Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 29

MTOTO WA MAAJABU: 29

Basi Mariam na Juma wakaondoka huku wakiwa na furaha sana kuwa wamewaweza wale watoto, waliondoka hadi nyumbani kwao walipofungua mlango na kuingia ndani walishangaa sana kujikuta wakiingia kwenye nyumba ile ile ya bondeni.
Hii ilikuwa ni ajabu sana kwao na hawakutegemea wala nini, cha kwanza kabisa waliwaza kuwa ni mauzauza ya ile nyumba na kuwafanya waogope zaidi, Mariam ndiye aliyeanza kuongea,
“Nini hiki Juma?”
“Mmmmh hata sielewi, haya mambo nilikuwa nayasikia kwako tu. Si tulikuwa tumeshafika nyumbani!”
“Ndio, hata mimi huwa hivi hivi hata siku ile ilikuwa hivi hivi ambapo nikajikuta tu nimelala pale nyumbani halafu wewe ukasema eti nimerudi usiku, sikurudi mimi bali ilikuwa hivi hivi”
“Mmmh mke wangu, tusianze mjadala inabidi tujue cha kufanya”
Hapa Mariam akawa mpole kwani aliona wazi jinsi gani kale katoto kao kanavyopenda kunyenyekewa, basi alipiga magoti pale na kusema,
“Mwanangu, popote pale ulipo najua wazi unanisikia, naomba tuhurumie wazazi wako. Akili zetu fupi zinatusumbua sana, tunashindwa kufikiria zaidi yani sisi tunafikiria ya hapa hapa, tuhurumie wazazi wako”
Pale pale wakasikia sauti ya mtoto na kushtuka sana, kumbe alikuwa pale pale sebleni pamoja na Anna, yani walishtuka hadi Juma alijikuta akipiga magoti pia, kisha yule mtoto akasema,
“Mama, na baba mimi sina tatizo na nyie ila ni kwanini mtake kuniacha mimi kwenye nyumba moja na Anna? Kulala nae isiwe sababu ya nyie kunihalalisha mimi niwe kwenye mikono ya Anna!”
“Tusamehe mwanangu, basi tumuache Anna hapa halafu turudi nyumbani?”
“Hapana mama, kama nyumbani huyu Anna tutarudi nae maana kuna mambo nahitaji kuyaona zaidi kupitia yeye. Kaniahidi kubadilika, nahitaji kuyaona hayo mabadiliko, huwezi ukamuacha Anna kwenye nyumba unayosema ni ya maajabu, hivi unajua ni nani kafanya usafi kwenye hii nyumba?”
Juma na Mariam waliangaliana na kujikuta wakiuliza kwa pamoja,
“Ni nani?”
“Hebu mpigieni simu shangazi”
Mariam alichukua simu yake pale pale na kumpigia simu wifi yake ambayo iliita sana na badae ndio ilipokelewa, mama shamimu aliongea kama katoka usingizini,
“Kheeee wifi ulilala?”
“Yani hata nashangaa, simu ndio imenishtua unajua nilishajiandaa hapa kwaajili ya kuondoka ila nilikaa kidogo tu na kupitiwa na usingizi hapo hapo. Nimechoka jamani hadi sijielewi
“Kheeee pole wifi”
“Ila naondoka, asanteni kwa kuniamsha. Ngoja niondoke naenda kwa mama”
“Ila ungetusubiri wifi!”
“Hapana, sitaweza”
Mariam alikata ile simu na kumuangalia yule mtoto wao kisha mtoto akawaambia,
“Ni hivi usiku wote wa jana, Anna alimchukua shangazi kiuchawi na kuja kumfanyisha kazi kwenye nyumba hii, usafi wote mnaouona ni shangazi ndio ameufanya kila kitu mnaona kipo sawa sababu ya shangazi”
Anna aliinamisha tu macho chini, kwakweli Mariam alishangaa sana na kuuliza,
“Anna kajuaje kuhusu nyumba yetu hii?”
Mtoto alitabasamu tu na kusema,
“Ambacho hujui mama ni kuwa Anna anakufahamu vizuri sana tangia zamani anakufahamu”
“Kheeee mbona sielewi”
“Utaelewa tu ila anakufahamu vizuri sana, na hii nyumba anaifahamu na ndiomana hajabisha kuletwa huku”
Kwakweli Mariam alishangaa tu ila alimuomba mtoto wake warudi ila mtoto aliwaambia kwa siku hii walale hapahapa halafu kesho yake ndio waondoke, hawakuwa na namna zaidi ya kukubali tu.

Mama Shamimu alifika muda huu kwa mama yake na kuanza kumuelezea kile ambacho kilimsibu siku hiyo,
“Yani mama ningekuwa nimefika hapa muda mrefu sana”
“Tatizo ni nini kwani?”
“Mama, hata sijui nimechoka vipi yani. Ni mejiandaa vizuri nikajilaza mara moja kheee kuja kushtuka ni Mariam anapiga simu yangu, hapo nimeamka na kukuta viungo vyote vinaniuma mama yangu”
“Dah pole sana, kale katoto eeeh!!”
“Halafu mama kale katoto ni kaajabu kweli, unajua kaajabu, yani ni kaajabu kweli unajua wewe kuna muda kanakufanyia vituko na kuna muda kanakusema vizuri”
“Kama vipi hivyo vizuri?”
“Mmmmh sijui Mariam aliwahi kusema kuwa wewe ni mchawi, basi kale katoto siku hiyo kakamwambia Mariam, sitaki tabia ya kumuita bibi yangu mchawi”
“Kheeee kumbe!!”
“Ndio hivyo mama”
“Hata kama, ukoo wetu haukataki wala kukatambua hako katoto, kila mtu ukimueleza tu kuhusu hako katoto kalivyo hakuna anayetaka kwenda kumuona Juma kabisa, yani hako katoto kamekuwa ni mkosi mkubwa sana kwenye familia”
“Ila mama, ngoja nikapumzike. Huyu mtoto namfahamu vizuri, sitaki kumuongelea sana”
“Kwani atakfanyeje na upo huku?”
“Mama, kumbuka ulianza kuharisha sababu ya kale katoto kama hujui, umepona baada ya Juma kufanya adhabu ya kukapeleka stendi kila siku, mmmh mama sitaki kukaongelea sana”
Ila mama Juma hakuona tatizo kukaongelea hako katoto kwwahiyo alikuwa akimshawishi tu mama Shamimu wawe wanakiongelea kile kitoto.

Ilipokuwa inakaribia jioni, Mariam akatoa wazo kuwa bora warudi tu maana hapo hata chakula hawajaweka watakula nini ila bado mtoto aliwakazania walale pale pale kitu ambacho Mariam alikipinga kabisa na kuzidi kumuomba mtoto wake kuwa warudi nyumbani na mwishowe yule mtoto alikubali kwahiyo wote kwa muda ule ule walianza safari ya kurudi nyumbani kwao.
Wakiwa kwenye daladala kwenye mida ya saa tatu usiku huku Mariam akiwa amempakata yule mtoto ila kuna mtu ambaye Mariam alikaa pembeni yake yule mtu alikuwa akiguna tu na alipigiwa simu na kuongea nayo kwa kiligha ila ile lugha Mariam alikuwa akiielewa ni kitu gani ingawa yeye alikuwa hawezi kuiongea ila ilikuwa ni lugha ya kwao, alimsikia akisema,
“Nimekaa na mama mmoja kwenye gari, kabeba mtoto wa ajabu sijapata kuona katika maisha yangu tangu ulimwengu uumbwe, hapa nilipo nina mashaka sijui kama nitafika nyumbani. Naomba mniombee tu”
Mariam alimuangalia yule mama kisha alimuangalia mtoto wake ambaye alimuona yupo kawaida tu, yani uajabu wa yule mtoto Mariam alikuwa akiuona kwenye matendo yake ila hakujua kama mtu mwingine anaweza kumuangalia tu huyu mtoto na kumuhisi kuwa ni mtoto wa maajabu ingawa kitu kama hiko kishawahi kutokea kwa baadhi ya watu kama yule muuza samaki aliyesema mtoto ni waajabu bila ya mtoto kuongea wala nini. Kwakweli Mariam alikuwa kamshika mtoto wake ila alikuwa na mashaka sana katika moyo wake, hata hakuwa na amani kabisa kabisa.
Basi lile daladala liliendelea kwenda, na mbele yule mama alishuka alionekana kushuka huku akisema,
“Asante Mungu, asante Mungu…..”
Yani Mariam alimuangalia huyu mama bila kummaliza, halafu kuna mtu mwingine alipanda na kukaa pale pembeni yake, yule mtu ndio alimuuliza Mariam kabisa,
“Samahani dada, kwani ni mtoto wa aina gani umebeba huyu?”
Mariam akamuangalia na kumuuliza,
“Kwani wewe unamuona ni wa aina gani?”
Mariam alikuwa amemfunika kidogo mtoto, akamfunua ambapo yule mtu alimuangalia sasa mtoto na kujikuta akisema,
“Dah!! Sijapata kuona mtoto mzuri kama huyu duniani”
Mariam akapumua kidogo maana alihisi kuna jambo baya litaongelewa, basi Mariam akatabasamu na kujibu,
“Asante”
Kisha yule mtu akaendelea kusema,
“Yani hongera sana, una mtoto mzuri sana hadi raha kumuangalia, hongera sana mtoto wako ni mzuri sana”
Hapa akajibu mtoto sasa,
“Hakuna mtoto mbaya duniani”
Yule mtu aliamua tu kukaa kimya kwani aliona hapa tena habari inakuwa nyingine na wala hawakuongea mpaka wakina Mariam waliposhuka na kuondoka zao.
Ilibidi Juma apitie kwenye vibanda wanavyokaanga viazi na ndizi na kununua kisha wakarudi navyo nyumbani kwao.

Leo wakiwa nyumbani, hakuwepo mama Shamimu maana tayari alishaondoka basi mtoto akasema,
“Ila shangazi hajaniaga jamani!”
Juma alijikuta tu akimuhurumia dada yake na kumuombea msamaha kwa mtoto wake,
“Naomba umsamehe shangazi yako, alighafirika tu naomba umsamehe sana”
“Mpigie simu na aniombe msamaha mwenyewe”
Basi Juma alimpigia simu dada yake ambaye baada ya muda mfupi tu alipokea kisha Juma akamwambia,
“Dada, naomba umuombe msamaha mtoto maana umeondoka bila ya kumuaga”
“Uwiiiii nilijisahau, naomba tu nimuombe msamaha”
Juma akampa ile simu mtoto sasa ambaye moja kwa moja alianza kuongea,
“Kwanini shangazi umeondoka bila ya kuniaga?”
“Naomba unisamehe mwanangu, nisamehe sana nao,ba unisamehe”
“Utakuja lini tena kunitembelea?”
“Nitakuja mwanangu, nitakuja tu hakuna tatizo”
“Lini sasa?”
“Baada ya miezi mitatu”
“Kheeee utakuja tena na hilo begi lako kubwa?”
“Hapana, nitakuja tu kuwasalimia na kurudi, naomba unisamehe sana”
Kisha yule mtoto alikata simu na kumuangalia mama yake ambapo alimuuliza,
“Mama, shangazi ameishi hapa kwa muda gani?”
“Mmmmh sijui miezi miwili sijui mitatu”
“Haya sawa”
Mtoto hakusema kitu kingine chochote kwahiyo walikuwa kimya tu wakiendelea na mambo mengine huku Anna akikumbusha kuhusu yale mahindi maana tayari yalikuwa ni makubwa, basi walienda kuchuma na kuchemsha kisha walianza kuyala huku wakiyasifia kuwa ni matamu, basi mtoto akasema,
“Mama, wewe ndiye tunayepaswa kukushukuru maana umelima mwenyewe, umepalilia mwenyewe na umeyahudumia haya mahindi mwenyewe”
Mariam alikaa kimya tu kwani kila akifikiria kuwa yeye ndiye aliyekuwa akilimishwa kiuchawi aliumia sana, na kufanya ashindwe kusema lolote wala kufanya lolote.

Kwasasa, Juma aliamua tu kushinda nyumbani kwake yani alikuwa haendi kwenye shughuli zake kabisa kwahiyo kila siku alikuwa akishinda nyumbani.
Siku hii alienda kununua samaki maana Mariam alimuagiza samaki, basi alipokuwa kule kwenye samaki ndipo alipomuona na yule muuza samaki ambaye huwa anpitisha mitaani, basi akamuita ila huyu muuza samaki mara nyingi huwa hamfahamu Juma, kwahiyo alisogea tu kuongea nae,
“Vipi kijana hujambo?”
“Sijambo kabisa mzee wangu, shikamoo”
“Marahaba, wewe ni kijana mdogo sana. Nilipata taarifa kuwa kuna nyumba sijui wanafuga majini ulienda kuuza samaki ni nyumba gani hiyo?”
“Mmmmh ni nyumba moja hivi ipo kama unapandisha kidogo kilima, yani ipo kwa juu juu hivi halafu eneo lile kama imejitenga maana ipo peke yake”
“Kwahiyo ana majini?”
“Ndio, anafuga majini yule kwakweli niliogopa sana hadi leo ile njia sipiti”
“Wewe ulijuaje kuwa ni majini?”
“Yani mimi mzee nimechanjiwa kwahiyo vitu ambavyo sio vya kawaida naviona mzee, yule mama mwenye nyumba huwa namuuzia samaki tena mara nyingi tu nishamuuzia, nashangaa siku hiyo aliita mtu amletee bakuli la kuwekea samaki kutoka ndani, khaaa akatoka jini mdogo na mkubwa”
“Khaaaaa!!”
“Halafu yule mama pale nje alianza kucheka pia, tena kile kicheko cha majini majini”
“Duh!! Pole sana, ukafanyaje sasa?”
“Asante, yani nilikimbia hata hela sikudai wala nini. Nilikimbia na sehemu ya kwanza nilisimama kwa mzee mmoja ambaye ni mjumbe wa mtaa na nilimueleza kila kitu kuhusu nilichokiona pale kwenye nyumba, ndipo wengine walitokea na kusema kuwa mzee wa hiyo nyumba anafuga misukule, yani kadri watu wanavyomsalimia ndivyo watu hao wanavyokufa, anayemsalimia mara nyingi ndio muda wake wa kufa unakuwa karibu halafu anageuka na kuwa msukule wa huko mzee, kwakweli niliogopa sana”
“Pole sana kijana”
“Asante”
“Nashukuru kwa taarifa, nitaifanyia kazi”
“Huwezi mzee, mtaa wote huu umeshindwa, nasikia walitaka kuchoma nyumba moto, khaaa mvua ya mawe ilipotokea ni balaa tena iliambatana na upepo mkali sana halafu badae ilinyesha mvua ya kawaida hadi panakucha, kwakweli pale pana majini, kuna njia pale karibu ila kwasasa hakuna mtu anyepita kila mtu anapaogopa”
Juma alimshukuru yule kijana na kuachana nae, kwakweli alijiuliza moyoni bila ya jibu, lile jambo la kuona anaogopewa kiasi kile mtaani lilimpa mashaka sana yani anaogopewa bila kujulikana maana sio wote wanaomjua.

Leo Mariam na Anna, alikuwa akiongea nae na kumwambia kuwa amuelekeze kupika ila isiwe kila siku anapika yeye,
“Yani Anna, hayo maswala ya kunifanya nilale halafu unifanyishe kazi siyataki kwakweli, naomba tu niwe nakuelekeza namna ya kupika. Ndio mama yako alikulea vibaya, ila isiwe tatizo la kututesa sisi wengine tusiohusika, naomba uje jikoni niwe nakufundisha hadi ujue kupika”
Kwahiyo Anna alienda jikoni ambapo Mariam alianza kumuelekeza namna ya kupika ila kila alipokuwa akimuelekeza aliona anajiwa na uzito sana kwenye mikono yake hadi aliamua kumfokea Anna,
“Yani nakuelekeza hapa hapa unaniroga! Mbona huna akili wewe janmani, akili zako ni vipi Anna, mbona unafanya mambo ya kijinga?”
“Samahani dada”
“Napoteza muda wangu kukuelekeza hapa kwa faida yako mwenyewe, ila wewe hutumii akili yani upo kutumia sijui vitu gani eti unaniroga mikono khaaa sijapata kuona mtoto mwehu kama wewe Anna jamani!”
“nisamehe dada”
“Nikusamehe nini mwehu wewe, haya kaa chini hapo uanze kupika yani nitakuwa nakuelekeza kwa mdomo tu na ukase mkono hapo jikoni”
Mariam aliamua kuinuka na kumuacha Anna akae jikoni huku akimuelekeza, yani kiukweli kwasasa Mariam hakumtaka kabisa Anna ila hakuwa na jinsi sababu ya mtoto wake.

Walipomaliza kula, Juma alikaa na familia yake na kuanza kuwaeleza yale ambayo aliongea na yule muuza samaki kisha aliwauliza,
“Jamani, kati yetu kuna jini?”
Mtoto akauliza pia,
“Kwani nani unamuona ni jini hapa baba?”
Juma alimuangalia huyu mtoto na kusema,
“Mimi sijui ila nimueuliza tu sababu ya haya mambo ambayo yametokea na jinsi ambavyo muuza samaki amesema”
Yule mtoto akasema,
“Hakuna jini hapa baba, labda angesema kamuona mchawi ambapo moja kwa moja jibu lingekuwa ni Anna tu hapo bila wasiwasi wowote”
Mariam akasema,
“Au Anna ni mchawi halafu ni jini pia maana mtu anawezaje kumchukua mwenzie wakati amelala na kwenda kumfanyisha kazi! Kiukweli Anna hadi unaniogopesha jamani, ni bora hata ungebaki kule kule”
“Nisamehe dada”
Yani Anna kwa kipindi hiki alikuwa akitumia zaidi neno nisamehe kuliko neno lingine lolote lile, walikuwa wakimuangalia tu ila walikuwa wakimchukia sana.

Zilipita kama wiki nne ambapo Mariam alianza kujihisi tofauti na kujihisi kuwa huenda akawa ana mimba maana aliona dalili zote za kuwa hivyo ila alitaka uhakika zaidi kwa siku hiyo kwenda hospitali.
Alimuaga kawaida tu mume wake kuwa anaenda hospitali maana siku hii hakutaka hata kusindikizwa na mume wake.
Basi akajiandaa na moja kwa moja kwenda hospitali kupima, na alipopima tu akaambiwa kuwa ni mjamzito basi alipotoka tu pale alimpigia simu mama mkwe wake ili kumuambia habari ile ingawa alijua wazi kuwa mama mkwe wake lazima achukie,
“Mama, nina mimba tena”
“Kheee Mariam, una wazimu wewe au ni kitu gani? Si tumekwambia hadi tufanye tambiko”
“Najua mama, sasa hilo tambiko hadi lini? Maana kila siku unasema hivyo hivyo, mimi nina mimba tayari”
“Sasa hivi hata ukibeba hiyo mimba kwa miaka mitatu usinisumbue maana mimi nimekwambia cha kufanya hutaki”
“Sasa mama ndio ishatokea nifanyeje sasa?”
“Unadhani nitakwambia nini hapo? Eeeeh nimekumbuka, sib ado mnaishi na yule mdada mchawi au ndio ulimuacha kwenye ile nyumba?”
“Alikataa mama, tunaishi nae bado”
“Basi nenda kamwambie kuwa una mimba, najua atakutoa tu hiyo mimba, halafu akishakutoa uende hospitali ukaweke kitanzi huko usituletee balaa kwenye ukoo sie”
“Mmmmh mama! Hutaki wajukuu kabisa”
“Wajukuu wa kishetani nani anawataka? Sitaki ushetani katika maisha yangu, hao watoto wa kishetani bakini nao wenyewe, mimi siwataki”
Ile simu ilikatika kisha Mariam akatabasamu tu na kusema,
“Kheee yani huyu mama mkwe jamani loh!! Ila huwezi jua pengine huyu mtoto anaweza kuwa bora mmmh!!! Ngoja nikifika tu nyumbani niseme kuwa nina mimba nione usiku wake itakuwaje!”
Mariam alijisemea kisha akarudi nyumbani kwake.

Mariam alipofika tu, kitu cha kwanza kabisa aliwaita wote kisha akawa pale kama anamwambia Juma ila ujumbe ulikuwa unafika kwa wote maana wote walikuwepo pale sebleni,
“Juma mume wangu, nina mimba. Karibia tutampata mdogo wake mtoto wetu”
Juma alitabasamu na kufurahi sana, yani akajikuta amesahau kabisa kama kuna mimba iliharibika mule ndani sababu mule ndani wanaishi na mchawi.
Juma alikuwa tu akimpongeza mke wake na kumlaumu kwenda peke yake hospitali,
“Ilitakiwa twende wote jamani Mariam”
“Usijali hakijaharibika kitu”
Ilikuwa ni siku ya furaha tu kwao, ni Mariam pekee ambaye kwa muda huo alikuwa na wazo kuwa Anna ana uwezo wa kuiharibu ile mimba.
Usiku wakati wa kulala, yani Mariam alipopitiwa na usingizi tu alihisi kama kuna mtu anamkandamiza tumboni halafu kama alitokea mtu mwingine na kumsukuma yule mtu halafu akasikia,
“Mama, amka”
Aliposhtuka alishangaa kumuona mtoto wake akiwa pembeni yake.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
Story ya MWANAUME WA DAR inaendelea leo.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni