Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 43

MTOTO WA MAAJABU: 43

Kila mmoja alibaki kushangaa pale, mara muda kidogo kuna mtu alifungua mlango na kuingia ndani na kufanya wote waogope ila Juma alishtuka sana kwani yule aliyeingia alikuwa ndiye binti ambaye mara nyingi alikutana nae njiani na alimpa dawa mbalimbali.
Juma alishindwa kuongea jambo lolote kwa muda ule ila walijikuta tu wote wakikaa chini huku wakimuangalia huyu aliyeingia ambapo alisema,
“Mimi ndiye Moza mwenyewe, msifanye kazi ya kubishana hapa, ila hata mimi naweza sema sio yule halisi bali naishi kwenye mwili wake na lengo kuu ni kulipa kisasi. Mnajua kwanini naishi kwenye mwili wa Moza? Nendeni mkafatilie chanzo cha kifo cha Moza hadi Moza kurudi na kuwa mzima tena na hapo mtajua imekuwaje niishi ndani ya Moza. Nilichukizwa sana na mambo aliyokuwa akiyafanya Rose, ila Moza alikuwa na nguvu ambayo ilinishawishi kuwa nae karibu ndiomana ilikuwa ni ngumu kushuhudia Moza akizikwa. Mimi ndiye ninayeishi kama Moza, na mimi ndiye niliyeishi kwenye mwili wa Salome, kwa lengo la Salome kumjua baba yake mzazi na kupata haki yake. Tuachane na hayo, naamini kwasasa swala la kumuwazia vingine Salome litakuwa limewaondoka kabisa, sasa ni hivi, mimi nimeanza kukufatilia Juma tangu ulipomuoa Mishi sababu Mishi nilimpa laana ya matendo yake aliyokuwa akiyafanya ya kuchanganya wanaume, nilikwambia wewe usije kumuacha Mishi kwani akili ya Mishi niliitambua vilivyo, nilitaka wewe ucheze nafasi yako kama mwanaume kwenye maisha ya Mishi ili Mishi abadilike ila badala yake ukasimama kama mume bwege na kuniudhi sana. Nikaanza pale kukufatilia wewe sasa, ila yule Mishi alikuwa na kiburi cha kufanya mambo sababu wewe ulikuwa huwezi kumfatilia, wewe ulikuwa husimami kwenye nafasi yako kama mwanaume, hadi Mishi kaenda kwa mganga na kupewa dawa ya kulala na mwanaume kwenye kitanda chako!! Bila mimi kukushtua kwa hakika usingemfumania Mishi kwa hilo, ulimpa uhuru sana, tena uhuru uliopitiliza na kunifanya nichukie sana kwa hilo Juma. Nilikaa karibu na wewe ila ulipomuoa huyu Mariam niliona ni sawa maana wote nyie wawili nilitaka kuwa karibu na nyie. Ila Mariam, dada yako ni mimi ambaye nilimmaliza…..”
Hapo Mariam akashtuka sana ila huyu Moza akasema,
“Usishtuke ila sikia ilivyokuwa, ni hivi dada yako alienda kwa yule babu na kumwambia kuwa ampe dawa Mishi ya kulala na yule mwanaume aliyelala nae, amwambie kuwa tatizo lingeisha, na kweli mimba ilitoka kwa tatizo lile ila lengo la dada yako lilikuwa ni Mishi aweze kuathirika sababu yule kaka alikuwa ni muathirika. Nikachukia sana, maana alichokifanya dada yako ni roho mbaya, nikammalizia huko na ujinga ujinga wake. Sasa nakuja kwa upande wako wewe Mariam, kitendo cha wewe kumpeleka rafiki yako kwenda kutoa mimba ni kitendo ambacho kilinikera sana na hivyo kufanya nipatwe na jazba na hasira nyingi mno na kufanya nizidi kukufatilia na ile mimba ya Mishi aliyoipata kwa vichaa ndio niliyokuwekea wewe na mtoto ni huyo unayemuona. Kwahiyo toka kipindi kile ulikuwa una mimba ila hukujijua hadi ulipoolewa ndio ikajidhihirisha na kukufanya uhangaike sana, kingene kilichofanya niwe karibu zaidi na wewe ni uvivu wako. Sikutegemea kama wewe ni mvivu kwa kiasi hiko ulichokuwa nacho, sikupenda huo uvivu wako. Haya niulizeni maswali muda huu nawajibu”
Wote waliangaliana na kushindwa hata kupumua vizuri, basi Juma alijivika ujasiri na kumuuliza,
“Kwahiyo wewe Moza ni nani?”
Moza alicheka na kuwaambia,
“Mimi ni msichana wa kazi, niliyetoka kwenye familia duni ambapo katika maisha yangu sikuwahi kuolewa wala kuzaa. Nadhani nimekujibu swali lako”
Juma akauliza tena,
“Samahani, wewe ni binadamu wa kawaida?”
Huyu Moza akacheka tena na kujibu,
“Kwahiyo unadhani mimi ni shetani au ni kitu gani? Mbona nilikuwa nakutana na wewe mara nyingi tu na kukushauri mambo mbalimbali! Swali lingine?”
Juma aliguna tu, muda huu ni Mariam ndio aliuliza swali,
“Samahani, kwani yule mganga alikufa na nini na je ni kwanini Mishi ni chizi?”
Huyu Moza akaangalia juu na kushusha macho chini kisha akasema,
“Yule mganga niliwahi kumwambia kuwa hiyo kazi sitaki uifanye maana huyu mtoto ambaye atakayezaliwa atabeba jina langu, yule mganga hakusikia na kufanya hiyo dawa yake na hapo nikachukia na kummaliza, sasa ilitakiwa huyo Mishi asiende msibani maana pale adhabu yake aliyojipa ni kubwa sana, ila kitendo cha yeye kwenda msibani ndio kitendo kilichomfanya awe chizi hadi leo”
Mariam na Juma waliangaliana na kujikuta wakiuliza,
“Je kuna namna ya kumsaidia?”
Moza akawaangalia na kuwaambia,
“Namna ya kumsaidia ipo ila inatakiwa mfanye nyie wenyewe maana nyie ndio tiba ya yule mtu”
Juma akauliza,
“Tiba ipi hiyo?”
Yule Moza akajibu,
“Mnatakiwa mkamuonyeshe Moza mtoto kwa Mishi na hapo mtamfanya Mishi awe mzima”
Mariam na Juma waliangaliana na kuuliza tena,
“Kivipi?”
“Kivipi nini na wakati huyo mtoto mliyebeba ndio Moza”
Mariam na Juma wakaangaliana tena na kuuliza,
“Kwahiyo huyu mtoto ni wa ajabu?”
Moza alicheka na kujibu,
“Hapana, huyo ni mtoto wa kawaida kama watoto wengine ila nataka aitwe Moza kama ukumbusho wa huyu ambaye ni jasiri wangu Moza”
Mariam akauliza tena,
“Lakini Moza si wewe?”
“Sawa, mimi ni Moza. Kwani kuna tatizo gani la mtoto kurithi jina langu? Ngoja niwaambie hiki, msipompa huyo mtoto jina langu basi sitoacha kuwafatilia, nitawafatilia hadi pumzi zenu za mwisho”
Juma na Mariam wakapumua kwakweli, kisha wakaangaliana na hapo Mariam akajivika ujasiri na kumuuliza Moza,
“Samahani, na huyu mtoto tunayeishi nae ndani ni nani?”
Moza akacheka tena na kuwaambia,
“Huyu mtoto sitawatajia jina lake ila akiondoka mtamkumbuka siku zote za maisha yenu, kwanza huyo mtoto ana nguvu kuliko mimi. Kumbuka Juma siku huyu mtoto alipomzaba kibao Pendo halafu mimi nilikupa mkono wangu wa kwenda kumponya Pendo, kumbuka sikuonekana kwa muda kwenye ile njia unayonikutaga sababu nguvu zilipungua. Huyu mtoto ana nguvu sana, ndiomana Anna alipogundua kuwa hapa kuna mtoto wa namna hii akataka kuja kuishi nae kwani anajua ni kitu gani atapata toka kwa huyu mtoto ila hajapatana nae sababu huyu mtoto hapendi uchawi”
Wote wakabaki wanaangaliana pale ambapo Moza aliwauliza tena,
“Swali lingine la ziada mlilokuwa nalo! Ulizeni”
Yani walijikuta hawana swali lolote kwa muda huo, kisha Moza aliwaaga na kuondoka zake yani alitoka tu mlangoni kawaida na kuondoka.
Ndani walibaki wakishangaa sana huku wakiangaliana bila ya kuwa na swali wala jibu.

Baada ya muda kupita ndipo Salome alipoongea maana alikuwa na maswali yake lakini wakati Moza ametokea alijikuta akishindwa kuuliza,
“Jamani mimi nilitaka kumuuliza kuwa aliingiaje kwenye mwili wangu hadi kuna baadhi ya watu wakajua mimi ni Moza?”
Mama Rose na yeye akaongea,
“Mimi swali langu lilikuwa ni kwanini aliamua kumuua mama yangu na kuchoma nyumba yetu ilihali angeweza tu kumpa mama adhabu?”
Mariam akawaambia,
“Sasa jamani mbona hamkumuuliza wakati yupo hapa?”
Juma na yeye akasema swali jingine alilokuwa nalo,
“Mimi nilitaka kumuuliza kuwa amewezaje kufanya hayo anayoyafanya?”
Mtoto aliwaangalia na kuwauliza,
“Kwahiyo mnamuhitaji tena Moza aje kujibu maswali yenu hayo?”
Wakabaki kimya huku Mariam akitikisa kichwa maana alihisi hata yeye ana maswali mengine ya kumuuliza Moza, yule mtoto alitlia kwa muda na kusema,
“Moza, bado unahitajika kwenye nyumba hii”
Na kweli baada ya muda Moza alifungua mlango na kuingia ndani, kisha alicheka jinsi ambavyo waliogopa sana halafu alianza kuongea,
“Nitajibu hayo maswali yenu mliyouliza sasa, Juma umeuliza kuwa natoa wapi nguvu nilizokuwa nazo. Mimi sio wa kawaida kama unavyofikiria, kwa kawaida mimi ni Moza ila mimi nilikuja kwa Moza baada ya kuona Moza ana malengo kama yangu. Moza hakupenda wachawi, hakupenda watu wenye roho mbaya, Moza hakupenda kuishi maisha mabaya ingawa ilimlazimu sababu ya wazazi wote wote kufa. Wazazi wa Moza hawakufa kawaida maana waliuwawa kichawi ila kwa macho ya kawaida utaona kuwa ni kifo cha kawaida. Ingawa ilikuwa ni kiuchawi ila Moza alishuhudia kifo cha wazazi wake kwa macho yake mwenyewe, na ameishi maisha ya shida sana, na ni Moza ndiye aliyenisaidia mimi nitoke nilipofichwa na yule mjinga Rose maana alinificha chini ya ua, nimewaambia fatilieni kifo cha Moza mtaelewa ni kitu gani kilitokea. Halafu kuhusu kuingia kwenye mwili wa Salome ni kutokana na upendo wa Moza na Salome, walikuwa si ndugu ila walipendana sana na huo ndio ukweli hata mkimuuliza hapo Salome kwa muda wenu atawaeleza jinsi gani anampenda Moza, na katika watu wasioamini katika kifo cha Moza basi Salome ni namba moja. Halafu kuhusu kumuua Rose na sio kumpa adhabu ni sababu hakutaka kuacha uchawi kwa njia ya amani, yani uchawi ulishamuingia kwenye damu yake akaona kuuacha ni kazi na kuamua kushindana na Moza tu. Na sababu iliyofanya nimuue Rose kwa kumchoma ndani ya nyumba yake sababu kile ndio kilikuwa kifo pekee cha Rose cha bila kufa na mtu mwingine ila ningemchagulia kifo kingine basi Rose angekufa na watu wengi sana. Nadhani nimemaliza maswali yenu, mwenye swali lolote tena kabla sijaondoka maana muda huu nikiondoka sitaweza kurudi tena”
Walikuwa wakiangaliana tu bila ya kuuliza swali lolote, basi Moza aliwaambia,
“Kama hamna swali naondoka ila sitaweza kurudi tena, nikiondoka sasa nimeondoka kabisa”
Na baada ya pale Moza aliondoka ila Mama Rose na yeye na Salome waliinuka na kuondoka bila ya kusema chochote kile na kufanya ndani wabakie wenyewe wenye nyumba tu.
Usiku ule Juma hakuzungumzia tena habari za yule mtoto wala Moza hata Mariam na yeye ilikuwa hivyo hivyo, walijikuta tu zile habari wameachana nazo kabisa. Basi wakalala na kuendelea kuishi kwa namna hiyo huku wakimuangalia tu mtoto wao kwa yale mambo aliyokuwa akiyafanya na kuendelea na mambo mengine tu.

Leo, Juma aliamua kwenda kumtembelea Pendo na familia yake, alifurahi sana kumkuta Pendo akiishi na mume wake pamoja na watoto wao, basi aliwasalimia pale na kuongea nao jinsi mambo yanavyoenda ila Pendo alimsimulia kitu kingine kilichofanyika kwenye familia yake,
“Juma nilipata mdada mwingine wa kazi kumbe alikuwa ni mchawi ila nimempeleka kwenye maombi naamini atabadilika tu kama akiamua kumtumikia Mungu”
Basi Juma alimtazama Pendo na kumwambia,
“Kuna mdada wa kazi nilikuwa nae ila ni mchawi mbaya, ila kaniambia kuwa anhitaji sana kuacha uchawi. Utamsaidiaje kama huyo?”
“Nipeleke alipo ili nimchukue na kumpeleka kwenye maombi”
Juma hakuona tatizo kwani muda huo huo aliondoka na Pendo hadi kwenda kwenye nyumba ile ambayo walimuacha Anna, ambaye alipowaona aliwasogelea na kuwasalimia kisha Juma akamwambia Anna,
“Ukombozi wako umekuja, huyu dada anataka kukukomboa ila ukombozi huo una masharti”
“Kheee masharti gani?”
“Nenda nae halafu utajua, si unataka kuacha uchawi wewe na umeamua kabisa?”
“Ndio nimeamua”
“Basi jiandae uongozane na huyu dada uende nae huko anapotaka kukupeleka”
Anna alienda kujiandaa, na hapo walianza safari ambapo Juma aliwaacha waondoke halafu yeye alirudi nyumbani kwake.
Ila njiani Juma alimpigia simu mama Rose ili kumpa ujumbe wa Anna, ambapo mama Roze alishangaa kidogo na kuuliza,
“Anna huyo kakubali kuacha uchawi?”
“Kakubali ndio”
“Huyo Pendo si anampeleka Anna kwenye maombi?”
“Ndio, Pendo kasema hivyo”
“Sasa kule huwa wanaambiwa waache uchawi au waombewe wafe, Anna atakubali?”
“Amekubali sio atakubali”
“Halafu hao wachungaji wajipange kama watakuwa hawajasimama vizuri lazima Anna awaangushe kiimani na kiroho nakwambia, maana Anna ni mdogo wangu namjua vizuri. Imeshindikana kila sehemu Anna kuacha uchawi labda akomeshwe na huyo huyo Moza, namjua Anna vizuri sana”
“Haya, tusiongee mengi tutasikia tu yatakayojili huko”
Basi Juma aliagana na mama Rose na kukata ile simu na kuendelea kurudi nyumbani kwake.

Juma alipofika kwake alimkuta mkewe na mtoto wake wakiwa wanakula kwa muda huo, basi akasema,
“Jamani hata kunisubiria?”
Mariam akajibu,
“Aaaah mimi njaa ilianza kuniuma ndio nikamwambia mtoto tule tu”
“Yani mke wangu hujaacha uchoyo tu?”
Kisha Juma akamuangalia mtoto ila kabla hajaongea kitu mtoto akacheka na kumwambia Juma,
“Baba, umejisumbua tu kumpeleka huyo Anna huko kwenye maombi”
Juma akamuangalia yule mtoto na kumuuliza,
“Kivipi?”
“Hivi nyie mnaamini kabisa Anna ataacha uchawi kirahisi hivyo? Anna alipewa uchawi na mama yake toka amezaliwa tayari alikuwa na uchawi, sio rahisi kwa Anna kukubali kuacha uchawi”
Mariam na yeye alimuangalia mume wake na kumuuliza,
“Kwahiyo Anna umempeleka kwenye maombi?”
“Ndio, Pendo kasema hiyo ndio njia ya kumsaidia”
Mariam akamuangalia mtoto na kumuuliza,
“Sasa ni kitu gani kinachoweza kumsaidia Anna aache uchawi aliopewa toka tumboni kwa mama yake? Anna anaongea kwa hisia kali sana kuwa kachoka uchawi hadi anatia huruma, ni kitu gani kitamfanya aache?”
“Hata huko kumuombea kutamfanya aache ila Anna hawezi kuishi bila kuwa mchawi, na mkitaka kugundua kuwa Anna hawezi kuacha uchawi, subiri ukijifungua mtoto akiwa mchanga kabisa muite Anna amuone halafu utaona atakachokifanya sema tu atashindwa sababu huyu mtoto ataitwa Moza, ila utaona tu atakachotaka kufanya”
Juma na Mariam wakaangaliana kisha Juma alikaa na kuanza kula kile chakula kilichokuwa kimetengwa.
Usiku wa leo, mama yake Juma alimpigia simu Juma na kuongea nae,
“Mwanangu, kwasasa hatuna kinyongo chochote kwako na mke wako, tunawatakia heri tu muishi vizuri na mzidi kupendana maana mapenzi ni ya wawili”
“Asante sana mama yangu, kwahiyo hata bamdogo na mjomba hawana tena kinyongo na mimi?”
“Ndio, wote hawana kinyongo na wewe mwanangu, kwahiyo usiwe na shaka wala tatizo lolote. Tunawapenda sana, naomba mtusamehe popote pale tulipowakosea na sisi tumewasamehe kwa yote mwanangu. Amani tu itawale”
Hili jambo lilimfurahisha sana Juma alijikuta akitabasamu tu, hata alipomueleza Mariam na yeye alifurahi sana kuhusu jambo hili.

Miezi ilikuwa imepita na mimba ya Mariam ilikuwa imekua sasa, mimba ilikuwa inatimiza miezi tisa, basi leo alikuwa amekaa na huyu mtoto wake na kumuuliza,
“Samahani mwanangu, je huyu mdogo wako wa kuitwa Moza na yeye atakaa miezi ishirini na tatu tumboni kwangu?”
Mtoto akacheka na kumwambia,
“Hivi mama ulivyoambiwa kuwa huyo ni mtoto wa kawaida hukuelewa?”
Mariam alimuangalia na kumuuliza tena,
“Kwahiyo leo umekubali kuwa wewe ni mtoto wa ajabu?”
Basi mtoto akamjibu kwa kumuuliza,
“Kwani wewe unanionaje?”
Hapo Mariam hakuwa na jibu ila alikuwa akijikanyaga kanyaga tu, basi yule mtoto akamwambia mama yake,
“Laiti ungemsikiliza kwa makini yule mliyekuwa mnamuuliza maswali basi ungeelewa, yani hadi sasa hujui ni kwanini mimi nipo kwenye maisha yako? Wewe ulisaidia kunitoa toka tumboni kwa mama yangu Mishi, mimi ni mtoto niliyetakiwa kuzaliwa na Mishi ila wewe na kiherehere chako ndio ukanitoa, ila hadi sasa nipo kwaajili ya uvivu wako ingawa umejitahidi kwasasa, nitaondoka pindi mama yangu akipona, licha ya makosa yake yote lakini bado nampenda sana”
“Sikuelewi”
Yani Mariam alikuwa akijibu huku akitetemeka kwani kama kuelewa ni tayari ameshaelewa ila tu alijifanya kuwa hajaelewa, na hapo hapo alianza kujihisi uchungu mkali sana na kuamua kuchukua simu na kumpigia mama yake pamoja na mume wake ili apelekwe hospitali.

Juma alifika mapema kabisa pamoja na mama yake Mariam na moja kwa moja walimpeleka Mariam hospitali ambapo baada ya muda kidogo tu alijifungua mtoto mzuri kabisa wa kike, yani Mariam alitabasamu na kufurahi sana wakati anakabidhiwa mtoto wake mkononi, ila muda ule ule mtoto akatoa haja kubwa na ndogo na kumfanya Mariam aanze kulia hadi nesi akasogea kumuuliza,
“Tatizo ni nini dada?”
“Mtoto kajisaidia nesi, haja ndogo na kubwa”
“Oooh vizuri sana, sasa unalia nini?”
“Mtoto wangu ni mtoto wa maajabu, naogopa sana jamani! Yani nimezaa kwa miezi iliyotimia kabisa na nimezaa mtoto wa ajabu?”
“Mtoto wa ajabu sababu ya kukojoa na kunya au kuna lingine?”
“Hamna lingine ila ni sababu hiyo hiyo”
Nesi akacheka na kumwambia Mariam,
“Yani ukiona mtoto wako kajisaidia baada ya kuzaliwa hii ni njia nzuri ya kujua usalama wa mtoto wako, maana kibofu ni kizima na njia ya haja kubwa haina matatizo. Hujawahi sikia mtoto kazaliwa bila njia ya haja kubwa au ndogo, hujawahi sikia mtoto kazaliwa bila sehemu yoyote ya kujisaidia? Kwahiyo ikitokea kama hivi ni jambo la kumshukuru Mungu Mariam kuwa mtoto umezaa mzima wa afya njema”
Basi Mariam akatabasamu na kusema,
“Mtoto wangu huyu ataitwa Moza”Kale katoto kalitabasamu na kufanya Mariam aogope tena ila nesi alimwambia ni kawaida kwa watoto kutabasamu hata usingizini.
Kidogo Mariam alipata amani kwasasa na kuruhusiwa sasa kutoka hospitali maana mtoto alikuwa salama kabisa.

Walivyorudi tu nyumbani, Juma alikumbuka swala la kwenda kumchukua Anna na kwenda nae pale nyumbani, kwahiyo Juma alifika na Anna wakati Mariam yupo kunywa uji sasa huku kichanga chake kimeshikwa na mama Mariam.
Yani Anna alipofika pale akatamani kumshika yeye mtoto hadi anaomba kwa magoti, yani mama Mariam alimshangaa sana,
“Huyu mtoto bado mdogo yani unaomba kumshika hadi kwa magoti?”
Yule mtoto mwingine akasema,
“Anna, unataka kumshika mtoto. Ipo hivi kama ukimshika huyu mtoto kwa upendo basi utakuwa salama ila ukimshika huyu mtoto kwa uchu basi utazikwa wewe kabla yake, ni mtoto wa kawaida huyu ila analindwa huyu mtoto”
Anna akajibu kwa kujiamini,
“kwanza nimeacha uvchawi, nataka kumshika kwa upendo tu”
Kisha yule mtoto akamwambia mama Mariam,
“Bibi, mpe Anna huyo mtoto amshike”
Basi mama Mariam alimpa mtoto Anna ila Anna hadi alionekana wazi kabisa akimtamani yule mtoto mara hapo hapo Anna alianguka chini na kuwafanya wamdake yule mtoto yani hakuna aliyeelewa pale ila yule mtoto aliwaambia kuwa Anna amekufa na hata Juma alipochukua usafiri na kumpeleka Anna hospitali lilikuja jibu lile lile baada ya vipimo kuwa Anna amekufa.

Juma hata hakujua ni namna gani atumie kuandaa msiba wa Anna, basi aliwaita tu ndugu zake waliokuwepo ili wajadili alimuita pia Pendo ili kujua kilichokuwepo.
Walipofika, Juma alienda kuzungumza na Pendo kwanza,
“Hivi kwani ilikuwaje na Anna huko?”
“Ni hivi, Anna nilimpeleka hadi kwa mchungaji ilia ache uchawi na kwangu alisema ataacha, ila tulivyofika kwa mchungaji aliulizwa na kusema kuwa hawezi kuacha uchawi, tena Mchungaji hadi akamfunulia maandika kuwa mwanamke mchawi hastahili kuishi ila hilo wala halikumpa tatizo Anna na alikataa katakata japo alifundishwa vitu vingi sana. Mchungaji akaniambia kuwa swala la kuacha kitu ni lazima mtu awe na utayari, hivyo nikaamua kumrudisha Anna kule nilikomtoa ila alinipa onyo kuwa ole wangu niseme kama hajaacha uchawi”
“Khaaaa kumbe Anna alikuwa anatuigizia kwa kipindi chote hiki?”
“Ndio hivyo yani”
Basi Juma aliongea pia na mama Rose ambaye alisema kuwa mdogo wake Anna akazikwe kwenye kiwanja chao ambapo nyumba yao ndio ilichomwa na mama yao ndani,
“Hata kaka zangu nao walizikwa hapo, kwahiyo Anna na yeye akazikwe hapo hapo nitakuwa nikiangalia makaburi yao maana sijali kitu bado ni ndugu zangu tu”
Basi wakashirikiana wote kwa mazishi ya Anna halafu marehemu Anna alienda kuzikwa ila wakati wamemaliza swala la mazishi ndipo alipopita Mishi akiwa na ule uchizi wake kama aliokuwa nao, ni hapo mama Rose aliposema,
“Jamani ni Mishi yule, masikini ni chizi kabisa kwasasa”
Basi Juma alimuhurumia na akakumbuka lile swala ambalo yule Moza aliwaambia, na hapo aliamua kumkamata Mishi na kumfunga mikono na miguu kisha kukodi gari na kurudi nae nyumbani kwake.

Mariam alishangaa sana kuona Juma karudi na Mishi pale kwao, akamuuliza mume wake,
“Sasa umemleta Mishi wa nini?”
“Umesahau tuliambiwa kuwa sisi ndio tunauwezo wa kumsaidia Mishi! Anatakiwa kumuona mtoto”
“Mmmh sasa nitamtoa mtoto nje wakati hata hajatimiza siku saba?”
“Naelewa mke wangu ila mtoe tu ili Mishi apate kumuona”
“Kwani bado unampenda Mishi?”
“Mmmmh Mariam, shida yangu ni kumsaidia Mishi”
Basi Mariam alienda kumchukua mtoto ila kabla hajatoka nae nje, yule mtoto wao mwingine akamfata Mariam na kumwambia,
“Mama, kwasasa umejirekebisha, nimependa moyo wako wa sasa. Umekuwa na moyo wa huruma na umekuwa muelewa, pia kwasasa mama yangu umekuwa ni mchapakazi ule uvivu umeuacha kabisa. Mimi ndio mtoto wa Mishi na mimi ndiye mwenye uwezo pekee wa kufanya Mishi aondokane na uchizi aliokuwa nao. Ila nakupenda sana Mariam maana ni mbishi ila ukitishiwa unaogopa, halafu nakupenda sababu unapenda kusema ukweli. Mimi naondoka mama, nakupenda sana”
Haka katoto kalimkumbatia Mariam kisha kalitoka na moja kwa moja kwenda kwa Mishi alipokalishwa na kumkumbatia halafu akaondoka hata alipoelekea zaidi hawakumuona maana alipotea tu, pale kila mmoja alishangaa na akili za Mishi zilirudi muda huo huo
Hawakuelewa kabisa ila walimchukua Mishi na kuingia nae ndani ambapo Mariam alimuwekea maji na kwenda kumsafisha maana Mishi alikuwa mchafu sana na kumpa chakula aweze kula na baada ya hapo Mishi alikuwa akishangaa tu, aliwakumbuka wale watu na alipomuona Mariam kabeba mtoto aliumia zaidi na kusema,
“Mimi na ujinga wangu nilimtoa mwanangu”
Mishi alionekana kutia huruma sana, kisha Juma akafanya jitihada na kumrudisha Mishi kwa ndugu zake ambao walifurahi sana kumuona na kumshukuru sana Juma.

Siku ya leo Mariam alikuwa amekaa huku akilia, hadi Juma alimshangaa na kumfata mke wake kumuuliza kitu kinachomliza,
“Vipi Mariam mke wangu nini tatizo?”
“Nimemkumbuka mtoto”
“Khaaa umemkumbuka mtoto si huyo hapo unae tayari!”
“Ndio ninaye ila nimemkumbuka yule mtoto wangu wa maajabu”
“Khaaaa Mariam una wazimu au ni kitu gani mke wangu?”
“Hapana sina wazimu, ona kama muda huu nimechoka ila natamani chakula kizuri jamani!! Mtoto angekuwepo si angenipikia jamani!”
Juma alicheka tu na kutikisa kichwa.

MWISHO
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
Story itakayofuata ni THAMANI YA PENZI, nitawaambia siku nitakayoianza ila tuendelee na utaratibu wetu ule wa michango.
Kunichangia Tigopesa 0714443444 mpesa 0765692210 code 255
Jina Atuganile Mwakalile.
Wapo wengine ambao huwa wanatuma hata bila ya mimikukumbusha, nawashukuru sana.
Toa maoni yako kwa story hii ya MTOTO WA MAAJABU.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni