Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 23

MTOTO WA MAAJABU: 23

Muda huu, Juma alifika nyumbani kwake na mama Rose ambapo alipomkaribisha ndani tu kulikuwa na Mariam ambaye alionana na mama Rose halafu mama Rose akasema,
“Kheeee huyu si ndio rafiki yake Mishi!”
Juma alishangaa kwani yeye hajawahi kufikiria kama huyo Mishi na mke wake wanafahamiana.
Juma alimuangalia mama Rose na kumuuliza,
“Kwani mnafahamiana?”
Rose akajibu,
“Ndio, namfahamu vizuri huyu. Kuna siku yeye na Mishi walikuja kunichamba”
Mara alitoka Anna chumbani, yani kufika pale sebleni mama Rose alishangaa sana na kusema,
“Kheeee hii nyumba kumbe inafuga majinamizi! Kwaherini”
Mama Rose alitoka ila Anna alimfata nje huku akimkimbilia na kumuita,
“Dada, dada, dada”
Mama Rose alisimama huku akiwa na hasira maana hakutegemea kumuona Anna pale, basi Anna alimsogelea na kumwambia,
“Dada usinitende hivi!”
“Mjinga wewem ambia uchawi wako ndio usikutende hivi, unajua mimi sina makosa wala yoyote hana makosa ila ni huo uchawi wako!”
“Ila mimi ni mdogo wako dada”
“Hata kama ila ondoa huo uchawi wako kwanza”
“Kumbuka mimi sijapenda kuwa hivi, ni mama ndio kanifanya hivi”
Mama Rose hakutaka hata kuongea zaidi kwani aliondoka zake na kumfanya Anna arudi tu nyumbani, akainama kwenye kochi huku machozi yakimtoka.
Kwa mara ya kwanza Mariam tangu ajue kuwa Anna ni mchawi, leo alimuonea huruma, alimfata na kumuuliza vizuri,
“Weee Anna, yule ni nani yako?”
“Ni dada yangu, kabisa yani dada yangu kabisa”
“Aaaah kumbe!! Sasa imekuwaje mbona akuite jinamizi?”
Anna hakuona aibu kuongea, bali aliongea tu, muda huu ni kama aliona liwalo na liwe,
“Ni sababu ya hilo hilo swala la mimi kuwa mchawi, sikupenda ila imetokea nipo hivi”
“Duh! Kwahiyo Anna uchawi umeutoa wapi wewe?”
“Kwa mama, yani mama ndio aliyenirithisha mimi uchawi”
“Kwahiyo Anna wewe ni mchawi kweli?”
“Ndio dada, mimi ni mchawi. Ndugu zangu wote wamenitenga sababu ya uchawi wangu, hakuna anayehitaji kuishi na mimi sababu ya uchawi”
Yani muda huu Mariam alijikuta akimuogopa Anna zaidi maana alijidhihirisha wazi kuwa ni mchawi na wala hakumuhoji sana kwani alimuacha tu na kwenda kwenye mambo mengine.

Jioni ilipofika, Juma kama kawaida yake alimbeba mtoto wake na kutoka nae maana ilikuwa ni adhabu kwake kwahiyo alikuwa hawezi kuacha bila kuifanya adhabu hiyo maana akiacha tu basi mama yake ataanza kuumwa, kwahiyo mama Juma alikuwa hajui ni kitu gani kinachoendelea kwa mwanae.
Alienda na mtoto wake hadi stendi kama kawaida halafu na kuanza kurudi nae, ila leo walikutana na yule jirani akiwa ameongozana na mtu mwingine ambapo yule jirani alisimama pale ili kumtambulisha jirani mwenzie kwa Juma,
“Huyu ni jirani yetu”
Basi yule jirani mwingine moja kwa moja alimuangalia mtoto ambaye Juma kambeba na kuanza kusema,
“Kheee una mtoto mzuri jamani, tena mzuri sana”
Yule jirani wa kwanza akasema,
“Watoto wote ni wazuri jirani”
“Hata kama, ila peye sifa anastahili kutoa sifa”
“Mmmmh shauri yako, endelea tu na hizo sifa zako”
Ila mtoto alikuwa kimya tu akiwaangalia huku yule jirani mwingine akiendelea kumwambia Juma,
“Hongera sana jirani, mimi nina mtoto wa kiume nadhani itafaa tukijenga undugu maana utakuwa mkwe wangu”
Juma hakutaka hizi mada kwani mtoto wake alimjua vizuri sana, kwahiyo alikuwa akimzuia jirani kwa hizi mada ili zisiendelee,
“Jamani mimi nina haraka”
Yule jirani akasema tena,
“Mbona swala la kuwa mkwe hujalijibu jirani!”
Yule mwenzie akasema,
“Mtu mzima akivuliwa nguo huchutama, na wewe hebu tulia ukwe gani na mtoto bado mdogo!”
Juma akaondoka zake na kuwaacha wale majirani wakibishana wenyewe, yani leo Juma aliona mtoto wake kajistai sana maana bila kujibu kitu ni jambo la ajabu sana kwa mtoto huyu.

Usiku wa leo, Juma na mke wake walipokuwa chumbani ilibidi Juma amuulize vizuri kulingana na yale madai ya Mishi,
“Samahani mke wangu, huyo Mishi unamfahamu wewe?”
“Hapana, simfahamu Mishi wala nini ila yule dada hata nimemshangaa, sijui ana mapepo loh!”
“Hana mapepo yule, huenda umefanana na mtu anayemfahamu Mishi vizuri!”
“Labda ila mimi simfahamu Mishi kabisa”
Kisha Mariam alianza kumueleza mumewe kuhusu Anna kuwa yule ni dada yake,
“Yani leo Anna kanidhihirishia wazi kuwa yeye ni mchawi, tena anasema kaupata kwa mama yake. Na yule aliyekuja leo ni dada yake”
“Duh!! Ila dunia ni duara jamani, sema nini ukweli nitaujua tu”
Waliongea ongea pale na kuamua tu kulala.

Siku ya leo, Mariam anaamka na kumuita Anna mapema kabisa, kisha akaongea nae maana alijihisi kuchoka sana,
“Anna mdogo wangu sikia, kiukweli nimechoka sana kupika, naomba leo mdogo wangu unisaidie”
“Ila mtoto hatopenda dada”
“Ndio, ila Anna si huwa unapika chakula kama changu jamani! Naomba unisaidie, chakula cha mchana tu ila pika moja kwa moja hadi jioni. Pika pilau”
“Mmmh dada, sijui kupika pilau”
Mariam alishangaa sana na kumuangalia Anna, kisha akamuuliza,
“Sijakusikia vizuri, umesemaje Anna?”
“Sijui kupika pilau dada”
“Kwahiyo lile pilau ambalo ulikuwa ukirupikia ni nani anakuwa amepika?”
Anna alikaa kimya hapo, kisha Mariam akamwambia,
“Anna, hata sihitaji maneno mengi. Naomba tu upike hilo pilau, leo nimechoka sana, nahitaji kulala mie”
“Mmmh dada jamani”
“Hakuna cha jamani hapa!”
Kisha Mariam akaondoka zake, yani alikuwa amesahau kabisa hoja ya mumewe kuwa ni yeye ndiye huwa anapika badala ya Anna.

Juma alikaa kwenye kazi yake ila bado aliona kuna umuhimu wa yeye kuzungumza na mama Rose, basi aliamua kumpigia simu ili aonane nae,
“Naweza kuonana na wewe!”
“Ndio unaweza ila sitokuja tena nyumbani kwako”
“Sawa, nitakuja mimi huko”
Muda huo huo, Juma aliondoka pale na kwenda kumfata mama Rose ambapo alikutana nae na kukaa nae kuanza kuongea nae,
“Samahani kwa leo, nilitaka nikuulize kuhusu yule mke wangu unasema ni rafiki yake Mishi kivipi?”
“Hiyo kivipi sijui ila mimi najua ni rafiki yake Mishi, nishawahi kumuona nae mara nyingi tu”
“Kwahiyo mimi nimeoa mtu na rafiki yake?”
“Ndiomaana yake, inamaana yule hajui kama umewahi kuishi na Mishi?”
“Hapana hajui, sikia nikwambie ipo hivi. Mimi kipindi cha nyumba nilikuwa na sura ya kuzeeka sana hadi walianza kuniita mzee Juma na ndio jina lililozoeleka kwangu, ila licha ya utu uzima sema kuna mambo ambayo yalinizeesha”
“Mmmmh kuna mambo yalikuzeesha kivipi?”
“Ni historia ndefu ila kuna mtu alifanya nirudi katika hali ninayotakiwa kuwa nayo na hii ni baada ya kumuacha Mishi, na hapo nikamuoa Mariam, ila ukimuuliza Mariam kama niliwahi kuoa atakukatalia. Mimi ni mkubwa ila sio mkubwa kama vile ambavyo nilizeeka”
“Duh!!”
“Haya, hebu niambie ni kweli ni yule yule mke wangu ndio rafiki yake Mishi?”
“Ndio, kwanini nidanganye? Nataka nini kwako?”
“Haya, na vipi kuhusu yule Anna! Kweli ni mdogo wako?”
“Ndio, yule ni mdogo wangu ila ni mchawi wa wachawi”
“Kaupata wapi uchawi?”
“Kwa mama yetu, mama alikuwa ni mchawi sana. Ila hatukujua, sema alikuwa ni mchawi hadi anafuga misukule ila alitupenda sana halafu alimpenda sana Anna, kumbe ndio kampa uchawi”
“Mmmmh sasa mama yenu yuko wapi?”
“Alikufa, yani tumepata shida maana nyumba yetu iliungua na kufanya trukose makazi ila tulichofanya ni kuuza ule uwanja halafu hela tulizopata tulienda kujenga nyumba sehemu nyingine na kuishi huko”
“Sasa imekuwaje huyu mdogo wenu hamuishi nae?”
“Siwezi kuishi nae kabisa, nikikwambia alichokifanya hata wewe huwezi kuniambia kuwa niishi nae, ni kweli samehe saba mara sabini ila Anna hasemeheki kabisa, siwezi kumsamehe mimi”
“Kwani alifanyeje?”
“Kwetu, mimi ndio wa kwanza kuzaliwa halafu mama alizaa mapacha wakiume tupu, na wa mwisho ni Anna, ila mtoto mjinga yule wakati tunaishi nae si amewaua wale mapacha kiuchawi”
“Duh!!”
“Kafanya mimi niwe sina ndugu maana ukoo mzima walitutenga, na mimi nikamfukuza na kuuza eneo lile kisha kwenda kuolewa, nilichukia sana kwa alichonifanyia yule mjinga na uchawi wake, hivi mtu kama huyo unamsamehe vipi jamani!”
“Dah!! Kwakweli hapo sina usemi kabisa yani. Huna kosa hapo mama Rose”
Basi Juma hakuwa na ya ziada ya kuendelea kuongea na huyu mama Rose, bali alimuaga na kuondoka zake.

Kama kawaida jioni ya leo, Juma alimbeba mtoto wake na kwenda nae kituoni kama ambavyo aliambiwa ila leo alikutana na yule jirani wa jana ambaye inaonekana aliambiwa jambo kwani hata kumsalimia Juma hakumsalimia mpaka pale Juma alipomuita na kumsalimia,
“Mbona jirani unapita tu bila ya kunisalimia?”
Yule jirani alimuangalia Juma ila hakumjibu kwani aliondoka zake, kisha Juma alijikuta tu akimuangalia mtoto wake kwani alimuhisi kama anataka kusema neno vile ila hakusema neno lolote.
Juma akaondoka na mwanae, kufika njiani walimkuta yule jirani kajikwaa na kuanguka, kwahiyo alikuwa chini akiugulia maumivu, hapo Juma alimuuliza,
“Tatizo nini tena jirani?”
“Nimejikwaa”
“Pole sana jirani, ila ilikuwaje?”
Kabla yule jirani hajajibu, yule mtoto wa Juma akasema,
“Akiwazacho mjinga ndicho humtokea”
Yule jirani alimuangalia yule mtoto kisha alimuangalia Juma na kusema,
“Kweli bhana, mimi ni mjinga yani nakubaliana na huyo mtoto kabisa, jana niliambiwa kuwa huyu mtoto anashushua sana. Leo sikutaka kuwasalimia ila nikawaza huenda mbele nikaanguka halafu wakanikuta itakuwaje? Na kweli nimeanguka na mmenikuta, kweli mimi ni mjinga, tena ni lofa, sirudii tena kuwaza ujinga”
“Pole sana”
Juma alimsaidia kuinuka pale, kisha kuagana nae na kurudi nyumbani kwake yani hakuna ambacho Juma alikuwa akiongea na huyu mtoto zaidi ya kwenda nae na kurudi nae.

Muda wa kula, Juma alipokula tu aliuliza maana alijua wazi ni mkewe kapika ila mke wake ndani alimwambia kuwa chakula cha siku hiyo kimepikwa na Anna, basi Juma akauliza,
“Kwani chakula kapika nani?”
Mariam akajibu,
“Kapika Anna”
Mama Shamimu akasema,
“Weeee wifi wewe, kapika Anna muda gani wakati nilikuona wewe upo jikoni ukipika! Tena leo hukutaka hata kuongea na mimi!”
Mariam akaweka kijiko chini na kumuangalia Anna kisha akasema,
“Yani Anna umediriki kunifanyia uchawi tena!”
Hapo ndipo Juma alipopata nafasi ya kuongea vizuri sasa,
“Mtu ameweza hata kuwaua ndugu zake ambao kazaliwa nao pamoja, sembuse wewe asiyekufahamu aliyekupata ukiwa na meno yote mdomoni. Yani kaua watu waliokuwa wakimsaidia kimaisha, waliomlea toka udogoni, sembuse kukutesa wewe mke wangu mvivu! Hapo hebu tumia akili tu kuwa huyu Anna hafai”
Mariam alichukia sana hadi aliacha chakula akataka kuondoka ila mumewe akamrudisha,
“Mke wangu, utasusaje chakula ulichopika mwenyewe! Hebu acha hizo Mariam, kwanza kumbuka kuwa wewe huwa hususi”
Mariam akafikiria kweli kuwa huwa hasusi hovyo haswaa kususa chakula hiyo kwake ilikuwa haipo kwahiyo alikaa na kula ila alikuwa na kinyongo sana na Anna.

Usiku ule, Mariam aliongea tena na mumewe kuhusu swala la kumuondoa Anna, maana alitaka yule Anna atoke kabisa katika maisha yao,
“Sasa mke wangu unadhani huyu Anna tutamtoaje?”
“Sijui ila nataka aondoke kabisa kwenye maisha yetu”
“Mmmmh sijui yani”
“Nenda kaongee na yule dada yake kuwa aende huko kwake”
Juma alimueleza mke wake kuhusu yule dada alivyomwambia hadi ile habari ya kuua ndugu zake wengine na kumfanya Mariam awe kimya tu huku akijilaumu kwa kusema,
“Yani ni mimi niliyemkaribisha vizuri yule binti ndio nimesababisha”
“Ndio ni wewe Mariam”
“Nadhani ni uvivu wangu ndio umesababisha yote haya”
Juma alitabasamu na kusema,
“Ooooh leo umejua eeeh!!”
“Tuachane na hayo, tulale tu maana nina mawazo sana”
“Ila mke wangu nahitaji”
“Hebu nitolee balaa mie, unaona kabisa nina mawazo kibao, hata hatujui ni jinsi gani tutaondokana na huyu mchawi halafu unaniambia habari za kuhitaji! Sitaki bhana”
Juma hakuwa na cha kusema zaidi ya kumuitikia mke wake tu kisha waliamua kulala tu kwa muda huu.

Leo asubuhi wakati Juma anaenda kazini, akaona ni vyema apitie ile njia ambayo huwa anakutana na yule binti maana alitamani sana kuyapata yale majani ambayo yalimsaidia sana kwenye swala la mke wake.
Alifika pale Juma na kuangalia sana, na kuita sana ila hakuitikiwa, hadi roho ilimuuma akakosa raha kabisa ila alipokuwa anashangaa shangaa akaona kama kuna maua yenye majani ya kijani sana kwa mbele kidogo, akafata pale na kukuta karatasi imeandikwa,
“Chuma maua haya”
Basi moja kwa moja Juma aliinama na kuyachuma na kuyaweka mfukoni, alisubiri maelekezo lakini hakupata ikabidi ajiongeze tu maana yale maua yalifanana na yale yale maua ambayo alipewa awali na yule binti kuwa ndio yanaweza kumsaidia katika swala zima la kulala na mke wake. Alifurahi huku akisema kimoyomoyo,
“Leo, nitamkomesha Mariam maana anachonifanyia sio kabisa”
Alikuwa akitabasamu huku akiondoka na yale maua.

Leo Mariam wakati anapika chakula cha mchana akajisahau na kuweka chumvi nyingi sana, kwahiyo wakati wa kula ilikuwa ni gumzo kwani kila mmoja alikuwa akilalamika kuwa chumvi ni nyingi hadi wifi yake akamwambia,
“Hivi Juma ndio ataweza kula chakula hiki kweli wifi?”
“Kwanini asiweze sasa? Hiki chakula ni cha moja kwa moja, siingii mara mbili jikoni mimi”
“Wifi, yani ungempikia tu mumeo chakula kingine. Umezidisha sana chumvi humu!”
“Kwani yeye hajui kama kuna kukosea? Sipiki tena”
“Mmmmh ila kwa unavyomfanyia sio vizuri, kumbuka yeye ndio baba wa familia, halafu yeye ndio mtafutaji wa kila kitu humu, angetakiwa kuwa anakula vizuri, hata kama sisi tukila visivyoeleweka lakini sio baba mwenye nyumba Mariam”
“Usinipangie maisha wifi”
Anna alichukua chakula kwenda kumlisha mtoto ila yule mtoto kabla ya kukila alimuita Mariam kwa sauti kubwa,
“Mama”
Mariam akageuka na kumuangalia,
“Nenda kanipikie chakula kingine”
Hapo Mariam hakubisha wala kukataa ila alikuwa na hasira sana, akainuka na kwenda jikoni akabandika chakula ila akapanga kuwa chakula hiko ndio atakijaza chumvi nyingi.
Basi akiwa anapika, akachukua chumvi ili ajaze, ila alishangaa kuona akishikwa mkono ni kama mtu anamzuia kuweka chumvi.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni