UKURASA WA 56 SEHEMU YA 09

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 9

Asubuhi na mapema, ilimkuta Masai kwenye luninga ambapo alikuwa anatizama taarifa za habari za siku hiyo huku habari kubwa ikiwa ni ile ambayo aliifanya yeye. 
Taifa zima kwa ujumla liliingiwa na mashaka hasa kwa kuwa mtu ambaye alikuwa amefanya hayo, walikuwa hawamjui hata kwa sura. Waliyachukua matukio mawili yaliyofanyika katika nchi yao na kujikuta wakiwa katika mashaka maubwa. Kwanza mauaji ya General, Bwana Pyong na pili kuharibiwa vibaya kwa ngome ya Waziri wa Ulinzi Mstaafu, Bwana Cheing.

Watoto waliamka na kwenda kwa Masai kwa furaha huku nyuma, mama yao alitamani hata awaambie msiende lakini haikuwa hivyo, ilimbidi akubaliane na Masai kwa wakati ule. Watoto walielekezwa kwenye jokofu na kwenye meza ambapo walikuta juisi na vifungua vinywa. Nao bila hiyana wakajikita na kuanza kula huku mama yao akiwa anamtazama Masai aliyekuwa anatafuna muhindi huku macho yapo kwenye luninga.

“Ni wewe umefanya yale yote?” Akauliza Mama Cheing, mke wa waziri mstaafu.

“Ndio.” Masai naye akajibu bila wasiwasi.

“Wanajeshi na polisi wa kawaida arobaini na mbili, wamepoteza uhai kwa usiku mmoja.” 

“Safi kabisa. Si wanajadai wanamlinda fisadi?”

“Upo matatani kijana, sidhani kama utatoka nchi hii salama.”

“Natoka na ukijua ya mumeo, nadhani hutokuja kumsamehe na utaona nilichofanya ni cha muhimu sana.”

“Haitokuja kutokea. Tena haitotokea kamwe. Kukubaliana na muuji kama wewe.” Masai akacheka kwa maneno yale.

“Umekaa na muuaji ndani ya ndoa yako kwa miaka sijui mingapi. Ukaona hazalishi, ukaenda kwa muuaji mwingine na kuzaa naye. Halafu sasa hivi sijui unaongea uozo gani.”

“Sina uhakika kwa maneno yako. Mara mia nimuamini mume wangu, yawezekana hajawahi kuua lakini wewe naona kwa macho yangu.”

“Unadhani mumeo hataamini kuwa ulimsaliti?” Macho yakamshuka yule mwanamama. “Tuache habari hizo, mapema utathibitisha maneno yangu.” Masai akaongea huku anatizama saa yake, akagundua ni saa tano asubuhi. Akaenda jikoni na kunawa na kisha akaenda kuvua mavazi yake ya asubuhi na kuvaa nguo za mazoezi. “Natoka mara moja.” Akamuaga mama yule ambaye alikuwa hajui hata ni mahali gani alipo. Yeye pamoja na wanawe walikuwa ni mateka. Hawakuruhusiwa kutoka ndani. Hivyo hata wakati Masai anatoka ndani, alifunga mlango wa kisasa kwa nje na kuwasha mitambo ambayo kama itatokea mama yule anataka kufanya baya lolote, ikiwemo kutoroka, basi Masai na waliyomtuma, wangepata taarifa na kufika kwenye ile nyumba.
****
Katika Makao Makuu Ya Polisi nchini Korea, daftari la kesi ya ugaidi likatua kwenye meza ya mwanadada Sheiming Kim. Binti mrembo lakini hatari sana linapokuja suala la kutetea nchi yake na kukamata waarifu.

Kim kama alivyokuwa anaitwa na ofisi nzima, alikuwa anapekua faili ambalo lilikuja na picha na ushahidi kuwa mtu wanayemtafuta bado yupo nchini mwao na anafanya mpango wa kufanya tukio lingine kubwa. Kim akapagawa kwa taarifa hizo. Akaanza kupekuwa huku na huko lakini wakati anapekua, akajikuta katika kero kubwa baada ya kunusa moshi wa sigara. Akaangalia mbele yake na alikutana na sura ya mtu anayemjua.
Boss, umechukua likizo, nini umefuata?” Akamuuliza yule jamaa ambaye alikuwa kasimama mbele yake. Alijulikana kwa jina Boss Six ama Inspekta Six. Alikuwa na asili mbili, moja ya Kikorea na nyingine ya Kiafrika. Yeye aliipenda Korea kupita maelezo licha ya wazazi wake kumsihi arudi Afrika.

“Kuna kukaa nyumbani kwa matukio haya?” Akauliza Six na mwanadada hakuwa na swali na badala yake, akampa zile karatasi. Six hakuzisoma sana. “Embu tutoke hapa, ngoja nikupeleke mahali ila usiage.” Six alimwambia Kim na mwanadada hakuwa na jinsi maana Six alikuwa mkubwa wake kwenye kazi.

Wakapanda gari la Six na moja kwa moja wakaenda hadi kwenye nyumba fulani ambayo ilikuwa pembezoni mwa mji. Tayari ilikuwa imetimu saa nane mchana. Six akasimamisha gari na kutoka na ilikuwa vivyo hivyo kwa Mwanadada Kim ambaye aliyashangaa mazingira ya nyumba ile ya kifahari na kisha akamfuata kwa nyuma mwenyeji wake ambaye aliingia ndani ya nyumba ile na huko mwanadada alikutana na sura ya Cheing ambaye alikuwa katika mawazo mengi na macho yake kuwa mekundu labda sababu ya kulia au kutolala.

“Mheshiwa kwanza pole.” Kim alimtoa kwenye mawazo mwanaume yule na Cheing alimtazama na kisha akamtazama Six.

“Tunaweza kumuamini na kumtumia?” Akamuuliza Six bila kuitikia pole ambayo alipewa na Kim.

“Hana shida. Ni muelewa na namuamini sana kwenye mambo kama haya.” Akajibu Six na kumtaka Kim akae kwenye kochi moja ambalo lilipatikana mule ndani.

“Binti. Familia yangu imechukuliwa na huyu kijana ambaye kaleta maafa nchini. Hivyo kwa taarifa zake, anasema anataka aonane na mimi na kunikamata.” Akaanza kwa kifupi Cheing.

“Kwani ulimfanya nini?” Kim akamuuliza.

“Sijajua binti yangu. Ila anasema nahusika na kuhujumu nchi pamoja na kuharibu maisha yao.” Akajibu Cheing.

“Wewe unamjua?” Akauliza swali lingine na kabla hajajibu simu ya ndani ya jumba lile ikaita. Macho yakamtoka Cheing.

“Simu za humu ndani zote ni mbovu.” Akaongea kwa mshangao na wakati huo simu iliendelea kuita. 

“Nenda kaipokee. Labda ni huyu gaidi.” Akaongea Kim na Cheing akasimama na kwenda kuipokea.

“Cheing. Naona una ugeni.” Akaongea Masai kwa sauti yake pana kiasi na Cheing akaweka sauti ambayo wote mule ndani wakaisikia.

“Simu za humu zilikuwa….” Hakumaliza kauli yake.

“Nimezitengeneza muda uliopita.” Cheing hakuwa na swali. 
Simu za nyumba ile zilifanya kazi kwani baada ya Masai kumuaga mke wa Cheing, alikwenda kwenye nyumba pekee ambayo Cheing aliimiliki na kutega vitu vyake ikiwemo kutengeza simu za mule ndani kwa ajili ya matumizi kama hayo.

“Unataka nini?” Akauliza Cheing.

“Nakutaka wewe saa kumi na mbili jioni.” Masai akajibu kwa makini.

“Wewe gaidi, unamtaka mheshimiwa wa nini?” Kim akaja juu kwa kuingilia yale maongezi.

“Sheiming Kim….” Masai akaita jina hilo. Mwanadada akabaki kimya. “Muadilifu mkubwa katika kazi zako, lakini hujui kama wewe ndiye umekaa na magaidi hapo.” Masai akaendelea na mwanadada akacheka kwa sauti.
Yaani wewe ulete maafa nchini, halafu useme eti sisi ndio magaidi?!” Kwa mshangao Kim akauliza. “Nitakukamata kwa mikono yangu na kukuua mwenyewe kama utaleta shida.”

“Siamini kama mtoto mzuri kama wewe na mwenye akili kama wewe, hujui hata kinachoendelea nchini mwako.” Masai akaongea kwa utulivu. “Mimi ni mtenda haki Kim….” Akajibu Masai.

“Mtenda haki gani umeua wanajeshi wote wale? Na polisi wenzangu.” Akabwata Kim.

“Umejiuliza wale polisi wote na wanajeshi wote walikwenda kufanya nini pale?” Swali hilo likamfanya Kim atulie kwa muda na kulifikiria mara mbili. “Ni wewe uliwatuma askari wako waje pale na silaha za kivita?” Akauliza tena.

“Wewe Gaidi.” Six akaongea kwa mara ya kwanza.

“Boss Six. Inspekta mhujumu kushinda wote wa Korea.” Akajibu kauli.

“Tutakukamata.” Akakata simu ile kwa kuirudishia mahali pake lakini mara alisikia kicheko cha Masai.

“Simu hii naweza kukata mimi pekee. Usijisumbue Six.” Sauti ya Masai ikaendelea kutawala mule ndani. 
“Kim…” Kisha akamuita mwanadada pekee ambaye alikuwemo mule ndani. “Huyo mjinga anayejiita Six ndiye aliyewatuma wale polisi wakaangalie nini kimetokea kwenye nyumba ya Cheing na huyu pia ndiye anajua shida ya huyo Cheing. Hujiulizi ni kwa nini wamejificha hapo na kufanya mambo bila ofisi kujua?” Masai akalibakiza swali hilo angani. “Huyo pia anashiriki kwenye kutoa siri za nchi yenu. Muda wowote anaweza kuisaliti nchi.”

“Una uhakika na ukisemacho?” Six akamuuliza Masai.

“Ndio. Na saa kumi na mbili jioni, Cheing akiletwa kwangu, nitautoa huo ushahidi wa picha na makaratasi.” Masai akajibu na wakati huo mwanadada Kim alikuwa anaanza kutokwa na tongotongo juu ya yanayoendelea nchini mwake.

“Huna jipya gaidi.” Akaongea Six.

“Hapana. Ninayo mengi ikiwemo kutaka kumpa sumu mkuu wako wa kituo lakini akanusurika na wewe kuhusika kwa ukaribu kumuua yule muandaaji wa chai ya mkuu wako maana ni yeye ndiye alikuacha jikoni siku ile na kupata nafasi ya kuweka sumu.” Akaongea Masai na Mwanadada Kim macho yakamtoka pima maana kesi ile ilifungwa toka miezi miwili iliyopita. “Na vipi wale wanadada unaowauzia Wamarekani kule kwenye Casino la Cheing?” Akamuuliza tena.

“Cheing una Casino?” Akauliza Sheiming Kim. Cheing akawa kimya asijue ajibu nini.

“Analo. Tena kwa jina la mdogo wake ambaye alimuua mwenyewe mwaka juzi.” Kimya kikatawala na hakuna ambaye alikuwa anataka kuongea zaidi ya Six na Cheing kuomba MUNGU yule mnoko akate simu. “Ohoo! Naona wote mpo kimya.” Masai akaongea kwa sauti ya utani.

“Tunataka umalize.” Akajibu Six huku anaelekea dirishani na kufunua dirisha kidogo ili aweze kuona kama mtu wanayeongea naye yupo maeneo hayo.

“Sawa. Mkiwa tayari kuniletea Cheing, chukueni kikaratasi kipo chini ya simu hii. Nipigieni.” Masai akawajibu. Cheing akainua simu na kukiona hicho kikaratasi. Kweli kilikuwa na namba za simu za nchini Korea. “Naona umekiona.” Sauti ya Masai ikasikika. “ Basi kwa herini. Na Kim, leo umependeza sana. Nimependa hizo sare na saa ambayo uliyoivaa. Ni saa ya zawadi toka kwa mumeo eeh! Huyo Six ndiye alimpa kesi hadi hivi sasa yupo gerezani akisubiri kinyongo. Mkikubali kumleta Cheing, nawapa ushahidi.” Masai akaongeza na simu ikakatwa.
Ina maana huyu mbwa yupo hapa muda wote” Six akaongea.

"Haiwezekani." Mwanadada Kim alitoka pale alipo huku akikataa yale aligoyaongea Inspekta Six. Alifunua madirisha lakini hakumuona mtu yeyote.

"Ndio nakwambia sasa. Kanipungia na mkono akiwa ndani ya gari." Six akathibitisha kauli yake. 

"Lazima awepo maeneo haya." Cheing akawa upande wa Six. "Na yawezekana hata haya maongezi anayasikia." Akaongeza. 

"Ila kweli. Na ndio maana pia alijua kuwa tutakuja hapa." Six akajazia maana ya maneno ya Cheing. Kimya kikatanda bila mtu kuongea. 

“Ni kweli maneno aliyoyaongea huyu gaidi?” Akamuuliza Six.

“Hayana ukweli Kim. Wanijua mimi.” Akajibu Six.

“Naomba nikukamate Boss maana macho yako yanaonyesha yanadanganya.” 

“Utanikamata ukiwa na uthibitishio.”

“Sawa na nataka we mwenyewe ndio ujilete” Kim akaongea na Six akakubali. Mwanadada hakuujua unyama wa Six. Hakuujua hata kidogo, na laiti kama angeujua, angemkamata haraka. Lakini wanasema, jambo usilolijua…..

"Familia yangu."Cheing alijikuta akilia kwa nguvu baada ya maongezi ya wale askari wawili kuisha. "Sijui wamekula nini wanangu na sijui mke wangu anafanywa nini kwa sasa." Cheing alilalamika huku machozi yakimtoka. "Sababu ya ujinga wangu, ubinafsi wangu, na ukatili wangu, leo hii naiweka familia yangu kwenye kitanzi." Akaendelea kulia huku akilalama mambo ambayo yakamuacha kinywa wazi Kim. 

Lakini mwishowe baada ya masaa mawili, alikata shauri na kutaka kuikomboa familia yake. "Siwezi na sitovumilia familia yangu kufa wakati mimi ndiye mkosaji. Nipo tayari kufa." Cheing akatwaa simu yake na kupiga namba ambazo zilikuwa kwenye karatasi. 

"Nilijua kuwa utaamua kufanya maamuzi ya kiume." Ilisikika sauti ya Masai. 

"Nihakikishie kuwa familia yangu ipo salama." Cheing aliongea huku akivuta kamasi. Masai akampa simu mke wa Cheing. Na Cheing aliposikia sauti ya mkewe, akazidi kulia. 

"Nadhani umehakikisha uwepo wa familia yako."Masai akaongea na Cheing hakujibu neno. "Je? Unataka uonane nao, au niwaachie bila wewe kuagana nao." Akauliza Masai. 

"Vyovyote itakavyokuwa." Cheing akajibu na Masai akacheka kisha akaanza kumpa maelekezo ya jinsi ya wao kukutana. 

"Na ninataka aje huyo polisi wa kike kwa ajili ya kuipokea familia yako na kumpa ushahidi anaotaka kuuona huyo mbwa mwingine anayejiita Inspekta."Masai akamaliza bila kusikiliza upande wa pili. Cheing akawaeleza wale mapolisi alichoambiwa na Masai na kisha akatoka pale sebuleni na kwenda chumbani kwake.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni