Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 37

MTOTO WA MAAJABU: 37

Muda huo mtoto nae akasogea kwenye maongezi yao na kumuuliza Juma,
“Baba una uhakika gani kama mimi ni mchawi?”
Juma akamuangalia huyu mtoto bila kumjibu kitu na kumfanya mtoto amuulize tena Juma lile swali kisha Juma akamjibu,
“Mimi sijasema kama wewe ni mchawi”
Mtoto akacheka kisha akamuangalia Zayana na kumwambia,
“Mmdogo, achana na huyo mwanaume utajutia maisha yako yote. Achana nae huyo nakwambia”
Zayana akamuangalia huyu mtoto ila hakumwambia kitu na kumfanya huyu mtoto aongee tena,
“Mamdogo, sirudii kukwambia ila huyo mwanaume hakufai, utajuta maisha yako yote nakwambia”
Halafu yule mtoto akaingia chumbani kwake, kwahiyo pale Juma alibaki na shemeji yake Zayana, kisha Juma akamwambia Zayana,
“Hapo sina usemi zaidi shemeji, acha niende kazini tu”
Juma akaondoka kwa muda huo na hata hakusema jambo lingine zaidi.
Zayana alikaa chini huku akitafakari, mama yake nae alitoka chumbani muda huu ambapo Zayana alimsimulia mama yake yale ambayo mtoto ameyasema, basi mama yake akasema,
“Inamaana hako katoto bado kana mambo ya ajabu?”
“Ndio mama”
“Mmmmh halafu unajua nakaogopa eeeh! Sijakaona nikajua hakapo”
“Ila kumbuka Mariam alisema tu kuwa kamelala”
“Sikia mwanangu, tujiandae tuondoke maana mimi hako katoto huwa hata sikaelewi”
Basi wakaenda kujiandaa ili waweze kuondoka kwani mama Mariam hakutaka kabisa kuwa karibu na yule mtoto sababu alikuwa akimuogopa.
Basi wakawa wanajiandaa huku wakijadili,
“Kwahiyo mama niolewe au nisiolewe?”
“Mmmmh sijui ila kama wanakataza mwanangu usiolewe maana hata mimi naogopa usijekupatwa na matatizo”
“Na kuhusu hii mimba je!”
“Hakuna tatizo, itabidi tu uzae mwanangu, usiwe na mawazo sana kuhusu hiyo mimba”
Zayana alikubaliana na mama yake na waliendelea kujiandaa kwaajili ya kuondoka.

Mariam muda huu aliandaa kifungua kinywa kwaajili ya ndugu zake, ila baada ya muda ndugu zake walitoka na kudai kuwa wanaondoka,
“Kheeee mama jamani asubuhi yote hii!”
“Ndio mwanangu, mambo ni mengi na majukumu ni mengi pia. Lazima tuondoke leo tena muda huu”
“Jamani mama jamani! Mnywe basi chai”
“Aaaaah Mariam tunatakiwa kuwahi”
“Hapana mama, nimeandaa chai kwaajili yenu”
Basi ikawabidi tu wakae na kunywa chai ambapo mama Mariam akamuuliza Mariam,
“Una mdada wa kazi siku hizi?”
“Mmmmh! Sina mama, yule mdada aliyepita alinifanyia vitu vya ajabu sana, kwahiyo sina mdada wa kazi”
“Kwahiyo hii chai umeandaa mwenyewe Mariam!”
“Ndio mama, kwanini umeuliza hivyo?”
“Kweli mwanangu umekua jamani, tena umekua sana, najua kawaida yako Mariam ni kuamka saa nne yani hapo hadi tungekuita kukuamsha, ila eti ushaandaa chai hii saa mbili duh! Umebadilika mwanangu”
Mariam akacheka tu na kumwambia mama yake,
“Hata nyumba tayari nimesafisha”
“Kheeee, wewe mwenyewe? Na jana umepika mwenyewe?”
“Ndio mama, kila kitu siku hizi nafanya mwenyewe”
“Duh!! Kweli umebadilika mwanangu ila ndio vizuri hivyo kwnai unafanya mama yako nijivunie uwepo wako, nisiwe na mawazo kabisa”
Mariam akatabasamu tu kwani hajawahi kuambiwa hivi na mama yake, ukizingatia kila siku mama yake alikuwa anamwambia bora umeolewa, ukizingatia mama yake alimwambia wazi mume wa Mariam yani Juma kuwa Mariam ni mvivu sana, kwahiyo Mariam alijisikia vizuri kuambiwa hivi na mama yake.
Walipomaliza kunywa chai sasa wakataka kuondoka ila mtoto akatoka ndani na kusema,
“Bibi, unajua kama hatujakaa hata kidogo kuongea! Sasa unataka kwenda wapi? Hunipendi mjukuu wako?”
Mama Mariam alimuangalia huyu mtoto kisha alimuangalia Mariam halafu alimwambia Mariam,
“Hivi ndio huyu mtoto wa miezi mingapi tu iliyopita tulikuja kukuhudumia kwaajili yake?”
“Ndio ni huyu mama”
“Mbona ananyoosha maneno hivyo?”
“Sababu amekua mama”
“Mmmmh!”
Mama Mariam akaguna halafu akajikuta akishindwa kuongeza neno kwa yule mtoto ila Mariam alielewa kuwa hawa wakilazimisha kuondoka ni kitu gani kitatokea, basi akamuuliza mwanae,
“Unataka waondoke lini?”
“Kesho au kesho kutwa, sana sana kesho kutwa. Nataka wakusaidie kidogo mama na kazi za hapa nyumbani”
Wakaangaliana kwa muda, basi Mariam alimshika mkono mama yake na mdogo wake na kwenda nao chumbani kishia akawaambia,
“Jamani nawaomba muondoke hiyo kesho kutwa, huyu mtoto wangu namfahamu vizuri sana. Nawaomba sana tafadhari”
Yani mama Mariam hakupenda kabisa ila ilibidi tu akubaliane na kile ambacho kimesemwa na Mariam.

Juma akiwa ofisini leo alishangaa kufatwa na Pendo ambaye alikuwa akiongea huku anatetemeka hadi Juma akamuuliza,
“Tatizo ni nini Pendo?”
“Naomba unisamehe Juma, tena nisamehe sana”
“Kivipi? Umefanyeje kwani?”
“Nisamehe kwanza halafu nitakwambia”
“Sawa, nimekusamehe”
“Ni hivi nilikuwa nakulazimisha kumchukua yule mdada wa kazi hata nikakununia na kuchukia kabisa ila ukweli wa hali halisi kuhusu yule mdada sikuufahamu, naomba unisamehe”
“Kwani imekuwaje?”
“Na bora hata hamjamchukua, yani sikujua kama yule mdada ni wa ajabu, kuna rafiki yangu alikuwa anahitaji mdada wa kazi ila alimchukua na kusema siku hizi kuna matukio mengi sana ya wadada wa kazi na yeye huwa akichukua mdada wa kazi cha kwanza anampeleka hospitali kumpima ukimwi na magonjwa ya zinaa kwani kuna watoto wameambukizw amagonjwa na wadada wa kazi, halafu kingine anasema huwa lazima mdada wa kazi ampitishe kwenye maombi kwanza kwani mambo mengi na dunia imeharibika. Sasa alimchukua nyumbani kwangu na moja kwa moja akaenda naye kwenye maombi, duh kilichotokea huko hapana aisee hadi naogopa”
“Mmmmh nini tena?”
“Kumbe yule mdada hakuwa binadamu wa kawaida, alikuwa ni chatu”
“Khaaaa weeee Pendo unazungumzia vuti gani?”
“Yani hapa nilipo natetemeka, yule mdada wangu mpya wa kazi alipogundua unajua amekimbia, naogopa mimi naogopa sana kumbuka siku zote hizi nimelala nao na kuishi nao, jamani naogopa sana”
“Pole sana Pendo”
“Asante, nisamehe sana kwa kukununia sababu ya hawa wadada jamani sikujua mimi naogopa hadi muda huu naogopa kabisa”
“Ndiomana kwasasa mimi na familia yangu tumeamua kutokuwa na mdada wa kazi ndani sababu ya mambo kama hayo. Unamkumbuka yule mdada wa kazi aliyepita alikuwa anafanya mambo ya kichawi ndiomana hatutaki labda tumtambue vizuri”
“Ila mbona mwanzoni ulikubali na badae ukabadili maamuzi, ulishtuka kitu gani tena?”
“Aaaah mke wangu alikataa tu jambo hilo”
Yani Pendo bado alikuwa akitetemeka, ilionyesha wazi kuwa ile habari ilimshtua sana ndiomana alikuwa bado anatetemeka.

Leo kweli kabisa mama yake Mariam alisaidia kufanya baadhi ya kazi mule ndani na kumfanya Mariam afurahi kwa hawa ndugu zake kuambiwa kuwa wabaki hapo nyumbani kwake.
Ila mama Mariam akasema,
“Jamani kuna mboga gani leo Mariam?”
“Kuna maharage mama na mchicha upo”
“Aaaah sitaki kwakweli, mimi nataka nyama tena nyama ya kuku”
Mariam akacheka na kusema,
“Sasa mama kwanini hukumwambia mkwe wako asubuhi!”
“Nimwambie nini kwani tulipanga kukaa mpaka leo? Si mtoto wako tu ndio kalazimisha tukae jamani”
“Sasa itakuwaje mama”
Wakati wanaongea Zayana alikuwa akicheka na kufanya wamuulize,
“Sasa unacheka nini Zayana?”
“Yani nimemwambia huyu baba kijacho wakati mnazungumza hapo, nikamwambia nina hamu ya kuku, eti kanitumia hela kasema nikanunue”
Zayana akaendelea kutabasamu, basi mama yake akasema,
“Yani huyo baba kwenye maswala hayo yupo vizuri sana, anajua kuhudumia hadi kumuacha mtu unajiuliza uliza mara mbili, nimuache huyu niende kwa nani?”
Wote wakacheka, kisha mama Mariam akamwambia Zayana,
“Basi mwanangu, nenda kanunue huyo kuku tule jamani mwanangu”
Zayana akatabasamu na kusema,
“Naenda kununua sasa hivi”
Basi akajiandaa na kuondoka kwahiyo Mariam alibaki na mama yake wakiendelea na mambo mengine ila mama yake alifurahi sana kuhusu swala la kwenda kununuliwa kuku, basi Mariam akamtania mama yake,
“Mama siku hizi unapenda kuku eeeh!!”
“Uzee mwanangu, tunataka vitamu tamu midomo icheze”
Mariam akacheka na kuuliza tena,
“Mwanaume wa Zayana ana hela sana eeeh!!”
“Hamna yupo kawaida ila ni mwanaume anayejali sana”
“Ila ndio mchawi”
“Aaaah hayo mambo tumuachie Mungu ndio anayejua, sisi tunaangalia nje tu. Ila ni maamuzi ya Zayana mwenyewe kama kuolewa nae au la”
“Kweli mama”
Wakawa wanaongea huku wakiendelea kufanya mambo mengine.

Zayana alipoenda sokoni kununua kuku kama alivyokuwa akihitaji, basi alifika moja kwa moja na kwenda kwa wale wauzaji na wanyonyoaji maana alitaka aende na nyama tu, basi alinunua na walianza kumnyonyolea ila kuna mbaba alienda kununua kuku pia akamkuta Zayana pale na kumsalimia pale na kuanza kumchombeza,
“Inaonekana unapenda kuku eeeh!!”
“Napenda sana, yani napenda sana nyama ya kuku kwakweli”
“Kwahiyo umechukua kuku wangapi?”
“Mmoja tu”
“Khaaaa mpo wangapi kwenu?”
“Watatu halafu kuna mtoto wa dada jumla tupo wanne”
“Basi sawa”
Yule mbaba aliinuka na kwenda kuongea na yule muuza kuku kisha akarudi pale alipo Zayana na kumsifia hadi wakabadilishana namba ya simu,
“Yani nimetokea kukupenda sana wewe binti, unaongea vizuri hadi raha jamani!”
“Asante sana”
Basi muda Zayana anachukua kuku alishanga akupewa kuku wanne ambapo yule baba akamwambia kuwa kamuagizia kama idadi ya watu nyumbani kwao, basi Zayana alichekelea na kuona raha sana.
Yule baba alimsindikiza Zayana hadi alipofika halafu yeye ndio aliondoka zake, kwahiyo yule baba alijua Zayana ndio anaishi mahali pale.

Zayana alipoenda kuwapelekea walifurahi sana hadi mama Mariam akasema,
“Khaaa haya ndio mambo ya kuzaa binti mzuri jamani yani hadi raha”
Mariam akasema,
“Mmmmh mama jamani kwani mimi sio mzuri?”
“Sina maana kuwa wewe sio mzuri Mariam, ila wewe ni mke wa mtu kwanza ofa za hivi hazikufai ila huyu mdogo wako bado”
Mariam akacheka na kumwambia mama yake,
“Kumbuka mshakula posa ya watu!”
“Aaaah tuachane na hayo Mariam, tupike kuku tule hapa, tule kuku hadi tujisikie jamani. Kwanza tupike kuku wawili”
Walifurahi pale na moja kwa moja walienda kupika wakisaidiana wote watatu ila mtoto alikuwa ametulia tu chumbani kwake.
Basi muda huu walikaa na kuanza kula, ila kuna mgeni alifika na kufanya Mariam ainuke na kwenda kufungua malngo ila alishangaa sana kwani hakumtegemea mgeni huyu, alikuwa ni mama mkw ewake. Akamkaribisha,
“Karibu mama”
“Asante”
Ila huyu mama alionekana kutokuwa na furaha kabisa, alipoingia aliwakuta ndugu wa Mariam wakiwa wanakula basi Mariam akamwambia mama mkwe wake,
“Umekuja muda mzuri mama, karibu mezani?”
“Mmmh hapana, endeleeni tu”
“Jamani mama, basi karibia hata utie baraka tu mama”
“Mmmmh sina baraka ya kutia hapo”
Basi mama Mariam na yeye alimuangalia na kumsalimia kisha kumkaribisha ila alikataa vile vile na kufanya Mariam aende akaendelee kula tu bila tatizo.
Walipomaliza kula, huyu mama mkwe alisema tu mambo mengine hata hakuongelea kilichompeleka pale wala nini kwahiyo Mariam hakujua kitu gani kilimpeleka mama mkwe wake siku ile.

Juma alipotoka kazini tu siku ya leo, moja kwa moja alienda nyumbani kwake kwani hakuwa na sehemu yoyote ya kupitia, alipofika kwake alimkuta mama yake ambapo yule mama aliaga kwa muda ule ule kuwa anaondoka zake ila alihitaji kusindikizwa na Juma tu maana alihitaji kuongea nae, kwahiyo Juma alimsindikiza mama yake stendi, ila mama yake alianza kumsema,
“Hivi Juma mwanangu ni lini utaamka jamani?”
“Kwanini mama?”
“Hebu angalia, mkeo anachokifanya, wakija ndugu zako hapendi na hawahudumii vizuri ila ndugu zake sasa wanakuja na wanahudumiwa vilivyo”
“Kwani vipi mama?”
“Kwanza si ulisema mkeo hapendi wageni wewe, sijui hata ndugu zake hawafiki pale kwako, kwahiyo wale waliofika pale ni wakina nani?”
“Aaaah mama jamani!!”
“Mama jamani kitu gani? Tena wanalala pale pale, mkeo ana roho mbaya tu. Hapendi ndugu zako, anawapenda ndugu zake”
“Jamani mama, wale wamekuja jana tu ujue na sidhani kama watakaa sana”
“Halafu ona ndugu zake anavyowalisha vizuri”
“Mmmmh mama”
“Guna tu, wakati alikuja babako mdogo pale hujajisumbua kumpikia kuku hata mara moja ila wale nimewakuta wanakula makuku jamani, mbona Juma upo hivyo mwanangu!”
“Mmmmh mama unajua unanipa lawama za bure tu, kwenye upishi mimi sipo halafu mke wangu mboga kubwa huwa anapenda samaki na mboga za majani, mara moja moja huwa tunapika nyama tena nyama ya ng’ombe ila mara nyingi pale huwa tunakula maharage na mchicha”
“Huo ni upuuzi, kwahiyo ndugu zako ndio walishwe maharage na mchicha halafu ndugu zake wale makuku! Huo ni ubaguzi, acha huo ujinga Juma, mwanamke gani anakuendesha kiasi hiko jamani! Mwanamke ana roho mbaya yule sijapata kuona”
“Usiseme hivyo jamani mama”
“Nisiseme hivyo kivipi? Ukoo ndio haumtaki hivyo yule mwanamke, hatumtaki, ukoo mzima hawamtaki tunamtaka yule tuliyekutafutia sisi. Hao wanaondoka lini?”
“Sijui mama”
“Kesho asubuhi nakuja, halafu utaona nakuja kufanya nini”
“Jamani mama”
“Hakuna cha jamani, nimechukia sana. Halafu janamke lako lilivyo choyo, hata kunipa mimi kipande kimoja hakuna, nawaangalia tu wanatafuna manyama ya kuku khaaa ule ukoo una roho mbaya sana sijapata kuona”
Yani Juma akajikuta hadi cha kujibu zaidi hana, basi mama yake akapanda daladala na kuondoka ila alikuwa amechukia sana kiasi kwamba aliondoka bila kumuaga vizuri mtoto wake.

Usiku wakati wa kulala, Juma aliamua kumuuliza mkewe kwa ujanja tu maana hata yeye chakula cha usiku ule alipewa zile nyama za kuku,
“Samahani Mariam leo ulienda kununua kuku?”
Mariam alicheka na kusema,
“Khaaaa sikujua kama ungeuliza hilo swali Juma”
“Kwanini nisiulize? Nimeenda kuangalia ninapoacha hela nimekuta zipo vile vile, umenunua na nini hiyo kuku?”
Basi Mariam alimsimulia mume wake jinsi ilivyokuwa hadi wakapika ile mboga ila tu hakumwambia kama kuna kuku alipewa yani alichomwambia ni kuwa alitumiwa hela na kwenda kununua hao kuku wanne, basi Juma akacheka tu na kusema,
“Ila nyie wanawake akili zenu jamani! Yani mdogo wako hata hajapata wazo la kutunza hela nyingine jamani! Yani kaenda kununua yote kuku khaaaa ila Zayana ana akili mbovu sana”
Mariam akacheka tu, kisha Juma aliuliza kuhusu mama yake na Mariam alimwambia jinsi mama yake alivyoenda pale, yani Juma alisikitika tu kusikia kuwa mama yake ndiye aliyekataa chakula yeye mwenyewe halafu alianza kumlalamikia kuwa mke wake ana roho mbaya, yani Juma alitikisa kichwa tu.
Kisha waliamua kulala kwa muda huo.

Asubuhi na mapema, mlango wa nyumbani kwa Juma uligongwa na kumfanya Juma aende kufungua ila alipofungua tu alimkuta mama yake na kumshangaa,
“Mama!! Muda huu kweli?”
“Kwani tatizo liko wapi? Nakuja kwa mwanangu muda wowote niutakao”
“Haya, karibu”
“Nipo na mgeni”
Kisha mama Juma alimuita yule mgeni ambaye alisogea karibu sasa, alikuwa ndiye mwanamke ambaye wanataka Juma amuoe ila Juma alishtuka sana kumuona yule mwanamke na kujibu pale kwa ukali kabisa,
“Simtaki huyo mwanamke mama”

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 07144434333 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni