UKURASA WA 56 SEHEMU YA 06

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 6

Masai akabonyeza tena rimoti yake na viatu vyake vikamrekebisha, badala ya kutua kwa tumbo, vikamfanya atue kwa miguu na bila kishindo. Kwa haraka akaimbilia pembezoni mwa ukuta na kuangalia juu kidogo kwenye pembe ya nyumba ile. Akashuhudia kamera moja ikiwa anaanza kuzunguka kuja upande wake. Masai akachomoa kifaa kingine ambacho kilikuwa sawa na kasha la kiberiti. Akakirusha kile kifaa, nacho kikaenda kunasa chini kidogo ya kamera, na kwa haraka akabonyeza saa yake matata aliyoivaa, na kamera ile ililala chini kwa sekunde na baadae ikanyanyuka. Tayari ilikuwa haina uwezo wa kuchukua tukio lolote la nje.

“Bado kamera tatu.” Alijiongelea na kuanza kupita pembezoni mwa ukuta huku mawani yake matata sasa ikiendelea kumuelekeza pa kwenda. Alifika sehemu, na mawani ile ikampa alama ya hatari na kisha ikaonyesha picha mbili za walinzi ambao nao walikuwa wanasilaha nzito za kivita sawa na wale wengine. Lakini hawa walisimama sehemu moja na macho yao yalikuwa kule ambapo Masai alikuwa anatokea.

“Mbwa kajidhatiti sana huyu. Kila sehemu kuna walinzi wawili. Tena waliyokuwa vema kivita. Sijui anadhani mimi ni Shetani.” Akajisemea tena huku anachomoa bastola yake na kuipachika kiwambo cha kuzuia sauti. Na baada ya hapo, akatoa kifaa kingine kidogo na kwa haraka, alikirusha kifaa hicho, nacho kilienda kutua nyuma ya wale walinzi na kisha kikatoa mlio mdogo wa mlipuko ambao uliwafanya wale walinzi wageuke haraka nyuma na kumpa mgongo Masai ambaye naye bila kupoteza nafasi, alichomoka toka kwenye uficho wake na kuwachapa risasi za vichwa kwa kasi ambayo hakuna ambaye aliitegemea, hata wewe msomaji. Walinzi wale wakadondoka huku bunduki zao zikitoa kelele kidogo. Masai kwa kasi, akakimbia hadi pale walinzi walipodondoka na kutizama huku na huko kuona kama kuna kamera au mtu mwingine yeyote ambaye anaweza akaleta tatizo kwenye harakati zake. Hakuona lolote na badala yake alisikia simu ya upepo ya mlinzi mmoja ikiuliza kama wote wapo.

“Kodi namba tano, toa taarifa.” Simu ile ilitamka maneno hayo na ukimya ukawala na moyo wa Masai ukamuanza kwenda mbio kwa sababu kama taarifa isingetoka, basi ni wazi kuwa ingejulikana kuwa yeye yupo pale na ingesababisha watu aliowafuata wangetoroshwa. “Kodi namba tano, toa taarifa.” Ikasisitiza tena ile sauti toka kwenye simu ya upepo.

“Kodi namba sifuri, salama.” Sauti nyingine ikajibu ule ujumbe na Masai akashusha pumzi ya ahueni. Kile kifaa alichopachika nje ya geti, kilipeleka mawasiliano hadi kwa watu waliomtuma. Hivyo kama kutatokea majibizano kati ya watu ambao tayari wamekufa, basi upande ule utajibu. Lakini ili wapate uhakika kuwa hao watu wamekufa, ni lazima waulizwe mara mbili ndipo nao wajibu.

“Sawa kodi namba tano. Endelea.” Ikajibu upande wa pili na Masai akaivuta miili ya wale walinzi pembeni na silaha zao akaenda kuziweka juu ya ukuta ambapo hamna atayeweza kuziona kirahisi.

Baada ya kuweka silaha zile sehemu anapotaka, alianza kuelekea mbele ambapo kulikuwa na mlango lakini juu ya mlango ule, kulikuwa na kamera ambayo ilisimama na kuonesha eneo lilelile la mlangoni. Masai akatoa kifaa kingine kama alichokitoa kwenye kamera za mwanzoni, nacho akakirusha kistadi na kwenda kukamata sehemu husika na kuifanya kamera ile ilale kwa sekunde kadhaa na kisha kuamka lakini ikiwa imepoteza uwezo wa kuendelea kuchukua matukio kule nje.
Kifaa ambacho kilifanya kazi ya kuzuia kamera za sehemu zile zisiendelee kufanya kazi, kiliitwa Magnet Anti-Camera yaani sumaku isiyopatana na kamera. Ilibuniwa China na ilikuwa inauwezo wa kufuata sehemu ambayo inamtandao wa CCTV na kisha kunasa hapo. Ni ufundi mdogo sana wa kurusha kifaa kile ndio ulihitajika ili uende kutua sehemu sahihi. Na Man'Sai, tayari alikuwa kafanikiwa kuangamiza kamera tatu kwa kifaa hicho.
Akasogea kwenye mlango na kutizama huku na huko na kisha akatoa simu yake ambapo aliunganisha nyaya fulani ambazo ziliungana na kadi maalumu mfano wa zile kadi za ATM. Akawasha simu yake na kubonyeza kidogo, kisha akatumbukiza kadi ile kwenye kitasa cha kielekretoniki, nayo ikazama bila shida. Akabonyeza namba fulani, na kitasa cha mlango kikakubali sheria kwa kufunguka. Masai akapumua kwa pumzi ya ahueni na kwa uangalifu mkubwa, akaanza kuingia ndani. 

Saa yake ya kisasa, iliwaka baada ya yeye kuingia ndani na ilionyesha ramani ya ambapo anatakiwa kwenda. Kwa umakini alianza kwenda kwa kufuata ramani ya kwenye saa yake. Sehemu zenye kamera, saa ile ilimshitua na yeye akafanya yaleyale ambayo aliyafanya kwenye kamera zingine. 

Alifika kwenye mlango wa chumba kimoja uliosomeka kwa maneno ya Kikorea lakini yakimaanisha Chumba Cha Mitambo. Masai alichomoa simu yake na kadi ya kufungulia milango, akafanya kilekile alichokifanya nje wakati anaingia. Alikuta wafanyakazi watatu wakiwa wanaangalia kompyuta zao ambazo zilikuwa zinaonyesha matukio ya nje. Kwa bahati mbaya walikuwa hawajui kama kuna mtu nyuma yao, na hiyo ilikuwa faraja kwa Masai ambaye alichomoa visu viwili na kisha kwa haraka, akamchoma nacho shingoni bwana mmoja aliyekuwa upande wa kushoto na kwa kasi ileile, alimziba mdomo bwana wa katikati huku yule wa upande wa kulia, naye akitumbukiziwa kisu cha shingoni. Akiwa anauhakika kuwa wale wawili hawana uhai, aliweza kumbana vema yule wa katikati hadi naye akapoteza uhai. 

Akamsukuma pembeni na kusogeza kiti pembeni, sasa akawa anazitazama kompyuta ambazo zilionesha sehemu kubwa ya jumba lile. Akatoa kifaa kingine toka kwenye mkoba wake mdogo alioingia nao ndani na kisha alikiunga. Nacho kikapeleka taarifa nzima makao makuu ya anapofanyia kazi. 

"Chumba namba tano, yupo mke wake." Safari hii sauti ilisikika kwenye saa yake. "Na chumba namba saba, ndipo kuna watoto wake ila kuwa makini, hujamaliza walinzi wote." Baada ya maneno hayo, Masai akaitikia na kisha akatoka ndani ya chumba cha mitambo tayari kwa kwenda vyumba ambavyo aliambiwa ndivyo anaweza kuwapata wahusika.

Alifika chumba namba tano, kisha akakitazama na kukivuka na kwenda hadi chumba namba saba ambapo alifungua mlango kwa njia ileile na kuzama ndani ambapo alikuta watoto wawili wakiwa wamelala huku mmoja akiwa na makadirio ya miaka saba na mwingine miaka minne. 

"Shing.. Shing.." Masai alimuita mtoto mmoja ambaye alikuwa ni wa kike na mkubwa kuliko yule mwingine. Shing akafumbua macho yake na kumuuliza Masai kwa Kikorea kama kuna tatizo. "Hamna shida. Muamshe mdogo wake twende sebuleni, tunatakiwa kuondoka usiku huu."Masai akajibu na mtoto yule bila kujua kuwa Masai ni adui, alimuamsha mdogo wake na kisha wakenda sebuleni ambapo Masai alienda kwenye luninga kubwa iliyopo kwenye sebule lile na kuizungusha hadi akaona nyuma yake. Akapachika vifaa fulani na kisha akarudisha ile luninga kama ilivyokuwepo. 

"Kamuamshe na mama aje. Sawa Shing?" Masai akamwambia na mtoto yule akaenda kwenye kabati kubwa lililopo mlemle na kuchomoa ufunguo ambao ulikuwa ni wa kadi. Akaenda kwenye mlango wa mama yake huku akimuacha mdogo wake wa kiume na Masai ambaye alikuwa anacheka cheka ili kutomtisha yule bwana mdogo. 

Baada ya dakika tatu, Mama yao alitokeza lakini alikumbwa na mshtuko mkubwa baada ya kukutana na sura ya Masai. 

"Usiwatishe watoto Mama Shing."Masai akamuwahi kwa lugha ya Kiingereza ambayo wale watoto walikuwa hawaielewi. Mama yule akatulia na kuchonga tabasamu na kisha akaenda kwenye kochi lingine na kukaa. "Usifanye ujinga wowote kwa sababu wanao watakuwa mali ya ardhi. Sawa?" Masai akachimba mkwara na mama yule alionekana kutii bila shuruti yale ambayo alikuwa anaambiwa na Masai. 
Kijana yule Muafrika, alisimama na kufuata rimoti ya luninga na kisha akaiwasha luninga ile.
Kifaa ambacho alikiunga kwa nyuma, kilisaidia kusafirisha mawasiliano hadi kwa Waziri Mstaafu wa Korea Kaskazini ambaye alikuwa na uhakika kuwa hamna mtu yeyote ambaye anaweza kuingia ndani ya familia yake na kufanya vurugu za aina yoyote. 

Kifaa kile kiliundwa kwa matirio ya kompyuta na kuwekwa programu za simu lakini kilikuwa maalumu kwa ajili ya kuungwa kwenye luninga na kuwasiliana na mtu umtakaye huku unamtazama.

Masai aliwasha luninga na kisha akatoa simu yake na kupiga namba kadhaa, simu ikaita na baadae ikapokelewa.

"Babaa." Watoto waliita kwa sauti ya juu kwa lugha ya Kikorea baada ya kumuona baba yao kwenye luninga. Mstaafu yule wa serikalini, alijikuta anakodoa macho bila kusema neno baada ya kumuona Masai akiwa katabasamu huku anatingisha mguu wake. Watoto walikuwa wanafuraha baada ya kumuona baba yao usiku ule. 

"Kijana, endapo utawagusa hao watu, hutorudi nchini kwako salama." Waziri mstaafu aliongea kwa Kiingereza ambacho kilikuwa hakieleweki kwenye masikio ya wanae. 

"Naonekana kama mtoto kwako eeh!" Masai aliongea. 

"Haijalishi, mtoto au mkubwa, ila naapa kwa Mungu, nitakuua." Akaongea tena yule Mstaafu. Masai akatabasamu na kisha akachomoa D-Eagle zake mbili za siliva na kuziweka mezani. 
Mama wa watoto alishituka na wale watoto walishangaa vile vyuma vilivyowekwa juu ya meza. 

"Msiogope watoto, baba anataka kuona kama naweza kuwalinda." Akaongea Masai kwa Kikorea na wale watoto wakageuka kwenye luninga na kumtabasamia baba yao. 

"Baba, anko huyu ni mzuri. Anavisu vingi sana. Anaweza kutulinda hadi urudi."Mtoto wa kike aliongea kwa furaha. Na Masai kuthibitisha hilo, akafungua mkanda uliyokuwa umebeba visu vingi vikubwa na vidogo na kuviweka pia mezani. Baba mtu akabaki anahaha asijue anataka kufanya nini.

"Unataka nini wewe paka." Akauliza kwa kiwewe. 

"Ohoo! Hujui paka anapenda samaki?" Masai akajibu. "Na samaki ni hawa," Akaionyeshea familia ya yule bwana. "Nitawala hadi mifupa. Nitawanywa mchuzi na nitakula hadi utumbo wao, kwa sababu mimi ni paka." Masai aliongea kwa sauti ya kutisha. "Lakini sitawala kwa sharti moja tu!"

"Sharti gani?" Jasho likiwa linamtoka yule Mzee, aliuliza kwa wahka. 

"Samaki mkubwa ukijileta." Kajibu Masai na Mzee yule alibaki hana neno la kuongeza. 

"Unalipwa kiasi gani na hao waliokutuma?" 

"Nalipwa roho yako tu. Sina malipo makubwa."

"Acha ujinga, pesa zipo kijana. Beba uondoke, na nitakusaidia kukuficha wewe na familia yako."

"Sina familia, kwa bahati mbaya. Mimi ndiye familia pekee."

"Basi nitakutorosha na kukupa pesa nyingi sana."

"Hizo hela ndizo zile ambazo ulihujumu wananchi kipindi kile?" Masai akamuuliza yule Mzee. 

"Wapi? Nilimhujumu nani?" Akauliza maswali mfululizo huku sasa moyo wake ukimuenda mbio.
Unaweza kukimbia lakini mbio zako ukawa unakimbilia jangwani. Unadhani huonekani lakini unaonekana vema tu." Masai aliongea huku akichanua tabasamu lake zuri mara kwa mara. Waziri Mstaafu wa nchi ile alikuwa kawehuka na asijue anataka kufanya nini. "Nakupa masaa kumi tu! Uwe umekuja sehemu ambayo nitakueleza." Masai akaongeza na kisha akaanza kumueleza ni wapi anaweza kupatikana baada ya kutoka pale. 
"Hakikisha unakuja peke yako ili kuepuka familia yako kupotea." Akamaliza na kukata yale mawasiliano.
DONATE VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Your donation helps the Admin to be even more active in sharing quality blog templates. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni