Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 19

MTOTO WA MAAJABU: 19

Hapo na Mariam aliingilia kati kumkataza wifi yake asimpe jina mtoto ndipo mama Shamimu aliposema,
“Kheee Mariam, bado roho mbaya hujaacha tu hadi leo jamani! Mimi ni shangazi wa huyu mtoto, nampa jina sasa tuone mtafanyaje, kuanzia sasa huyu mtoto ataitwa Khadija”
Hapo hadi Juma aliogopa maana yule mtoto alikunja sura sana akionyesha kuwa amekasirishwa, na alikuwa amekaa kwenye kochi ila akashuka chini.
Walimuona mtoto wao akianza kumuelekea mama Shamimu sasa, kwakweli Juma aliinuka na kwenda kupiga magoti mbele ya yule mtoto huku akisema,
“Samahani mwanangu, huyu kapitiwa tu, naomba nisamehe mimi mwanangu”
Huyu mtoto hakujibu ila alirudi kwenye kochi na kupanda kukaa, ila muda huu Juma alimuangalia Anna na kumwambia tena kwa upole kabisa,
“Anna nakuomba kamlaze mtoto chumbani”
Anna hakubisha kwani aliinuka na kumbeba mtoto kisha akaenda nae chumbani yani Juma alibaki anapumua tu kwa hofu na uoga, yani kile kitendo kilikuwa kinamshangaza sana mama Shamimu ilibidi kulipotulia kidogo aiuliza,
“Jamani mbona sielewi kitu!”
Juma akamsogelea na kumshika dada yake mkono na kwenda nae nje yani mpaka muda ule Juma alikuwa haamini amini kama dada yake amepona maana asingejua cha kufanya nae baada ya kupigwa shavu.

Moja kwa moja Juma na dada yake walienda kwenye kivuli na kuongea ambapo Juma alimsihi kwanza dada yake kutokumuita jina lolote yule mtoto.
“Nakuomba dada yangu, usimuite jina lolote lile huyu mtoto wangu nakuomba sana”
“Kwanini Juma?”
“Dada, kwa kifupi mtoto wangu sio wa kawaida”
“Kivipi?”
“Ni hivi dada yangu, mara ya kwanza kabisa mama alisema kuwa mtoto aitwe jina lake la Ashura ila mke wangu aliambiwa na mtoto kuwa halitaki jina hilo ilikuwa balaa sana hapa nyumbani wakati mtoto amekataa hilo jina”
“Kheeee kipindi hiko mtoto alikuwa na muda gani?”
“Naona sijui kwenye siku nne hivi, halafu kuna kipindi mama akamuita mwenyewe Ashutra, khaaa mtoto huyu alimsonya mama yangu”
“Na ninavyosema ni kuwa yule mgeni aliyezimia Juzi ni sababu ya kumuita jina mtoto wangu ndiomana sikutaka ijirudie kabisa”
“Hebu subiri kwanza Juma, kwahiyo mtoto wako pale alipo anaongea?”
“Ndio, tena anaongea maneno yote. Sasa wewe unashangaa kwenye kuongea tu! Mbona hujashangaa kwenye kutembea?”
“Unajua kwasasa ndio kama unanifungua macho hivi! Sio kipindi kirefu kusikia kuwa mkeo kajifungua ila nilivyokuja na kumuona mtoto ni mkubwa sikuwa na tatizo lolote, ila swala la kuongea hapo ndio sielewi. Mbona sijawahi kumsikia akiongea? Halafu toka ana siku nne ana ongea jamani!”
“Nini siku nne dada!! Ni toka amaezaliwa huyu mtoto anaongea ndiomana nakwambia kuwa mwanangu sio wa kawaida”
“Kheeee basi mwanao ni mtoto wa maajabu jamani, kwanini inakuwa hivyo lakini? Wewe Juma upo kawaida, mkeo yupo kawaida ila unaenda kuzaa mtoto wa maajabu, kwanini lakini?”
“Hata najua basi dada, halafu kumbuka mimba ya huyu mtoto ilikaa miaka miwili, yani mke wangu alikaa na mimba miaka miwili ndio akajifungua”
“Kheeee mimba kama ya tembo loh!! Mambo ya ajabu haya unaniambia kaka, mnawezaje sasa kuishi na mtoto wa aina hii humu ndani?”
“Hatuna cha kufanya dada, unadhani tutafanyaje? Ni mtoto wetu unadhani tutafanyaje?”
“Tena futa hiyo kauli kaka, hiko kiumbe cha ajabu sio mtoto wenu kabisa, mnaonaje mkikitupa huko, mnaendelea kukikumbatia cha nini? Hayo ni maajabu”
“Khaaaa dada, tatizo nimeshamzoea tayari. Namtupaje wakati nimzoea, ananiogopesha lakini nimeshamzoea, ilimradi hatudhuru ndani basi hana tatizo kwetu”
“Kheeee umerogwa wewe, poleni sana. Sio mtoto huyo mliyenaye, usikute ni kajini, poleni sana”
Kisha Juma akamuuliza dada yake,
“Eeeeh dada, una mpango wa kukaa hapa hadi lini sababu hatujaulizana!”
“Weeee unadhani nina hadi lini hapa! Kesho naondoka, siwezi kwakweli hayo maajabu mbaki nayo wenyewe mlioyazoea. Tena ngoja nikapange nguo”
“Mmmmh dada”
“Hakuna cha kuguna, mkeo ni mvivu hatari. Kila leo niwe naangalia tu na kumuona amelala kila muda hakuna anachofanya, yeye kazi ni kula, kunywa na kulala. Huo ni ujinga, mwanamke gani anataka kuishi kama yeye? Hata kama mwanamke ni mama wa nyumbani ila anatakiwa ajishughulishe, kufanya kazi za nyumbani napo ni kujishughulisha ila mtu anakuwa kula kulala wa nini! Sipawezi hapa aisee”
Mama Shamimu aliagana na Juma pale na moja kwa moja kwenda chumbani kwake kupanga nguo.

Wakati mama Shamimu akipanga nguo zake vizuri kwaajili ya safari ya kesho aliamua kumpigia simu mama yao ili kumwambia kuwa anaenda nyumbani,
“Mama, nakuja. Huku paenishinda, nakuja ili niishi kidogo hapo nyumbani mama yangu”
“Pamekushinda kwasababu gani?”
“Mama, haka katoto ka Juma sio katoto wala nini, katoto haka lazima katakuwa ni kajini. Nikija nitakusimulia vizuri mama yangu, niliyoyaona ni mengi halafu haya niliyoambiwa ndio nimeogopa zaidi, nakuja kesho mama nitakusimulia”
Muda huu Mariam alikuwa mlangoni kwa wifi yake kwahiyo alipomaliza tu kuongea na simu akaingia na kumuuliza,
“Kwani wifi uliyoyaona ni yapi tena?”
“Hivi nyie mnajiona mnaishi na mtoto humu ndani! Huyo sio mtoto ni jini”
“Mmmmh kwanini wifi?”
“Kama hamuamini, siku moja muite huyo mtoto wenu jini halafu uone kitu kitakavyokuwa”
“Mmmmh wifi jamani! Yani mtoto wetu tukamuite jini!”
“Khaaa, hivi Mariam hujafunguka macho tu! Hakuna mtoto hapo ni mauza uza tu hayo, nawahurumia sana kwa jinsi ambavyo mnashindwa kuamka na kuona kuwa hapo hamna mtoto”
“Kumbuka dada nimebeba mimba kwa miaka miwili”
“Hata ungebeba kwa miaka saba ila hujazaa mtoto, umezaa jini”
Mama Shamimu aliendelea kupakia nguo zake kwani alionekana kushukizwa sana na mambo yake.

Usiku ule, Juma alikaa na mke wake chumbani wakiongea kuhusu lile tukio la mtoto wao na mama Shamimu halafu na kuhusu mama Shamimu kuondoka,
“Yani najua dada yangu yule ananitangazia kila sehemu mambo yote na watu wote wayajua tu kuwa mimi nina mtoto wa ajabu jamani!”
“Ila na wewe kwanini ulimsimulia kila kitu dada yako?”
“Sikuwa na jinsi ili tu asirudie tena kumuita mtoto wetu kwa jina lolote lile Mariam, mimi nimefanya yote yale kumuokoa yeye mwenyewe unadhani angedhabwa kibao na mtoto wetu ingekuwaje? Nani angemsaidia kupona? Mimi naogopa sana toka lile tukio la Pendo naogopa sana”
“Lazima kuogopa ila ndugu zako hadi wanakera, unajua wana kiherehere sana, wanakera jamani sijapata kuona”
“Ila atatutangaza sana yule”
“Mwache tu atutangaze, hakuna cha kufanya. Hii ni aibu yetu, mtoto ni wa kwetu kwahiyo lazima tukubali kuaibika mume wangu”
Walikubaliana tu mule na kulala ingawa ukweli ulijulikana hapo kuwa jamii yote itajua ukweli ingawa ile mimba iliyokaa zaidi ya miaka miwili walikimbia kwa watu wao wa karibu na kuhamia huko mbali ili isitokee mtu kuuliza ni kwanini hiyo mimba huzai muda unapita tu, ila huku tangu wameamia hakuna mtu aliyekuwa akiwafatilia kwahiyo waliishi kwa amani ila yule dada wa Juma alimpa mashaka sana Juma kwani alijua pale kila kitu kitasemwa kwa watu tu.

Mapema kabia leo, mama Shamimu alikuwa tayari ameshajiandaa kwaajili ya kuondoka ila Juma alimtaka wanywe chai kwanza halafu ndio amsindikize ambapo alifanya hivyo, na walipomaliza ndio walivuta mizigo kwaajili ya kuondoka ila kitoto cha Juma kikawasogelea na kumwambia Juma,
“Baba, mwambie shangazi aniombe msamaha”
Kila mtu pale ndani alimuangalia mwenzie hakuna aliyeelewa na wala hakuna aliyejibu kwa muda ule, kisha baada ya muda kidogo Juma alimuangalia dada yake na kumwambia,
“Dada Khadija, nakuomba tu umuombe msamaha mtoto”
Ila mama Shamimu aling’aka pale na kusema,
“Weeee anitoleee balaa mimi, unafikiri huo ujini wake ndio utanitisha mimi!! Hii ni namba nyingine, mimi ni kisiki cha mpingo siendeshwi hovyo na mambo ya kijinga, nishwahi kuonana na wachawi macho kwa macho sembuse huo jini aliyejificha kwenye umbo la binadamu tena mtoto! Asinibabaishe mimi”
Mama Shamimu alinyanyua mizigo yake na kuwaambia,
“Kama mnataka nisindikizeni, msipotaka niacheni niende mwenyewe”
Juma hakuwa na la kufanya zaidi zaidi aliamua tu kumsindikiza dada yake huku akiwa ameambatana na Mariam ila nyumbani alibaki Anna na mtoto.

Basi waliondoka huku mama Shamimu akilalamika njia nzima kuwa mule ndani wanendekeza mambo ya kijinga,
“Yani sijaamini hata na wewe Juma umefungwa ufahamu na kile kitoto kidogo! Mimi siwezi kusumbuliwa na mtoto wa vile”
Kisha Mariam akamwambia mama Shamimu,
“Ila wifi, kwani ungemuomba msamaha ungepunhukiwa na nini?”
“Nimuombe msamaha kwa lipi? Na kwanini nimuombe msamaha? Mimi sio mjinga kama mnavyofikiria, sifanyi mambo ya kijinga mimi. Hii ni namba nyingine kabisa, kama anawachezea basi abaki kuwachezea nyie wenyewe na sio mimi kabisa”
“Mmmmh dada, sijaamini kama ungekuwa mkali kiasi hiko!”
“Nimekwambia Juma, mimi sipendi ujinga”
Basi walifika stendi ambako alipanda gari na kuwaaga na kuondoka zake, kwahiyo Mariam akawa anarudi na Juma nyumbani huku akimwambia,
“Yule dada yako shauri yake, asije kushangaa karudishwa tena nyumbani kwetu!”
“Mmmmh haiwezekani, arudishwe kivipi sasa?”
“Kimazingara kama ambavyo mimi nilikuwa narudishwa, nina uhakika ni mtoto ndio anafanya hayo mambo”
“Ila haiwezekani, kumbuka tumempandisha kwenye daladala kabisa na tumeshuhudia daladala ikiondoka!”
“Haijalishi Juma, kuna siku mimi nilienda kwetu kabisa, nikashuka hadi stendi ya kwetu nikapita njia ya kwetu kufika tu nyumbani kugonga mlango nikafunguliwa na yule msichana wetu wa kazi aliyepita, nilishangaa sana kuwa nimerudije kwangu wakati niliondoka kwetu? Halafu kumbuka kuwa kuna siku nililala kwetu ila nikaja kujikuta kuwa nimelala huku nyumbani kwahiyo kila kitu kinawezekana”
“Inamaana ni uchawi huo au!! Ila mke wangu kumbuka dada yangu kasema yeye ni kisiki cha mpingo”
“Kumbuka hata mimi niliwahi sema kuwa sirogeki na nilikuwa naamini hivyo sababu ya kinga niliyokuwa nimepewa kwa yule mganga ila mbona narogeka sasa? Mtoto ananiroga atakavyo”
“Ila mke wangu, inawezekana ikawa Anna ndio amesababisha mtoto wetu kuwa hivyo!”
“Weeee kale katoto kapo vile hata kabla ya Anna, ndiomana mimi nakukatalia kuhusu kumtoa Anna, unadhani ni mdada gani wa kazi ataweza kuishi na kale katoto? Hakuna, wacha yule yule Anna aliyemzoea”
Walikuwa wakiongea tu, ila wakati wanakaribia kufika kwao, walikutana na mmama ambaye ni jirani yao ila kwavile nyumba za pale zipo mbalimbali ilikuwa ni ngumu kuonana mara kwa mara, wakasalimiana pale ambapo yule mama akauliza,
“Kheeee kumbe ulishajifungua dada?”
“Ndio, nilishajifungua”
“Mtoto gani?”
“Wa kike”
“Aaaah!! Anaitwa nani?”
Hapa ndipo huwa paguma kwa Juma na Mariam, ila Mariam akamwambia huyu mama,
“Anaitwa mtoto”
“Aaaah sawa, nitakuja basi kumsalimia”
Walishindwa kumkatalia ilibidi tu wamkubalie ingawa walijua ni tatizo pindi akifika huko nyumbani kwao.
Basi moja kwa moja walirudi nyumbani kwao na kuendelea na mambo mengine.

Leo asubuhi wakati Juma anajiandaa kuondoka kwenda kwenye shughuli zake, alimkumbusha mke wake kuhusu alichosema kuwa dada yake angerudishwa kichawi,
“Umeona Mariam, dada Khadija haijawezekana kumrudisha kichawi. Yule dada ni mzito”
“Mzito wa wapi, mtaani kwake kwenyewe kakimbia wachawi, angekuwa mzito si asingekimbia wachawi sasa!”
“Lakini si unaona, wewe huwa unarudishwa ila yeye siku imepita na leo ni siku nyingine ila hajarudishwa, inabidi mtoto wetu tuwe tunamletea watu jeuri na wagumu kama dada yangu”
Mariam aliitikia tu, kisha Juma aliondoka zake halafu Mariam nae aliendelea na mambo yake ya kulala.

Siku ya leo, Juma alipita kwenye ile njia ambayo huwa anakutana na yule binti, nia yake ilikuwa ni kumshukuru maana lile jambo la Pendo kupona kabisa lilikuwa ni kubwa sana kwake. Ila alifika eneo lile na kusimama sana bila yule binti kutokea, kabidi aite kama yule binti alivyowahi kumwambia,
“Rafiki yake Mishi, rafiki yake Mishi”
Lakini yule binti hakutokea, alisubiri sana Juma na mwisho wa siku akaona ni vyema tu akaondoka na kwenda kuendelea na shughuli zake ila kiukweli Juma alikosa raha kabisa kwa kutokumuona yule bintiu.
Muda wa kutoka tena Juma alipita pale pale ambapo huwa anakutana na yule binti, alimuita ila yule binti hakuitika, wala hakutokezea hadi mwisho wa siku ikabidi tu Juma aondoke zake kurudi nyumbani kwake.
Juma alipokuwa njiani kurudi kwake, alikutana na yule jirani yao ambaye walikutana nae jana, walisalimiana kisha yule jirani alimuuliza Juma,
“Kwani mkeo ana matatizo ya masikio?”
“Kwanini?”
“Nilienda nyumbani kwako leo kama nilivyoahidi jana, nimepiga hodi sana tu lakini hakuna aliyenifungulia ila nikazunguka hivi na kumuona mkeo yupo shambani anapalilia mahindi, nikamuita pale lakini hakuitika wala hakugeuka aliendelea kupalilia mahindi tu”
“Duh!! Kwanini usingemsogelea umshtue?”
“Nisingeweza, nyumba yako kule nyumba si umeizungushia maua ya miba!”
Ndipo Juma akakumbuka kuwa huwezi kwenda nyuma ya nyumba yake bila kupita mlango wa mbele maana kule nyuma alipanda kote maua ya miba, kwahiyo ipo kama uzio wa mahali pale. Alimuangalia yule jirani yake na kumwambia,
“Ngoja nitamueleza hayo tu hakuna tatizo, itakuwa hakukusikia”
Basi Juma aliagana na yule jirani ila moja kwa moja Juma alijua tu ni kazi ya Anna, inamaana siku hiyo alikuwa amemuweka mkewe apalilie mahindi, yani alisikitika sana na kusema,
“Ndiomana mke wangu anachoka sana, apike, apalilie mahindi, afue, jamani huyu Anna ana nini! Nifanye nini kumtoa nyumbani kwangu? Ila nikimtoa tutafanyaje na yule mtoto? Aaaahh najikuta nikikosa hata maamuzi kwakweli”
Juma aliondoka tu na kurudi nyumbani kwake.

Leo baada ya kupata chakula cha usiku, walikaa pale sebleni wakiongea maana ilikuwa ni mapema sana kwenda kulala, Mariam alimwambia Juma,
“Mama yako kanipigia sana simu leo sijui kuna nini! Hebu mpigie”
Juma akachukua simu yake na kumpigia mama yake ambaye kwa muda mfupi tu alipokea na kuanza kuongea nae,
“Weee Juma, dada yako alisema kuwa jana anakuja ila hadi leo hajafika halafu simu yake ukipiga haipatikani”
“Duh!! Huku alishaondoka tangu jana, labda kaenda moja kwa moja nyumbani kwake”
“Hapana, Khadija hana mambo ya uongo. Huwa akisema kitu lazima kiwe kweli, hawezi kusema anakuja huku halafu aende nyumbani kwake hakuna kitu cha namna hiyo”
“Ila mama, huku tulimsindikiza hadi kituoni na alipanda daladala tuliacha daladala ikiondoka”
“Sasa atakuwa ameishia wapi? Nishaanza kupata wasiwasi, na haya mambo ya ajali jamani”
“Usiseme hivyo mama, sidhani kama amepata ajali hata hivyo ajali ingetokea tungesikia tu mama yangu. Hakuna ajali yoyote natumaini dada Khadija yupo salama”
“Sasa mbona hapatikani? Yani kutokupatikana hewani ndio kunanipa mashaka, hebu nenda mkaulizie vizuri kuhusu gari alilopanda Khadija, si unajua mama yenu nina presha jamani!”
“Sawa mama, nitafatilia na nitakupa jibu tu”
Juma akamuangalia Mariam na kumuelezea ila Mariam akamwambia mumewe,
“Kabla ya kujisumbua kwenda huko stendi kuulizia basi alilopanda wifi limekuwaje, muulize kwanza mtoto wako!”
“Kivipi?”
“Nakwambia muulize, maana dada yako aliondoka kwa mbwembwe hapa sijui kama yupo salama”
Juma alimuangalia Mariam kisha alimuangalia mwanae ambaye alikuwa amekaa kwenye kiti huku akiogopa ogopa kumuuliza maana hakujua kuwa ataanzia wapi, ila alishangaa mtoto akimwambia,
“Niulize baba”
Juma alitetemeka kwanza na kumuuliza,
“Shangazi yako yuko wapi”
Kale katoto kalicheka kiasi na leo ilikuwa ni mara ya kwanza kuona kale katoto kakicheka, na kalikuwa kazuri sana hata Juma aliweza kuuona uzuri wa yule mtoto wake, ila baada ya kumuangalia kwa muda yule mtoto aliwajibu,
“Yupo hapo nje”
Juma na Mariam waliangaliana kwa mshangao, kisha Juma akainuka na kwenda kufungua mlango kweli kabisa alimkuta dada yake mlangoni akiwa na mafurushi yake huku kamshikilia mtoto wake.

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni