Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 35

MTOTO WA MAAJABU: 35

Basi Juma aliacha lile fagio lake ili kwenda kumkaribisha yule baba yake mdogo ila muda huu na mtoto na yeye alikuwa kamfata Juma nyumba.
Walipoingia sebleni, yule baba ndio alikuwa anakaa ila yule mtoto akamwambia,
“Babu, toka nje”
Yani Juma na Mariam walijikuta wakimuangalia huyu mtoto bila majibu.
Ila mtoto akazidi kusema,
“Babu toka nje”
Yule babu alisimama kwa uoga sana bila kujua ni kwanini atoke nje ila hata yeye alijikuta akiogopa kumuuliza huyu mtoto, yule mtoto akatabasamu na kusema,
“Hivi wote mnachoshangaa mnashangaa nini? Unawezaje kumruhusu baba yako na mkwe wako aingie ndani kukiwa kuchafu hivi!”
Wote walijikuta wakiangalia mule ndani, ni kweli nyumba ilikuwa ni chafu kisha mtoto akasema,
“Kama nyie mnapenda uchafu basi sawa ila mimi sipendi uchafu na kwamaana hiyo, babu yangu hawezi kukaa mahala pachafu, naomba babu utoke nje ili mama asafishe kwanza humu ndani halafu ndio babu utaingia ndani, lazima uheshimiwe wewe ni baba na ni mkwe wake, huwezi kukaa kwenye sebule chafu hivi”
Yani Mariam alijihisi aibu sana, basi Juma na yule babu waliamua kutoka nje maana Juma ilibidi tu aende kumuomba radhi yule babu ila muda huo huo yule mtoto na yeye alitoka nje na kumfanya Juma asiongee sana na yule baba yake mdogo na kubaki tu wakimuangalia yule mtoto ambaye alionekana kama kucheza michezo ya kitoto.

Mariam alichukia sana, tena sana yani hakujua kama huyu mtoto angemuumbua kiasi hiki, akakumbuka jinsi alivyomwambia kuwa yeye aoshe vyombo halafu yeye asafishe ndani ila kwa uvivu wa Mariam aliona shida kusafisha vizuri mule ndani ila leo mtoto kamuumbua, alichukia sana na kuanza kusafisha nyumba hivyo hivyo huku kachukia.
Alipomaliza kusafisha, alienda na kuwakaribisha ndani ambapo waliingia sasa na kukaa huku yule babu akimwambia Mariam,
“Pole sana mkwe”
“Asante”
Mariam alijibu kwa aibu huku macho yake ameyainamisha chini.
Walipokuwa wakiendelea na maongezi, mtoto akasema,
“Mama, kamuandalie babu chakula maana lazima atakuwa na njaa si unajua katoka safari”
Yani Mariam alitamani hata kumtukana huyu mtoto ila hakuwa na cha kufanya tu, na moja kwa moja aliinuka na kwenda kuandaa chakula.
Alipika huku akiwa amenuna kabisa, kisha akakitayarisha kile chakula mezani na kumkaribisha mgeni ila alikuwa amenuna sana.
Yule babu na wengine walienda mezani na kula chakula huku babu akisifia uzuri wa kile chakula na kumsifia sana Mariam kwa mapishi yani Mariam alikuwa amechukia sana hata hakufurahia jambo lile hata kidogo.

Jioni ilipofika, wakiwa wanaongea ongea pale mtoto yule akawakatisha maongezi yao na kusema,
“Mama, unajua babu amechoka, ungeenda kumsafishia chumba chake ili aweze kupumzika”
Yule babau na yeye aliongezea pale,
“Dah! Na kweli nimechoka sana mjukuu wangu”
Basi Mariam aliinuka kwa hasira yani alikuwa amevuta mdomo haswa na kwenda kusafisha kile chumba ila alikuwa anaona uvivu hatari yani alikuwa anafanya ile kazi basi tu, ilimradi amefanya ila kiukweli hakupenda hata kidogo na alipomaliza ndipo alipoenda kumuita ambapo yule babu alishukuru sana na kwenda kupumzika, ila wakiwa pale sebleni Mariam alimuuliza Juma,
“Huyu babako mdogo anaondoka lini?”
“Mmmmh Mariam mke wangu, mbona mapema sana?”
“mapema kitu gani? Mimi nilishakwambia sipendi wageni halafu wewe unaenda kuniletea wageni ili iweje?”
“Sasa tutakuwa ni watu wa aina gani mke wangu ambao hatutembelewi na wageni?”
“Lini nimeenda kwao kulala mimi? Nikienda huwa nawasalimia na kurudi ila wenyewe wanataka kufanya maamo kabisa, mbabu huyo si ana mji wake jamani, halafu licha ya hivyo ana watoto wake kwanini asiende huko kukaa? Hadi aje kwako wewe mtoto wa kaka yake?”
“Hebu Mariam mara nyingine uwe na staha, kumbuka yule ni baba yangu mdogo yani mdogo wake baba yangu mzazi, halafu kumbuka baba yangu mimi alikufa zamani sana kwahiyo yule unayemuona ndio kabeba asilimia kubwa ya maisha yetu kwasasa, mimi ni mtoto wake pia, na hata hajasema bado alichokuja kufanya halafu tayari ushaanza kumuwekea vikwazo kweli tutafika mke wangu?”
“Aaarrgh muone vile”
Mariam akainuka na kwenda chumbani yani hakupenda kabisa jambo lile.

Usiku wakati wa kulala, Mariam alianza tena kumlalamikia Juma maana aliona sasa atateseka na kazi za mule ndani,
“Juma, ni wewe ndiye umekubali kuwa baba yako mdogo aje mahali hapa halafu mtoto wako akiwa ananiumbua unachekelea mwenyewe, inamaana wewe hujui kusafisha nyumba? Hujui kupika wewe? Hujui kusafisha chumba wewe? Kwanini kuacha niteseke ilihali unajua fika kuwa mimi ni mjamzito?”
“Mmmmh naomba unisamehe mke wangu, nisamehe sana kuanzia kesho nitajitahidi ila mimi nitaenda kazini”
“Hakuna kwenda kazini hadi huyo mbabu wako aondoke, mimi siwezi kufanya kazi kama mtumwa, unalijua hilo kabisa, sikuwa na mimba tu na sikuweza kufanya kazi, sembuse kwasasa nina mimba!! Kwakweli siwezi kufanya kazi, nisamehe bure tu”
“Haya mke wangu nimekuelewa hakuna tatizo mke wangu, naomba tulale”
“Ndio ila niliyokwambia yaweke akilini, nisije nikajibu vibaya mimi nikaonekana sijui mke gani”
Yani Mariam alikuwa akiongea kwa jazba kabisa kuonyesha jinsi gani kachukia kwa swala la yeye kuambiwa afanye kazi kwaajili ya yule mgeni aliyewafikia.

Asubuhi ya leo walikaa pamoja wakipata kifungua kinywa, na baada ya hapo walikaa kufanya maongezi huku Mariam akisinzia tu pale ila alishtuliwa na kauli ya mtoto,
“Mama, jamani vyombo hadi vinanuka toka juzi usiku havijaoshwa jamani mama!”
Mariam akamuangalia Juma ambapo Juma akasema,
“Hakuna tatizo, nitaenda mimi kuviosha”
Mtoto akatikisa kichwa na kumuangalia babu yake kisha akamuuliza babu yake,
“Eti babu ni halali hiyo? Mama yupo amekaa tu halafu baba aende kuosha vyombo, ni halali hiyo?”
Babu na yeye akasema,
“Hapana si halali, kijijini sisi huwa hatuishi hivyo sijui kwa watu wa mjini ila si halali kwakweli. Kusaidiana kupo ila sio huku yani mke amekaa tu halafu mume aende kuosha vyombo hapana si halali”
Mariam hakujibu kitu pale ila aliondoka kwa hasira sana na kubeba vyombo hadi nje kwenda kuviosha yani alikuwa amechukia sana.
Mariam alikuwa akiosha huku akiwaza ni kitu gani cha kumfanya huyu mtoto maana aliona kamavile mtoto anamfanyia makusudi tu na usikute ni jambo ambalo mtoto amepanga kulifanya kwake kwahiyo Mariam alikuwa akinuna muda wote.

Usiku wa leo ndio Mariam alianza kulalamika zaidi kuhusu zile kazi yani alilalamika sana na kumwambia Juma kwa ukali,
“Jamani Juma nimechoka, yani nimechoka kabisa inaonyesha wazi unafurahia hiki ambacho mtoto anakifanya, mimi nimechoka kwakweli. Kwanini Juma lakini”
“Ila mke wangu, ulitegemea mimi nifanye nini sasa? Ulitaka nifanyeje jamani? Kumbuka kila nikitaka kukusaidia kazi, mtoto anaanza kumwmabia yule babu sijui inaruhusiwa kufanya hivi na hivi mpaka bamdogo anaanza kunihisi vibaya kwakweli, yani nashindwa mke wangu”
“Kama unashindwa mwambie huyo bamdogo wako aondoke, kwani Juma unashindwa nini jamani khaaaa!! Kwakweli nimechoka mimi, tena nimechoka sana jamani Juma. Usinifanyie hivi jamani”
“Pole mke wangu ila nitajua cha kufanya usijali”
“Nisijali nini sasa jamani kwa mambo kama haya? Hata huna huruma na ujauzito wangu, hata hunihurumii kwa hali niliyokuwa nayo?”
“Nakuhurumia mke wangu, tena nakuhurumia sana ila sina cha kufanya”
“Usinichanye na jibu lako hilo la sina cha kufanya, nitakuja kufanya jambo hapa na kukufanya ujutie katika maisha yako yote”
Mariam akalala muda huu bila kuongezea neno hapo.

Kulipokucha tu, Mariam akamuomba Juma pesa ili akaangalie mboga ila Juma alisema kuwa ataenda mwenyewe,
“Hivi wewe mwanaume una nini lakini? Ndiomana yule anakuitaga mwanaume wa kipemba, ni wivu gani huo uko nao? Tumezaa na hapa nilipo ni mjamzito, unadhani nitachepuka na nani? Niache nikanunue mboga na mimi niangalie mji nipunguze mawazo”
“Basi twende wote”
“Uende wote na nani? Nisamehe sana, siwezi kwenda popote na wewe. Naomba leo nikanunue mwenyewe”
Juma akapumua ila hakutaka marumbano na mke wake, hivyo akampatia pesa ili aende kuangalia hiyo mboga aliyokuwa anaisema na muda huo huo Mariam alijiandaa na kutoka nyumbani kwake, kwahiyo Juma alibaki yeye na baba yake pamoja na mtoto wake.
Waliamua kupika chai na kunywa ila yule babu alikuwa akisikitika na walimpomaliza kunywa chai alimuomba Juma waende kuongea kidogo ambapo Juma alitoka nje na yule babake mdogo.
“Kwanza kabisa Juma unajua kilichonileta hapa?”
“Mmmmh sijui baba, nilijua umekuja kusalimia tu”
“Licha ya kusalimia ila kipo kilichonifanya nije hapa”
“Kitu gani hiko baba?”
“Ni kuhusu mtoto wako”
Juma akashtuka kidogo kwani akajua ni lazima na ndugu zake nao washatangaza mambo ya ajabu ya yule mtoto, 
“Ndio baba, kafanyeje?”
“Sikia, kwa habari nilizosikia ni kuwa Juma ana mtoto wa ajabu sana sijui mtoto anafanya mambo ya miujiza, sijui mtoto anafanya mambo ya uchawi, nikasema acha niende kujishuhudia huko huko ili nijue jinsi ya kumsaidia huyo Juma”
Basi Juma alitulia akimsikiliza baba yake,
“Ndio baba nakusikiliza”
“Ila toka nimekuja sijaona kama mtoto ana tatizo ila tatizo hapa ni mke wako”
“Kivipi baba?”
“Mmmmh sijapata kuona mke mvivu kama mke wako”
“Kwanini baba?”
“Jamani mke hadi anakumbushwa usafi wa nyumba yake na mtoto! Mke hata hajui kama wageni wanatakiwa kula hadi mtoto amkumbushe? Mke hata hajui wajibu wake hadi aambiwe na mtoto, tena unaona sawa tu kwa wewe kufanya shughuli za kike wakati mkeo amekaa jamani Juma ni aibu gani hii? Umeoa au umeolewa?”
“Jamani baba ni kusaidiana”
“Kusaidiana sio kwa namna hiyo mwanangu, labda uniambie mmeamua kwenda kuosha wote vyombo au mmeenda wote kufua, ila sio wewe uende kuosha vyombo kwa niaba ya mkeo halafu yeye amekaa tu, sio heshima hiyo kabisa, wewe ni mwanaume”
“Mmmh ila baba mke wangu ni mjamzito”
“Aaaah kumbe ni mjamzito?”
“Ndio baba”
“Basi sina usemi zaidi ila mke wako ni tatizo kushinda huyo mtoto wako, nimemaliza”
Juma hakujua cha kuongea zaidi na baba yake maana aliona aishie pale pale kuongea nae kwani tatizo la mke wake alikuwa analijua yeye mwenyewe.

Mariam alipokuwa sokoni alikutana na mdogo wake wa siku nyingi na kumfurahia sana, alimsalimia pale na kumuuliza,
“Vipi ushaolewa?”
“Namshukuru Mungu, ndoa yangu umepita yani yule kiumbe nyumbani kwako alinitia uoga sana”
“Yule Anna!”
“Ndio dada, bora ungeniambia mapema”
“Ila nimeshamuondoa pale nyumbani kwangu, hayupo tena. Unaweza kukaribia muda wowote”
“Sawa nitakaribia dada, vipi huku sokoni?”
“Nimefata mahitaji ila nimechoka jamani, kazi nyingi mdogo wangu. Nahitaji msichana wa kazi kiukweli”
“Mmmmh dada, wadada wa kazi wanasumbua siku hizi, unamuhitaji kweli?”
“Ndio namuhitaji, ngoja nikupe namba zangu ili hata ukisikia anapatikana mahali unitafute ili awe binti yangu wa kazi”
Basi yule binti alibadilishana namba na Mariam na kisha kuagana nae, ambapo Mariam alienda kununua mahitaji ila alipotoka sokoni alienda stendi kukaa maana hata hakutaka kuwahi nyumbani kwake sababu ya zile kazi, yani Mariam hakuna kitu alichokuwa akichukia kama kufanya kazi.
Alikaa pale stendi kwa muda mrefu hadi kuna watu walikuwa akifika pale na kuongea na yeye hadi kumzoea kidogo, kwahiyo alikuwa akisikiliza stori za watu wale na inapobidi na yeye alikuwa akichangia, mmoja alianza kusema kuhusu mtoto wake,
“Jamani mwanangu kaongea mapema huyo, huwa ananiumbua hatari, kitu kidogo tu unakuta kashaenda kusema kwa muhusika”
Wenzie wakawa wanacheka na kusema,
“Hivyo ndio vitoto visivyofaa”
Mwingine akawaambia,
“Ila na sisi wazazi mengine tunayataka, sasa mtoto kama kafikia hivyo mpeleke shule, wanapelekwa shule watoto wasioweza kuongea sembuse huyo anayeongea? Mpeleke shule mtoto wa hivyo, akacheze na wenzake huko, akacheze na walimu hata usumbufu nyumbani anapunguza kwa kiasi kikubwa sana sababu anarudi akiwa amechoka”
Lile wazo la kumpeleka mtoto shule ikaonekana wengi sana wanalisapoti na kumfanya Mariam na yeye aone kuwa ni jambo jema kuwa akamshauri mume wake waweze kumpeleka yule mtoto wao shule maana aliona kama ni sehemu ya kumfanya mtoto arudi amechoka basi ni sehemu nzuri sana ilia ache kufatiliwa mambo yake na yule mtoto.

Wakina Juma walimsubiria Mariam hadi walichoka yani hadi Juma aliamua mwenyewe kuingia jikoni na kufanya mapishi ya siku hii maana aliona wazi wakiendelea kumsubiria Mariam basi wataumbuka kabisa.
Basi Juma aliandaa chakula na kumkaribisha baba yake halafu yeye alitoka ili aende kumfata Mariam, ila alipofika nje tu naye Mariam ndio alikuwa anafika,
“Khaaa jamani wewe mwanamke, kuniweka roho juu juu kiasi hiki ndio nini?”
“Kheee kumbe unanipenda eeeh!!”
“Khaaaa jamani Mariam, unajua wazi ni jinsi gani mimi ninakupenda wewe, Kila siku nakwambia Mariam kuwa wewe ni kila kitu katika maisha yangu. Usinifanyie ujinga tafadhari.”
“Sasa ujinga gani niliokufanyia mimi? Ujinga umeutaka wewe kumuacha babako mdogo akae hapa hadi leo”
“Mmmmh usiongee kwa nguvu Mariam, nitajua cha kuongea na huyu mzee na kesho ataondoka ila usiongee kwa nguvu mke wangu”
Mariam akaingia ndani na mboga zake, akamsalimia tu huyu baba kisha moja kwa moja akaenda chumbani kupumzika.

Jioni ilipofika, Juma akasema kuwa ataenda kupika mwenyewe chakula cha usiku ila mtoto akadakia na kusema,
“Kwanini asipike mama jamani wakati yupo?”
Juma akamwambia mtoto,
“Na wewe, mama yako ni mjamzito”
“Hata kama, ila mama ni mvivu kwa asilia, kwani anaumwa? Kuna wengine wanakuwa wajawazito halafu wanaumwa, hao afadhali kidogo ila mama haumwi hata ukucha ila kazi kusema mimi mjamzito, mimi mjamzito, kwakweli mama ni mvivu sana tena sana”
Juma hakujibu kitu ila aliinuka tu na kwenda kupika kwani alimuona jinsi mkewe alivyokuwa na amenuna kwa muda huo.
Leo walipomaliza kula, yule babu alimuita Juma na kuongea nae,
“Mwanangu, kwakweli mimi kama baba yako siwezi na sifurahishwi na hii hali kabisa kabisa”
“Mmmh kwanini baba?”
“Ni aibu na kunifedhehesha sana kama mzazi, mwanangu kesho naondoka narudi kwangu. Tayari jibu la maswali yangu nimeshapata, tatizo la nyumbani kwako sio mtoto wako bali ni mke wako ndio tatizo tena ni tatizo kubwa sana. Unatakiwa kuwa makini mno”
Juma akapumua ila lile swala la huyu baba kuondoka kesho, alilifurahia kwakweli maana hata yeye alitamani tu huyu baba aondoke ili awe huru na mke wake.

Usiku wa siku ile, Mariam alimwambia Juma lile wazo la mtoto yule kupelekwa shule ila Juma alishtuka kidogo na kumuuliza Mariam,
“Unaona ni sawa kwa mtoto yule kwenda shule?”
“Ndio, wanapokea watoto wasioongea sembuse huyo wa kwetu anayeongea?”
“Hiyo hivyo tu ila tambua wa kwetu ni mtoto wa aina gani”
“Natambua mume wangu, ila bora aende huko tupunguze karaha zingine”
“Sawa, sasa huko shule tutasema mtoto anaitwa nani? Kumbuka hata sisi wazazi wake hatujui jina lake”
“Mmmmh hilo nalo neno ila kesho nitamuuliza ili atutajie jina lake yeye mwenyew,e ila huyu mtoto aende shule bhana itakuwa vizuri maana nyumbani ananipa presha tu kila siku”
Wakakubaliana kuhusu jambo hilo kuwa huyu mtoto wao aende shule tu.

Leo mapema kabisa, babu alijiandaa kwaajili ya kuondoka, kwahiyo walimtayarishia chai akawa anakunywa.
Mariam alitoka nje, ila na mtoto na yeye akatoka nje ambapo Mariam akaona ndio muda mzuri wa kumuuliza yule mtoto anaitwa nani,
“Eti mtoto wetu, jina lako ni nani?”
Mtoto akatabasamu na kumwambia Mariam,
“Angalia kule”
Mariam akageuka na kuangalia, ila alipatwa na kizunguzungu cha gafla na kuanguka.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni