MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 26

MTOTO WA MAAJABU: 26

Mama Shamimu alikuwa wa kwanza kutoa pole na kufanya Anna nae atoe pole ila mtoto akasema,
“Anna, hebu tuonyeshe jinsi gani umemuua mdogo wangu?”
Anna alishtuka sana kuambiwa vile.
Yule mtoto akamuuliza Anna,
“Sasa unashtuka nini? Ulidhani watu hawatajua? Ni kweli wote wanaweza wasijue lakini sio mimi, najua kila kitu. Haya sema hapa ni kwanini umemuua mdogo wangu?”
Anna akajifanya kulia ili aonewe huruma, yani Mariam alichukizwa sana ukizingatia na yale ya yeye kufanyishwa kazi zote mule ndani na Anna, ndio akazidi kupatwa na hasira,
“Yani Anna, kukulea kote huku kama mdogo wangu bado umeenda kunifanyia vitu vya ajabu kiasi hiki! Kweli Anna wewe Anna”
Mariam akainuka na kuanza kumpiga Anna yani alikuwa na hasira nae sana, na alimpiga sana hadi Anna alianza kutokwa na damu na hakuna hata mmoja mule ndani aliyekuwa akimtetea kwani uchungu wa jambo lile alikuwa nao Mariam mwenyewe.
Baada ya kumpiga sana, ndipo mtoto akasema,
“Sasa mama inatosha, inatosha mama. Baba mzuie mama inatosha”
Ilibidi Juma amtulize mke wake ila Mariam alikuwa na hasira sana,
“Yani umenitumikisha ndani ya nyumba yangu mwenyewe, haitoshi umeenda kunitoa mimba mchawi mkubwa wewe, na humu ndani unaondoka Anna, tena usiku huu huu Anna unaondoka, sikutaki humu ndani”
Mtoto akasema,
“Tulia mama, naomba utulie. Anna hawezi kuondoka maana muda wake wa kuondoka ni bado”
Mariam alimjibu huyu mtoto yani leo hakuogopa wala nini kumjibu huyu mtoto,
“Ni nani atakayeweza kuishi na Anna humu ndani! Ni na ni atakayeweza kuvumilia matendo kama hayo? Niogope kubeba mimba eti Anna atanitoa!”
“Mama, tulia. Usijali kitu, huyu Anna kwasasa hatothubutu kukushika kwa chochote kile. Hakuna atakachoweza juu yako mimi ndio nimesema”
Juma akaamua kumwambia huyu mtoto pia,
“Basi tunaomba na sisi huyu Anna asitushambulie”
Huyu mtoto alitabasamu na kusema,
“Hakuna wa kukushambulia baba yangu, sio Anna tu wala sio yeyote yule”
Mama Shamimu akaona kuwa atabaki mboga mwenyewe, basi akapiga magoti na kusema,
“Na mimi mtoto mzuri, nisaidie mimi shangazi yako”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Kumbe kwenye matatizo huwa ushangazi unafanya kazi eeeh! Usijali shangazi yangu, huyu Anna hatokushamulia.”
Kisha huyu mtoto akamgeukia mama yake na kumwambia,
“Mama, nakuomba tu jambo moja. Acha uvivu, sitaki tena uendelee na uvivu mama yangu”
Kisha alimgeukia Anna na kumtaka kuwa waende wakalale, yani Anna aliogopa sana ila aliamua tu kwenda kulala na huyu mtoto yani liwalo na liwe.

Mariam alikaa chumbani na mume wake akilalamika sana, yani aliona ni balaa kubwa sana kumleta Anna katika maisha yao,
“Yani mume wangu, mimi ni mjinga sana. Nilikuwa najidai hata mfanyakazi akilalamika namwambia kuwa ondoka tu maana nitapata mwingine, ni kweli niliamini kuwa watu wanashida na kazi ila sikujua kuwa watu hawapendi kutumikishwa, hawapendi kuteswa huwa wanafanya tu sababu ya shida. Sasa nimeenda kumpata Anna ambaye niliona ni mchapakazi kumbe ananifanyisha kazi mwenyewe!”
Mariam akainama chini na kulia kisha akasema,
“Ulikuwa ukiniambia mume wangu ila nikapuuzia, ona sasa Anna kumbe ndio kashiriki kuitoa ile mimba yangu!”
Juma akamuangalia Mariam na kumuuliza,
“Kwahiyo kwasasa upo tayari kuzaa na mimi?”
“Ndio nipo tayari, kwanini nisizae na wewe wakati wewe ni mume wangu?”
“Aaaah nimefurahi sana kusikia hivyo mke wangu, nimefurahi sana. Mwanzoni ulikuwa hutaki kuzaa na mimi sababu ya mimba iliyokaa miaka miwili”
“Ni kweli ile mimba ilinichanganya sana, ila huyu mtoto mbona tumeshindwa kuwa mbali nae! Na unajua anatulinda huyu!”
Juma alicheka na kusema,
“Kheeee leo ndio unasema kuwa anatulinda jamani Mariam! Ila na mimi sioni baya la mtoto, tumpende tu na atatusaidia na mengi”
Wakajikuta wakijadili mambo mengi sana ya familia yao hadi walipoenda kulala.

Juma aliwahi kutoka kazini leo, na moja kwa moja alimtafuta mama Rose ilia pate kuongea nae kuhusu Anna, kwani kwa yale ya jana aliona bado kuna umuhimu wa kumuelewa zaidi Anna, na kwanini mtoto wake anaelewana na Anna.
Alienda kukutana nae pale pale ambapo huwa anakutana nae siku zote,
“Yani kilichonifanya nije, ni kumzungumzia huyo huyo mtoto Anna”
“Khaaa bado una mambo tu ya hako katoto kachawi!”
“Yani huwezi amini, yule mdogo wako amemtoa mimba mke wangu”
“Kheeee yani mkeo alikuwa na mimba halafu Anna akajua loh! Pole sana, kale katoto ni kachawi sana, pole sana”
“Kwahiyo kula mimba ndio zake?”
“Ngoja nikueleze mimi vizuri ili ujue ni kwanini namchukia ingawa ni mdogo wangu, nilikwambia kuwa ameua ndugu zetu mapacha wawili. Hilo halitoshi, ni hivi mimi nilikuwa naishi na kale katoto maana nilikuwa nakaonea huruma kataenda wapi? Pale unavyomuona hawezi kufanya kazi yoyote, ndio kalelewa hivyo na mama. Kwahiyo hakuna kazi ambayo Anna anaifanya, sasa mimi nikawa naishi nae vizuri tu kama mdogo wangu huku nikimuelekeza baadhi ya kazi na mambo ya kufanya, nikabeba mimba ya kwanza, kakaila, nikabeba ya pili kakaila….”
Juma alimkatisha kidogo na kumuuliza,
“Kakaila ndio nini?”
“Yani kamekula mimba zangu hizo, kameziondoa nikawa sina mtoto. Nikaja kupata mimba nikafanya siri hadi nikajifungua, Anna akala mtoto wangu akiwa mchanga, ndio nikapata mimba hiyo mtaalamu akaniambia kuwa mtoto nimuite Rose, jina la mama maana mama yetu alikuwa akiitwa Rose, shida kubwa ni Anna asiweze kumtani mwanangu na hapo ndipo Anna alipoua wale mapacha, nikaamua kumfukuzia mbali Anna na kuanza kuishi maisha yangu, ndio nina mtoto mwingine kwasasa sababu Anna hayupo katika maisha yangu, yule mtoto ni mbaya sana, hafai kabisa sijui kwanini mnaendelea kuishi nae. Fukuzia mbali huko”
“Dah! Pole sana, kweli ni mchawi mdogo wako, kwa hayo maelezo tu ni wazi Anna ni mchawi wa wachawi ila pale kwangu nitamfukuza tu”
“Mfukuzeni, aondoke zake. Mnakaa na lijitu chawi kama lile la kazi gani? Sipati picha mama angekuwepo uwiiii dunia ingegeuka juu chini chini juu maana mama yangu alikuwa ni hatari sana”
Juma alimsikiliza kwa makini huyu mama Rose, kisha alimuaga na leo mama Rose aliamua kumsindikiza Juma.
Njiani kuna binti ambaye Juma alishtuka kumuona, ila yule binti na mama Rose walionekana kufahamiana kwani walikumbatiana kwa furaha,
“Karibu sana nyumbani kwangu”
“Asante dada, nimeona leo nije kukutembelea”
“Jamii yote imenitenga, umebaki wewe tu katika maisha yangu!”
“Usijali dada tupo pamoja”
Juma alishindwa kuvumilia na kumuuliza mama Rose,
“Kwani nani huyo?”
“Aaaah huyu ni mdogo wangu anaitwa Salome”
Mama Rose alipojibu tu hivyo, moja kwa moja aliondoka na Salome, yani Juma alibaki akishangaa tu.

Leo Mariam akiwa amekaa ndani alimsikia muuza samaki akipita, basi alitoka nje na kumuita ambapo yule muuza samaki alisogea karibu na kumfanya achague wale samaki,
“Kheee una samaki wazuri sana leo”
“Asante dada, najitahidi kuleta vitu vizuri ili kuwafurahisha wateja wangu”
Basi Mariam akachagua pale samaki ambapo yule muuza samaki alianza kumchambulia, huku Mariam akimuita Anna aweze kumletea chombo cha wewe kuwekea samaki.
Baada ya muda kidogo tu Anna alitoka ndani akiwa na bakuli kubwa huku amembeba yule mtoto, kufika pale kwa muuza samaki yani ilikuwa kama muuza samaki kapigwa shoti kwani alijikuta akimshangaa sana Anna na yule mtoto, mpaka Mariam alimuuliza,
“Wewe una tatizo gani?”
Muuza samaki alikuwa akitetemeka na kumuuliza Mariam,
“Samahani, hao ni watu kweli”
Mariam akamshangaa na kumwambia,
“Wewe weka samaki, mambo ya humu ndani hayakuhusu wala nini”
Akamsogezea lile bakuli na moja kwa moja Mariam alimtuma tena ndani Anna,
“Nenda kalete hela kabatini tumpatie”
Anna akaenda ndani na mtoto, yule muuza samaki akaweka samaki na kuondoka zake, yani hakutaka hata kuendelea kubakli eneo lile, ni kama amepatwa na kitu cha kuogopesha sana. Hata Mariam alimshangaa sana ingawa alienda ndani kuosha wale samaki na kuanza kuwakaanga.

Juma aliporudi leo, alimuuliza mtoto wake kama yeye kashamaliza adhabu ya kumbeba na kwenda nae stendi au bado, ila yule mtoto alimuuliza pia,
“Wewe unaonaje? Umemaliza adhabu au bado?”
Juma akafikiria na kusema,
“Nadhani nimemaliza, maana mwanzoni ulisema wiki mbili ila kwasasa ni zaidi ya wiki mbili”
Mtoto akatabasamu na kusema,
“Ni kweli ila twende na mimi leo”
Basi Juma hakuwa na namna zaidi zaidi kuamua kwenda kuoga na kujiandaa kisha kumbeba mtoto wake na kwenda nae kule kituoni ambako huwa anaenda nae.
Wakati wanaenda, wakakutana na yule jirani yao na wakina Juma, basi yule jirani alimsalimia Juma lakini alimsalimia kwa uoga uoga sana, mpaka Juma alimuuliza,
“Mbona hivyo wewe? Mbona unaonekana kuogopa?”
“Hapana siogopi wala nini ila nashangaa tu”
“Kheeee, sasa unashangaa nini?”
“Hapana, kwaheri”
Yule jirani akaondoka kwa haraka haraka na kumfanya Juma asielewe chochote kile kinachoendelea kisha akampeleka tu mtoto wake stendi kama ambavyo huwa anampeleka.
Wakiwa stendi, akatokea yule jirani mwingine ambaye alianguka siku ile, ila na yeye alimsalimia Juma kwa uoga uoga na kumfanya Juma azidi kuhisi huenda ni sababu ya matendo ya mtoto maana yule alijibiwa vibaya na huyu alianguka na wote wanamuogopa.
Ila wakati anaondoka pale stendi, ndipo alipopita jirani mwingine ambaye jirani huyu ndiye ambaye a,likuwa wa kwanza kabisa kumkaribisha Juma katika mtaa huo, ila jirani huyu na yeye alimsalimia Juma kwa kutetemeka na hakuweza hata kuongea nae zaidi wala nini, kwahiyo moja kwa moja aliondoka na kumfanya Juma awashangae sana majirani zake ila aliamua tu kurudi nyumbani.

Usiku ule Mariam alimsimulia mume wake kuhusu muuza samaki alichokifanya na jinsi ambavyo aliondoka bila hata ya kuchukua hela yake,
“Kheee inamaana Anna na mtoto wamemtisha nini?”
“Hapo hata sijui”
“Halafu leo kila ninayekutana nae anatetemeka kunisalimia”
“Labda sababu ya mtoto anavyowajibu”
“Sidhani, maana kuna ambaye nimekutana nae hata sijawahi kuonana nae na mtoto ila na yeye katetemeka kunisalimia na kaondoka hata hatujaongea chochote, nahisi kuna kitu hapa katikati”
Walijadili sana ila mwisho wa siku waliamua tu kulala kwa muda huo.

Ile hali ya watu mtaani bado Juma ilimshangaza sana, kwani kwasasa walikuwa hawamsalimii kabisa, yani sio tu kutetemeka bali hakuna aliyekuwa akimsalimia, wote walikuwa wakimpita kama hawamuoni vile na kumfanya awe anashangaa sana ila hakuwauliza kitu chochote.
Leo alienda kazini kama kawaida, ila alipokaa na wenzie aliamua kuwaambia tatizo la msichana wake wa kazi,
“Jamani mimi nina msichana wa kazi mchawi”
Wote wakashtuka na kumuuliza vizuri,
“Kheee umejuaje?”
“Kajisema mwenyewe, kumbe alikuwa akimtumikisha mke wangu, kazi zote alikuwa akifanya mke wangu badala yako. Yani hadi sasa nahisi kutetemeka tu na sijui cha kumfanya huyu binti”
“Aaaah Juma, acha zako hujui cha kufanya? Mfukuze bhana”
“Hataki kuondoka, kila ninapomfukuza anarudi”
Mmoja akashauri,
“Basi mkorogee sumu ya panya aende akafie mbele huko”
Mwingine akasema,
“Hilo sio suluhisho, mtu mwenyewe mmesema ni mchawi, mnaweza shangaa mmekoroga sumu ya panya halafu kawawekea wenyewe, mkajikuta mmejiua wenyewe, cha muhimu hapo ni kutafuta cha kufanya tu hakuna namna”
“Sasa ndio nifanyeje?”
“Yani angekuwa kwangu ningemkatakata na mapanga, unaona shida gani kuwaambia wjirani zako wote kuwa huyo binti ni mchawi wakusaidie kumtoa?”
“Au jamani mimi naona ni bora siku moja twende nyumbani kwake tumsaidie kumuondoa huyo mchawi, ang’ang’anie kwake hapo!”
Hili wazo la mwisho kidogo lilikuwa gumu kwa Juma ukizingatia mambo ya mtoto wake ndio kabisa yani, akaona ni mtihani mzito sana huo. Ila aliwaitikia tu kuwa kuna siku atawaita nyumbani kwake sema hakuchukulia maanani.

Leo Juma akiwa anatoka kazini, kuna jirani yake alimfata tena huyu jirani hajawahi kuongea nae kabisa, na hivi karibuni alikuwa hasalimiani nae ila huyu jirani alimsalimia leo na kumwambia,
“Ndugu yangu, watu husema ninyime chakula lakini usininyime maneno, naomba na mimi nisikunyime haya maneno”
“Maneno gani hayo?”
“Ni hivi, mtaa mzima unajua kuwa nyumbani kwako unafuga majini”
“Kheeee nafuga majini! Kivipi?”
“Nasikia muuza samaki alikuja nyumbani kwako kuwauzia samaki, mara mke wako akaita watu wamletee bakuli, hao watu hawakuwa watu wa kawaida walikuwa ni majini”
“Kheeee mbona sielewi”
“Ndio uelewe hivyo, mtaa mzima ninavyokwambia wanajua kuwa unafuga majini na leo asubuhi kulikuwa na kikao cha kukujadili wewe”
“Khaaaa hadi kikao cha kunijadili kimewekwa?”
“Ndio, walikuwa wanajadili kusema kuwa ndiomana mvua hazinyeshi inavyotakiwa, ndiomana jua ni kali, ndiomana watu hawaendelei hapa mtaani sababu ya wewe kufuga majini, tena mmoja akasema kuwa mke wako amekaa na mimba kwa miaka mitatu sijui, kuna makubwa sana yanaendelea”
“Dah!! Jamani”
“Sasa kilichobnifanya nikuambie ni kuhusu kilichoamriwa kwako”
“Kitu gani hiko?”
“Ni hivi, wamesema kuwa leo usiku watakuja nyumbani kwako na kumwagia petrol nyumba yote kisha watawachoma mkiwa humo humo ndani ili wewe na yeyeyote aliyendani mteketee na kufa, hata hayo majini yako nayo yateketee na kufa”
“Khaaaa jamani!”
“Ndio hivyo jirani, mimi roho imeniuma. Ingawa hatuna ukaribu ila huwa nakuona una roho nzuri, nakumbuka kuna siku umenikuta na mwanangu mgonjwa njiani ukanisaidia hadi hospitali na tukapata matibabu sababu yako. Kwakweli nakumbuka sana fadhila zako kwangu. Nimeumia mno kusikia habari hii ya wewe kufuga majini. Nikasema ngoja nikuvizie nikwambie ili ikiwezekana muondoke kabla giza halijaanza”
“Duh!! Asante kwa taarifa”
Yani Juma aliondoka muda huo huku akiwa amepaniki kabisa, hata hakujua ni wapi pa kuanzia wala nini maana alikuwa amepaniki.

Alipofika nyumbani hata hakujua aanze na jambo gani ila aliita familia yake yote sebleni na kuanza kuwaelezea kila kitu ambacho yule jirani amemwambia, Mariam alishtuka na kuogopa sana,
“Kheeee kwahiyo wanataka kutuchoma ndani ya nyumba jamani!!”
“Ndio hivyo mke wangu, sijui tunaenda wapi muda huu”
Mama Shamimu akadakia,
“Naomba niondoke sasa hivi niende kwa mama”
Mtoto alikuwa kimya tu wakati wakijadili, na wakajikuta wakiafikiana wote kuwa waende kwa mama yao na moja kwa moja kwenda kujiandaa maana hapo ilikuwa ni kufunga nguo tu na kubeba.
Walipotaka kutoka walishangaa kuona milango haifunguki, Juma aligeuka na kuuliza,
“Imekuwaje tena?”
Mtoto akauliza pia,
“Mnaondoka wote na mimi mnaniachaje?”
Juma akawaza ila hakuwa na jinsi akaamua kumwambia huyu mtoto kuwa wanaondoka nae, ila yeye akawaambia kuwa hakuna kuondoka hadi waweze kula kwanza kwahiyo waende kupika yani mule ndani walichukia sana kwani walijua wazi wale watu wa kuchoma nyumba watawafikia tu.
Wakati wanakula ndipo waliposikia sauti za watu wakiwa wamezunbguka ile nyumba yao, Juma alienda kuchungulia dirishani na hofu ikamtanda kwani aliona wale watu wakimwagia petrol kuizunguka nyumba yao, Juma alijikuta akisema,
“Jamani ndio tumeshakufa tayari”
Mtoto wao akacheka na kusema,
“Baba unaogopa kifo eeeh!!”
Mama Shamimu na Mariam nao wakasema,
“Wote tunaogopa kufa”
Mara wale watu wa nje wakawasha moto na kuanza kushangilia pale nje huku ndani wakiwasikiliza tu na kuogopa ila mtoto alianza kucheka na alicheka sana, gafla ilianza mvua ya ajabu tena ilikuwa ni mvua ya mawe na kusambaratisha watu wote pale nje.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni
close