UKURASA WA 56 SEHEMU YA 08

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 8

"Watu wa kwanza kujua kuwa Chude Bobo imepatikana, ni Korea Kaskazini, na Mumeo ambaye alikuwa anamtumia Pyong kama muangalizi wake lakini Pyong huyu akawa anamsaliti kwenye familia yake hadi akaamua kuzaa na wewe."

"Tafadhali, usiongee hayo mambo." Mama yule akaja juu. 

"Unadhani mimi nimejuaje haya? Na kwa nini huniamini mimi kuhusu mumeo?" 

"Sikuamini kwa sababu hayupo hivyo."

"Ila wewe kuzaa na Pyong ni sahihi na unaamini. Tuliyotendwa sisi huyaamini." Masai hakutaka jibu, akaendelea. "Mumeo alimuagiza Pyong atume majeshi Tanzania kwa ajili ya kuitafuta hiyo Chude Bobo. Majeshi yakatumwa. Na yakatumwa mengi zaidi na zaidi. Tukapoteza familia na watu tunaowapenda. Tukawajeruhi wengine na furaha yetu ikamezwa na wageni." Masai aliongea kwa masikitiko. "Ila baadae tulipotea au kufa, na tulipofufuka, ndipo tukawa hivi. Tukatafuta maana ya Chude Bobo, tukaijua. Tukatazama ugenini ni wapi? Tukagundua ni pale Dodoma, na tuliangalia zile nyuzi kumi na tatu ni wapi, tukagundua ni posta ya pale Dodoma. Tukaenda na kukuta Chude Bobo." Masai akatulia kidogo."Halafu Chode Bobo yenyewe ni kitabu. Kitabu tu! Kimebadilisha maisha yetu na sisi kuwa wauaji, kuwa watu wakutanga tanga duniani kama mbwa asiye na matunzo. Kitabu kimesababisha leo hii kuwateka hata watoto wasiyo na hatia." Masai akajikuta anaongea kwa uchungu. "Sikupenda niwe hivi. Nilipenda nisome na kuwa mtu maarufu duniani kwa kufanya yaliyo mema. Nilipenda kuwa na familia yangu binafsi na maisha rahisi tu! Nyumba ya vyumba vitatu, na gari dogo tu! Sihitaji maisha ya kistaa, suti nne zingetosha sana mi’ kubadili mionekano yangu, lakini si hivyo tena. Sasa hivi nabadili muonekano kila kukicha ili msinijue, sina familia na mwanamke niliyepanga kuishi naye, hajui kama nipo hapa leo. Inauma sana, ila yote sababu ya kitabu tu. Na huko posta tulikoswa koswa kwa risasi na tulijeruhi wengine." Masai akalalamika na bila kutegemea, machozi yakamtoka. Akacheka na kuyafuta. "Mumeo akataka hicho kitabu. Akamtuma Pyong ndio tukaja hapa Korea. Kumbe kitabu chote si kitu, ila Ukurasa wa Hamsini na Sita tu! Ndio unahitajika. Nilipewa hizo taarifa, nikauchana ule Ukurasa. Unamajina kumi na tano, na mumeo ndiye wa kwanza. Licha ya kutufanyia hayo yote, ila mimi nafanya kazi ambayo nimeagizwa tu!" Masai akawa kamaliza kumuelezea Mama yule ambaye alikaa kimya na kutazama chini. 

"Ukurasa wa Hamsini na Sita." Mama yule alijiongelea peke yake. 

"Lazima utakuwa unaujua tu!" Akaongea Masai.
Naujua ndio. Kumbe wewe ndiye unao?" Mama yule akauliza swali ambalo tayari lilikuwa na jibu. Masai hakumjibu zaidi ya kumtazama. "Ni ukurasa ambao unamajina ya watu hatari sana duniani. Hamna ambaye angekuwa jasiri kiasi hicho na kuwashughulikia watu hao. Imekuaje wewe? Una nini kikubwa hadi uchukue jukumu hilo?" Mama yule akauliza tena. 

"Jiulize mumeo kaingiaje kwenye kitabu cha watu hatari duniani."Masai akajibu. Mama yule akatikisa kichwa kwa masikitiko na Masai akawa anatoka kwenye chumba kile. Maneno ya Masai yakamuumiza kichwa mama yule. Akawa anataka kumuamini Masai lakini alimuamini sana mumewe kuliko kijana yule wa Kitanzania. Akabaki kwenye mabano. 
****
Baada ya Masai kutoka kwenye kile chumba, akaufunga mlango kwa nje. Alifanya hivyo akiwa na uhakika kuwa hamna ambaye atatoka wala kulalamika. Kama choo na bafu, vyote vilipatikana mule ndani. 

Akatoka hadi nje ambapo alichukua gari lake, ikiwa tayari imetimia saa nane ya usiku. Akachoma mafuta kwa dakika arobaini na tano hadi ilipokuwepo ile hoteli aliyopangishiwa na wakubwa wake wa kazi. Akapeleka gari lake palepale alipopaki kabla hajaondoka katika hoteli ile. Akatoka garini na kushusha begi lake la silaha, na kisha akachomoa kibao kingine kuonesha sehemu ya kuwekea magari, akabonyeza kibao hicho, mwanga ukawaka na akaenda hadi kwenye gari ambalo liliwakiwa taa. Katika mkoba alioukuta kule kwenye hoteli, pia alikuta ufunguo wa gari lingine pamoja na kibao cha sehemu ya kuwekea magari. Hivyo ndivyo ilivyokuwa. 

Akapanda gari lile ambalo nalo si haba, lilikuwa ni zuri na la gharama. Akaliwasha na kuondoka eneo lile na moja kwa moja akaanza kuifuata ile barabara ya kwenye ile nyumba ya Waziri wa Ulinzi Mstaafu. 

Akiwa kabakiza kilometa chache kabla ya kufika kwenye lile jumba, Masai aliongeza kasi na kuwasha taa zake kwa mwanga mkali zaidi. Walinzi waliokuwepo, waliweza kuliona gari hilo likija kwa kasi na wao wakajiandaa kwa mashambulizi. 

Lilipofika karibu zaidi, walinzi wale walinza mashambulizi ya risasi lakini kila kitu ambacho Masai kilikuwa kimeandaliwa ipasavyo, kuanzia ulinzi hadi silaha. Chevrolet jeusi, ndio gari ambalo Masai alikuwa analiendesha. Lilikuwa haliingizi risasi na liliundwa kwa mishemishe za Kijasusi pamoja na za Kijeshi, hivyo walinzi walikuwa wanafanya kazi ambayo haina madhara kwenye gari la Masai ambaye naye hakuwa nyuma kuwaonesha kazi wale watu.
Show time."Masai aliongea akimaanisha kuwa ni muda wa maonyesho. Akabonyeza vitufe fulani kwenye 'dashboard' ya gari lake na kwenye gari lile sehemu ya katikati ikachomoka 'min machine gun' iliyoanza kutema risasi nyingi sana huku Masai akiwa anaangalia kwenye luninga ndogo ya kwenye gari pale ambayo ilionyesha watu wote kama vivuli. Na kijana yule alipotaka kuwashambulia, aliielekezea bunduki yake kwenye hivyo vivuli. 

Sifa kubwa ya bunduki ambayo ilikuwa inauwasha moto usiku ule wa manane, ni kwamba, ilipogusa chuma kwa muda mrefu, chuma kile kiligeuka na kuwa mlipuko. Na vyuma laini kama vyuma vya gari, vilitobolewa vibaya na kulipuliwa kwa kupaishwa juu. 

Kijana yule alipokaribia geti la nyumba ile, alibonyeza vitufe vingine na upande wa kushoto na kulia wa gari lile, kukatoka mabomu ambayo unaweza kuyaona kwenye roketi za kivita lakini sasa zilionekana kwenye gari analoendesha Masai. Akabonyeza mara moja na bomu likachomoka na kwenye kuponda geti. Akabonyeza lingine na bomu lile lilipitiliza kwenye geti na kwenda kupiga nyumba ile kubwa. 

Akapitiliza na gari lake hadi kwenye uwanja mkubwa unaopatikana kwenye jumba lile. Akaingiza gari lake kwa mbwembwe zote kwa 'kupiga msele' mkali na kulisimamisha gari lake na kwa haraka alifungua mlango wa gari lake na kutoka huku akichomoa bastola zake mbili toka mgongoni na kuanza kumshambulia mlinzi mmoja baada ya mwingine na yeyote ambaye atajitokeza mbele yake kama adui. 

Masai alicheza na bastola zake kwa ustadi na baada ya dakika kadhaa, alikuwa kajibanza kwenye ukuta fulani ambao ulikuwa unatazama mlango wa kuingilia ndani kwenye nyumba ile. Akazirudisha bastola zake na kisha akapapasa juu ya ukuta ule na kukutana na bunduki mbili ambazo aliziweka usiku uliopita baada ya kuwamaliza walinzi wa eneo lile. 

Alisikia vishindo vya watu vikija upande wake na sauti za amri zilisikika zikiwatawanya wale wanyantiaji. 

"Naona mzee kaamua kuleta jeshi la Korea. Nadhani atakuwa kawaambia nahusika na mauaji ya General Pyong. Ngoja niwaonyeshe jeshi la mtu mmoja linavyofanya kazi." Alipomaliza maneno hayo, akaweka tayari bunduki yake na bunduki nyingine aliing'iniza kwa nyuma. Alitulia kwa muda na ghafla aliona mtutu wa bunduki ukiwa umetangulia, kwa haraka akavuta bunduki ile na kwa bahati nzuri akamvuta na mwanajeshi mmoja, ambaye alimuweka mbele yake na kisha akajitokeza na kuanza kuwamwagia risasi wanajeshi wengine ambao nao bila kufikiria, walianza kutema risasi zao na kwa bahati mbaya zikawa zinamkuta yule mwenzao. Hadi Masai anafika kwenye ule mlango wa kuingilia, mwanajeshi aliyemuweka mbele yake kama kizuio cha risasi, alikuwa kachakaa vibaya sana. Bunduki yake ilikwisha risasi na kwa haraka alimsukuma yule mwanajeshi kwa wenzake na kwa kasi ya ajabu, aliizungusha ile bunduki aliyoning'iniza na kuanza kutema cheche zake na safari hii, kwa makini zaidi.
Akaweka ufunguo wa kadi kwenye sehemu ya kufungulia mlango, na mlango kwa bahati yake, ulifunguka kwa sababu bado umeme ulikuwa unapatikana. Masai akaingia ndani ya nyumba ile na hakufunga mlango bali alikimbilia mbele kidogo na kuchomoa mabomu mawili toka kwenye hifadhi yake ya silaha. Akayarusha kule mlangoni na yeye akakimbilia kule kwenye chumba cha mke wa Waziri Wa Ulinzi Mstaafu na wakati huo milipuko ya mabomu ilisikika nje. 

Akaingia chumbani na kuchungulia uvunguni ambapo alivuta mkoba fulani mweusi na kisha akatoka nao chumbani na kwenda nao hadi kwenye korido moja na kufungua mkoba ule. Alikuta bomu moja la masaa likiwa limejaa kwenye mkoba ule. Akaliseti vema lilipuke ndani ya dakika tano. Na baada ya hapo, akalitupia sebuleni na yeye akaanza kukimbilia upande ambapo alipapiga bomu kwa gari lake. Kulikuwa na uwazi wa kupita, na alipopita, alikutana na gari lake huku walinzi na wanajeshi wengi wakiwa wanahangaika kupita kwenye ule mlango alioupita yeye. 

Akalivamia gari lake na kuliwasha na kisha kwa fujo zote akalitoa eneo lile akiwaacha wanajeshi wakihaha kumtafuta.

"Hizo zitakuwa salamu kwa huyu mjinga pamoja na wengine ambao watafuata." Masai aliongea huku akiwa katika mwendo wa kasi ndani ya gari lake. Akiwa katika mwendo huo, mlipuko mkubwa ulisika nyuma yake na yeye alitizama mlipuko huo kupitia vioo vya gari lake. "Hiroshima" Alifananisha mlipuko ule na bomu la nyuklia lililotupwa Hiroshima, Japan na Mmarekani. Bomu ambalo ndilo lilimaliza vita vikuu vya pili vya dunia.

Alirudi kwenye hotel ambayo alipaswa kufikia na kuliweka gari eneo maalum la kuegeshea magari na kisha akarudisha kibao ambacho alikitoa pale mwanzo. Alifanya hayo yote mwenyewe kwa kuwa kulikuwa hakuna wahudumu wa kuyafanya hayo usiku ule mpana na wenye maruwe ruwe.

Baada ya kuhakikisha kuwa gari lipo mahali husika, alielekea mapokezi na kugonga kengele ambayo mwanadada wa mapokezi alipoisikia, aliwahi kuamka na kwenda kumhudumia Masai ambaye alichukua ufunguo pamoja na bahasha ya kaki ambayo ilipelekwa pale kwa ajili yake.
Akaondoka eneo lile huku akiwa hana wasiwasi wowote, na moja kwa moja alikwenda kupanda lifti iliyompeleka hadi kwenye ghorofa ambalo ndipo chumba chake kilikuwepo.

Akaufungua mlango na kutizama huku na huko kuimarisha usalama na baada ya hapo hakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kusoma bahasha aliyopewa ambayo haikuwa na vitu vingi zaidi ya kuambiwa muda wa kuondoka pale na vitu ambavyo viliongezwa kwenye gari lake aliloliacha huku akiambiwa lile ambalo alienda nalo kufanyia vurugu, limeondoshwa usiku uleule.

Baada ya kuisoma, akaichoma moto karatasi ile na kisha akaenda bafuni na kujiweka safi. Na baada ya hapo akachukua suti nyingine matata na kuitinga mwilini mwake. Akajitazama kwenye kioo na kujiona yupo safi lakini nywele kidogo zilikuwa hajazitana. Akachukua kitana na kuzitana vema na baada ya hapo, akachukua mkoba wake ambao ulikuwa maalumu kwa kuhifadhia bastola zake, akatoka ndani ya chumba kile tayari kwa kwenda kukabidhi funguo za chumba.
****
DONATE VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Your donation helps the Admin to be even more active in sharing quality blog templates. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni