UKURASA WA 56 SEHEMU YA 07

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 7

Mzee yule alijikuta akipagawa kama kichaa kimempanda, akatwaa simu yake na kupiga namba kadhaa. Akawapigia simu walinzi wake waende kwake na hata wale ambao waliobaki pale nyumbani, nao walishituliwa na kisha kwa kiwewe walitaka kwenda kuingia ndani lakini kwa bahati mbaya, milango yote Masai aliifunga na funguo zao za kadi, hazikuwa na uwezo wa kufungua mlango wowote katika nyumba ile. 

"Watoto, kuna hatari sana hapa nyumbani. Nataka kuwapeleka kwa baba yenu, sawa?" Masai aliwaambia wale watoto na bila hiyana, wakakubali na Masai akawaambia waende chumbani kwao wakachukue nguo. Mama yao naye alitaka kwenda lakini Masai alimkataza na kumtaka arudishe makalio yake kwenye kochi. 

"Unadhani kwenye nyumba hii utatoka?"Yule mama akamuuliza Masai. Kijana wa Kitanzania akatabasamu kidogo na kisha akasogea hadi mbele ya mama yule. 

"Tunafanya mambo yetu kitaalamu. Unadhani mjenzi wa nyumba hii hatumjui na kwa mawazo yako unadhani sijui kuwa chumbani kwako ndio njia ya kutokea nje?" Maneno hayo yakamfanya Mama yule abaki kinywa wazi. Na Masai hakutaka mjadala tena, akatulia na kuanza kutengeneza silaha zake. 

Baada ya dakika kadhaa, watoto wale walirudi wakiwa na mabegi madogo ya nguo, wakiyabeba migongoni mwao. 
"Haya watoto, twendeni chumbani kwa mama eeh." Watoto wakafurahi na kuanza kuelekea huko. 
Mama wa watoto naye alifuata nyuma yao lakini pia Masai hakutaka kumuacha mbali naye akihofia asije kutoa taarifa kwa walinzi na kwenye njia aliyopanga kutorokea akutane na vizuizi. 

Walifika chumbani na Masai alimtaka mama yule naye achukue nguo kadhaa za kuvaa. Baada ya dakika, mama yule alikuwa kapata nguo anazohitaji na Masai akaenda hadi lilipo kabati la nguo na kukamata kitasa cha kabati. Akafungua na kwenye mlango wa kabati lile kulikuwa na kioo. Masai akawaita wale watoto na kuwataka wajitazame kwenye kile kioo. 

"Umejuaje haya wewe mtu?" Yule mama ikabidi amuulize Masai. 

"Sijatumwa kucheza Korea Kaskazini, nimekuja kufanya kazi tu!" Akajibu Masai. 

"Ila inaonekana unajua mengi sana kuhusu sisi. Lakini sijajua kosa la mume wangu." Mama yule akamwambia Masai. 

"Utajua kesho mapema sana."Masai alimjibu mama yule na wakati huo, wale watoto walikuwa mbele ya kioo. "Kaeni kama baba alivyowaambia." Masai akawataka wale watoto na yule mtoto mdogo alichutama huku yule mrefu akashika kiuno na kutabasamu. Miale myekundu ilichomoka kwenye kioo na kuanza kuwaskani wale watoto na baada ya kumaliza, ukuta mmoja ndani ya chumba kile ulifunguka na ghafla wale watoto wakaanza kukimbilia kule kwenye chumba kilichofunguka. "Twende Mama." Masai akamwambia mama yule naye bila hiyana akawafuata wanawe.
****
Masai akiwa na familia ya Waziri wa Ulinzi Mstaafu ambaye ndiye Waziri aliyemtaka Jenero Pyong akawatafute Masai na Malocha kwenye ule Mkasa wa Jina, alikuwa nje na wale watoto huku akiwa makini kabisa asiweze kuonekana. 

Gari lake lilikuwa mbali naye lakini aliliona japo si vema kwa sababu ya giza ambalo lilikuwa limetanda usiku ule. Akatamani kulifuata gari lake lakini alisita kwa sababu alijua litakuwa limezungukwa na walinzi au wanajeshi wowote ambao wangemletea zengwe. 

Kwa akili ya haraka, alitoa ufunguo wa gari lake na kisha akaubonyeza. Gari lile lote liliwaka taa na kung'aa hadi likafanya walinzi waliokuwa gizani kuonekama vema. Masai akachomoa simu yake, kisha akafanya kama anaivua kava la nje, lakini hakuwa anavua kava bali simu ile ikafunguka katikati kama vile kompyuta mpakato. Akabonyeza kidogo, na gari lake likawaka na Masai akaliona kwenye kioo cha simu yake. 

Akaparaza kioo cha simu ile, na picha ya gari ikaondoka na kuja picha ya ramani. Akaona gari lake lilipo na kwa umakini mkubwa, akachora kwa kidole sehemu ambazo gari lile linatakiwa kuzipita hadi lifike mahali anapotaka. Baada ya zoezi hilo, akabobyeza sehemu ya 'Options' au chaguzi, kisha akachagua 'self defence' yaani aliruhusu gari lile lijilinde lenyewe. 

Walinzi walikuwa wanalizunguka gari lile wasijue wanataka kulifanya nini. Wakichungulia ndani hawaoni mtu lakini gari lilikuwa linanguruma. Na wakati wao wanashangaa, Masai yeye aliliruhusu gari lile liondoke na lifuate njia ambazo alizichora kwenye ramani. Gari likashituka kidogo na walinzi wale wakarudi nyuma huku mitutu ya bunduki zao ikiwa sawa. 

"Tuondokeni hapa." Masai aliiambia ile familia aliyoiteka na kisha akambeba mtoto yule mdogo huku yule mwingine akibebwa na mama mtu ambaye alikuwa hana jinsi bali kukubali kila analoambiwa na Masai. 

Kijana Wa Kiafrika, aliiacha nyumba kubwa bila kuonekana na walinzi waliokuwa wameizunguka lakini wasijue kuwa kulikuwa na njia ambayo iliwatoa watu ambao walikuwa wanawatafuta. Na njia hiyo iliwapeleka mbali na ambapo hawawezi kuonekana kirahisi. Masai aliingia ndani ya daraja na kwa makini alitembea huku mtoto mdogo aliyembeba akiwa kamkumbatia kwa nguvu kwa sababu ya uoga wa giza nene walilokuwa wanaenda kulikabili. Mawani mbili zilitolewa, moja akavaa Masai na nyingine akavaa yule mama, hiyo iliwasaidia wao kuona vema gizani. 

Gari ambalo lilishituka kidogo na kuwafanya walinzi warudi nyuma, lilijipiga gia lenyewe na kuanza kuondoka kwa vurugu na kuwafanya walinzi waanze kupiga kelele na kukoki bunduki zao. Bila kuchelewa, wakaanza kulimwagia risasi gari lile ambalo halikuingiza risasi hata moja. Kasi ilikuwa kubwa toka kwenye gari lile ambalo liliwasha taa zake na kunyoosha barabara ambayo Masai alichorea kwenye simu yake. 

Likiwa katika kasi hiyo, magari mawili yaliyokuwa wazi, tumezowea kuyaita 'GOFU' yalijitokeza pembeni ya barabara na kuingia kwenye ile barabara ambapo gari la Masai lilikuwa linapita. Wanausalama wanne, wawili toka kwenye gari moja na wawili toka kwenye gari lingine, walisimama vema pembeni ya gari lile na kuanza kulimiminia risasi gari, lakini hamna ambacho waliambulia zaidi ya kupoteza muda tu. 

"Haliingizi risasi." Bwana mmoja aliongea kwa Kikorea. 

"Ni gari la wapi hili?" Mwingine akauliza. 

"Sijui. Halafu tulilikagua na tuliona halina dereva. Sasa sijui kaingiaje." Mwingine akaongea na dereva wa kigofu kile, akatoa ishara kwa gari lenzake na gari lile likawasha taa za kumruhusu afanye anachotaka. Dereva akakimbiza gari kwa kasi ya mwisho na kulikuta gari la Masai ambalo alienda nalo sambamba. Akatizama vema ndani ya gari lile na hakuona vema sababu ya vioo vyeusi vilivyofungwa kwenye gari lile.
Weapon activation" Gari lile liliongea lenyewe likitaka kuruhusu silaha yake. Huo ndio ulinzi binafsi ambao Masai aliuruhusu kwenye gari lake. Ghafla taa za pembeni za gari lile zikafunguka na kurusha mabomu kuelekea kwenye lile gari la maadui ambalo lilienda naye sambamba. Bila kutegemea, mabomu yale yakatua kwenye injini na kuilipua. Kwa kuwa gari lilikuwa mwendo wa kasi, lilifumuka vibaya na kurushwa angani na kisha mlipuko mkubwa ulisikika na wakati huo, gari la Masai lilihigeuza na kutizama lile gari lingine la maadui na wakati huo lenyewe likiwa linarudi kinyume. Taa za mbele zikafunguka, na kurusha mabomu mawili ambayo nayo yalienda kulipiga vibaya lile gari kwa kushtukiza kwa sababu walikuwa kwenye mshangao wa kuliangalia gari lao lingine likipotea. 

Baada ya matukio hayo ya kushtukiza, gari lile likajizungusha tena na kukaa sawa na kuondoka eneo lile likiwa limeibuka mbabe kwa magari menzake ambayo yalikuwa ya kijeshi. 
****
Baada ya dakika ishirini, Masai alikuwa kwenye ile barabara ambayo ilikuwa inampeleka hadi kwenye hoteli akiyoipanga. Akatizama saa yake na aliona bado dakika kadhaa ili gari lake lifike pele. Na baada ya dakika hizo, gari lake lilifika na Masai akatabasamu na kisha akalitaka lijizime na kujifunga vitu vyote ambavyo aliviruhusu. Baada ya zoezi hilo, akawapandisha wale watoto sehemu ya nyuma na mke wa Waziri wa Ulinzi Mstaafu sehemu ya mbele ya abiria. 

Masai akageuza gari na badala ya kuanza kupanda ile barabara kuelekea kwenye ile hoteli, yeye aliishuka akienda kwingine kabisa. 
Baada ya nusu saa, alikuwa amefika katika nyumba moja iliyokuwa pembezoni mwa Mji kabisa. Alimuamsha Mke wa Waziri Mstaafu na kisha kwa pamoja walishirikiana kuwabeba watoto ambao tayari nao walikuwa wamebebwa na usingizi. Masai alifika katika mlango wa kuingilia wa nyumba ile na kubonyeza namba fulani zilizokuwa kwenye kibonyezeo kilichobandikwa ukutani. Mlango ulifunguka na kijana wa Kitanzania alizama ndani na baada ya kuingia tu! Taa za nyumba ile ziliwaka zenyewe na eneo zima ya jumba lile lilionekana vema. 

"Eti Mama, hapa nahitaji pesa za mumeo?" Masai akauliza baada ya kuiangalia nyumba ile kwa dakika kadhaa. 

"Nani kakutuma lakini?" Akauliza Mama yule kwa huruma. 

"Nimetumwa na wananchi wa Korea kuwaletea mtahiniwa wao." Masai akajibu kwa kifupi na kuanza kuelekea kwenye mlango mwingine. Mama yule alimfuata huku naye akiwa kabeba mtoto wake mwingine. Wakaenda hadi chumba kimoja na kuwalaza wale watoto. 
"Mumeo ni mtu wa ajabu sana. Unajua bila yeye, mimi na wenzangu tusingekuwa hivi?" Masai alimwambia mama yule huku akiwa anamtazama pale kitandani alipokuwa amekaa akichezea nywele za wanaye. 

"Aliwafanyaje?" Akauliza yule mama. 

"Kuna kitu kinaitwa Chude Bobo, umewahi kukisikia?" Akauliza. 

"Niliwahi kumsikia akiongea neno hilo mara kwa mara miaka ya nyuma lakini sikujua ni nini kwa sababu hakuwa akitaka kabisa kunishirikisha kwenye mambo yake."

"Okay. Ni jina la kitabu ambacho Chude kwa lugha sijui ya wapi, inamaanisha mgeni na BOBO ile B ni 13 na O ni nyuzi. Kwa hiyo ilikuwa ni nyuzi 13 kwa 13 (BOBO=13°13°). Hapo walimaanisha kuwa, hiyo Chude Bobo ipo Ugenini nyuzi kumi na tatu kwa kumi na tatu." Masai akawa anamuhadithia mama yule. "Sisi tulikutana na jina lile kwenye jumba moja ambalo halijakwisha ujenzi huko Tanzania." Mama yule akashituka. 

"Wewe Ni Mtanzania?" Akauliza kwa mshangao. 

"Ndio. Mtanzania halisi kabisa."

"Ndio wale mliyoteswa sana na baadae ikagundulika mmeuawa na watu wasiojulikana?" 

"Mume wako alihusika katika vifo vyetu."

"Haiwezekani. Mume wangu hawezi kufanya hivyo hata kidogo."

"Unaongea kwa sababu huna hulijualo. Ila ungekuwa unajua lolote, usingeongea hayo."

"Si rahisi kuamini usemayo kijana."
Labda hadi Hayati Pyong angekuambia kuhusu mumeo." Mama yule akamtazama Masai kwa mshituko. 

"Pyong amekufa?" Akauliza.

"Ndio. Tena kifo rahisi sana. Ila nilimuahidi kitu kimoja kabla hajafa." Masai akajibu. Mama yule akamtazama akiwa hataki kusikia ambacho Pyong aliahidiwa na Masai lakini kijana yule alimwambia. "Nitawatunza watoto wake na nitawalinda. Na ndicho nachofanya kwa sasa." Mama yule akashusha pumzi kwa kasi. 

"We ni nani lakini?" Akauliza tena. 

"Naitwa Frank Masai au Man'Sai, The Undercover Agent wa Kitanzania nayefanya kazi katika shirika la kipelelezi duniani (A.W.A -All World Agents) na nimeagizwa hapa kuja kumchukua mumeo." Akajibu Masai. Mama yule alikaa kimya na kubaki akimtazama Masai asijue anataka kuongea nini. "Hiyo Chude Bobo," Masai akaendeleza hadithi yake kuhusu Chude Bobo. "Jina lake sisi tulilipata kwenye pagala huko Dodoma Tanzania, na mimi na rafiki tukaanza kulitumia bila kujua linahusiana na nini. Likawa maarufu sana kwa pale Dodoma. Tulikuwa hatujui maana yake na wala mimi sikuwa hivi unavyoniona, ila lile jina ndilo likaniunda mimi na kuwa mpelelezi wa siri pale Tanzania na baadae nikaitwa A.W.A." Masai akatoka pale aliposimama na kwenda kwenye mlango na kuuegemea.
DONATE VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Your donation helps the Admin to be even more active in sharing quality blog templates. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni