MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 32

MTOTO WA MAAJABU: 32

Mariam akajikaza tu,
“Unataka tuwapikie nini?”
“Baba, si ameleta nyama! Tuwapikie pilau basi”
“Mmmmh sawa, ila viungo vya pilau vinanichefua!”
“Nitapika mimi mama”
Yani Mariam alizidi kushangaa kwakweli kwa hiki ambacho mtoto wake anakisema.
Mtoto alimuangalia na kumwambia,
“Mama, mbona unashangaa?”
Mariam hakujibu ila mtoto akamwambia tena mama yake,
“Tena mama, yale maharage kidogo nayo uyabandike, yaanze kuchemka hapo nitayaunga halafu nenda kachume ile mboga aliyopanda Anna ili nayo tuipike”
Hapo Mariam aliuliza,
“Sasa si umesema ni pilau! Inakuwaje tena na maharage, mara mchicha vya nini hivi?”
“Aaaah mama, hizi ni mboga tu kama mboga zingine huwa zinanogesha chakula na kufanya uchangamfu wakati wa kula. Aliyesema ukila pilau usile na mboga ni nani? Sasa leo nitakupikia na utafurahi, nyama nyingine itakuwa kwenye pilau na nyingine nitairosti pembeni”
Yani Mariam alimuangalia huyu mtoto wake bila kummaliza, kiukweli alikuwa akishangaa tu mpaka mtoto alipomwambia,
“Mama, acha kushangaa muda unakwenda inabidi vyote nilivyosema viandaliwe”
Mariam baada ya kufikiria kidogo akaamua tu kwenda kuwasha moto na kuandaa kila kitu kisha yule mtoto alimwambia Mariam aweke kiti ili asimamie juu na kupika yani Mariam bado alibaki kaduwaa kwakweli na kufanya vile vile ambavyo mtoto wake amemwambia basi Mariam akachukua kigoda na kukiweka karibu na jiko ili kumuangalia huyu mtoto kitu ambacho atakifanya pale jikoni, na kweli kabisa yule mtoto alisimama pale na kuanza kupika yani Mariam alisimama tu pembeni akistaajabu yale mambo.
Kwakweli Mariam hakubanduka pale jikoni ili aone kama kuna uchawi wowote unatumika pale ila alimuona tu huyu mtoto akipika kama wale watu wafupi sana wakipika na alipika kila kitu alichokisema huku Mariam akimshuhudia pale na kumsaidia baadhi ya vitu vidogo vidogo tu, kwakweli Mariam alikuwa akimshangaa sana kiasi kwamba mtoto akamwambia,
“Mama, si utaenda kukata kachumbari au vitunguu vinakuchefua pia?”
Mariam alimuangalia mtoto na kumjibu,
“Nikikata vitunguu vingi vinanichefua”
Mtoto akamwambia Mariam,
“Usijali mama, niandalie hapo vitu vyote vya kukatakata”
Kwakweli Mariam leo alikuwa akistaajabu tu, akaanza kumuandalia yule mtoto vitu vyote vinavyotakiwa kukatwa katwa kwaajili ya kachumbari na alipomaliza alimkuta yule mtoto nae akimaliza kugeuza chakula ambapo alimwambia Mariam,
“Sasa mama, ni kazi yako kupalilia chakula hapo”
Mariam akamshusha yule mtoto kwenye kile kiti halafu yeye akapalilia kile chakula huku muda huu mtoto akiwa anakatakata kachumbari, yani kila kilichokuwa kikifanywa na huyu mtoto kilimuacha Mariam mdomo wazi maana Mariam alibaki kushangaa tu kwa kila kitu kilichokuwa kinatendeka mahali pale.

Hadi chakula kilipokuwa tayari na kwenda kukiandaa mezani, bado Mariam alikuwa akishangaa tu kwakweli huku akitamani kumuuliza yule mtoto maswali mengi lakini aliona wazi akishindwa, kisha yule mtoto akamwambia Mariam,
“Mama, nipakulie kidogo nile kabisa ili nikakae ndani maana baba kasema hao wageni wasinione”
Mariam alimpakulia chakula ambapo yule mtoto alikula kisha akainuka na kwenda kukaa ndani kama ambavyo alisema, kwakweli bado Mariam alikuwa akistaajabu kwa yale yote ambayo yametendeka pale nyumbani, ilikuwa ni kitu cha ajabu sana kwake ukizingatia hajawahi kukutana na jambo kama hili hapo kabla.
Muda kidogo, Juma alifika na wageni wake, wale wageni walikuwa ni watano ambapo Mariam aliwakaribisha vizuri tu ndani kisha Juma akamshika mkono Mariam na kwenda kuongea nae chumbani,
“Mmmmh hawa wageni nimewaambia kuwa tupitie tukale wamegoma na kusema kuwa niliwaahidi kwamba leo wataenda kulak wangu, wamekataa kabisa kupita na kula popote pale, wamesema watakula kwangu hapa hata sielewi cha kufanya na wewe ulisema hupiki. Hebu tupeane ushauri mke wangu”
“Ushauri wa nini? Chakula kipo mezani”
Yani Juma alimkumbatia mke wake kwa furaha maana hata ile asubuhi wakati mtoto anasema kuwa atamsaidia mama yake kupika, wala hakutilia maanani hii kauli kwahiyo hakujua kama ni kitu hiko kimetokea ila alimshukuru tu Mariam na moja kwa moja walitoka sebleni ambapo Juma aliwaambia rafiki zake,
“Tena tumekuja muda muafaka maana mke wangu ameshaandaa chakula jamani, karibuni tujumuike”
Wale rafiki wa Juma walitabasamu na wote waliinuka kuelekea sehemu ambayo Juma aliwaelekeza yani pale kwenye meza ya chakula na kila mmoja anakaa na kupakua kile chakula huku wakila na kila mmoja alikuwa akiguna kwa utamu wa chakula kile, mmoja aliamua kuongea tu pale pale huku akimuangalia Mariam ambaye alikuwa amekaa pembeni maana yeye hakwenda kula,
“Shemeji, mimi sio mpenzi wa pilau na wala huwa sili pilau kabisa ila tulipoitwa hapa mezani na kuona pilau nikasema leo nimepatikana nikapakua kidogo sana ila naongeza shemeji, sijapata kula pilau tamu kama hii jamani khaaa!”
Wenzie wakacheka huku akiongeza kile chakula na kula huku wengine wakisifia pale pale na kuendelea kula, yani Mariam alikuwa akitabasamu tu hadi walipomaliza, mwingine akasema,
“Mimi huwa sili maharage nyumbani kwangu ila hapa natamani hata haya maharage niyabebe na kuondoka nayo kabisa kwa utamu huu”
Walicheka tena, huku wakimalizia tu
Walipomaliza walikaa kidogo tu na kuaga ila wote walikuwa wakimshukuru Mariam kwa kile chakula na kumshukuru Juma kuwakaribisha nyumbani kwake kupata chakula kitamu vile.

Juma aliamua kuwasindikiza yani njia nzima walikuwa wakisifia tu utamu wa kile chakula, mwingine akasema pale,
“Jamani mimi huwa sipendi kachumbari, yani huwa sili kachumbari kabisa khaaaa sio kwa kachumbari ile, bwana Juma naomba mke wangu aje kujifunza kwa mkeo maana mke wangu ananipikia chakula hicho mchuzi bahari nyama unatafuta jamani khaaa!! Mke wako ni noma”
Yani Juma alikuwa akitabasamu tu, na yeye aliona utamu wa kile chakula, ingawa huwa mke wake anapika chakula kizuri sana ila hiki cha leo kilikuwa kimezidi uzuri na kumfanya kila wanapomsifia atabasamu tu mpaka wanafika stendi na kupanda basi na kuondoka.
Juma alikuwa akirudi nyumbani kwake na kukutana na yule jirani yake ambaye walikuwa wanakutana mwanzoni kabisa na kuna siku alishushuliw ana mtoto wa Juma, ila leo alimsalimia Juma kama ambavyo alikuwa akimsalimia zamani,
“Jirani naomba unisamehe tu kwa yale yote ambayo yamepita baina yetu”
“Aaaah usijali jirani, mimi huwa sikai na kinyongo, nilishakusamehe jirani”
“Nashukuru sana jirani, vipi lakini mama na mtoto wanaendeleaje?”
“Hawajambo, ni wazima wa afya”
“Basi ni vyema”
“Sasa, kuna msiba kwa majirani zetu wa kule juu, mwambie mama nitakuja kumpitia siku ya kuzika ili na yeye akaonekane kwenye msiba”
“Aaaah hapana usije, hawezi mke wangu kwenda kwenye msiba bila ya mimi”
Yule jirani alishindwa kusema zaidi na kumuacha tu Juma aondoke zake maana yeye hakuona kama ni tatizo kwa yeye kumpitia Mariam kwenda naye kwenye msiba.

Usiku wa leo Juma anamuuliza vizuri mke wake kuhusu kile chakula maana uzuri wake kilivunja rekodi,
“Mke wangu, kwanza hongera halafu kile chakula jamani mbona kilikuwa ni kitamu sana kuliko vyakula vyote ambavyo umewahi kupika”
Mariam akacheka na kusema,
“Sio mimi niliyepika kile chakula”
Juma alishangaa na kuuliza kwa makini,
“Ni nani sasa kapika?”
“Ni mtoto ndio kapika”
Juma alishangaa zaidi na kutaka kujua yule mtoto amepika vipi hiko chakula, kisha Mariam alianza kumuelekeza yani Juma alishangaa sana,
“Hata mimi nimeshangaa pia, huwezi amini sijatoka jikoni toka alivyoanza kupika hadi mwisho, nilitaka kuona kama yule mtoto anafanya mambo ya miujiza au ni kitu gani maana pale nilitegemea kuona mkono mrefu ukikoroga yani siku ote huwa sina imani na huyu mtoto”
“Hivi mfano mke wangu ingekuwa kama hivyo ambavyo unawaza ingekuwaje?”
“Mmmmh hata sijui yani kwa uoga huu nilionao sijui jamani ingekuwaje duh! Ningeogopa sana, sijui hata ningefanyeje mimi. Ila nilijikaza huku nikimuangalia kila alichokuwa akikifanya, nilikuwa naangalia kama atatumia nguvu nyingine ila hapana alisimama kwenye kigoda na kupika kwa mikono yake mwenyewe”
“Mmmmh haya, tujiulize nani kamfundisha kupika?”
“Hilo swali hata mimi nimejiuliza tena sana na wala sijapata jibu kabisa, naogopa mimi naogopa kabisa. Huyu mtoto tuseme alikulia tumboni au ni kitu gani? Maana haya mambo ni makubwa jamani sidhani kama kuna mtu ambaye anaweza akategemea kwa mtoto mdogo vile kupika chakula kama kile”
“Unajua nashangaa hadi muda huu mke wangu, ila tulale tu maana sielewi”
Wakaamua kulala ila lile lilikuwa jambo la ajabu sana kwao.

Leo Juma alipokuwa kazini tu alipata sifa za kila namna, yani kila aliyefika kwake alikuwa akisifia jinsi mke wa Juma alivyokuwa anajua kupika, yani kuna mwingine alienda kuzungumza na Juma,
“Hivi kwanini ndugu yangu mkeo asifungue chuo cha mapishi?”
Juma akatabasamu na kuuliza,
“Hivi inawezekana eeeh!!”
“Ndio inawezekana, kuhusu kupata wanafunzi sio shida maana wake zetu ndio watakuwa wanafunzi wake namba moja”
Mmoja akadakia na kusema,
“Tena mke wangu mimi ndio anapaswa kuwa mwanafunzi wenu wa kwanza, sababu hayo maharage anayopika mke wangu ni Mungu tu anajua, harage kama unataka kupigana nalo! Ila wanaume tunakutana na mengi sana tunavumilia tu, huo wali siku nyingine mara apike bokoboko, siku nyingine mara ukukabe kila tonge unalomeza, siku nyingine mara aunguze basi tabu tupu, bora mkeo aanzishe chuo cha mapishi tu, na akianzisha niambie nimuandikishe mke wangu huko maana nimechoka kupikiwa mauza uza”
Juma alikuwa akicheka, mwingine akasema,
“Sasa ile mboga ya majani uwiiii kama sio mchicha vile, jamani Juma mkeo kajifunza wapi mapishi?”
Juma akatabasamu na kusema,
“Ndiomana nampenda sana yule mwanamke yupo vizuri kila idara”
“Kwakweli hongera sana, unastahili kusifiwa kwa hilo, nina uhakika hapa kila mtu anatamani kupata mke kama ambaye umempata wewe. Hongera sana ila swala la kufungua chuo cha mapishi naomba ulifikirie, tunahitaji sana wake zetu wapate ujuzi hapo”
Yani Juma ilikuwa ni furaha sana kwake kwa kila sifa ambayo ilitolewa kwaajili ya kile chakula ambacho walikula rafiki zake, akajisemea moyoni kuwa akitoka siku hiyo ni lazima apitie kuwachukulia zawadi mke wake na mtoto kwani aliona wazi kuwa wanastahili kupata zawadi.

Mariam kama kawaida alikuwa akibaki na huyu mtoto na alikuwa akimuangalia kwa karibu sana kila kitu ambacho kilikuwa kinafanywa na huyu mtoto, alitaka kuhakikisha kama huyu mtoto ni wa kawaida ila hata kama bado kuna mambo ambayo sio ya kawaida mengi tu kwa huyu mtoto.
Basi muda huu alikuwa amekaa sebleni na huyu mtoto ambapo mtoto alimwangalia Mariam na kumwambia,
“Najua mama hapo unatamani sana kuniuliza kuwa nimejifunza wapi kupika!”
Mariam akashtuka na kumwambia mtoto,
“Ni kweli, nilikuwa natamani sana kujua jambo hilo”
“Ni hivi mama, nimejifunza kupika kutoka kwako. Wewe mama ni mpishi hodari sana, kwahiyo nimerithi kutoka kwako”
“Mmmmh ila mbona chakula kilikuwa kitamu sana”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Ndio hivyo mama, vya kurithi vinazidi, umesahau hilo mama yangu?”
Mariam hakuwa na jibu kwahiyo alikuwa akimuangalia tu huyu mtoto kisha mtoto alimuuliza Mariam,
“Hivi bado tu hujanizoea mama?”
“Mmmmh hapana nimekuzoea”
Mariam alijibu tu vile ila kiukweli bado hakuwa na mazoea ya kiasi kile na mtoto wake maana bado kuna mambo alikuwa na mashaka nayo.

Muda huu Juma alirudi akiwa na zawadi zake mkononi ambapo alimkuta mkewe na mtoto wapo pamoja na kuwasalimia pale kisha akawaambia,
“Nimewaletea zawadi, kwakweli nimefurahishwa sana na kazi ya jana, kila mtu ananisifia kwakweli”
Akatoa zawadi kwanza aliyomletea mkewe na kumkabidhi ambapo Mariam aliifungua pale pale huku akiiangalia na kufurahi sana,
“Asante sana mume wangu, yani nimefurahi nilikuwa nahitaji kitenge hiki balaa. Asante sana”
“Sijui utashona sijui utafanyaje”
“Nitashona gauni moja zuri la kuvaa kipindi mimba yangu ikiwa kubwa”
Juma akacheka tu na kutoa zawadi aliyomletea mtoto ila kabla ya kumkabidhi mtoto akasema,
“Hebu ifungue baba”
Juma aliifungua ile zawadi, ilikuwa ni mdoli ambapo alijua mtoto wake angafurahi sana sababu watoto wengi huwa wanapenda midoli, ila alishangaa mwanae akimwambia,
“Khaaa baba, umeniletea mdoli jamani. Wa nini mimi?”
“Mmmmh jamani, wewe si mtoto na watoto hupenda kuchezea midoli”
“Baba, ni mtoto gani anaweza kupika kama mimi? Mimi ni mtoto kweli ila akili zangu na mawazo yangu sio ya kitoto, sipaswi kupewa mdoli mimi”
“Kheeee kwahiyo ni zawadi gani gani inakufaa?”
“Mimi niletee kipande cha kuni”
Hapa hata Juma mwenyewe alishangaa kusikia kipande cha kuni maana hakumuelewa mtoto wake ila hakuwa na budi zaidi ya kumuitikia tu kuwa atamletea hicho kipande cha kuni.

Usiku wakati wa kulala, Juma alizungumza na Mariam kuhusu hicho kipande cha kuni kwani moja kwa moja Juma alihisi mkuwa lazima huyu mtoto anataka kufanya mambo kama yale ya kupeleka kuni kwa mama Mariam, basi akamwambia Mariam,
“Haya sio kama mambo yako kweli?”
“Mmmmh au anataka na wewe upeleke kwenu kuni kimiujiza?”
“Itakuwa, ila mimi naogopa hayo mambo ya kimiujiza yani uambiwe umeleta kitu wakati hujaleta kweli?”
“Hapo sasa jamabi, mambo mengine ni ya ajabu sana”
“Kuna kitu nitafanya cha tofauti ila hicho kipande cha kuni nitamletea”
“Kitu gani hicho mume wangu?”
“Utaona tu, wewe subiri ila kuna kitu cha tofauti sana nitakifanya maana huyu mtoto anataka kutufanya humu ndani kama mapunguani vile, mimi nimemletea zawadi eti amekataa zawadi yangu anataka kipande cha kuni khaaa”
“Mmmmh!!”
Mariam aliishia kuguna tu na muda huo walilala tu.

Kulipokucha asubuhi na mapema Juma aliondoka zake kwenda kwenye shughuli zake, nyumbani walibaki Mariam na mtoto kisha mtoto alimuuliza Mariam,
“Mama, mbona wewe nilipokwambia uniletee zawadi ya kipande cha kuni ulifanya haraka sana kwanini baba anakaidi?”
“Anakaidi kivipi? Kwani kasema hakuletei? Atakuletea tu siku haijaisha”
Sawa, ila anachotaka kufanya kitamgharimu badae”
“Kwani anataka kufanya nini?”
Yule mtoto hakumjibu na kufanya kidogo Mariam ashikwe na mashaka pale na kuamua kumpigia simu Juma ila Juma hakupokea ile simu kabisa, kila Mariam alipompigia hakupokea mpaka Mariam akamtumia ujumbe,
“Juma kama unataka kufanya kitu tofauti na kuleta hiyo kuni tafadhari usifanye maana mtoto anasema itakugharimu”
Akatuma ule ujumbe na kuendelea na mambo mengine.

Juma hakukaa sana ofisini bali aliondoka na kuelekea kwao ambapo njiani alikota kipande cha kuni, moja kwa moja alienda nacho hadi kwao akakikata katikati na kukiacha kimoja kwao na kingine kuondoka nacho. Kwahiyo alimsalimia tu mama yake na kumuacha na kile kipande cha kuni halafu akaanza kurudi nyumbani kwake.
Alipokuwa anakaribia na nyumbani kwake alisikia simu yake ikiita, akaitoa na kukuta imekatika ila akaona ujumbe wa mke wake na kushtuka sana maana tayari alishafanya tofauti, mara simu yake ikaanza tena kuita akaangalia na kuona mpigaji ni mama Shamimu, basi akapokea na kuanza kuongea nae,
“Kheeee wewe Juma umefanya nini wewe! Haya sijui gongo uliloliacha hapa sijui kuni lipo kumchapa mama”
“Kivipi?”
“Linamchapa hadi mama kazimia”
Yani Juma hakuelewa kabisa kile alichoambiwa.

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
Story ya MWANAUME WA DAR inaendelea leo.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni
close