Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 27

MTOTO WA MAAJABU: 27

Mara wale watu wa nje wakawasha moto na kuanza kushangilia pale nje ila mtoto alianza kucheka na alicheka sana, gafla ilianza mvua ya ajabu tena ilikuwa ni mvua ya mawe na kusambaratisha watu wote pale nje.
Pale ndani wote walikuwa kimya, na ile mvua ilidumu kwa takribani robo saa kisha ikaanza mvua ya kawaida, yani Juma alikuwa akimuangalia tu huyu mtoto wao bila kujua ni kitu gani cha ziada kipo kwa huyu mtoto wao ambapo mtoto aliwaambia,
“Endeleeni kulak wa amani, mnaogopa nini sasa? Acha waone nyumba nzima ni wachawi na majini ili watuogope kabisa, wasitufatilie wala kutusogelea”
Walimuangalia huyu mtoto na hakuna mtu ambaye aliweza kumuhoji zaidi zaidi walipakua chakula tena na kuanza kula maana lile janga la wale watu kuzingira nyumba lilifanya kila mmoja kusitisha lile zoezi lao la kula.
Walipomaliza kula, ndipo mtoto alipowaambia kuwa wanaweza kulala sasa, ila ile mvua haikukatika wala nini yani iliendelea kunyesha tu, na hakuna aliyehoji pale ndani kwao kwani kila mmoja alienda kulala.
Leo mama Shamimu aliingia chumbani kwake huku akiwa na uoga sana, kwani hakujua hatma yake kwenye hiyo nyumba, alitamani hata itokee afukuzwe tu kwenye nyumba hiyo ila haikuwa hivyo wala nini.
Alikuwa na uoga sana, hata lala yake ya leo ilijaa uoga mwanzo mwisho.

Mariam na Juma wakiwa chumbani wakajikuta wanaanza kujadili kuhusu mtoto maana yale mambo hayakuwa ya kawaida,
“Hivi Juma unamuona mtoto wetu kuwa wa kawaida kweli?”
“Mmmh! Hapana mtoto wetu sio wa kawaida yani sio wa kawaida kabisa”
“Unahisi mtoto wetu ni nani?”
“Sijui, yani sihisi chochote”
“Ila mimi nahisi kitu sema naogopa kusema”
“Kwanini unaogopa?”
“Wewe, tu anawaletea mvua ya mawe ambayo haijawahi kunyesha kwenye mji huu halafu utasemaje hapo! Angalia sasa, mvua ya kawaida hadi sasa bado inanyesha, si balaa hili yani huyu mtoto sio wa kawaida kabisa ila vingine siongei”
“Basi mke wangu tusiongee sana, tulale tu kwasasa”
Waliamua kulala tu kwa muda huo, kwani mambo yaliyoendelea hawakuyaelewa kabisa.

Kulipokucha, Juma aliamka kama kawaida na kujiandaa ila kwakweli alikuwa anaogopa hata kutoka nyumbani kwake, alikuwa akijiuliza kama ni sawa kwa yeye kutoka nyumbani kwake na kwenda kwenye shughuli zake. Basi mtoto alipotoka na Anna ndipo alipotaka kumuuliza ila alijikuta kama anashindwa maana alijikuta tu akiwa anamuogopa huyu mtoto ila mtoto alimwambia,
“Baba, nenda tu kazini hamna kitakachokupata”
Juma alimuangalia mtoto na kumwambia tu,
“Asante”
Kisha akaenda chumbani na kutoka na mwamvuli kwani mvua bado ilikuwa inaendelea kunyesha, alipokuwa anatoka mtoto alimuuliza,
“Unaenda wapi na mwamvuli baba?”
“Kuna mvua nje”
“Aaaah kumbe bado inanyesha, acha mwamvuli hiyo mvua inakatika muda sio mrefu”
Juma akaacha mwamvuli na kutoka, na kweli baada ya muda kidogo tu ile mvua ilikatika, kwakweli hili swala lilikuwa la ajabu sana kwa upande wa Juma.

Mama Shamimu akiwa bado chumbani aliamua kuchukua mabegi yake ili akawaage apate kuondoka, basi alitoka sebleni na kumkuta Anna na yule mtoto wamekaa basi akawaam bia,
“Jamani mimi nataka kuondoka”
Muda huo Mariam nae alikuja na kumuangalia wifi yake na kumuuliza,
“Wifi jamani, unataka uende halafu mimi uniache na nani?”
“Khaaa jamani, si unabaki na mwanao na mdada wako wa kazi!”
“Jamani, wifi nakuomba usiondoke”
“Hapana, hakuna anayeweza kubadili fikra zangu”
Mariam akamuangalia mtoto wake na kumwambia,
“Tafadhari naomba asiondoke”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Leo nimefurahi sana, kumbe mama unaniamini eeeh!! Sasa shangazi na wewe unataka kuondoka kwenda wapi?”
“Nataka kwenda nyumbani kwangu”
“Nyumbani kwako ulisema mtaa mzima wamejaa wachawi, je utakuta wachawi wameisha? Wachawi huwa hawaishi maana hata akifa mama mtu basi huwa wanawaachia watoto wao, mfano mzuri ni huyu Anna, mnadhani uchawi kautoa wapi? Kwa mama yake, kwabhiyo uchawi huwa hauishi, sidhani huko nyumbani kwako kama kupo sawa!”
Mama Shamimu akajitetea,
“Ila nilikuwa nataka kwenda kuangalia mji wangu na mali zangu nione mambo yanaendaje pale”
Ila mtoto kwa muda huu akatoa kauli moja tu,
“Shangazi, hakuna kwneda popote bila ruhusa yangu”
Mama Shamimu alichukia sana na kurudisha mabegi yake ndani, alikuwa na hasira mno juu ya yule mtoto alichokuwa anafanya.
Ila badae, mama Shamimu alimuita Mariam chumbani kwake na kuanza kuongea nae,
“Ila wifi, kumbe unafurahia mambo haya?”
“Jamani, mimi nafurahia saa ngapi?”
“Kwanini umwambie mtoto anizuie?”
“Ila hebu kuwa na huruma hapo wifi yangu jamani, Anna mchawi, mtoto wangu anafanya mambo ya ajabu halafu kweli unataka kuniacha katika hali kama hii jamani wifi yangu! Hebu nihurumie jamani, usitake kunifanyia hivi nakuomba”
“Ila nimemkumbuka mwanangu Shamimu”
“Naelewa wifi ila naomba unisaidie kwa hili, nakuomba wifi yangu, nakuomba sana. Usiniache peke yangu”
Yani Mariam alikuwa akionyesha sura ya huruma sana, ila Mariam alipoondoka mama Shamimu aliamua kumpigia simu mama yao ili kumueleza yale mambo yaliyokuwepo,
“Kheeee mlitaka kuchomewa nyumba?”
“Ndio mama, wananchi wa hapa wote wamechukia wanasema tunaishi na majini ndani”
“Hivi Juma anafikiria nini kuhusu mambo hayo jamani! Juma ni mwanaume lakini kwanini anashindwa kufikiri kama mwanaume?”
“Hata mimi namshangaa mama”
“Ngoja nimuite ili niongee nae”
Mama Shamimu alikata simu ya mama yake, ila kiukweli hakupenda tena kuendelea kuishi hapo kwenye nyumba ya Juma.

Juma leo aliwahi kutoka kwenye shughuli zake maana mama yake alimpigia simu kwahiyo moja kwa moja aliunganisha kwao, ingawa kulikuwa na umbali kiasi ila huwa haoni tatizo kwenda kwao kuzungumza na mama yake kuhusu mambo yanayoendelea kwenye familia yake.
Alimkuta mama yake yupo akimsubiri, na moja kwa moja huyu mama alitaka maelezo ya kuchomewa nyumba ambapo Juma alimueleza ilivyokuwa hadi mwisho kisha mama Juma akamuuliza juma,
“Hivi wewe yule mkeo si mjamzito wewe?”
“Hapana mama, ile mimba ilitoka”
“Ooooh asante, Mungu ni mkubwa kwakweli maana yalikuwa ni mauzauza mengine hayo. Haya sasa tuongelee hayo mauza uza ya nyumbani kwako”
“Ndio kama hivyo mama”
“Kwanini msiamue moja, yani wote mje huku nyumbani ila hayo majini yenu ndio myaache huko?”
“Kwanza mama, haiwezekani kumuacha yule mtoto pale nyumbani, yani kama tukija huku ni lazima tuje nae maana yule mtoto hawezi kukubali”
“Ila Juma mwanangu kuna kitu nimefikiria ila usichukie”
“Niambie mama ni kitu gani, sitachukia wala nini mama yangu”
“Ni hivi, yule mkeo Mariam nahisi kabisa kuna jambo alilifanya pindi akiwa na mimba ya yule mtoto wenu au huenda ile mimba aliipata kwa waganga huko, unajua kipindi umemuoa ndio kipindi ambacho ulikuwa unahitaji mtoto kwa sana, kwahiyo inawezekana kabisa mkeo alienda kwa waganga huko, tena inawezekana alipelekwa hadi kwa mashetani na majini ndio kapatia mimba ile huko”
“Mmmmh! mama”
“Usigune tu, bali tumia muda wako umuulize vizuri mke wako ni kitu gani alifanya kipindi anasaka mimba ya yule mtoto, muulize kwa makini sana kitu alichofanya mke wako”
“Kama akisema hakufanya kitu?”
“Akisema hivyo ujue wazi ni muongo, hakufanya kitu wakati mambo ni wazi kabisa yanaonekana, mtoto yule ni uthibitisho tosha kuwa mkeo alifanya mambo ya ajabu. Kumbuka hadi kujifungua kwenyewe nimempelekea dawa akaogee, kumbuka mtoto yule kafanya hospitali wote wakimbie, kumbuka mtoto yule hakuna chanjo hata moja aliyopata sababu ya mambo ya ajabu aliyoyafanya hospitali. Muulize mke wako ili tujue kuwa tunaanzia wapi kwenye mambo haya kwakweli.”
“Mmmmh!! Sawa mama, nitamuuliza ingawa najua wazi hakuna jambo la tofauti ambalo mke wangu amelifanya. Ila sijui maana wanawake wana siri nyingi sana”
Juma aliongea na mama yao ambapo mama yao alimsisitiza kuwa wanatakiwa kuhama pale wanapoishi maana yule mtoto atawaletea mabalaa.

Leo usiku Juma aliamua kuongea na mke wake kuhusu kile ambacho mama yake alisema ila alipomuuliza Mariam alikataa kabisa,
“Sasa mimi niende kutafuta mtoto kwa mganga kwasababu gani? Kwani nilikuwa na tatizo la kizazi mimi? Kwa waganga tumeanza kwenda baada ya mimba kupitiliza muda wake, hapo kweli tumeenda kwa waganga na wala sikuwa peke yangu bali tumeenda wote ili kutafuta suluhisho la mimi kujifungua, hapo ndio nikanywa dawa za kila aina, nikafanya mambo ya kila namna, hapo ndipo nilipokuwa na tofauti ila mimi sikuwahi kwenda kwa mganga yoyote hapo kabla.”
“Ila Mariam ni bora ungekuwa mkweli ili tujue cha kufanya”
“Halafu mimi nahisi mama yako ndiye aliyeniroga”
“Duh!! Mama yangu tena amekuwa mchawi jamani Mariam! Kweli mama yangu tena aliyehangaika kukutafutia dawa ili ujifungue ndio kawa mchawi?”
“Ndio, huoni dawa zote zilidunda mpaka dawa aliyotafuta yeye? Usimtetee mama yako Juma, mimi nina uhakika asilimia zote kuwa mama yako ndiye aliyesababisha haya yanayoendelea sasa. Ila nadhani hata yeye hakuelewa kama anatengeneza kitu cha ajabu ila kitu alichokitengeneza ni kibaya sana”
“Hebu nyamaza Mariam, tulale tu kwasasa maana naona umeanza kunikoroga, yani mama yangu kawa mchawi dah!”
Juma aliamua tu kulala, kwa muda huo hata Mariam na yeye alilala.

Leo wakiwa wamekaa baada ya kazi zote, pale sebleni yule mtoto alimuangalia Mariam na kumuuliza,
“Mama, unaujua uchawi wewe?”
Mariam alikaa kimya hadi mtoto alimuuliza tena,
“Mama, unaujua uchawi wewe?”
“Mmmh ! Kiasi”
“Unaujuaje?”
“Mmmmh siujui ila mtu kama hivyo nasikia kwamba mtu Fulani mchawi na mtu Fulani mchawi basi”
“Sasa una uhakika gani kama bibi yangu ni mchawi?”
Hapa Mariam alijikuta katoa mimacho tu, kisha yule mtoto akamwambia Mariam,
“Na uache tabia yako ya kusema kuwa bibi yangu ni mchawi”
Yani Mariam alikaa kimya kabisa kwani hakutegemea kama huyu mtoto angemwambia hivi.

Leo wakati Juma akitoka kwenye shughuli zake, ndipo alipokutana na yule jirani ambaye alimpa taarifa za kwenye mtaa kuwa wanataka kuchoma nyumba yake huku na wenyewe wakiwa ndani, basi yule jirani alimsalimia na kuanza kumwambia,
“Hivi lile tukio la siku ile ulilishuhudia au?”
“Tukio gani?”
“La kuchoma nyumba yako”
“Mimi nilikuwa ndani yani ya nje siyajui kwakweli”
“Yani siku ile watu walikuja mapema sana kwako na kumwagia petrol na kuchoma nyumba uwiiii sijui ikawaje ile mvua ya mawe na upepo sijui vilitokea wapi jamani, unajua watu waliumia hatari waliumia sana na wengine bado wapo nyumbani kwao wakiuguza majeraha”
“Vipi wewe hukuhumia?”
“Hapana, mimi sikuhumia”
“Au hukuja?”
“Nilikuja, unajua nilikuwa na uchungu hatari. Nikasema nakuja kushuhudia hadi mwisho itakavyokuwa, basi ile mvua ilipoanza na upepo mkali ikawa ngumu kabisa na kufanya kila mtu akimbie hovyo hovyo ila huwezi amini nilikimbia hadi nyumbani kwangu na sikulowa wala nini”
Juma alimshangaa yule jirani yake na kumuuliza,
“Hukulowa?”
“Ndio, hata mke wangu alinishangaa kuwa imekuwaje sikulowa kabisa”
“Khaaaa kumbe una mke!”
“Ndio, kwani hukujua kama mimi nina mke?”
“Hapana, nimeuliza tu”
“Mmmmh au sababu nimekwambia umbea? Yani hapa mtaani huwa wanasema sana kuwa mimi mbea kama mwanamke, nashangaa na wewe unashangaa kuwa mimi nina mke! Mimi nina mke ndio na watoto wawili, wamefanana na mimi hatari”
“Hongera sana kwa hilo”
“Asante, ila bado wanaendelea kupanga mipango mingine kuhusu wewe nimewasikia. Kuwa makini sana ndugu yangu, mimi sio mbea kivile ila tu huwa nikiona kuna jambo la kumuumiza mtu ndio huwa najikuta nikishindwa kuvumilia na kusema hilo jambo. Naomba unisamehe tu kama nimekukwaza”
“Hapana hujanikwaza, kwanza umenisaidia sana”
Juma aliagana na huyu jirani yake na kuondoka zake.

Juma alipokuwa nyumbani kwake, aliwasimulia kuhusu yule jirani kitu alichomuambia ila mtoto akamsema Juma,
“Sasa, baba kwanini umshangae yule kuwa na mke wakati amekwambia mambo mazuri ya kukusaidia wewe mwenyewe!”
Juma alishangaa na kumuangalia mtoto wake, kisha akamuuliza,
“Kwani ulikuwepo kwenye mazungumzo yetu?”
Mtoto alitabasamu na kumwambia baba yake,
“Kwasasa, mimi nimekuwa na kadri ninavyozidi kukua ndivyo uwezo wangu unavyoongezeka, kwahiyo kwasasa kuwa makini sana kwa chochote unachokisema na chochote unachokifanya”
“Mmmmh!!”
Mtoto akaendelea kuongea,
“Halafu kuhusu wale watu kukubunia mbinu nyingine, usiwe na shaka maana hakuna kitu kama hiko. Hakuna watakachoweza kufanya wala nini kwahiyo msiwe na wasiwasi wowote ule”
Wote walikaa kimya wakimuangalia tu, kisha kila mmoja kuinuka na kwenda kupata chakula cha usiku.

Wakati Juma kaenda kulala, akapigiwa simu na mama yake na kuanza kuongea nae ambapo mama yake alitaka kujua kama Juma ameongea chochote na mke wake,
“Umemuuliza mke wako?”
“Amekataa mama”
“Anakataa bure, lakini kuna mahali ameenda huyo”
“Ngoja nikupe uongee nae”
Basi Juma alimpa Mariam simu aongee na mama yake, ambapo yule mama alimuuliza Mariam,
“Kabla ya kupata mimba ya huyo mtoto wenu ulienda kwa mganga gani?”
Mariam alichukia kidogo kwa lile swali na kumwambia,
“Halafu mama nakuheshimu sana, tena nakuheshimu sana, ungejua huyo mtoto bunayemjadili anavyokupenda na kukuheshimu basi hata usingehangaika kuuliza maswali yasiyokuwa na kichwa wala miguu”
Kisha Mariam aliikata ile simu na kumtaka Juma walale, yani Juma alikuwa akimsikiliza sana Mariam na kumfanya aache simu pembeni bila kumpigia tena mama yake na kulala tu kwa muda huo.

Leo wakati Juma yupo kazini, rafiki zake wakakumbusha kuhusu swala la mdada wa kazi wa Juma, kisha walimuuliza Juma,
“Vipi yule mdada mchawi ulishamuondoa?”
“Hapana, bado”
“Kwanini sasa?”
“Hata sijui ni jinsi gani nitamuondoa”
“Hebu acha ujinga Juma, sisi tulishakupa mbinu. Leo tunaenda wote nyumbani kwako kumuondoa”
“Hapana, nawaomba tusiende leo, nitawaambia siku ya kwenda”
“Sisi tunaenda na wewe leo leo”
Juma aliwakatalia kabisa ila rafiki zake waling’ang’ania.
Juma ilibidi awatoroke tu muda wa karibia na kuondoka, ila kuna mmoja alimuona na kuwatonya wengine hivyo walianza kumfata Juma yani Juma alipokuwa anafika kwake aliwaona tayari wale rafiki zake wapo nyuma yake ila kabla hajasema kitu, yule mtoto wa Juma alitoka nje na kusimama mlangoni kisha akawaambia wale rafiki wa Juma,
 “Ishieni huko huko” 

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile.
Story ya MWANAUME WA DAR inaendelea leo.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni