UKURASA WA 56 SEHEMU YA 02

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 2.
KOREA KASKAZINI

Baada ya umeme kukatika ndani, General Pyong akaanza kuhaha huku na huko asijue anataka kufanya nini. Ndani ya dakika kadhaa, alikuwa kachachawa vilivyo kwa sababu si kawaida kwa nchi ile kukatikiwa kwa umeme.

Umeme ulirudi ghafla na hapo General Pyong alikutana na sura ambayo kamwe hakuwahi kuwaza kuiona. Ndio, hakuwahi kuiwaza kuiona kwa sababu haikutakiwa kuwepo pale kwa muda ule.

DAKIKA KADHAA NYUMA KABLA YA MALOCHA KUINGIA KUPELEKA CHUDE BOBO.

Mwendo wa dakika ishirini ulitosha kufika sehemu moja iliyokuwa na mgahawa mkubwa ambao watu mbalimbali walijumuika usiku ule na kupata chakula pamoja na vinywaji. 
Mwenyeji wao aliwapitisha njia kadhaa na baadae alifika katika mlango mmoja ambapo ulifunguliwa na kijakazi wa kike.

“Anahitajika mtu mmoja tu! kuingia.” Aliongea kijakazi yule kwa kiingereza cha kuungaunga na Masai alimpatia mkoba Malocha ili aingie yeye. Masai akabaki nje ya mlango na Malocha akaingia ndani.

“Tunaweza kwenda huku sehemu ya kusubiria wageni kaka yangu.” Kijakazi yuleyule ambaye alimruhusu Malocha kwenda kwa General Pyong, alimwambia maneno hayo Masai na bila kusita alikubaliana na kijakazi yule ambaye alitangulia mbele na Masai nyuma hadi katika chumba kingine ambacho nacho kilikuwa kimetengenezwa kwa njia ileile za matirio ya makaratasi.

”Unaweza kuingia kaka.” Aliongea kwa Kiingereza kijakazi.

“Shunshey.” Masai akamjibu dada yule kwa Kichina na kumfanya mwanadada kijakazi akodoe macho asiamini alichokisia.

“Unajua Kichina?” Aliuliza pia kwa Kichina Kijakazi wa kike.

“Hata Kikorea.” Badala ya kujibu kwa Kichina, mwanaume akajibu kwa Kikorea Kaskazini na kuingia mule ndani na hapo alikutana na sura za watu wapatao wanne wamekaa wakipata chai na wakati huo mlango wa chumba kile ulifungwa na bwana mmoja ambaye alionekana kama mlinzi.

Huku nje, kijakazi alijikuta akipagawa baada ya kugundua Masai anaweza kuongea lugha zote ambazo zinatumika ndani ya chumba kile. Akatamani aingie ili awape taarifa, lakini akahofia sana usalama wake hasa kwa sababu alielewa ni nini kinaenda kutokea.

“Ndio huyo mjinga tuliotumwa tummalize,” Aliongea Mkorea mmoja aliyekuwa anakunywa chai kana kwamba anapiga hadithi na mwenzake kwa lugha yao. Masai akawaangalia na kujifanya hajaelewa chochote.

“Namuonea huruma. Anakufa bado kijana,” Akajibu mwenzake na wote wanne waliokuwa wamekaaa kwenye meza moja ya pembeni, wakacheka kwa sauti.

“Sasa sijui kwa nini aliamini kuwa wazazi wake wapo hai na wakati kitambo sana wamekwishaoza. Huyu ni mjinga sana,” Bwana mwingine aliongea kwa sauti yake ileile na wakati huo Masai alikuwa amekaa kama wafanyavyo Waasia kwenye meza fupi ambayo ilikuwa na birika pamoja na kikombe cha chai.
Waafrika wote ni wajinga tu. Tena huyu ukute ndiye mwalimu wao mkuu,” Yule Mkorea wa mwanzo akaongea tena na kufanya maongezi yao yazidi kunoga kwa vicheko.

“Muacheni anywe chai yake ya mwisho. Akimaliza hiyo tu! Ni kipondo hadi anapasuka kichwa.” Bwana mwingine alizidisha utamu wa maongezi kwa kutumia lugha yao ya Kikorea. 
Masai akamimina chai kwenye kikombe cha udongo, na kisha akainywa kwa pupa na kutua kikombe hicho kwenye meza. Kisha akawatazama wale mabwana ambao walizuga kuwa hawamfatilii.

“Tunaweza kuanza mchezo sasa. Nimekwishapata kikombe changu cha kwanza na cha mwisho cha chai.” Aliongea Masai kwa Kikorea na kuwashtua wale mabwana. Macho yakawatoka na kushindwa la kufanya zaidi ya kunyanyuka wakiwa wanachomoa visu vikubwa toka kwenye maficho yao. Wakavikamata mikononi mwao.

Kwa makini, Masai akiwa palepale amepiga magoti (Mtindo wa Kukaa wakati wa kula huko Asia hasa China, Korea, Vietnam na Japan), akashika birika la udongo lililokuwa na chai, na kulirusha kwa nguvu ambapo lilimkuta kwenye paji la uso bwana wa kwanza ambaye alijikuta akilia kwa sauti ya juu kwa maumivu.

Kabla wenzake hawajajua nini kimetokea, walishtukia mwenzao mwingine anapigwa kwa meza ndogo iliyokuwa inatumika kwa ajili ya kuwekea ile chai. Na hapo ndipo walipogundua kuwa hamna Mwafrika mpumbavu duniani ila ni watu watulivu na wapenda amani sana.

Wawili wale waliokuwa wamesimama bado wasijue wenzao nini kimewapata, walishtukizwa na ujio wa Masai mbele yao huku mwanaume akiwa hana sura ya mchezo hata kidogo. Wakiwa na visu vyao vikubwa mikononi, walitaka kuanza kuvitumia lakini tayari mpinzani wao alikuwa amekwisha wawahi na kuwadhibiti mikono yao kwa pamoja.

Kwa nguvu za umoja wao, wakaanza kumsukuma kwenda kule alipotoka na wakati huo yule mfungua mlango alikuwa anajitazamia filamu ya bure kabisa kati ya Wakorea na Mweusi toka Tanzania.

Waliendelea kumsukuma na Masai alipotazama nyuma, aliona anaenda kugota kwenye ukuta wa matofali badala ya wa makaratasi. Ilionekana wazi kile ndicho chumba cha mwisho hivyo uzio wake ulikuwa ni imara.

Kijana wa Kitanzania, alilala chini haraka huku bado kakamata mikono yao. Hali hiyo iliwafanya wale mabwana wa Kikorea nao kuinama na nafasi hiyo Masai aliitumia kwa miguu yake kumuwekea jamaa wa kwanza kifuani na kisha akamnyanyua kwa nguvu zake zote na kumrusha kwa nyuma ambapo alijigonga ukutani na kilio kikali cha maumivu kikamtoka. Sasa akawa kabaki bwana mmoja na kisu chake.

Akapigwa mtama mmoja matata sana na kujikuta akilamba sakafu bila kupenda huku kwa ustadi mkubwa Masai akijibetua na kusimama wima kisha akampiga teke zito la tumboni yule aliyekatwa ngwara.

Bwana aligongweshwa ukutani alikuwa anagaa gaa hapo sakafuni na kitendo bila huruma, Masai alimfuata na kumpiga mdomoni kwa kutumia goti lake, yule bwana akajigonga kisogo kwenye ukuta na kuzidi kupatwa na maumivu.
Alipowaangalia wale aliowapiga kwa dhana hafifu, alishuhudia wote damu zikiwatoka vichwani. Akamtamzama mfunga na mfungua milango, na kwa tahadhali alianza kumfuata lakini cha ajabu bwana yule alifungua mlango ule na kumuoneshea atoke nje.
Mshindi hutoka bila kuguswa na asiyehusika na mpambano.Tutakutana tena baadaye kama kazi hii nitahusika.” Aliongea yule bwana na Masai alitoka na hapo uso kwa uso alikutana na Malocha aliyekuwa ametoka kukabidhi kitabu kiitwacho Chude Bobo.

“Vipi mbona unahema?” Aliulizwa Masai.

“Wajinga walitaka kuniua. Sina wazazi wala nini,” Masai aliongea harakaharaka na hakumuacha Malocha aendelee kumuuliza. “Chukua usafiri wowote hapa, na potea eneo hili. Rudi Tanzania na kuendelea na kazi tuliyoianza. Mimi nitapambana na watu hawa wachafu waliyoifukia familia yangu na dunia. Ukitaka kuwasiliana na mimi, namba zangu ni hizi,” Akampa mawasiliano Malocha ambaye wakati anataka kumuuliza Masai, alisikia sauti ya General Pyong akiuliza Ukurasa Wa Hamsini Na Sita ulipo. “Ondoka Maloo. Msalimie Lisa.” Masai alimsisitiza huku anamsukumia nje ya mlango.

Baada ya kuhakikisha kuwa Malocha katoka ndani ya jengo lile, haraka kijana wa Kitanzania alienda kwenye switch kubwa ya umeme na kuizima na kisha kwa haraka, akachomoa kifaa fulani toka kwenye soksi yake na kuanza kupandikiza kitu huku akisaidiana na mwanga mdogo toka kwenye kurunzi ya kalamu aliyokuwa kaikamata kwa midomo yake.

Kwa rimoti ndogo aliyokuwa kaikamata mkononi, aliwasha umeme wa mgahawa ule na hapo uso kwa uso akakutana na General Pyong ambaye alikuwa katika taharuki kubwa baada ya kukutana na sura ya mweusi mwenye hasira za kumeza hata nyumba.

“Ninao mimi ukurasa wa hamsini na sita.” Aliongea Masai ambaye alikuwa kasimama katikati ya chumba kile alichokutania Pyong na Malocha.

“Nipe kabla sijakuua.” Aliongea Pyong.

“Familia uliyoituma niiue, tayari inaugulia maumivu. Ni kheri nawe ukimbie au uniambie nitakachokuuliza.” Kwa nyodo nyingi Mtanzania asiye na jina, aliongea mbele ya Mkorea anayeheshimika nchini kwake.

“Unadhani kila kitu ni bure katika hii dunia?” Aliuliza Pyong huku akianza kuzunguka ndani ya kile chumba kwa umakini, macho yake yakiwa yanamtazama mpinzani wake.

“Kama unajua si bure, kwa nini unataka kupoteza muda wako kwa kutaka Ukurasa wa Hamsini na Sita?” Akaulizwa Pyong.

“Nahitaji kwa sababu ni ukurasa wetu.” 

“Mbona upo kwangu? Unajua kuwa umetugharimu maisha yetu huu Ukurasa? Familia zetu hazipo duniani, na mbaya zaidi, tumekuwa watu hatari kuliko ambavyo tulipanga kuwa?” Akaongea kwa hisia Masai.

“Sijali hilo. Nachotaka ni ukurasa wa hamsini na sita.” Pyong, aliongea na kisha toka kiunoni kwake, alichomoa visu viwili vyenye sentimita kama thelathini na tano na mbele vina ncha kali.

“Naona umedhamiria. Karibu kwenye ufalme wa kifo.” Masai naye alitamka huku akikaa tayari kwa mpambano.
****
Malocha baada ya kufukuzwa kwenye ile nyumba na rafiki yake, alitoka nje haraka na kuangaza huku na huko kuona kama atapata msaada wa haraka lakini hakuuona na badala yake aliona kundi la watu kadhaa likiacha shughuli zake na kusimama tayari kumfuata. Hali ikawa tete kwa kijana yule ambaye naye si haba alikuwa anaweza kuupanga mkono na kuwanyamazisha wapinzani wake. Lakini kichwa chake kiliwaza mengi sana kwa haraka. Vipi wale wapinzani wakiwa na bunduki na silaha za moto kama hizo? Ataweza kupambana nao?

Alipopata jibu, aliamua kwa haraka kuanza kuondoka eneo hilo huku tahadhari akiwa nayo kuliko kitu chochote. Alitembea kwa haraka na wale mabwana walikuwa wanamfuata nyuma kwa mwendo uliokuwa unaongezeka kila Malocha alipokuwa anaongeza mwendo.

Mwisho wa safari yao, uliishia kwenye soko moja ambalo lilikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu. Hapo Malocha aliipata ahueni na kuanza kujichanganya na watu hao huku macho yake yakiwa makini zaidi juu ya wale wanaomfuata.

Katika hekaheka hizo, akafanikiwa kutoka kwenye kundi la watu. Na kwa kasi isiyo na kifani, alinza kukimbilia eneo moja lililokuwa na barabara. Wapinzani wake walikwishajua lengo la Malocha, ni wazi alikuwa anataka kuchukua gari au usafiri wowote wa kumtoa eneo lile. 
Wale mabwana kwa kuligundua hilo na kwa kuwa wao walikuwa wamezongwa na watu, waliamua kutumia bastola zao kwa kuziweka hewani na kuanza kuwatisha watu walale chini. Waoga wa silaha walilala chini na kuwafanya wale mabwana wapite kirahisi huku macho yao yakiwa yanamlenga Malocha.

Kijana wa Kitanzania huku moyo ukiwa unamfukuta, akaanza kukimbia kunyoosha barabara na wakati huo maadui zake walikuwa wanamfukuza kwa nguvu zao zote. Hali ikawa tete kwa Malocha.

“Mpige miguu.” Adui mmoja alitoa wazo na jamaa mmoja alipiga goti na kuweka silaha yake kwenye jicho akiwa analenga miguu ya Malocha.
Akiwa tayari amechukua vema miguu ya Malocha, mara alikatishwa utamu wake kwa teke zito toka kwa mtu aliyekuwa juu ya pikipiki. Wenzake wakatazama ni nini kimemtokea mwenzao, hapo walikutana na sura iliyokuwa imevaa kofia ya kuendeshea pikipiki. 
Maadui wote wakarudi kutaka kupambana na mwenye pikipiki lakini mtu yule alionekana mzoefu wa pikipiki kuliko labda kitu chochote. Akasugulisha lami tairi za pikipiki yake, moshi mzito unaonuka mpira ukawa unafuka eneo lile na kuwafanya wapinzani wasione kitu na huo ndio ulikuwa wasaha wa mwenye pikipiki kuondoka haraka eneo hilo kwenda anapokimbilia Malocha.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni