UKURASA WA 56 SEHEMU YA 04

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 4

Akaanza kuijaza risasi kadhaa ambazo zilikuwa zimefungwa kwenye mkanda uliokuwa umezungushwa kwenye ile bunduki. Wakati huo Range Rover ilianza kusogea karibu huku vijana wake wakianza kuhangaika kutoa vichwa madirishani tayari kwa kuivamia pikipiki ambayo ilikuwa imempakia Malocha.

“Wanataka vita hawa.” Malocha aliongea na dereva mtundu wa pikipiki alitizama nyuma kupitia vioo na kushuhudia bwana mmoja akiwa kajitokeza kichwa na bunduki aina ya SMG ikiwa mikononi kwake na jicho moja akiwa kalifumba kuonesha kuwa anarenga pikipiki yao.

“Hang Up (Jishikilie)” Mwanadada, dereva wa pikipiki aliongea hayo na Malocha kwa haraka alikamata vema kiti alichokalia na miguu yake aliibana vizuri kwenye pikipiki. Ghafla mwanadada alikata kona kali ya kushtukiza na wakati huo huko nyuma ilisikika SMG ikikohoa risasi kadhaa ambazo zote ziliishia kwenye nguzo za taa zilizokuwa zimesimama kwenye barabara.

“Shit.” Alibwatuka bwana mwenye SMG baada ya kuingiza kiwiliwili chake ndani ya gari na wao kukata kona ileile ambayo Malocha na dereva wake waliingia. Hapo walishuhudia umbali wa ajabu walioachwa na fundi wa kuendesha pikipiki. Wakachoma mafuta na kuendelea kuwafukuza.

“Wamefika tena wajinga.” Malocha aliongea baada ya kuona gari linalowafukuza likiwa umbali mdogo na wao.

“Waoneshe kazi hao.” Akajibiwa na mwanadada ambaye kwa ustadi na kwa akili ya ajabu, alikanyaga breki na kuanza kuirudisha nyuma pikipiki na wakati huo Range ile ilikuwa inakuja kwa kasi nyuma yao. Malocha akaanza kufyatua risasi mfululizo kwenye boneti ya gari lile. Bunduki ile inauwezo wa kufyatua risasi mara saba bila kujazwa na ndio maana Malocha alifurahi sana kuipata.

Ilipokwisha risasi, tayari bonet ilikuwa imenuliwa vibaya sana na injini kupasuka. Mwanadada akaacha kurudi nyuma na kwa haraka akaingiza gia ya kuondoka huku Malocha naye akijigeuza kiustadi na kukaa vema kama inavyotakiwa kwenye pikipiki. Na wakati huohuo pikipiki yao ikiwa inaondoka eneo la tukio, mlipuko mkubwa wa gari ukasikika. Range Rover inakuwa haina chake kwenye himaya ya wakina Malocha.

“Hamna usumbufu tena.” Aliongea mwanadada na kuzidi kuchoma mafuta kwenda alipopanga.
******
“Karibu Malocha. Hapa ndipo kazini kwetu.” Aliongea mwanadada matata kisura na kiumbo baada ya kufika sehemu ambapo kulikuwa kuna uzio mkubwa na ndani ya uzio huo kulikuwa na magari mengi makubwa ya kusafirishia mizigo.
Walifika na geti lilifunguliwa, kisha mwanadada aliendesha pikipiki yake hadi kwenye chumba kimoja na kushuka sanjari na Malocha ambapo kwa pamoja walitoa kofia za pikipiki vichwani mwao. 
Hapo ndipo uzuri wa mwanadada yule mwenye asili ya Asia lakini rangi yake nyeusi kama Muafrika ikimpa uzuri ambao Malocha alitulia kwa muda na kumtazama kwa matamanio.

“Ahsante,” Alishukuru Malocha akibabaika kidogo. “Huendani kabisa na yale mambo uliyoyafanya dakika chache.” Akaongeza.
Ha hahaa,”Akacheka mwanadada. “Wanaume ni kazi rahisi sana kuuawa na mwanamke. Anadhani anachokiona nje ya mwili ndicho kilichondani ya roho,” Malocha akakaa kimya kutafakari maneno yale. Ni kweli yalichoma panapo mtima wake. “Twende huku ukakutane na bosi.” 
Aliongeza maneno hayo mwanadada huku akitoka nje na kuanza kwenda mahali ambapo yeye anasema ni kwa bosi.

“Lakini wewe ni mzuri na mrembo…..” Malocha aliongea hayo na kabla hajamaliza, alikatishwa na mwanadada.

“Nafahamu na ninaelewa. Ahsante kwa hilo Malocha.” Kijana wa Kitanzania akashusha pumzi bila kupenda.

“Namaanisha, unapaswa kuwekwa ndani na kuolewa na bwana mwenye pesa au yeyote yule na kisha kuanzisha familia bora.” Akaongea baada ya pumzi ndefu. Mwanadada yule akajipekua kwenye koti lake na kutoa wallet kisha akatoa picha.

“Huyo ni mume wangu na huyo ni mtoto wangu. Lakini wote niliwapoteza kwenye mapambano kama haya. Sihitaji kuwaingiza watu wasiyo na hatia kwa kile nilichokianza.” Malocha akakaa kimya huku akiitazama ile picha ambayo ilikuwa inamuonesha kijana mmoja wa kizungu akiwa kavaa suti na binti mmoja mwenye miaka kama mitano kwa makadirio.

“Pole sana.” Kwa upole Malocha aliongea.

“Naitwa Kelly. Nadhani huna maswali tena wala ushauri.” Aliongea mwanadada huku akielekea kwenye mlango mwingine wa kioo cheusi.

"Okay Kelly. Nimefurahi kukutana na wewe." Akajibu Malocha huku naye akiwa nyuma ya mwanadada yule akielekea kule anapoenda. 

"Tunaenda kwa mkuu wetu sasa. Anakusubiri kwa hamu kubwa." Akaendelea Kelly. 

"Umejuaje kama anasubiri kwa hamu?" Akauliza Malocha. 

"Kwa sababu anatusikia hapa na nawasiliana naye na ndiye alikuwa ananielekeza barabara za kupita wakati ule naendesha pikipiki." Akajibiwa. 
Na wakati huo walikuwa wananyoosha kolido ndefu ambayo mwisho wake ulikuwa ni kwenye mlango mmoja wa kioo. 

Kelly akabonyeza namba kadhaa, na mlango ule ulifunguka na moja kwa moja Kelly akanyoosha hadi kwenye dawati la kisasa ambapo dada mwingine mrembo wa haja, alikuwa amekaa nyuma yake. 

"Karibu Dada Kelly." Mwanadada yule ambapo kibao chake kilisomeka kama Sekretali, alimkaribisha Kelly kwa furaha. 

"Ahsante Missah. Nimekaribia." Akashukuru Kelly huku anampa mkono mwanadada aliyejulikana kwa jina la Missah. 
Alikuwa mweupe na mwenye asili ya Kiafrika na Kiarabu. Alipendeza kwa mavazi yake na aliposimama, alionekana kavaa sketi ya mpira na iliyovuka magoti. Alikuwa mrefu licha ya kuvaa viatu vya chini. Alibeba umbo la Kiafrika zaidi kuliko la Kiasia. "Kutana na Malocha Malingumu. Yule bwana wa Tanzania niliyekwambia namfuata." Malocha akasogea mbele Missah na kumyooshea mkono wake wa kuume. 

"Habari yako mrembo." Alisalimu Malocha huku anabusu mkono wa Missah. 

"Woow. Nimekutana na ‘jentromeni' Dada Kelly." Missah aliongea huku anafurahia kitendo alichokifanya Malocha. "Sikudhani kama utakuwa hivi. Nilidhani upo kama wapelelezi wengine wa Kiafrika. Sura ngumu ngumu na wanavaa kihuni, kama yule Masai." Missah aliongea.
Unamjua Masai?" Malocha akauliza. 

"Ehee! Yule tena. Ni very handsome, ila mavazi yake tu. Ndio nachokaga. Niliwahi kukutana naye mara moja. Nilimpa maelekezo ya kufika Cuba." Akajibu Missah. 

"Aisee. Mkuu anatusubiri Malocha. Missah yupo singo, unaweza kuomba naye mtoko." Kelly ilibidi aingilie kati maongezi yale.

"Okay. Miss Missah, leo tunaweza kuwa pamoja?" Malocha akatupa kete yake. 

"Bila shaka Malocha. Kwa leo tu, mimi na wewe." Missah naye hakuwa na ajizi. Kisha Malocha na Kelly, wakaenda mlango unaofuata baada ya ule wa mapokezi. Missah akabofya kitufe kilichopo chini ya dawati lake na mlango ule ukafunguka.

Waliingia ndani ya ofisi kubwa ambayo ilikuwa na luninga zipatazo tano. Kila upande kuliwekwa luninga na kwa mbali, bwana mmoja alikuwa akasimama kwenye dirisha akitazama nje. 

"Hivi ulisema kuwa mkuu atakuwa anasikia kila kitu? Kwa hiyo hata maongezi yangu na Missah kayasikia?" Malocha aliuliza kwa kunong'oneza. 

"Ukishaingia humu ndani, hamna chochote kinachofanya kazi. Iwe simu, kompyuta, kamera, redio na vyote uvijuavyo ambavyo vimetokana na mkono wa binadamu, havifanyi kazi. Ni vile vilivyoumbwa na MUNGU tu, ndio hufanya kazi."Akajibu Kelly na wakati huo yule bwana aligeuka na kuanza kuja kwa kasi walipokuwa wamesimama Malocha na Kelly. 

"Kelly. Karibu sana mama." Akiwa kavaa mawani iliyoziba jicho moja, bwana yule alimsalimu Kelly na Kelly aliipokea salamu ile kwa heshima. "Naona umefanikiwa kumleta huyu bwana." Akamgeukia Malocha. "Habari yako Bwana Malocha." Akamsalimia. 

"Njema. Habari yako bwanaaa..." Akaacha hewani sentensi yake ili bwana yule ajutambulishe. 

"Naitwa Bwana Brighton Sancho. Na ndiye Naongoza oparesheni nzima ya kuwasaka watu wa kwenye Chude Bobo kwa upande wa Korea Kaskazini na Asia." Akajibu Sancho na wakati huo, Kelly aliruhusiwa kutoka ndani ya ofisi ile. 

"Kivipi tena, unaposema kuwasaka watu wa Chude Bobo?" Akauliza Malocha huku Sancho akimuonyesha sehemu ya kuketi. 

"Kwenye kile kitabu cha Chude Bobo, kuna majina yanayopatika ndani ya Ukurasa fulani. Majina hayo ni lazima yatafutwe mmoja baada ya mwingine na kupelekwa kwenye mahakama ya dunia ya makosa ya jinai. Hapa napokueleza, Masai anaelekea huko katika kisiwa kimoja kwa ajili ya kumkamata Waziri wa Zamani wa Ulinzi wa hapa Korea." Akajibiwa. 

"Unazungumzia Ukurasa wa Hamsini na Sita ambao aliuchukua Masai?" 

"Ndio. Ni ukurasa wa hamsini na sita. Na ndio Chude Bobo wenyewe. Yale makaratasi mengine ni porojo tu. Japo yanakitu kama utayasoma."

"Ila kitabu chenyewe tayari wanacho wale Wakorea wa kule."

"Hapana. Kitabu kipo mikononi mwetu. Yule bwana aliyekipokea, Masai alimchana chana mishipa ya damu. Na Masai alipoondoka, kijana wetu aliingia kwenye kile chumba na kuchukua kitabu." Akajibu Sancho na kukiweka kitabu mezani. Malocha akabaki kaduwaa. Akameza mate na kumuangalia Sancho. 

"Unadhani Masai atafanikiwa misheni mliyompa?"
Huwa tunatuma mtu ambaye ni lazima afanikiwe. Na tunaamini Masai ndiye chaguo sahihi."

"Na kuna majina mangapi kwenye ukurasa?"

"Kumi na tano."

"The Shadow, yupo?" Akauliza Malocha. 

"Ndiye wa Mwisho."

"Navyomjua Masai, atafanikiwa ila mtapata hasara."

"Hasara ipi?" 

"Vifo vya watuhumiwa wa kwenye huo ukurasa. Yote ni kumfikishia ujumbe The Shadow."

"Yawezekana ukawa sahihi." Sancho aliongea huku maneno yale yakizama vema kichwani mwake. 

"Naomba niongezeke kwenye hii kazi." Malocha akaomba ridhaa ambayo ilipingwa vikali na Sancho. 

"Hapana. We kesho utarudi Tanzania. Sisi tumemuomba raisi wako mtu mmoja tu! Ambaye ni Masai. Kama kuongeza, tutaongeza watu wetu." Maneno hayo na mengine mengi, yakamfanya Malocha awe hana na la kusema. 

"Sawa." Akakubali kiroho upande.

"Ila kazi anayokwenda kuifanya mwenzako, si kazi lelemama. Ni hatari kuliko hatari yenyewe. Anaenda kucheza na tobo la Jehanamu. Ni kazi ambayo wapelelezi wetu hawataki hata kuiona." Akaongea Sancho mwenye asili ya Kibelgiji. 

"Namjua Masai. Hatokubali kushindwa japo kuna sehemu zitamshinda."Malocha aliongea kwa sauti huku anamtazama Sancho usoni. Wakaongea mengi zaidi hadi wakaridhika na ndipo Malocha alitoka na kwenda moja kwa moja kwa Missah ambaye alitoa mawasiliano yake. Baada ya hapo, Malocha alitoka nje na alikuta gari moja la gharama likimsubiri. Akapanda na safari ya kwenda kwenye hoteli anayotakiwa kulala, ikashika hatamu. 
****
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni