PENZI LANGU LINAVUJA DAMU SEHEMU YA 02 | BongoLife

$hide=mobile

PENZI LANGU LINAVUJA DAMU SEHEMU YA 02

RIWAYA: PENZI LANGU LINAVUJA DAMU

MTUNZI: HUSSEIN O. MOLITO (Mwandishi wa kitabu cha “ SIKU 71”)

SIMU: 0718 97 56 59

SEHEMU YA 2

Niliyageuza macho yangu na kumuangalia Haiba. Nilipokelewa kwa tabasamu murua lililoukosha moyo wangu. Nami kama ada yangu, wala sikutaka kupoteza maksi kizembe mtoto wa kiume. Nilimlipa tabasamu lenye afya zaidi yake.
   “kumbe wewe ni mcheshi hivi.”
Kauli hiyo ilinifanya nishtuke ndani kwa ndani. Maana ni kitu nilichotarajia kukifanya kwake kuanzia muda huo. Kumbe tayari alishang’amua kitu kilichopo kwenye ubongo wangu. Hakika nilifarijika. Ni sawa na kupewa ushindi mezani. Bila jasho nimepatiwa pointi tatu muhimu kabisa. Basi si kichwa kuvimba hapo. 

   Nikaanza kujishaua na kuweka kola ya shati langu sawa utafikiri ucheshi niliosifiwa ulikua kwenye mavazi yangu.

   Kila nilichokifanya muda huo, kiwe cha makusudi au bahati mbaya, kilimfanya mtoto huyo atikise kichwa huku akitabasamu.
   “Ahsante.. Hata wewe mcheshi pia.” nilirejesha majibu yalimfanya acheke kabisa na si kutabasamu kama awali.
   “ucheshi wangu umeuonea wapi?” 
alinuliza na kunifanya nipate muda wa kumtazama.
   “si nimeuona kupitia tabasamu lako. Hakika midomo na macho yako yanasadifu kilichomo ndani yako.” nilijaribu kudadavua kile kilichonijia kichwani mwangu muda huo. Maana sikuona njia ningine ya kuitetea hoja yangu zaidi ya kuendeleza sifa juu ya sifa.
   “haya.. Ahsante.”
Jibu hilo liliweza kuniambia sasa alihitaji kujua maendeleo ya laptop yake na si kitu kingine.
   “karibu hapa ili uangalie tatizo linaloisumbua Laptop yako.” Niliongea maneno hayo na bila kusita msichana huyo mbichi kabisa alisimama na kuanza kutupa hatua zake kwa kurusha miguu kistaarabu na kunisogelea. 
   
   Hakika hata na mimi joto la mwili likanipanda baada ya kumuona mtoto mzuri kama huyo akitii amri ya kunisogelea kirahisi kabisa bila kunibishia.

   Yale manukato yaliyobadilisha hali ya hewa ya ofisi yangu sasa yalinipiga haswa na kuzipa burudani pua zangu. Sijui alijipulizia manukato ya gharama kiasi gani, Maana harufu yake ilinifanya nitamani kumuuliza. Ila ubongo wangu wa nyuma ukaniambia Molito hicho sicho ulichomuitia Haiba kwenye kiti hicho. Basi nikawa mpole na kuichukua Laptop yake.
  “nimeichunguza kwa makini sana. Nimepata majibu sahihi kabisa juu ya ugonjwa ulioukumba Laptop yako.” nilifungua maongezi huku nikinyoosha maelezo kama vile nimefanya mimi huo utafiti. 
“nimegundua kua tatizo sio window kama nilivyozani hapo awali. Ila tatizo lipo kwenye kioo. Mashine yako inawaka lakini haioneshi kwakua kioo kimekufa. Ngoja nikujaribishie ili ujionee mwenyewe jinsi mafaili yako yanavyoonekana kupitia kioo hiki cha kwangu.” niliongea maneno hayo na kuichukua Laptop hiyo na kuiweka mezani kisha nikachomoa waya uliokuwepo kwenye mashine yangu na kuchomeka kwenye Laptop ya Haiba.
Ile nataka kuwasha tu, 
Laaahaulaaa! 
   Umeme nao ukakatika.

   Kile kiwewe kikanifanya nisahau upande aliokaa Haiba na kuamua kukaa ili kuanza kuilaumu Tanesco kwa kitendo chao cha kukata umeme wakati nataka kujizolea maksi nyingine za ufundi wa kuaminika kwa mtoto Haiba. Nilipokaa tu nikaisikia sauti ya mrembo huyo iliyonishtua sana.
   “Unanikalia!”
Aisee!
   Nilinyanyuka haraka na kukaa pembeni yake. Nilimshika Haiba ili kupooza maumivu ya kumkalia. 

   Hata sijui akili yangu ilikumbwa na kitu gani. Maana sikuwaza kua nilipomkalia ni mapajani. Hivyo nilipoyagusa na kuyapapasa kwa mikono yangu, nilihisi ulaini wa ajabu kama pamba vile. Hapo hapo akili ikarejea haraka na kuniambia, we Molito hayo unayoyapapasa ni mapaja.
doh! 
   Nilishtuka na kuachia mikono yangu haraka. Ila viungo vya uzazi viliweza kuniambia kua nilichokigusa ni kitu chenye hisia kali. Hivyo huenda nilichokifanya wakati huo nilifika mbali. Huenda nikawa nimemchukiza Haiba na kunishushia heshima yangu yote niliyojiwekea kwa binti huyo mbichi.
   “Naomba niende. Nitarudi kesho.” Nilishtushwa na sauti ya Haiba baada ya kufanya tukio hilo. Kiza kilikua kinene sana. Hata mbalamwezi tu haikuwaka muda huo, hivyo hatukua tunaonana sawia zaidi ya taswira tu na mawazo kulingana na sauti inapotokea.
   “umeme wetu naujua mwenyewe. Yaani hii line kuna watu wakipiga simu tu wanarejesha sasa hivi. Hivyo vuta subira kidogo.” nilijaribu kumzuia baada ya kuhisi huenda tukio langu la kumshika mapaja yake ndicho kilichomkimbiza hapo muda huo.
   “Muda umeyoyoma sana, na kutoka hapa na nyumbani kwetu ni mbali kidogo.” 
jibu hilo lilinipa amani kidogo. Maana hata kama alichukia kitendo changu ila hakutaka kuonyesha hasira zake juu yangu.
   “hapa sasa kidogo nina amani.......itakua amechukulia ni ajali kama ajali zingine.”
Nilijipa moyo kidogo ili ile hofu ya kumuudhi mtoto mzuri kama huyo iniondoke moyoni mwangu.
   “kaa kidogo tu. Yaani zikipita dakika kumi bila Tanesco kurejesha umeme, hata mimi nafunga ofisi naenda zangu nyumbani kupumzika.” niliongea hayo na kumuona Haiba akirejea kukaa kuashiria kua alikua tayari kubaki hapo kwa dakika kumi nyingine.
   “huna simu ya tochi uwashe.. Giza limetawala sana.”
Sauti yake ilinifanya nitoe simu yangu ndogo. Ila ubongo wangu uliniambia ‘wee Molito, hebu rudisha kimeo chako mfukoni. Unaweza kupoteza maksi zako kwa hicho kisimu kilichopitwa na wakati.’ nilirejesha haraka simu yangu mfukoni na kunyanyuka.
   “naomba nisubiri kwa dakika moja, naenda kununua mshumaa.” 
niliongea maneno hayo na kwenda dukani. Uzuri hakukua na foleni. Niliomba mshumaa na kutoa shilingi mia tano. 
   “chenji nitakuja kuchukua.”
Yaani hata kusubiri chenji nusu dakika tu niliona nachelewa, nilihisi Haiba anaweza kuondoka.
Basi nilifika na kuchukua kiberiti changu ambacho kwa hisia tu nilikua najua kipo wapi na kuwasha njiti hiyo. Ili nalenga tu kwenye mshumaa. Nikasikia kelele za watoto huko nje. 
   “uwooooooooooooooooo”
Sekunde hiyo hiyo na taa yangu ikawaka.

   Niliachia tabasamu na kumfanya Haiba acheke kabisa.
   “jamani nimekutia hasara ya kwenda kununa mshumaa bure.” Haiba aliongea maneno hayo na mimi nikaenda kukaa kwenye nafasi yangu ya awali.
   “leo ndio nimegundua umuhimu wa simu ya tochi na umuhimu wa kuwa na mshumaa karibu . Naweza kusema ahsante tu kwa hili funzo.” niliongea hayo na kumfanya azipokee sifa nilizompa kwa tabasamu.

   Adhana iliadhiniwa kuashiria kua zilibakia dakika chache tu ili kutimia saa mbili kamili. Hata mimi nilihisi huenda huyo binti alikua na wasiwasi kuchelewa kurudi kwao. Maana hata mimi mwenyewe sidhani kama ningemruhusu mtoto mzuri kama huyo awe mbali na nyumbani kwa muda mrefu kiza kikishaingia.

   Basi nikawasha computer zote mbili. Na kioo cha computer yangu kikaleta majibu ya yale niliyokua namuambia kwa nadharia hapo mwanzo.
   “jamani, sasa ili kuiponyesha hii laptop yangu itanigharimu kiasi gani cha fedha?” 
hilo swali lilinifanya nimuangalie usoni. Hakika alikua anatia huruma. Na niliweza kugundua kua alikua anahofia kwa ukubwa wa tatizo huenda ikawa gharama kubwa sana kulitibu tatizoo hilo.
Ni kweli, kwa kipindi cha mwaka 2010 shilingi laki moja na elfu ishirini ilikua ni pesa nyingi sana. 
 
  Japo mimi nilikua naitengeneza kwa wiki moja. Nikimpa bosi shilingi elfu thelathini na tano yake nakua mnene na kiasi kinachobaki kwangu nilikua nakitumia kununua nguo na kuwapa nyumbani kidogo ili nionekane mwanaume nafanya kazi. Usiku nakula kwa baba na kulala bure, wala sikua na hofu ya kulipa kodi. 
 
   Basi nilimtazama Haiba na kumtajia bei niliyotajiwa na Killer kwa ajili ya ubadilishwaji wa kioo cha Laptop hiyo.
   “shilingi laki moja na ishirini. Laptop yako uhakika kabisa inakua mpya kama zamani.”

   Nilijishangaa sikuweka hata mia ya ganji kama nilivyoshauriwa na Killer. Maana hiyo pesa yote inaenda dukani. Hivyo nilitakiwa kusema laki moja na nusu.

   Nilimuona kabisa akiipokea bei hiyo kwa unyonge. 
   “nitaenda kumuambia baba. Hivyo nitakupa majibu.” aliongea hayo na kuiweka laptop yake kwenye begi.
   “usiku sasa hivi na umesema unaishi mbali, huoni unaweza kuhatarisha laptop yako na watoto wa mbwa ukikutana nao kwa bahati mbaya?”

   Niliongea maneno hayo bila kujua nilikua natumia mfano wa kutisha kiasi gani. Mana nilipotaja watoto wa Mbwa nilikua nimetaja kundi hatari zaidi kwa mahala tunapoishi.
   “yaani umenitajia hao viumbe mpaka nywele zangu zimenisisimka. Naiacha basi, nitakuja kuipitia kesho.” Haiba aliongea hayo na mimi nikaafiki. Nikaliweka begi lake vizuri.

   Basi akaniaga na mimi nikamruhusu aende huku macho yangu yakimsindikiza mtoto huyo. Mangi wa duka lililokua mbele yangu alikua ananiangalia tu.
   “kaka hiko chuma ulichokifungia ndani ni cha moto hatari... Aisee kweli wewe ni kipenzi cha Warembo.” 
kauli ya Mangi ilikua inanikebehi. Maana vurugu zangu zote zilizima kwa mtoto mzuri Haiba. Maneno ya Mangi yakamchongea na kunikumbusha kua niliacha chenji kwake baada ya kununua mshumaa. Nikaamua kuifuata.
   “nipe chenji yangu we mlugaluga wa Njiro. Ninapoitwa kipenzi cha warembo muwe mnaelewa na kukubaliana na mimi.” 
nilijisifia na niliweza kumuona Mangi akinikubali. Maana kwa muonekano wa Haiba naamini hakuna mwanaume duniani ambaye atasema kua huyo msichana alikua na uzuri wa kawaida.
Hata hamu ya kuendelea kukaa hapo ofisini ilikuwepo basi, nyimbo zote nilizona mbaya. Yaani kiiufupi ladha ya kuchezea kitu chochote kwenye computer iliniishia kabisa.

   Nilihesabu pesa nilizoingiza siku hiyo. Si haba. Zilifika shilingi elfu kumi na tano. Kilikua kiwangu kizuri kabisa ambacho kikifika hua na amani moyoni mwangu.

   Basi nikafunga ofisi na kuanza safari ya kurudi nyumbani. Eti hata njaa nayo ilitokomea alipoelekea Haiba. Nakaenda kuoga na kwenda kulala.

   Simaanishi niliweza kufumba macho na kupoteza fahamu kwa kugubikwa na usingizi, bali namaanisha niliulaza tu mwili wangu kitandani na macho yakabaki kodo huku fikira zangu zikijaribu kuumba kile ninachokifikira kwa binti huyo.
 
   Niliona tu picha yetu ikiwa kwenye fremu tukiwa tumeoana. Molito akiwa kwenye kanzu ya mafuta mafuta na Haiba kwenye vazi matata la kihindi.
   “Molito huyu huyu au kuna Mwengine atakuja kumiliki hiki chombo?” 
nilijiuliza kwa sauti na sikusubiri majibu. Nilijifunika shuka ili kupisha ndoto zingine zije. Maana zile za kuota bila kufumba macho zilikua zinatumia sana ubongo na kuuchosha ubongo wangu kwa kuwaza vitu ambavyo si rahisi kufanyika. 

   Kwanza ile kutuonyesha kwenye ufahari kama ule nikahisi kabisa sio mimi. Maana hadhi yangu ilikua haifanani kabisa na hadhi ya sherehe hiyo yenye mavazi ya kihindi na kanzu za laki nne. Ilinichukua muda mrefu sana kupambana na mawazo niliyoyaita potofu mpaka kuupata usingizi halisi. Usingizi mzito usiokua na ndoto ndani yake na kuamka saa moja asubuhi.

   Nilienda kuoga haraka na kuondoka. Niliwahi ofisini na kuagiza chai kwa mama ntilie jirani yangu.

   Ilipofika saa Tatu na nusu, Haiba alifika ofisini kwangu. Siku hiyo hakuvaa miwani. Halafu nilimuona akiwa amevaa sketi fupi mpaka juu kidogo ya magoti yake. 

   Nilijiuliza huyu dada mbona yupo tofauti na wasichana wengine wenye muonekano unaofanana na wake? Wasichana wengi wenye asili yake hua wanavaa sana mashungi na wengine hujifunika mpaka nikabu kabisa. Ila yeye alikua huru kuvaa chochote kile alichojisikia kuvaa.

   Bado kidogo nimuulize habari za shule, ila niligundua kua siku iliyopita ilikua jumamosi na siku hiyo ni jumapili.

   Tulisalimiana na kumpatia begi lake la Laptop baada ya kugundua ndicho kitu alichoijia asubuhi ile.
   “Naitwa Molito.” 
Ilibidi tu nijitambulishe, maana niliona kama yeye ameridhika vile kutolifahamu jina langu.
   “Haiba, nadhani hujasahau.” aliongea hayo na kuachia tabasamu.
   “siwezi kukusahau mtoto mzuri kama wewe... Kwanza jana usiku umenitesa, na picha ya mapaja yako ikifika tu mie nabadili stesheni.” 
hayo maneno niliongea ubongoni tu. Jeuri ya kumtamkia mtoto mzuri kama huyo ningeitoa wapi? Basi macho yakaishia kumtazama tu mpaka alipokata kona na kuondoka. Niligeuka mbele kumuangalia Mangi. Nilijua kwa umbea wake lazima tu atakua anatuangalia. Kweli niliweza kumuona anatabasamu tu kama juha. 

   Akanionyeshea dole gumba kumaanisha kua ameamini kile alichokua anakihisi. Nami kwakua napenda maujiko, nikamrejeshea dole gumba na kuingia ofisini kwangu.

   Uchizi wa kupenda picha niliendelea kuwa nao. Hata wapiga picha waliugundua uchizi wangu na kuzidi kujipitisha kwangu kila dakika . Basi na mimi sikuacha kuwaungisha.

   Ofisini kwangu kulikua na ubao kama ule wa matangazo ya shuleni. Nilikua nautumia kubandika picha za hapo ofisini tu. Hakika niliipenda ofisi yangu. Na bosi naye alinipenda kwakua nilikua nampa pesa zake bila kulalamika biashara mbaya wala nini. Hata kama kuna siku umeme haukuwepo siku nzima. Nilikua radhi nikose faida ili yeye apate.

   Ilipita wiki moja bila kuiona sura ya Haiba. Nilitegemea hicho kitu kutokana na pesa niliyomtajia.
    “ningelikua na uwezo, ningelikuwekea tu kioo hicho mimi mwenyewe kwa fedha zangu” kuna wakati nilijiisema. Maana watoto warembo kama yeye hawatakiwi wapate tabu kwenye dunia hii.
   Siku ya jumapili, mishale ya saa nane mchana wakati napata chakula na juisi halisi ya matunda, ndipo nilipoiona sura ya Haiba iliyotokea kama mzimu mbele yangu. Basi nikafurahi sana na kumkaribisha chakula.
   “akuu, mimi nataka cha kwangu.”
Jibu hilo lilinifanya ninyanyuke haraka kwa ajili ya kumuagizia chakula.
   “hee, mimi nakutania tu. Nimeshashiba.”
Kauli yake hiyo haikuweza kunizuia kumuita mama ntilie aje amsikilize mgeni wangu.
   “naomba juisi ya embe.”
Aliagiza kinywaji peke yake. Nikaridhika na kumkaribisha ndani. Kilichonishangaza ni vile alivyokuja kukaa kwenye sofa la watu wawili ambalo mimi nipo. Nilihisi huenda kwakua ndipo Computer yangu inapoelekea, ila nilipata jibu lingine kua hakua ananiogopa tena kama hapo awali. Ameshanizoea. 

   Kila siku niliyomuona Haiba nilikua namuona mtu mpya kabisa mwenye sura moja. Nilitamani kumuuliza wewe ni mwanamitindo? Maana kila siku alikua anafanya kitu tofauti na kubadili muonekano wake. Hajawahi kukosea wala kuboa. Bali kila siku alikua ananifanya niuuone muonekano wake mpya ni bora kuliko muonekano uliopita.
   “Ahsante kwa ofa yako.”
Nilimshuhudia akiongea hayo baada ya kuvuta mrija uliopo ndani ya kikopo cha juisi hiyo halisi na kupita katikati yake na kuelekea kwenye kinywa kidogo kilichokolea rangi nyekundu aliyopaka makusudi kufananisha na nguo alizovaa na hereni zake.

   Nami nilimuiga kufyonza juisi kwanza kisha nikaipokea shukurani yake.
   “Ahsante nusu..”
nilijibu hivyo na kumfanya ashangae. Mashangao mzuri wa kimapozi kwa kiyatoa macho yake ambayo hayakunitisha. Bali yalikua yaninionyesha ni uzuri kiasi gani aliokua nao binti huyo msupu.
   “kwanini nusu jamani?” aliuliza huku akifyonza tena juisi kupitia mrija. Kwangu mimi niliona kama mitego, maana kwa jinsi mdomo wake anavyoukusanya na kujikinga rangi zake za midomo isinatie kwenye mrija, ndivyo alivyonitesa mwenzake kwa mawazo ya kijinga yaliyokuja haraka kichwani. ‘haka katoto kana makusudi?’ fikira zangu zikaniambia. Namimi nikakubali kweli kalikua na makusudi kwa kweli.
   “Nimekupa ofa ya chakula na juisi. Wewe umeagiza juisi peke yake. Huoni kama umeagiza oda nusu? hivyo hapa kila kitu itabidi kiwe nusu. Hata shukurani iwe nusu..Yaani nusu nusu.”
Kauli zangu zilikua za kawaida. Ila huyo binti bandama lake lilikua linafanya kazi sawasawa. Maana alikua anacheka tu hadi machozi kwa mbali yakawa yanamlengalenga.
   “usinichekeshe tena Molito. Nitapaliwa na juisi.”

   Kulikumbuka jina langu tu ikawa kitu kingine kwenye daftari la furaha moyoni mwangu. Kwa kauli yake alinizuia kuendelea kuongea na kunifanya nitabasamu tu. 

   Maana kuna wakati hata sikupanga kumchekesha kabisa. Japo nilikua nafarijika pindi nikimuona anacheka.

   Baada ya kumaliza Juisi yake na mimi nikawa nimshamaliza chakula changu. Nikaweka sahani pembani na muhusika akaja kuchukua vyombo vyake bila kunidai pesa. Maana alikua anajua mida yangu ya kumlipa.
   “nimeshapewa hizo pesa. Nitaipata lini laptop yangu?” Haiba aliongea maneno hayo na kutoa pesa na kunikabidhi bila kuhesabu. Na mimi nikazichukua na kuziweka kwenye droo bila kuzihesabu. 
   
   Kitendo hicho kilimshangaza sana Haiba. Hakuvumilia kuongea kile kilichomshangaza dhahiri machoni mwangu.
   “mbona hujazihesabu pesa nilizokupatia!... Zikiwa pungufu je?” swali hilo nililiritarajia na tayari nilikua na majibu yake.
   “sababu ni moja tu, Nimetokea kukuamini.” majibu yangu yalimfanya atabasamu kuashiria kua ameupokea vizuri uaminifu wangu juu yake.
   “ila sio vizuri kumuamini kila mtu kwenye pesa. Dunia imeharibika sasa hivi. Umdhaniaye ndiye kumbe siye.” Haiba alinikumbusha na kumfanya nimuangalie. 
   “hata mimi naitumia hiyo kanuni ya kutoamini watu. Ila wewe imetokea tu na ukiniuliza kwanini sina majibu kwa kweli.” niliongea hayo na kumfanya Haiba acheke.
   “Molito unanifurahisha sana. Natamani kuwa hapa kwa siku nzima. Maana unaniondoa msongo wa mawazo wa matokea ya mitihani.” nilijikuta nikijipongeza moyoni. Maana kitu pekee nilichohitaji kutoka kwa Haiba. Ni ukaribu naye tu. Nilitamani hata nimsindikize ili wasichana wanaoringa hapo mtaani waone kua nina msichana kisu zaidi yao. Nilitamani nafasi hiyo itokee. Ila uzuri wa Haiba ulinifanya nishindwe kusema chochote. Sikua na nguvu za kuweza kumshawishi kuwa vile ninavyotamani awe, ila sifa zake alizonisifia zilikua zinanifanya niamini kua huyu mbuzi ipo siku atafia tu kwa muuza supu.
   “yaani unatamani kile kitu ambacho mimi natamani?” niliuliza na kumtazama Haiba usoni mwake. Tuligonganisha macho yetu kwa sekunde kadhaa. Eti na mimi nikaona aibu, huu udhaifu sikuwahi kuupata kwa msichana yeyote yule. Maana nilipokua shuleni walikua wananiita Kanumba. Jina la nyota maarufu mcheza filamu kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Nilifurahi sana. Maana nilikua nacheza vile vipande vigumu. Tena mtu niliyekua namfuatilia ni mwengine kimataifa. Shah Rukh Khan, nyota wa India na dunia yote inamtambua. Maana yale mahaba ya kiwango cha lami yalikua kwake. Sikuwahi kuwa muoga kuongea maneno mazito ya mapenzi mbele ya walimu wangu na mamia ya wanafunzi walionizunguka kila sherehe shuleni hapo. Hivyo sikua muoga kabisa. Hata wasichana niliokua nao kimahusiano hapo nyuma sikuhofia waliponiambia wanataka kuondoka. Tena wengine tuliachana hata kabla hatujashiriki ngono. Niliamini Shah Rukh Khan mimi wa Bongo nitakuja kuwa mtu maarufu. Hivyo watakuja huko mbele makundi kwa makundi. Tena watanililia na kuniambia wananipenda. Wengine watatamani hata sahihi yangu. Wengine watakua radhi kuachana na wapenzi wao na kuwa na mimi. Hivyo kila alieondoka niliamini ipo siku atarudi analia. Hivyo jina la kipenzi cha warembo nilibatizwa na kulipokea kwakua lilikua halinidhalilishi, bali lilikua linasadifu na ukweli halisi. Maana ni kweli nilikua napendwa na warembo na mimi nilikua napenda kuwa karibu nao hata kama si kimapenzi.

   Yote hayo yalizima kama mshumaa kwa mtoto Haiba. Hakuna u’Kanumba wala u’Shah Rukh Khan tena. Nilikua paka mjanja niliyekua namuogopa panya. Ni ngumu kutokea lakini kwangu ilinitokea bila hiyari yangu.

   Wote kwa pamoja tulikua tunaangaliana kwa kutegeana, ila tukikutanisha macho hatudumu hata sekunde tano tayari tushakwepesha macho yetu na kuangalia pengine.
   “Kwani wewe unawaza nini juu yangu?” duh! Hilo swali lilikua limekaa kichokozi haswa. Nikamuangalia na kumuona ameinamisha kichwa chake chini.
   “Mimi natamani tu uwe rafiki yangu.” ujasiri wa kukopa kwa ajili ya kulishinda pepo la uoga ulinijia na kuongea hayo.
   “usijali, tumeshakua marafiki tayari.” majibu ya Haiba yalinisuuza moyo wangu.
   “ila hujanijibu itakua tayari lini?” haiba akaamua kirejesha mada halisi iliyokua mezani.
   “nadhani kesho. Maana leo hii ungekuja asububuhi nimgeenda kariakoo kununua hicho kioo.” nilimjibu na kumfanya aridhike.
   “kesho nitakuja jioni. Si unajua sie bado tunasongoka. Hatuna muda wa kupumzika kabisa.” alijibu hivyo na kunyanyuka.
   “kuna ubaya kama nitaamua kukusindikiza?” nilijikuta nimemuuliza hivyo baada ya kunipa mgongo. Aligeuka na kunitazama.
   “na ofisi unamuachia nani?” aliuliza hilo swali na kunikazia macho kidogo kumaanisha alikua anasubiri majibu.
   “nafunga, nataka nielekee nyumbani kuipeleka Computer yako. Kesho nikiamka tu, safari ya kwanza kariakoo.” majibu yangu yalimfanya atabasamu.
   “sawa, unaweza kunisindikiza.”
Majibu yake yalinifanya nizichukue hizo pesa alizonipa na kuziweka kwenye mfuko wangu. Kisha nikachukua begi lake la laptop na kufunga geti la ofisi yangu.
Tulitembea kwa mwendo mdogomdogo huku tukiongea na kucheka. Watu wa hapo mtaani walibaki kutoa macho tu. Nilijua kabisa kama naangaliwa, basi ndio nikazidisha sifa na kumchekesha mtoto mzuri ili acheke mpaka kila mtu aone natembea na mtoto wa daraja gani.
   “Nakuona kipenzi cha warembo!”
Kuna msichana mmoja akaropoka. Nilijisikia vibaya kweli. Maana ni kweli nilikua nalipenda hilo jina, ila hapo hapakua mahala sahihi pakuniita.
   “wanakuita kipenzi cha warembo?” Haiba hakuruhusu hilo lipite akiwa kimya.
   “ndio jina langu la utani. Maana warembo wanapenda sana kuangalia filamu. Na mimi nafanya biashara ya vitu wanavyovipenda.” akili ya uokozi ilinipa jibu kali lililommaliza Haiba na kufanya atabasamu.
ITAENDELEA......

COMMENTS

BLOGGER
Jina

Affiliate Marketing,3,AFTER DEATH (BAADA YA KIFO),4,Afya Yako,179,AJIRA/JOBS,8,ANGA LA WASHENZI,1,ASIA DIGITAL,2,Baba Kiumbe Wa Ajabu,20,BAKING,1,BARUA ILIYOWAHI KUNIUMIZA,7,betting,1,Biashara,16,biashara mtandaoni,5,BIKIRA YANGU,1,BIKRA YANGU HAKI YA BABU,25,BISCUITS,2,BLACK AMERICA,33,blogging,1,BONGO MOVIES,12,Bora ungekufa kesho,1,CHOICE OF MY HEART (chaguo la moyo wangu),16,CHOICE OF MY HEART (chaguo la moyo wangu),1,CHOMBEZO,56,CHOZI LISILOFUTIKA,1,Chunusi,1,CHUPI MKONONI,4,CITY LIGHT,5,Classified,11,DARASA LA MAHUSIANO/MAPENZI,69,Darasa la mapenzi na ndoa,213,DEREVA TAXI,18,DUDU WASHA,4,Elimu na ushauri wa maisha,131,FIFA.com - Latest News,18,Hadithi,73,HALIMA,2,HOUSE GIRL WA DADA,8,I WILL BE BACK,15,I'M NOT A BOY,1,Jam,1,JAMANI BABA,8,JAMBAZI MTAMU,3,JAMII MEDICAL AWARENESS(JMA),1,JASTINA,7,JIBU,2,JIKONI,1,JINSI PAKA ALIVYOMALIZA FAMILIA YETU,5,Jobs,19,Joke,5,Kampuni,2,Kanyago,8,KEKI YA CHAI,1,kibamia,9,KIFO MKONONI (BIKIRA YA BIBI HARUSI),20,Kijijini kwa bibi,19,Kilimo,2,kofia za steaming,2,loans,1,LOVE BITE,10,Love Story,12,Mada,3,Mada ya Leo,7,Mahusiano,126,Makala,13,make money online,3,Mapenzi,2,Mapenzi na ndoa,3,MAPENZI YA KICHAWI,6,mapenzi/Ndoa,115,Mapishi,243,Mfalme Gilbert,4,Micro loans,1,MOYO ULIOJAA MAUMIVU,46,MPENZI CHEUPE | WHITE LOVER.,8,Mpiga Picha,3,MTOTO WA MAAJABU,44,MUME WANGU SHUJAA WANGU,3,MUUZA MAZIWA,10,MWAJUMA UTAMU,11,MWALIMU MKUU,10,MWANACHUO,5,Mwanafunzi Mchawi ( A Wizard Student ),9,NAITAFUTA FURAHA YANGU,3,NAMTAKA MPENZ WANGU ARUDI,8,Natura shampoo,2,Natural hair,6,Ndoa,1,News,41,Ngozi,1,Ngumu Kumeza,11,Nguvu za kiume,2,NILIKUWA NA MPENZI,4,NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA,2,NILIYOYAONA DARFUR YANATISHA,1,NIPE KIDOGO,2,NISAMEE RATIFA,25,Noti Bandia,6,Nyama,1,Nyumba ya maajabu,1,Nywele,3,ONLY YOU,10,PENZI KABLA YA KIFO,5,PENZI LA MME WA MAMA,3,PENZI LANGU LINAVUJA DAMU,10,PENZI TAMU,6,PENZI ZITO,7,Riwaya,107,Roast,1,ROSTI YA MBUZI,1,SAFARI YA KUZIMU,19,SALA YA SARAH,1,SANGARE,25,Shahiri,1,SIFA ZINAUWA,3,Simulizi,209,SIMULIZI - ULIKUWA WAPI,8,SITO ISAHAU,8,Soup,1,SPHAGETTI BOLOGNESE,1,Sports News,4,SUBIRA HUVUTA HERI,21,Sumu Mwilini,1,Tangazo,4,U KILL ME,3,Ujasiriamali,13,UKURASA WA 56,10,ULIKUWA WAPI,2,ULIMWENGU WA MBWA MWITU,1,UNBREAKABLE LOVE,1,USO WA FEDHA | FACE OF MONEY,35,UTAM WA KITUMBUA,2,UTAMU WA JIRAN,1,UTAMU WA MAMDOGO,3,Videos,46,VISA NA MIKASA,10,WAPANGAJI WENZANGU,1,Young paster,40,YouTube,74,
ltr
item
BongoLife : PENZI LANGU LINAVUJA DAMU SEHEMU YA 02
PENZI LANGU LINAVUJA DAMU SEHEMU YA 02
BongoLife
https://www.bongolives.com/2019/10/penzi-langu-linavuja-damu-sehemu-ya-02.html
https://www.bongolives.com/
https://www.bongolives.com/
https://www.bongolives.com/2019/10/penzi-langu-linavuja-damu-sehemu-ya-02.html
true
170677852813010960
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS PREMIUM CONTENT IS LOCKED STEP 1: Share to a social network STEP 2: Click the link on your social network Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy Table of Content