chakula. 
Mwenyeji wao aliwapitisha njia kadhaa na baadae alifika katika mlango mmoja ambapo ulifunguliwa na kijakazi wa kike.

“Anahitajika mtu mmoja tu kuingia.” Aliongea kijakazi yule kwa kiingereza cha kuungaunga na Masai alimpatia mkoba Malocha ili aingie yeye. Masai akabaki nje ya mlango na Malocha akaingia ndani.

Dakika kadhaa, Malocha alikuwa ameweka mezani mkoba aliokuwa nao na kumsogezea General Jing Pyong.

“Nadhani mambo yamekamilika.” Aliongea Malocha kwa Kiingereza.
General Jing Pyong akafungua mkoba na kutoa kitabu. Akakitazama kidogo na kumuangalia Malocha. Kilikuwa kimefungwa vyema na karatasi la nailoni juu yake. Ilionekana hamna aliyekifungua.

“Tumemalizana. Mwambie mwenzako, atapata ujumbe wake wa kuwaona wazazi baada ya dakika mbili.” Akaongea hayo Pyong na kumfanya Malocha atoke nje ya nyumba ile.

Pyong akatwaa simu yake na kuipiga sehemu kisha akaweka sikioni.
“Chude Bobo ninacho. Kumbe ni kitabu.” Aliongea.

“Ndio ni kitabu. Angalia ukurasa wa hamsini na sita.” Sauti ikamwambia. Alikuwa ni waziri wa ulinzi wa nchi ile. Yuleyule ambaye mwanzoni alipewa taarifa na huyu mtu kuwa Chude Bobo imeonekana Tanzania. Pyong akafungua kitabu haraka na kuutafuta ukurasa wa hamsini na sita, lakini hakuuona na badala yake aliona umechanwa.

“Haupo mkuu.” Akajibu kwa kupagawa.

“Shit. Huo ukurasa ndio Chude Bobo.” Alibwata Waziri.
Pyong akasimama na kutazama huku na huko na kuikata ile simu. 

“UKURASA WA HAMSINI NA SITA UPO WAPI?” Alifoka kwa sauti ya juu na sana mara ghafla umeme ukakatika ndani ya nyumba ile.
****
TANZANIA

John Lobo alikuwa hoi taabaani baada ya kukatwa koromeo lake na Malocha Malingumu. Alikuwa anagalagala kwenye rami huku kakamata koo lake na damu zikizidi kumwagika na kumchafua vibaya sana. Licha ya hayo yote, hakuacha kutambaa kwa tumbo kuelekea barabarani aokoe roho yake ambayo ilikuwa inatapatapa taabani kwa maumivu ambayo Malocha aliyaacha katika mwili wake.

Tapatapa hizo zikiwa zinaendelea toka kwa John Lobo ambaye alikuwa anendelea kujivuta kwa kwa tumbo bila kukata tamaa, mara mbele yake alisimama mtu mrefu akiwa kavalia suruali ta kadeti na viatu vya vikubwa na vya gharama. John Lobo kwa shida alinyanyua shingo yake huku bado kakamata shingo yake na kumshuhudia mwanaume ambaye hakuwahi kuhisi katika maisha yake kuwa atakuwa mbele ndani ya dakika zile.

Gunner Samuel Bokwa, alikuwa mbele ya John Lobo na kisha alinyoosha mkono wake kumuelekea lakini Lobo hakuweza kufanya lolote zaidi ya kuingiwa na giza zito machoni mwake. Akazimia na hiyo ndio ilkuwa nafasi yake Gunner kumchukua na kumpeleka hospitali ambapo alimpatia kijana yule matibabu yote muhimu na yaliyoweza kumrudisha tena katika hali yake.

Mwajabu. Mwanamke ambaye alipatwa na mkasa wa kusikitisa wakati kundi la Malocha na Masai wakiwa wanarudi nyumbani kwao naye akiwa ndani ya gari lao. Lilitokea gari la maadui na kutwanga gari la wakina Malocha risasi nyingi sana. Katika taflani hiyo, Mwajabu ambaye alisimama kama mpenzi wa Malocha, alipigwa risasi kadhaa na kumfanya awe hoi taabani. Hata pale alipopelekwa hospitali, aliwekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Siku hii alikuwa ameruhusiwa kutoka hospitali, na alikuwa amerudi nyumbani kwake maeneo ya Nkuhungu Dodoma. Alipaangalia nyumbani kwake na kujikuta akitabasamu kwa kutoamini kama kweli alikuwa amerudi nyumbani na maisha mengine yangeanza kuendelea. Dereva wake akashuka toka garini na kwenda kufungua geti kisha akarudi na kuingiza gari maalumu lililokuwa limemchukua Mwajabu toka hospitali.

Baada ya gari kukaa nafasi yake maalumu, mlango wa nyumba yake ulifunguliwa na alitoka binti mrembo na mwenye tabasamu pana usoni pake. Alikuwa anavutia kwa kumuangalia, na bado alikuwa mbichi sana jambo lililomfanya azidi kuwa kivutio kikubwa kwa mwanaume yeyote ambaye angemuona.

“Dadaa.” Aliita binti yule ambaye kwa makadirio, unaweza kumbatiza miaka ishirini au ishirini na mbili.

“Heey. Amina.” Alijibu mapigo Mwajabu huku akiwa katabasamu na kushuka toka garini, kisha wakakutana na kukumbatiana.

“Karibu tena nyumbani dada.” Aliongea binti mrembo ambaye aliitwa Amina.

“Nimefika aisee. Kitambo sana.”

“Namshukuru MUNGU nipo salama, na wewe umerudi tena nyumbani, basi hiyo ni faraja tosha.”

“Ahsante sana mdogo wangu.” Alijibu Mwajabu na baada ya hapo, mambo ya kushusha mizigo midogo toka garini, yalianza na hayakuchukua muda sana, yakawa yamemalizika.

Amini ni binti mdogo ambaye alimaliza kidato cha nne mwaka uliopita na kubahatika kuchaguliwa kuendelea na masomo yake katika shule moja ya wanawake iliyopo Dodoma. Ni mdogo wa damu kabisa wa Mwajabu. Baada ya Mwajabu kupatwa na mkasa alioupata, Amina aliamua kurudi nyumbani kwa dada yake ili akae na nyumba na wakati huo kule masomoni, alimua kuwa anaenda kutwa badala ya bweni. Dada yake ndio karudi siku hiyo baada ya kukaa hospitalini kwa miezi mitatu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata.

“Dada kuna ujumbe wako ambao nilikuwa nataka nikupe tangu mrefu sana, lakini nilishindwa kwa sababu ya hali yako.” Aliongea Amina wakati wanapata chakula cha usiku pamoja na dada yake.

“Mmgh,” Akaguna Mwajabu. “Ujumbe wa nani tena.” Akauliza kwa hamasa.

“Ngoja nikakuletee, utamjua mwenyewe.” Aliongea Amina na hapohapo bila kusubiri jibu toka kwa dada yake, alienda hadi chumbani anapolala na kupekenyua mkoba wake na kisha alirudi sebuleni wanapopatia chakula na kumkabidhi dada yake bahasha moja ya kaki ambayo ilikuwa haijafunguliwa hata kidogo na kwa juu yake iliandikwa AIFUNGUE MWAJABU BIN ALMUOD.
Mwajabu aliifungua bahasha ile kwa kihoro na alikutana na karatasi nyeupe ambayo ilikuwa imeandikwa kwa wino wa kalamu. Akaanza kusoma kilichokuwa kimeandikwa mle

”Kwako Mwajabu.

Natumai unaendelea vyema na u mzima wa afya. Kwanza samahani kwa matatizo yaliyokukumba. Najua hayo yote ni kwa sababu yangu. Sikupenda wewe upatwe na mkasa ambao mimi na wenzangu tuliweza kusababisha. Kazi zako zimesimama, na hata kipato hakiingii tena wakati upo hospitalini, yote kwa sababu ya kukuingiza katika dhoroba ambayo tulipaswa tupambane nayo sisi na si wewe.

Licha ya hayo yote, pia napenda kukupongeza kwa kupigania pumzi yako hadi sasa. Wewe ni mwanamke shupavu na mwenye moyo mgumu kama kipande cha chuma. Nispokusifu kwa hili, hakika nitakuwa nimemkosea hata Muumba,” Binti Mwajabu alijikuta akichanua tabasamu na kuzidi kujikita ndani zaidi kwenye kusoma ujumbe aliopewa na mdogo wake. “Kama unasoma maandishi haya, tambua kuwa nakusifu mbo kwa ujasiri na roho ngumu uliyoinesha.
Mwajabu, nilikutana na wewe kama bahati tu! Uzuri wako wa haiba, ucheshi pamoja na usikivu wako, ulinivutia ndani ya dakika chache sana na kunifanya nitake kukujua zaidi lakini matatizo yaliyotukumba, nikajikuta napoteza tumaini la kukujua. Na kibaya zaidi, hata ukipona nahisi nitakaa mbali na wewe kwa sababu ya kukuweka mbali na matatizo hasa kwa shughuli ambazo nazifanya. Tafadhali, naomba usijisikie vibaya. Nafanya haya ili kukuweka mbali na matatizo kama yaliyokukumba. Na nitafanya haya kwa wanawake wote duniani. Lakini sitafaya hivi daima, hili natambua na naliweka akilini. Kama nitataka kuanzisha familia, basi nitakutafuta wewe pekee. Kama utakuwa umeolewa, basi sitakuwa na haja na mwanamke mwingine.

Baada ya maneno haya machache. Nataka kukwambia kuwa, shughuli zetu zimekuwa nzito mara kenda zaidi ya pale mwanzo. Tupo katika mapambano makubwa katika kulikomboa taifa letu na dunia wa ajumla. Si ajabu ukasikia kuwa tumeiaga dunia. Na wala usilie kama ukisikia hayo, furahi na kupiga vigelegele kwa sababu tutakuwa tumekufa wakati tunaipigania furaha itawale dunia hii. Tutakuwa tumekufa kishujaa.

Kwa sasa siwezi kukwambia tupo wapi, lakini bado tupo kwenye mkasa uleule unaoendelea kukua kila kukicha. Endapo nitarudi salama Tanzania, nitakutafuta na kukujulia hali.
Ndani ya bahasha hii, kuna ufunguo wa posta. Namba hizi, SLP 547 ndizo namba za ufunguo huo. Nenda kafungue, kilichomo humo, ni chako kama shukrani na vilevile ni pole kwa matatizo yaliyokukuta. Zaidi naomba kilichomo ukitumie kwa manufaa ya maisha yako. Mimi naishia hapa, nitakutafuta tena nikirudi.

MALOCHA MALINGUMU.” Barua iliishia hivyo na Mwajabu alikung’uta bahasha ile na kweli, ufunguo wa Posta ulidondokea mezani. Akauchukua na kuuhifadhi palipo salama. Akaikunja kaatasi ile na kuirudisha ndani ya bahasha na kisha akamuangalia mdogo wake ambaye alikuwa makini sana kwenye simu yake, nadhani alikuwa ‘anachat’.

“Ni Malocha.” Akaongea Mwajabu.

“Ahaaa! Kumbe ndio yule. Mweusi hivi anamwili kiasi.” Aliongea Amina huku akitoa sifa ambazo anazo Malocha.

“Alikupa mwenyewe hii barua?” Aliuliza kwa hamaki Mwajabu.

“Ndio. Alikuja hadi hapa mwezi uliopita.” Akajibu Amina.

“Kha! Sijui kapajuaje.” Alinong’ona peke yake Mwajabu.

“Ndio shem nini?” Amina alimuuliza dada yake na kumfanya dada yule atabasamu kwa tabasamu mwanana.

“Hapana. Ila nd’o yule ambaye alinipakiza kwenye gari lao na kusababisha nipigwe risasi.”

“Ahaaa! Okay. Ila si nd’o shem Dada?”

“Hapana. Kwa sasa kasema atakaa mbali na mimi pamoja na wanawake wote duniani ili kuwaepusha na matizo kama yaliyonipata.”

“Ila akirudi utakuwa tayari kuwa naye?”
Nitakubali ndio.” Mwajabu alimjibu mdogo wake na kumfanya Amina anyanyuke na kwenda kumkumbatia dada yake.

“Nadhani ni chaguo sahihi kwako Dada. Anafaa kuwa na wewe. Hilo sitakupinga.”Aliongea Amina huku akiwa kamkumbatia dada yake aliyekuwa kakaa kwenye kiti na akipapasa mkono wa mdogo wake.

“Ahsante Mdogo wangu.” Alijibu hivyo Mwajabu.
****
Mchana mwingine wa jua kali katika Mji wa Dodoma. Kebu rangi ya njano ilisimama mbele ya posta kuu ya Mjini Dodoma na Mwajabu alishuka huku akimsihi dereva amsubiri palepale bila kuondoka. Moja kwa moja, Mwajabu akaenda kwenye sanduku lililoandikwa 547 na kulifungua. Huko alikuta bahasha ndogo tu. Akaichukua na kurudi nayo ndani ya kebu. 
Kebu hiyo ikageuza na kurudi kule ilipotokea mwanzo na ndani yake, Mwajabu aliweza kuifungua bahasha hiyo na kusoma kilichomo. Alikuta karatasi ya benki (cheque) ikiwa imeandikwa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kingeweza kumsaidia sana mwanadada yule. Mwajabu akatabasamu na kutikisa kichwa kwenda kulia, kushoto.

“Malocha.” Akanong’ona jina hilo huku tabasamu likiwa bado limetawala usoni pake.
****
DONATE VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Your donation helps the Admin to be even more active in sharing quality blog templates. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni