Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 20

MTOTO WA MAAJABU: 20

Juma na Mariam waliangaliana kwa mshangao, kisha Juma akainuka na kwenda kufungua mlango kweli kabisa alimkuta dada yake mlangoni akiwa na mafurushi yake huku kamshikilia mtoto wake.
Juma alimshangaa sana dada yake pale nje, ila alimshika mkono na kumuingiza ndani maana dada yake alionekana hadi akitetemeka peke yake, basi alimkalisha kwenye kochi na kumuuliza,
“Imekuwaje dada?”
Mama Shamimu alijibu,
“Njaa inaniuma sana”
Yani hakuna maelezo mengine zaidi ya kusema anajihisi njaa sana, ikabidi Juma amwambie Anna kuwa amuandali dada yake chakula, Anna alifanya hivyo kisha mama Shamimu na Shamimu walipata kula, walikula sana yani njaa inaonekana ilimshika sana ndiomana alikuwa akitetemeka.
Alipomaliza kula alidai kuwa amechoka sana anahitaji kupumzika yani Juma na Mariam hawakuelewa ni kitu gani kimempata huyu ndugu yao ila Mariam alimsaidia hadi chumbani ambako alijilaza tu na mtoto wake.
Muda huu Juma na mke wake hata walishindwa kumuuliza mtoto wao kuwa ni kitu gani kimetokea bali nao moja kwa moja waliamua kwenda chumbani kwao tu.

Juma na Mariam wakiwa chumbani waliulizana kuwa ni kitu gani ambacho kimetokea na kusababisha yale yaliyopo,
“Unadhani dada yako atakuwa kapatwa na nini?”
“Mmmh sijui kwakweli”
“Bado una imani na mtoto wetu humu ndani?”
“Bado sijui ila mtoto wetu ni mzuri sana”
“Ndio ana sura nzuri ila je moyo wake ni mzuri? Na mbona anafanya mambo ya ajabu na ya kutisha?”
“Kwenye mambo ya ajabu na ya kutisha hapo sielewi kitu, ndiomana nasema kuwa anayemtumia mambo ya ajabu mtoto wetu ni huyu mdada wa kazi”
“Ila kumbuka kuwa huyu mtoto kaanza kuwa wa ajabu kabla ya huyu mdada wa kazi! Nadhani hadi siku moja akufanyie ujinga ndio uelewe”
“Mmmh mke wangu tulale maana sielewi kitu”
Waliamua tu kulala kwa muda huu kwani muda nao ulikuwa umeenda.
Kulipokucha, Juma aliahirisha kazi zake leo kwani aliona kuwa anapaswa kumsikiliza dada yake kuwa ni kitu gani kilichompata.

Leo Juma na Mariam waliwahi kutoka chumbani ila sebule haikusafishwa kama kawaida wala chai haikuandaliwa ikabidi Mariam amuulize Anna,
“Mbona hujasafisha nyumba Anna?”
“Nimekatazwa dada”
Mariam akashangaa sana na kumuuliza Anna 
“Umekatazwa? Umekatazwa na nani?”
“Na mtoto wenu dada, kaniambia nisifanye kazi yoyote leo”
“Kheeee kwanini?”
“Mimi sijui dada labda umuulize yeye mwenyewe”
“Kheee naanzaje kumuuliza jamani!”
Mariam alijikuta akimtazama yule mtoto wao ambaye alisema,
“Niitieni shangazi hapa”
Hakuna aliyejibu zaidi ya Mariam kwenda na kumuita wifi yake ambaye alifika pale huku akiona aibu kumtazama yule mtoto ambapo yule mtoto alimwambia mama Shamimu,
“Piga magoti uniombe msamaha”
Kiukweli kila mmoja pale alishangaa yani Juma ndio alishangaa zaidi ila mama Shamimu aliinuka alipokuwa amekaa na kupiga magoti mbele ya yule mtoto huku akimwambia,
“Naomba unisamehe”
Yule mtoto akamuuliza,
“Nikusamehe kwa kosa gani?”
“Kwa kukudharau mwanzoni”
Kisha yule mtoto akasema,
“Adhabu yako shangazi, kazi za humu ndani zote kwa wiki nzima utazifanya wewe ila tu mama atakusaidia kupika chakula maana mimi sitakula chakula ulichopika wewe”
Kisha kale katoto kalishuka pale kwenye kochi na kuelekea chumbani, kwakweli ilikuwa ni kitu cha kuwachanganya sana.
Mama Shamimu alikaa sasa maana hakuelewa kitu kwakweli, Juma alimuuliza
“Kwani ilikuwaje dada?”
“Hata sijui nianzie wapi jamani kuwaelezea”
“Tuelezee tu dada, anzia popote kumbuka tulikusindikiza hadi ukapanda daladala”
“Kweli kabisa ila cha kushangaza kituo cha mbele nikashuka na kuanza kurudi huku, nipo hapo pembezoni mwa nyumba yenu siku zote hizi, siwezi hata kuwaita”
“Kheeee mbona maajabu!”
“Dah yani sina hamu hapa nilipo, nimesimama kwa siku zote mbili, hakuna kukaa, hakuna kulala na wala hakuna kula sina hamu kabisa.”
“Pole sana dada”
“Asante, sina hata hamu hapa jamani!”
“Sasa hiyo adhabu utaiweza dada?”
“Nitajaribu ila nikishindwa itabidi mnisaidie”
Basi Mariam alilalamika kidogo pale,
“Yani mimi ndio sielewi, sijui ni nini huyu mtoto anataka kwangu jamani khaaa!”
Walibaki tu wakisikitika ila ilibidi wafanye maamuzi tu ya kuanza kufanya kazi kama mtoto alivyosema, kwahiyo kwa muda huu mama Shamimu alianza kusafisha nyumba yani alikuwa akifanya hii kazi huku akilalamika sana, alimlaani sana huyu mtoto alimuona ni mtoto asiyefaa kabisa.

Mchana wa leo, mama Shamimu akamuomba wifi yake apike chakula maana yule mtoto alisema kuwa chakula apikiwe na mama yake kwani hataki chakula kilichopikwa na mtu mwingine.
“Wifi jamani upike basi”
“Yani wiki yote hii natakiwa nipike jamani! Mbona hatari, nitaweza kweli mimi!”
“Utaweza tu Mariam, mbona kupika sio kazi ngumu”
“Sio ngumu kwako wifi ila kwangu ni ngumu sana, kwanza huwa sipendi mimoto moto mimi basi tu”
Kwa siku ya leo Mariam alienda kupika ila alikuwa akilalamika sana yani hadi amemaliza na wanakula alikuwa akilalamika sana.
Usiku huu Mariam alimlalamikia sana Juma maana kwake aliona itakuwa adhabu kubwa sana,
“Hivi mimi ndio niwe napika wiki nzima jamani!”
“Kwani mke wangu unalalamika nini? Kupika si kazi ya kike lakini?”
“Wapi imeandikwa kuwa kupika ni kazi ya kike? Acha zako Juma, kwa kifupi tu ni kuwa mimi binafsi siwezi kabisa kufurahia swala la kupika tena wiki yote hii!”
“Ila mtoto anataka kula chakula kilichopikw ana wewe tu!”
“Mmmmh mbona huwa anapika Anna, na mtoto anakula chakula hicho!!”
“Una uhakika gani kuwa Anna ndio alikuwa anapika?”
“Sasa apike nani wakati Anna ndio ilikuwa kazi yake?”
“Ngoja nikuulize swali mke wangu, je ni vizuri kupika ukiwa unajua kuwa unapika au kupika ukiwa hujui kuwa unapika?”
“Kivipi?”
“Hata nikikueleweshe hautaelewa sababu hutaki kuelewa”
“Sasa ndio nini hivyo Juma? Kama kusema si useme tu”
“Tulale tu sasa, naona tutabishana hadi kesho”
Mariam alimuangalia mumewe ila hakusema neno lolote zaidi zaidi alijilaza tu huku akiwa na hasira sana.

Juma akiwa kwenye shughuli zake leo, Pendo ndo alienda na kuanza kuongea nae hii ni toka kipindi kile ambacho Pendo alipata matatizo. Basi Pendo alimuuliza Juma,
“Hivi Juma, yule mtoto wako ni wa kawaida kweli?”
Hapo Juma ndio akaelewa kuwa Pendo anakumbukumbu za lile tukio ambalo lilimtokea ila Juma aliamua kujigelesha.
“Mmmmh Juma mbona hunijibu?”
“Sasa nikujibu nini? Mwanangu ni wa kawaida tu. Tuongee mengine Pendo”
“Tuongee mengine yapi? Mwanao kanizaba kibao hiko hadi niliona kifo jamani, khaaa yule sio mtoto, yule sio mtoto kabisa na jina la Pendo umbadilishe”
“Sawa nimekuelewa Pendo, ila naomba hayo mambo yaishie kwako na kwangu”
“Sasa nikwambie kitu!”
“Niambie”
“Unajua ni kitu gani nimejifunza kwa mwanao pale baada ya lile tukio?”
“Kitu gani?”
“Kumbe sio vizuri kushobokea shobokea watoto ambao huwajui, ni vyema kumfahamu kwanza mtoto unayemshobokea, yani mimi nilikuwa naona kifo hiki hapa kabisa kwa kitendo ambacho yule mtoto amenifanyia. Ila namshukuru Mungu nimepona, sasa hivi nitakuwa makini sana, ujinga wa kuvamia vamia watoto wa watu na kujifanya nawajua sana nauacha kabisa”
“Sawa ila usiseme kwa wengine Pendo, ibaki kuwa siri yet utu”
“Sawa, hakuna tatizo ila siwezi kusahau”
Juma alimuangalia tu Pendo na wala hakutaka kumuuliza zaidi maana alihisi pengine Pendo anaweza kujua na lile swala la kushikwa shavu na kupona kabisa, mwishowe ataona kamavile Juma ni mchawi kwahiyo Juma hakuendelea kuongea tena kuhusu mtoto wake.

Leo Mariam akiwa ametulia pale nyumbani, ndipo alipofika yule jirani yao, aliweza kuonana nae sababu alikuwa yupo nje kwa muda huu, yule jirani akasema,
“Bora hata nimekukuta hapa nje, najua ukikaa ndani ningegonga hadi ningeondoka”
“Karibu sana”
Basi na yule jirani alikaa pale nje na kuanza kuongea na Mariam, aliongea nae mambo mengi ya ule mtaa,
“Vipi mwanamke mwenzangu, huonekani kwenye sherehe, huonekani kwenye msiba, tatizo ni nini?”
“Dah! Sijazoea’
“Haya mambo kwani kuna aliyezoea? Tunafanya ili kuboresha ujirani, ushirikiano ni ushindi”
“Ndio lakini mimi sijazoeana na watu”
“Sasa hao watu utawazoea vipi kama unajifungia ndani? Huwezi kumzoea yoyote kama unajifungia, unatakiwa ushirikiane na watu, ukisikia harusi au msiba. Mfano majuzi tu hapo kulikuwa na msiba, ungekuja pale hata kujishughulisha kwenye kazi kadhaa kama kupika, kuosha vyombo watu wanasema kweli kuna mwanamke mwenzetu sehemu fulani hata ukipatwa na matatizo inakuwa rahisi kwa watu kuja kukuona ndugu yangu”
“Duh! Kwahiyo mtu akifika huko msibani lazima apike au aoshe vyombo!”
“Yani ni katika ujirani tu na kusaidiana kazi, unaweza fanya hata kugawa chakula ila uonekane na wewe unajishughulisha. Mbona unaongea vizuri tu wewe!! Ni lazima watu utafahamiana nao vizuri.”
Mariam akaguna tu, yule jirani akaomba maji kwahiyo Mariam akamuita Anna amletee yule jirani maji ila baada ya Yule jirani kupokea yale maji baada ya Anna kuondoka tu alimuuliza Mariam,
“Umemtoa wapi huyo binti?”
“Aaaaah ni msichana wangu wa kazi”
“Ndio, umemtoa wapi?”
“Alikuja tu mwenyewe, alikuwa ana shida na kazi”
“Kwahiyo hupafahamu kwao, hufahamu ndugu zake wala nini?”
“Hapana siwafahamu hata hivyo ni yatima”
“Hata kama ni yatima lakini lazima ana ndugu zake tu”
“Aaaah mimi naona kumfahamu yeye inatosha”
“Pole sana”
“Pole ya nini tena?”
Yule jirani alishusha chini kile kikombe cha maji na wala hakunywa wala nini badala yake alimuaga tu Mariam na kuondoka zake.

Usiku wa leo, Mariam alimsimulia mumewe Juma juu ya yule jirani yake na kile ambacho amekifanya, Juma alishangaa sana na kumuuliza vizuri mke wake,
“Kwahiyo hayo maji hakunywa?”
“Hakunyw andio, tuliyamwaga tu. Kaniuliza maswali kibao kuhusu Anna, na mwisho wa siku kaniambia pole sana”
“Namshukuru kwa hilo”
“Kwanini?”
“Labda wakija watu wa nje kama hivyo wataweza kubadili akili yako Mariam, na utaweza kutambua kuwa Anna ni binti wa aina gani, mimi kama baba wa familia naumia sana, nateseka maana ukweli wote ninaujua ila wewe unazidi kukumbatia makosa ya Anna”
“Niweke wazi nikuelewe”
“Nishakuelewesha hadi basi, Anna ni mchawi anatakiwa tumuondoe humu”
“Sawa, sasa tukimuondoa Anna, tunafanyeje na huyo mtoto wetu? Unadhani kuna ambaye ataweza kumlea huyo mtoto kama ambavyo Anna anamlea?”
“Mmmmh hapo pagumu mke wangu, ila kiukweli Anna hatufai kabisa, tena hatufai hata kidogo”
Mariam alitafakari kidogo na kumuomba mumewe tu kwa muda huo wapate kulala.

Leo Mariam alisema kuwa hatopika tena chakula, ila mama Shamimu na yeye alishachukia yani yeye kufanya kazi zote wakati mdada wa kazi yupo tu, akaamua kumpigia mama yake na kumueleza kila kitu,
“Hebu kampe simu Juma niongee nae, asiniletee ujinga mie”
Mama Shamimu alitoka chumbani na kumfata Juma sebleni aliyekuwa amekaa na mke wake ambaye alikuwa alimlalamikia kuwa amechoka kupika, Juma alichukua ile simu,
“Hivi wewe Juma una akili gani? Kweli unakubali dada yako ateseke sababu ya hiko kitoto!”
“Sina cha kufanya mama”
“Huna cha kufanya kivipi? Huo ni upuuzi huo”
“Sasa mama nifanyeje jamani!”
“Si mlisema kinaongea eeeeh! Mpe simu niongee nae”
Juma akampa simu mtoto ambaye moja kwa moja aliiweka sikioni ila baada ya kuongea kidogo tu, huyu mtoto alibamiza simu chini yani Juma alisikitika na kuokota simu ya dada yake ikiwa vipande vipande.
Mama Shamimu alichukia sana ila hakujua cha kufanya na hakuna aliyejua kuwa mtoto aliongea nini na bibi yake.
Basi Juma akaenda kuchukua simu yake na kumpigia mama yake ambapo simu haikupokelewa kwanza, alipopiga tena ndio ilipokelewa, Juma alimuuliza mama yake kuwa imekuwaje,
“Naumwa mwanangu, tena naunwa sana”
Hadi sauti ya mama yake ilibadilika kabisa, ilionekan ni mgonjwa haswa, Juma alishangaa na kuuliza,
“Kwani imekuwaje mama?”
“Mwanangu hako katoto kachawi, tumbo la kuhara limenishika uwiii ngoja niende chooni”
Yule mama akakata simu yani Juma hata hakujua ataanzia wapi.

Juma aliamua kutoka nje yeye, Mariam na mama Shamimu ili wajaribu kuongea na wajue cha kufanya.
“Hivi jamani tufanyeje? Mama nyumbani huko ni mgonjwa hoi sababu ya mtoto”
“Juma mdogo wangu, mficha maradhi kifo humuumbua”
“Sasa dada nifanye kitu gani?”
Mama Shamimu alifikiria jambo na kusema,
“Jamani, mnaonaje haka katoto tukakatupe baharini?”
“Mmmh jamani mtoto wangu tena tukamtupe baharini?”
“Mtoto wako ila huyo sio mtoto kaka, ona kama hivyo mama anaumwa ila chanzo ni huyo mtoto. Atatuua ukoo mzima”
“Tufanye nini?”
“Twende tukamtupe kaka, hii ni kwa usalama wako na usalama wa familia.”
“Ila dada kumbuka kuwa sina mtoto mwingine zaidi ya huyu tu!”
“Naelewa kaka ila utapata watoto wengine na usikute ni yeye ndio anakuzibia nafasi ya wewe kupata watoto wengine. Kubali tukamtupe huyu mtoto kaka”
Juma aliamua tu kukubaliana nao maana hadi ndugu zake walianza kumpigia simu ila wajue kuwa itakuja kuhusu huyo mtoto.

Kulipokucha kabisa, waliamka saa kumi alfajiri kabla wengine hawajaamka na kwenda chumbani kwa Anna kisha wakamchukua mtoto na kuondoka nae pale kabisa ilikuwa rahisi kwao na wala hawakupata maswali maana Anna alikuwa amelala fofofo. Walitoka nje na moja kwa moja walipanda bajaji ambayo Juma alikuwa ameikodi na kuanza kuelekea hukowalikopanga ili kumtupa mtoto, halafu mtoto alikuwa bado amelala kwahiyo hii ikawa ni furaha sana kwao.
Walovyofika baharini, Juma alikataa kumtupia ndani ya bahari alidai tu awekwe kwenye pango akiamka anaweza chukuliwa na mtu mwingine kwahiyo walifanya hivyo.
Na sasa waliamua kurudi nyumbani huku wakiweka mikakati ya kumfukuza na Anna pia, yani Mariam alikubali sababu mtoto hayupo tena.
Walifika nyumbani kwenye mida ya saa moja asubuhi, ile wanafungua mlango walimkuta Anna akimnywesha uji yule mtoto.

Itaendelea.....!!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile. 
Leo Story ya MWANAUME WA DAR itaendelea.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni