Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 22

MTOTO WA MAAJABU: 22

Basi Mariam alifungua mlango na kuingia ndani na Neema, muda huu Anna nae alikuwa ametoka jikoni kwahiyo walikutana macho kwa macho na Neema, yani Neema alishtuka na kusema,
“Mungu wangu, nimekutana na wewe uwiiiii ndio ndoa yangu inayeyuka hivi!”
Mariam hakumuelewa kabisa, ilibidi amuulize,
“Neema una maana gani?”
Neema na yeye alimuuliza Mariam,
“Dada umemtoa wapi huyu? Ni mchawi wa wachawi huyu”
“Kheeeee kivipi?”
“Nimejuta hata kukutana na wewe, nimejuta hata kukueleza kuwa nakaribia kuolewa kwani najua ndoa yangu ndio imeyeyuka tena sijui hata kwanini nilikueleza, ni mchawi sana huyu msichana, yani Anna nakwambia ndoa yangu ikipotea Anna, nitakufanyia shughuli”
Yani Mariam alikuwa akishangaa tu, Anna na yeye alikuwa yupo kimya tu kanakwamba yale anayoambiwa hayamuhusu, kisha yule Neema akasema,
“Mimi naondoka dada, ila nkama nikipatwa na tatizo lolote lile basi ni huyu mchawi ndio amelisababisha”
Kisha Neema aliondoka bila kusema neno lingine, muda huu Mariam alijikuta akiangaliana kwa muda na Anna yani Mariam hakummaliza kabisa Anna, na swali la kwanza kabisa alimuuliza,
“Anna, wewe ni mchawi?”
Anna alikaa kimya kwa muda na kujibu,
“Hapana mimi sio mchawi dada”
Mariam alimuangalia sana Anna na kumuuliza tena,
“Anna, wewe ni mchawi?”
Anna alijibu vile vile kuwa yeye si mchawi, mama Shamimu na yeye akasogea pale na kusema,
“Yote yaliyoongelewa nimeyaona na kuyasikia, Anna kuwa mkweli. Wewe ni mchawi, yani siamini kuwa nimekimbia uchawi wa nje nilipotoka halafu nimekuja kukutana na uchawi ndani”
Anna aliwaangalia na kujibu tena,
“Hapana, mimi sio mchawi”
Hata walivyokazana kumlazimisha bado alikataa kabisa kuwa yeye sio mchawi kiasi cha kwamba walishindwa hata cha kufanya na kubaki kwa hasira zaidi.

Muda huu mama Shamimu na Mariam walitoka nje na kuongea kuhusu Anna maana yale waliyoyasikia yalikuwa na maana kubwa sana kwake.
“Sasa wifi tufanye kitu gani?”
“Yani mimi ukiniuliza cha kufanya nitakujibu kwa jibu moja tu wifi kuwa tumfukuze, maana mimi kwa kawaida huwa siwezi kuishi na mtu asiyeeleweka kiasi hiki, yani mtu haeleweki mbele wala nyuma halafu niishi nae hapana kabisa siwezi kufanya hiko kitu”
“Kwahiyo tumfukuze?”
“Ndio Mariam, utaiushije na mwanamke mchawi? Halafu kama ulivyosema kuwa sio mara ya kwanza hii, ushashangalia na watu mbalimbali kuhusu huyo mdada wa kazi, hata mumeo ameshasema mara kadhaa kuhusu huyo mdada wa kazi, ni kufukuza tu hakuna namna hata kidogo”
“Naafikiana na wewe wifi halafu nimeanza kuhisi kitu huenda alikuwa akinifanyisha kazi kichawi huyu mjinga”
“Ndio hivyo ila kwasasa ndio kajifanya kufurahi tu baada ya yule mtoto kutupa adhabu ila yule binti ni wa kuondoka, tena leo leo”
Mariam na mama Shamimu wakakubaliana hivyo, na wakakubaliana kuwa Juma akirudi waongee vizuri na kumfukuza kabisa.

Juma aliporudi tu, pale pale Mariam hakungoja hata aingie chumbani kwani alianza kumuelezea kuhusu binti aliyefika nae leo, yani Juma alitikisa kichw atu na kusema,
“Ila mimi nilikuwa nakwambia Mariam, huyu binti ni mchawi. Unaona yale mahindi pale nje, umepanda mwenyewe, umepalilia mwenyewe hata yemanza kuzaa ni nguvu zako mwenyewe, humu ndani ulikuwa ukisafisha nyumba mwenyewe na ukipika mwenyewe”
“Duh!!”
“Usishangae ndio hivyo, huyo binti ni mchawi ndiomana mimi simtaki ila ukakazana kuwa mimi sijui nimewahi kumtaka kimapenzi, hivi mimi nikitake hiko kibinti kweli!! Bora leo umeamka Mariam, fanyeni mnachotaka kufanya ila swala la mimi ni kuwa huyu binti aondoke humu ndani”
Anna alikuwa amekaa kimya tu huku akiangalia chini, kisha Mariam akarudia swali kama la mchana,
“Anna, wewe ni mchawi?”
Anna nae akarudia jibu lile lile,
“Hapana, mimi si mchawi”
Hapo mara yule mtoto akaongea,
“Anna, kubali tu ukweli kuwa wewe ni mchawi na uwaulize wanataka nini baada ya kugundua uchawi wako!”
Kimya kilitanda ila Mariam alijitoa muhanga na kujibu,
“Tunataka aondoke”
Kale katoto kalitabasamu kisha kakasema,
“Yani na wewe mvivu bila aibu unajibu tunataka aondoke, utanilisha wewe, utaniogesha wewe, utakuwa unalala na mimi? Utanihudumia wewe! Kama vyote hivi huwezi basi Anna haondoki hapa kwa amri zenu bali ataondoka pindi tu nitakapotaka mimi. Haya na wewe baba ni muda umefika wa kwenda na mimi barabarani, ila nenda kaoge kwanza”
Juma hakusema neno zaidi zaidi alienda kuoga huku Mariam na mama Shamimu wakiwa wanaangaliana tu bila ya jibu.

Muda huu Juma alikuwa ameondoka na haka katoto na kwenda nako kituoni kama kawaida yake halafu nyumbani walibaki mama Shamimu, Mariam na Anna, hapo hapo mama Shamimu na Mariam wakaungana na kuanza kumpiga Anna huku wakimwambia,
“Wewe si mchawi sana eeeh! Haya tufanyie huo uchawi wako mjinga mmoja wewe”
“Na hapa utaondoka tu, eti kale katoto kamekutetea. Jua hii ni nyumba yangu na mume wangu, sio mali ya yule mtoto kabisa kwahiyo hapa utaondoka”
Mama Shamimu alimburuta Anna na kumtoa nje kabisa huku akimtaka Mariam kwenda kumtolea mizigo yake Anna apate kuondoka.
Kwakweli mama Shamimu alimsema sana,
“Yani unajifanya mtu kweli, unajifanya mpole mwenyewe kumbe hakuna lolote. Ujinga ujinga tupu, huna hata jipya unawaza ujinga tu, unawaza uchawi tu, mtoto mdogo kama wewe kuwa mchawi hata haipendezi, huo uchawi utakusaidia nini? Hadi watu wanakuogopa wanahofia ndoa zao zitayayuka sababu ya uchawi wako!! Na humu ndani utaondoka tu, huna nafasi kabisa humu ndani”
Mariam alipeleka mzigo wa Anna pale nje huku akisema kwa kubana sauti,
“Ooooh sijui nimefukuzwa, ndugu zangu hawanitaki, watakutaka vipi wakati wewe ni mchawi! Nani atakutaka wakati wewe ni mchawi namba moja! Nenda tu, begi lako hilo ulilokuja nalo”
Anna hakujibu ila alimuuliza swali Mariam,
“Dada, kumbuka uliniahidi kuwa utakuwa dada yangu hadi mwisho wangu”
“Ndio mwisho wako umefika, sina undugu na wachawi mimi”
Anna akainuka kama kutaka kuondoka ila akamuona Juma akirudi na mtoto kisha Anna akasema,
“Mkombozi wangu huyo anakuja”
Mama Shamimu na Mariam walikaa kimya, yule mtoto alivyofika na Juma alionekana kuwa na sura ya hasira sana ila hakuongea kitu bali alishuka kwa baba yake na kumshika mkono Anna kisha kuingia nae ndani, kwahiyo pale nje Juma aliwauliza,
“Imekuwaje tena na nyie?”
Wakamsimulia kisha akawaambia,
“Mmeyataka mengine jamani, mimi sihusiki kabisa na mambo hayo”
Kisha Juma aliingia zake ndani huku Mariam na mama Shamimu wakiwaza kuwa ni kitu gani kitaendelea baada ya hapo.

Mpaka muda wanalala, yule mtoto hakusema jambo lolote lile, kwahiyo walienda kulala tu ila kiukweli Mariam alikuwa na mawazo sana kwani alikuwa anawaza ni jinsi gani alimuamini Anna halafu kuja kujua mambo kama haya, kwakweli alikosa amani kabisa moyoni kwake hata usingizi hakuupata vizuri, alimuamsha mumewe na kumuuliza,
“Hivi Juma ulijuaje kuwa Anna ananitumikisha mimi?”
“Sikia nikwambie, radha ya chakula cha Anna ni radha ya chakula chako halafu kuna siku niliwahi kukukuta chumbani na muda huo huo nikakuona upo nje ukilima”
“Kheee kivipi?”
Juma alimuelezea ilivyokuwa, kwakweli Mariam alibaki kushangaa tu ni kama akili zake kwasasa ndio zilikuwa zinarudi, Juma alimkumbusha hadi kile kisa cha wao kuwa macho kwa usiku wote halafu na kitu ambacho Anna alipika, ndio Mariam alizidi kufunguka ufahamu wake,
“Halafu ni kweli Juma, jamani binti kanitumikisha huyu balaa”
“Pole mke wangu, ila nafurahi sasa akili zimekurudia vizuri mke wangu”
“Asante, sina raha kabisa kumuamini shetani dah!”
Basi Juma muda huu alimbembeleza mke wake tu ili wapate kulala.

Mapema kabisa Juma alienda kaze kwenye shughuli zake, huku wakina Mariam wakibaki nyumbani na majukumu yao, ila walivyomaliza wakati wamekaa tu yule mtoto akaongea,
“Jamani, mimi nilishawaambia kuwa huwa sipendi kuongea sana sababu naumwa na mbavu. Mama na shangazi mmeniudhi sana siku ya jana, hivyo basi, shangazi adhabu yako haitaishia wiki mbili tu bali itaenda mwezi mzima”
“Kheeeeee!!”
Kale katoto kaliendelea kuongea,
“Na hata baada ya shangazi kuondoka, wewe mama ndiye utakayechukua majukumu ya nyumba nzima”
Yani Mariam hata hakujua alie au afanye kitu gani ila alichojua kufanya kwa muda huo ni kujuta kumpata huyu mtoto katika maisha yake.
Halafu kila mmoja aliendelea tu na majukumu yake huku Anna ndio akibaki na yule mtoto yani Anna hakuwa na kazi yoyote kwa kipindi hiki zaidi ya kubaki na mtoto tu.

Juma akiwa kwenye shughuli zake leo alijikuta akiwaza mambo mengi sana, cha kwanza kabisa alimuwaza yule mama Rose na aliwaza ukaribu wa mama Rose na Mishi, basi aliwahi kutoka na kumpigia mama Rose ili apate kuongea nae,
“Samahani dada, je tunaweza kuongea?”
“Sawa hakuna tatizo.”
Basi yule mama Rose alimuelekeza Juma mahali ambako angemkuta yeye ambapo Juma alifanya hivyo na kumfata mama Rose ili apate kuongea nae, na kweli alikutana nae ambapo alimuelekeza, na kuanza kuongea nae,
“Unajua nini, siku ile sikukuelewa vizuri kuhusu Mishi”
“Kwani wewe Mishi yupi unayemfahamu? Ndio huyo niliyemuongelea?”
“Mmmh inawezekana maana unayoyasema kama yanashahabiana”
“Hebu niambie vizuri halafu mimi nitakueleza”
“Kipindi cha nyuma nilioa mke aliyekuwa akiitwa Mishi ila mke huyu alinifanyia vituko sana, naweza kukusimulia hadi ukanionea huruma”
“Kwahiyo yuko wapi sasa?”
“Sijui na wala huwa sipendi kumuongelea ila tu nilipenda kujua kuwa wewe Mishi umemfahamu vipi?”
“Si nimekwambia jinsi ilivyokuwa, yani huyo Mishi alitembea na ndugu zangu, katembea na mchumba wangu, katembea na mume wangu, tena nikaja kumfumania akiwa na mimba kubwa tu huku akiwa kitandani na mume wangu, yani huyo Mishi ni mpuuzi mmoja asiyejielewa kabisa”
“Pole sana, ila kuna kitu huwa kinanitatiza sana kuhusu huyo Mishi”
“Kitu gani hiko?”
“Kipindi namuoa, sikujua kama ana mimba, ila kuna mtu alitokea na kusema kuwa Mishi alibakwa na kupata ile mimba, nilijitahidi kuukwepa ukweli ila ilishindikana, na Mishi aliambiwa kuwa aache kuchanganya wanaume ila kuna makosa alifanya akapotea kabisa na mimba yake, mara nyingi sana nimejikuta nikitamani kujua ni kitu gani kimeendelea katika maisha yake”
“Ila hata mimi sijui alipo, kwani huna mke kwasasa?”
“Mke ninaye, ila mke wangu hajui kabisa habari za Mishi”
“Sikia kaka, najikuta nikitamani kumfahamu mke wako”
“Kwanini?”
“Basi tu, natamani kumfahamu”
Juma hakuwa na kinyongo ila alikubaliana nae kuwa atamtafuta siku nyingine ili aweze kumpeleka kwake kwenda kumfahamu huyo mke wake, na muda huo Juma aliagana na yule mama Rose.
Muda huu wakati Juma akiwa anaelekea nyumbani kwake, alikutana na Pendo njiani ambapo Pendo alimsalimia na kumuuliza pale,
“Unajua leo umeondoka mapema sana, sikujua kama ningekutana na wewe njiani!”
“Kweli nimeondoka mapema, ila najitahidi niwahi nyumbani, kwani saa ngapi saa hizi?”
“Ni saa moja kasoro kumi hii”
Juma alishtuka sana kuona muda umeenda sana, alimuaga Pendo kwa haraka haraka na kuondoka kwani alikuwa na kile kibarua cha kumpeleka mtoto wake barabarani, sasa muda ulienda vile aliona ni balaa na aliona wazi kuwa atachelewa.

Na kweli Juma alichelewa kufika nyumbani kwake leo, kwani aliingia kwake kwenye mida ya saa mbili usiku, kitu cha kwanza kabisa alimuulizia mtoto maana hakumkuta pale sebleni,
“Mtoto yuko wapi?”
“Amelala tayari”
Juma akapumua kwa kuona kuwa mtoto amelala, basi akaamua tu na yeye kula, kuoga na kwenda kulala huku akijiambia kuwa mtoto atampeleka kesho yake.
Ila usiku ule alikuwa na maswali mengi sana kuhusu mama Rose, na alikuwa akijiuliza ni kwanini huyu mwanamke anataka kumfahamu mke wake? Hapo hakupata jibu ingawa alitamani sana kujua kuwa ni kwanini ipo hivyo.
Aliwaza na kupitiwa na usingizi tu, ila kwenye mida ya saa nane usiku, Juma alishtushwa na mlio wa simu yake na kuamua kuichukua akakuta ni mama yake ndio anampigia, alipopokea alishangaa maam yake kuongea kuwa anaumwa sana,
“Nini tatizo mama?”
“Nilikuwa mzima tu, hata nimeshangaa nikianza lile tatizo la kuendesha yani najihisi kila kitu mwilini kimeisha”
“Dah!! Pole mama yangu”
“Asante, tafuta jitihada nipate msaada Juma hata wa kwenda hospitali. Hali yangu ni mbaya sana”
Juma alikata ile simu na kujikuta akikumbuka kauli ya yule mtoto kuwa kitendo cha yeye kutoka nae hadi stendi na kurudi nae ndio itakuwa tiba ya mama yake, basi muda huo huo Juma aliinuka bila kujali kuwa muda umeenda sana.
Alienda hadi chumbani kwa Anna na kufungua mlango kisha akambeba mtoto na kutoka nae nje, yani hakujali ni usiku wala ni nini.
Alitembea na mtoto yani palikuwa ni kimya kabisa, hakuna sauti ya mtu wala kitu gani, ni yeye tu Juma aliyekuwa akitembea huku kambeba mtoto ila alikuwa akitembea kwa tahadhari kubwa sana.
Alitembea hadi stendi ambako nako palikuwa kimya kabisa, kisha ndio akaanza safari ya kurudi yani alikuwa mwenyewe njiani, ila alijivika ujasiri tu wa kutembea muda ule.
Hadi alifika nyumbani kwake, moja kwa moja alimriudisha yule mtoto chumbani akiwa kalala vilevile halafu na yeye ndio alirudi chumbani kwake.
Moja kwa moja Juma alichukua simu yake na kumpigia mama yake,
“Mama, unaendeleaje?”
“Kwakweli Juma umekuwa kama dawa yangu, huwezi amini ile hali kwasasa imekata kabisa”
“Ooooh mama, nashukuru sana kusikia hivyo maana nilikosa hata raha kabisa mama yangu”
“Pole mwanangu, usiku mwema”
Juma sasa ndio aliweza kuagana na mama yake na kuweza kulala sasa.

Leo, mama Shamimu akimuita pembeni Mariam na kuongea nae maana hata yeye binafsi kuna vitu ambavyo alikuwa haelewi,
“Hivi Mariam ngoja leo tuongee, naomba tuongee kirafiki yani hata sio kama mawifi”
“Ndio, nakusikiliza”
“Hivi Mariam kabla ya kubeba mimba ya mtoto huyu hukutumia dawa za kienyeji kweli?”
“Wifi sikia, unakumbuka jinsi uzazi wangu ulivyosumbua? Ila sikuthubutu kutumia madawa ya kienyeji”
“Mbona mtoto katoka hivi! Kuwa mkweli Mariam ili upone, ili tujue ni wapi tunaaniza kuhusu swala la huyu mtoto”
“Kweli dada, labda tu wakati mimba imekaa bila kuzaa ndipo nilipozunguka kwa wataalamu na kutumia madawa mbalimbali ili niweze kujifungua ila iligonga mwamba hadi ile dawa ambayo mama aliniletea”
“Alisema ameitoa wapi?”
“Sijui aliitoa wapi ila ile dawa ndio iliyonisaidia mimi hadi kuweza kujifungua wifi yangu”
“Kwa hili kuna umuhimu wa kuongea na mama ili tujue ni kitu gani kilifanyika maana haya mambo haya dah!! Hadi sielewi yani, nadhani kuna jambo tunatakiwa kufanya Mariam”
Wakakubaliana pale kuwa watamuuliza vizuri kuhusu ile dawa iliyomsaidia Mariam kwani walihisi huenda ikawa ni msaada juu ya yule mtoto.

Sababu Juma alihitaji sana kujua ni kwanini mama Rose anataka kumfahamu mke wake, basi leo leo akampigia simu na kumuomba kuwa atembelee nyumbani kwake,
“Basi uje kunichukua pale tulipokuwa tunaongea”
“Sawa hakuna tatizo, nakuja kukufata”
Juma aliacha shughuli zake na moja kwa moja kwenda kumfata mama Rose ambapo alimsubiri ndipo mama Rosr alitokea ila leo alikuwa yeye peke yake bila mtoto, ikabidi Juma amuulize,
“Mtoto yuko wapi?”
“Aaaah nimemuacha nyumbani, naenda huko kwako sijui nitakutana na watu gani, macho ya watu nayo sio mazuri kwa watoto”
“Aaaah kumbe!”
Kisha Juma akaongozana nae huku wakiendelea na maongezi mengine kwa muda ule.
Muda huu, Juma alifika nyumbani kwake na mama Rose ambapo alipomkaribisha ndani tu kulikuwa na Mariam ambaye alionana na mama Rose halafu mama Rose akasema,
“Kheeee huyu si ndio rafiki yake Mishi!”
Juma alishangaa kwani yeye hajawahi kufikiria kama huyo Mishi na mke wake wanafahamiana.

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
Story ya MWANAUME WA DAR inaendelea leo.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni