Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 18

MTOTO WA MAAJABU: 18

Pendo akatabasamu na kumsogelea yule mtoto kisha akainama na kumwambia,
“Pendo, niamkie mtoto mzuri”
Pendo alishangaa yule mtoto akimnasa kibao cha nguvu.
Kwakweli Pendo aliogopa sana na kuinuka ila alishikwa na kizunguzungu kikali sana kilichompelekea aanguke na kupoteza fahamu, kwakweli Juma hata hakuelewa maana jambo hili lilitokea ndani ya muda mfupi tu, Juma alijikuta akiita,
“Mariam, wee Mariam wee”
Hapo Mariam akiwa ameambatana na wifi yake walitoka nje, Juma aliwauliza kwa ukali,
“Mmemuachaje huyu mtoto nje?”
“Mmmmh sijui shemeji ametokaje, labda sababu mlango ulikuwa wazi”
“Kelele na wewe Anna, mchawi mkubwa wewe”
Mariam hakuelewa kitu, na kumuuliza mumewe,
“Kwani nini kimetokea?”
Juma hakujibu kwanza na kusema,
“Ngoja nikaite bajaji halafu nitawaelezea”
Juma alienda kuita bajaji ila pale kila mmoja alikuwa akishangaa maana hakuna aliyekuwa akijua kuwa ni kitu gani ambacho kimetokea pale kwa muda, ukizingatia tukio lile limeshuhudiwa na wale wale wahusika.
Dada yake Juma akauliza,
“Kwani imekuwaje hapa jamani?”
“Kuna anayeelewa basi wifi!”
“Kwani huyu mwanamke aliyeanguka hapo humjui?”
“Hata simjui, ndio leo namuona hapo, naogopa hata kusogea maana sielewi ni kitu gani kimetokea”
Muda kidogo Juma alifika na bajaji na kumpakia Pendo kwenye bajaji akisema kuwa anamuwaisha hospitali na atawaeleza labda akirudi.
Wakina Mariam wakarudi ndani tu bila ya kuelewa kitu chochote kilichotokea, kisha mama Shamimu akahoji swala la Juma kumuita Anna mchawi, akamuangalia Mariam na kumuuliza,
“Vipi mbona mumeo kamuita huyu binti mchawi?”
“Wifi yangu, yani huyo kaka yako anajitambua mwenyewe, aliwahi kumtaka huyo binti ila binti alimkataa basi toka hapo ndio anamuita mchawi”
“Kheee jamani, wanaume wabaya sana. Yani kumtaka binti mdogo hivyo! Unajua Juma kachelewa tu kuzaa ila angewahi huenda huyu binti angekuwa ni binti yake”
“Umeona wifi eeeh! Lakini yeye anajiona mtoto na kumtaka mtoto mdogo hivyo”
“Sasa baada ya hilo tukio umeamuaje? Maana wamama wengi ikitokea hivyo huwa wanawaondoa wale wadada wa kazi”
“Umuondoe halafu umlete mwingine wa kumkubali! Huyu huyu aliyemkataa ndio ananifaa, binti ana misimamo sana huyu hadi raha nakwambia, huwa sina mashaka hata nimuache yeye na mume wangu tu kwa wiki nzima sina mashaka”
Mama Shaminu alimpongeza kwa hilo la kumuamini sana binti yake wa kazi na pia hakupenda kwa swala la kaka yake kumtaka binti wa kazi kimapenzi yani hakupenda kabisa.

Usiku wa leo, Juma alikaa chumbani na Mariam ili kumuelezea kile kilichotokea maana Pendo alikuwa amelazwa,
“Yani mdada wa watu kalazwa, imeniuma sana”
“Kwani ilikuwaje?”
“Si hako katoto kamempiga kibao”
“Duh!! Lakini mume wangu huwa naongea mara kwa mara kuhusu huyu mtoto lakini hunielewi wala hunisikii, huwa nikikwambia linakuingia kulia na kukutokea kushoto yani huwa hunielewi kabisa”
“Sasa, tufanye nimekuelewa, nini kinafuata sasa. Kitu gani kinafanyika kwa mtoto?”
“Sijui ila mimi naona tuzunguke kwa waganga wa kienyeji ili tujue kuwa tatizo la mtoto wetu liko wapi? Kwanza ni mtoto mzuri, kila mtu akimuona anavutiwa nae kabla hajajua matatizo ya huyu mtoto ila mtu akijua kuwa mtoto alijikata kitovu mwenyewe huyu ndio mtu lazima aogope kiasi, mtu akijua mtoto alipozaliwa aliongea huyu, lazima aogope, mtoto kazaliwa na meno tena meno imara kabisa sio meno ya plastiki wanayosemaga wala nini ila kazaliwa na meno mazima kabisa, lazima mtu aogope, katoto kadogo ila kana mambo ya ajabu hatari hadi anaogopesha kwakweli”
“Mke wangu kwakweli, inatakiwa tufikirie cha kufanya mapema kabla maharibifu hayajatokea mengi kwetu”
Yani walipanga mambo mbalimbali pale na kuamua tu kulala kwani Juma alipanga kesho yake tena kwenda asubuhi kumuona Pendo.

Leo Juma alienda tena hospitali kwakweli hali ya Pendo haikuwa nzuri kabisa, usoni alikuwa amevimba sana upande mmoja wa shavu lake, Juma alielewa kuwa ndio upande ambao Pendo alizabwa kibao na mtoto wake, alisikitika sana. Pendo hakuwa wa kujibu chochote wala nini, hospitali walimuwekea drip utu ya maji na chakula maana hakuna alichokuwa anaweza kufanya.
Juma alirudi kazini ila kusema ukweli aliogopa zaidi ya kusema tu kuwa Pendo anaumwa,
“Ila mara ya mwisho jana uliondoka naye wewe Juma?”
“Ndio niliondoka nae, ila hakukaa sana nyumbani kwangu na baada ya muda tu akaniaga ila alipokuwa kwake alinipigia simu kuwa anaumwa”
“Mbona leo nimepita nyumbani kwake sijamkuta? Halafu Pendo asije kazini bila ruhusa kweli inawezekana? Ingekuwa ni wewe Juma hakuna mwenyewe angeshangaa sababu wewe ni kawaida yako ila Pendo kweli jamani!”
“Huwezi jua labda kaenda hospitali”
Juma aliogopa kusema ukweli, yani alihisi kama watu watamshikilia yeye na imani za kishirikina, alitaka Pendo apone angalau kidogo ndio awaambie watu kuwa Pendo amelazwa hospitali gani.
Kwahiyo alikuwa na kibarua cha kwenda kumuona Pendo, asubuhi, mchana na jioni.
Hadi muda anaenda nyumbani kwake alikuwa akisikitika sana na yale ambayo yametokea.

Leo jioni, mama Shamimu akiwa anaongea na wifi yake Mariam alimkumbusha kuhusu kupika chapati,
“Wifi jamani, nimejikuta nikitamani chapati zilizopikwa na wewe balaa. Nakumbuka umewahi kutupikia chapati mara moja tu na tulijiramba sana, asubuhi basi tupikie wifi”
“Khaaaa wifi yangu, kabla sijabeba mimba nilikuwa ni mvivu na kama kupika nilikuwa nikipika mara moja moja sana. Nilivyokuwa na mimba ndio kabisa yani, nilikuwa mvivu mara dufu yani nikifanya kazi ni mara moja moja sana, na ilikuwa inatokea nini utakuta mtoto ananipiga sana mateke hadi nishike kazi ndio anatulia ila nilipojifungua jamani uwiiiii ule uvivu wangu umerudi maradufu, yani siku hizi hata kushika chombo kusuuza siwezi ndio sembuse kupika chapati! Weee wifi wewe, mimi siwezi kabisa kufanya kitu kama hicho wifi yangu”
“Inaonyesha mtoto wako hakupenda uvivu wako ndiomana alikuwa akikupiga mateke hadi ushike kazi, ila wifi yangu watu wengi wakizaa hata kama walikuwa wavivu awali basi ule uvivu wao huwaisha na huwa wanaanza kufanya kazi kwani hapo mtoto anamtegemea yeye. Ila wewe huna shida sababu mdada wa kazi yupo”
Mariam alitabasamu tu, hakuna kitu Mariam alikuwa hapendi kama kuambiwa kuwa aende kupika chakula Fulani, alikuwa hapendi kabisa.

Kama kawaida walikula chakula cha usiku, Juma na yeye alirudi na kujumuika nao ila bado hakupata nafasi ya kuweza kuongea na dada yake kwani majukumu yalimbana sana kutokana na mgonjwa ambaye alikuwa akimuhudumia hospitali.
Walipoenda kulala, Juma alimueleza mkewe hali halisi aliyokuwa nayo Pendo,
“Jamani Mariam,, kweli huyu mtoto wetu sio, yani huyo sio wa kawaida kabisa. Unajua ule upande wa shavu ambao Pendo alipigwa na mtoto wetu! Basi ule upande umevimba hatari, umetutumka sana hata sielewi itakuwaje halafu hii jioni nimeenda ndio kama upande ule umezidi”
“Dah! Ni hatari, na madaktari wwanasemaje kwani Juma?”
“Madaktari hata hawaelewi, wanachukua tu vipimo mbalimbali ila hawaelewi kuwa tatizo ni nini, kwanza sijasema kuwa alizabwa kibao ila nimesema tu kuwa alianguka na kuzimia maana swala la kunaswa kibao sikujua wangelichukuliaje kwahiyo sijasema kabisa”
“Duh!! Kazi ipo Juma, huyu mtoto huyu tuliyenaye loh!!”
Juma alikuwa amechoka sana na kuamua tu kulala kwani swala la kwenda hospitali na kurudi ofisini lilikuwa ni kibarua tosha kwake.

Muda huu wa asubuhi wakati mama Shamimu amekaa mezani akipata kifungua kinywa na mtoto wake Shamimu pamoja na Mariam yule dada aliguna na kusema,
“Mmmmh wifi asante, nafurahi sana kula chapati zako leo”
Mariam alicheka na kusema,
“Hizo chapati nipike muda hani na nilikuwa nimelala mie, nimeamka sio muda mrefu. Ni mambo ya Anna hayo”
“Kheee umemfundisha nini! Mbona kama umepika wewe!”
“Na yeye anajua kupika, sijamfundisha wala nini ila Anna ni kiboko, anapika vizuri sana hizi chapati najua hata mimi sizifikii hata robo kwa mapishi yake”
“Ila na wewe wifi yangu upo vizuri, haya hongera na kwa Anna pia”
Anna alikuwa akipita huku akitabasamu tu jinsi ambavyo alisikia kuwa wakimsifia kwa mapishi ya zile chapati.
Walipomaliza kula mama Shamimu akamwambia wifi yake,
“Kwahiyo wifi huyu binti hapumziki jamani! Kazi zote humu ndani afanye yeye tu! Kupika, kufua, kuosha vyombo, kumuhudumia mtoto, kusafisha nyumba jamani humpi hata muda wa kupumzika!”
“Kupumzika huwa anapumzika sababu kazi huwa anazifanya kwa wakati, sasa akiziacha unafikiri ni nani atazifanya jamani wifi!”
“Ungekuwa unamsaidia”
“Khaaaa nimsaidie nini wakati yeye ni msichana wa kazi”
“Sikia wifi, kuwa msichana wa kazi sio kwamba unakuwa ni kiumbe cha tofauti na binadamu. Unakuwa ni binadamu wa kawaida mwenye damu na nyama, kwahiyo ni lazima uchoke. Mara nyingine ni maisha tu ndio yanafanya tuombe kazi za ndani ila na wao wanachoka kama watu wengine, wana haki kama watu wengine, wanatakiwa kusaidiwa na wanatakiwa kupumzika. Kama hivyo unaweza kujitolea kupika au kuosha vyombo au kusafisha nyumba, ilimradi unamsaidia ili hata asijihisi vibaya na apate amani ya moyo”
“Mmmmh siwezi mimi jamani siwezi”
Mama Shamimu akamuita Anna ambaye kwa muda mfupi tu alienda, kisha alimwambia,
“Anna, leo niachie chakula cha mchana nitapika mwenyewe na cha jioni nitapika mwenyewe. Wewe pumzika kwenye kupika binti yangu”
“Asante”
Kisha Anna akaondoka zake, mama Shamimu aliendelea kumsema Mariam ila hata alivyomsema wala hakuna chochote alichomuelewa.

Mchana huu, Juma akiwa ametoka kumuona Anna, yani alijikuta akikata tamaa kabisa, alijikuta akisononeka sana, alijikuta akitamani tu kusema ukweli kwa watu wote kwani hali ya Anna ilikuwa ni mbaya sana halafu na lile shavu lake nalo lilivimba sana.
Kwa muda huu aliamua kupita ile njia ambayo huwa anakutana na yule binti, na kweli alivyopita na kusimama kwenye lile eneo kwa muda kidogo alitokea yule binti na kumsalimia pale kisha yule binti alimuuliza Juma,
“Huwa nikikuona maeneo haya najua tu kuwa una matatizo, vipi una tatizo gani Juma?”
Juma alimuelezea kuhusu yule Pendo ambapo yule binti alicheka na kusema,
“Ila Pendo nae ni kiherehere chake tu ndio kimemfanya apigwe, haya maswala ya kujifanya tukiwaona watoto ndio tunawajua sana tuyaache”
Juma akamwambia,
“Naomba nisaidie, maana hali ya Pendo inakuwa mbaya sana hata sijui kama atapona”
“Unadhani nikikusaidia atapona?”
“Ndio, naamini msaada wako, najua ukinisaidia basi Pendo atapona”
“Sikia Juma, nitakusaidia ila ngoja nikupe onyo asitokee mtu mwingine yoyote wa kumuita yule mtoto kwa jina wanalotaka wao, muda ukifika yule mtoto atasema mwenyewe jina lake, swala la kumpa yule mtoto majina ya tofauti litawatokea puani. Sijui tumeelewana? Kuwa makini sana, asitokee mtu yoyote wa kumpa jina yule mtoto”
“Nimekuelewa kabisa, nisaidie ili Pendo apate kupona”
Yule binti alimnyooshea Juma mkono wake na kumwambia amshike mkono kama watu wanaosalimiana ambapo Juma alifanya hivyo ila alijihisi kuna nguvu isiyo ya kawaida imemuingia kwenye mwili wake kisha yule binti akamwambia Juma,
“Huo mkono ulioshikana na mimi nakuomba usimshike mtu yoyote, usishike chochote mpaka utakapoenda kumuona mgonjwa na unachotakiwa kufanya ni kumshika huyo mgonjwa kwenye shavu lililovimba halafu majibu utayapata, sitaongea mengi ila ndio hivyo. Kwaheri sina muda mrefu leo”
Yule binti akaondoka zake kwahiyo Juma hakupata muda wa kumuuliza maswali yoyote wala muda wa kumuaga vizuri.
Juma aliondoka hapo na kurejea hospitali maana aliona akienda pengine basi anaweza shikana na wazi mikono wakati kaambiwa kuwa mkono ule asishike kitu wala mtu yeyote.

Juma alipofika hospitali tu, moja kwa moja aliingia kwenye wodi aliyolala Pendo, hapo hakumsikiliza nesi aliyemzuia wala nani kwani hakutaka mtu yeyote amshike mkono wake au amzuie kwa chochote kile ambacho anakitaka yeye.
Basi Pendo alikuwa vile vile huku shavu likiwa limeumuka hatari, Juma aliweka mkono wake kwenye shavu la pendo yani alijihisi mwilini kama nguvu zinamuisha hivi ila alimuwekea mkono tu Pendo hadi pale alipojihisi kizunguzungu na kuamua kukaa chini kabisa ila baada ya muda mfupi tu Pendo aliamka na kukaa na wala hakuwa na uvimbe gtena kwenye shavu wala nini, Pendo alikuwa akishangaa sana na kuuliza,
“Nipo wapi hapa?”
Akajiangalia na kuona zile sindano za dripu alishangaa sana na kuuliza,
“Kwanini nipo hospitali?”
Juma aliinuka na kumwambia,
“Pendo ulizimia ndiomana nikakuleta hospitali”
Kisha Juma akamuita nesi ambaye alishangaa pia, ila walipompima Pendo waligundua hana tatizo lolote katika mwili wake ikabidi wasubiri hadi jioni na kuamua tu kumpa ruhusa.
Juma alimsindikiza Pendo hadi nyumbani kwake, yani alikuwa haamini kwakweli kile ambacho kimetokea., ulikuwa ni kama muujiza kwa upande wake.
Pendo anamuuliza vizuri kilichomtokea ila Juma hakumwambia kabisa kwani alichokuwa anataka yeye ni Pendo kupona na sio kumwelezea kilichotokea, kwahiyo kama kuelezea ni akumbuke mwenyewe kuwa ni kitu gani kilitokea.

Kwa furaha ambayo Juma alikuwa nayo, aliamua kupitia sokoni kabla ya kurudi nyumbani kwake, na leo kule sokoni alibeba matunda ya kila aina ila kuna binti Fulani alimuona kule sokoni na alishawahi kumuona kabla, alijikuta akisimama na kumshangaa, alimuangalia kwa muda mrefu sana kwani kuna kitu alikuwa akikiona ni tofauti kwa yule binti, alimsogelea na kumsalimia,
“Habari yako binti!”
“Nzuri shikamoo”
“Sijui unanikumbuka?”
“Hapana sikukumbuki”
“Umeacha uchawi?”
“Hapana, mimi sio mchawi na wala uchawi siujui”
“Unakumbuka laana uliyoweka kwangu? Unakumbuka jinsi ulivyonilaani wewe binti?”
Yule binti hakumsikiliza Juma wala nini kwani muda ule ule aliondoka na wenzio na hakuonekana kabisa eneo lile, yani Juma alimuangalia yule binti bila kummaliza ila tu alimuona kuwa huyu binti amekuwa mkubwa na amebadilika vitu vingi ingawa sura yake ilikuwa ni vile vile, kwahiyo hakubadilika sura kabisa, Juma alijikuta kuchukia kwa kitendo cha yeye kumuona yule binti.
Kisha akachukua bajaji na kuamua tu kurudi nyumbani kwake.
Juma alivyofika na yale matunda, ni dada yake ndio aliyapokea na kuanza kuyaosha vizuri na kwenda kuyahifadhi huku Juma akielekea chumbani kwake.

Ila leo Juma alilala akiwa na furaha kiasi, na ile furaha ilikuwa ni sababu ya kupona kwa Pendo, yani kitendo cha Pendo kupona alihisi kama kuna mzigo mzito sana umetua kutoka kwake maana hili swala la pendo kuumwa lilikuwa likimkosesha raha kabisa.
Leo alivyoamka tu, alitoka nje na kufanya shughuli chache nje ila hakwenda popote ambapo alimkuta dada yake akiwa anafagia uwanja, basi alimshangaa na kumuuliza,
“Dada, kumbe unafagia uwanja?”
“Ndio, unadhani mimi ni mvivu kama huyo mke wako wa kulala hadi saa tatu? Yani mwanamke hata hajifikirii kuwa ana mtoto wala nini ila anachoendekeza yeye ni usingizi tu, kwakweli Mariam anakera sana”
Mara nyingi sana Juma huwa hapendi mke wake asemwe vibaya kwahiyo alimbadilishia mada dada yake na kuendelea na mambo mengine ambapo na yeye aliamua kuondoka pale na moja kwa moja alirudi chumbani ambapo mke wake alikuwa amelala hoi.

Baada ya chakula cha mchana walijikuta familia nzima wakiwa wamekaa sebleni huku wakizungumza mambo mbalimbali ambapo mama Shamimu alimuuliza Juma,
“Hivi Juma, mtoto wenu anaitwa nani maana nilimuuliza Mariam akasema nikuulize wewe”
Juma akatabasamu tu na kusema,
“Mwanangu bado sijampa jina”
“Kheeee kwanini hujampa jina jamani!! Majina yote yaliyopo duniani unashindwa kumpa mtoto jina kweli!”
“Aaaah dada, sijapanga kumpa jina kwasasa hadi afikishe miaka mitano”
“Kheee makubwa hayo, naomba mimi nimpe jina”
Hapo Juma aling’aka na kushtuka sana huku akimzuia dada yake kumpa jina mtoto,
“Mmmmh dada, hapana hapana hapana kabisa usimpe jina mtoto wangu”
“Kwanini nisimpe jina, wakati huyu mtoto anaweza hata kuitwa jina langu”
“Aaaargggh dada, hunielewi au nini, nimesema usimpe jina mwanangu. Mimi ndio mwenye amri humu ndani”
“Kheeee Juma, kitu kidogo hivyo umechukia? Mimi nampa jina tuone nini kitakachotokea”
Hapo na Mariam aliingilia kati kumkataza wifi yake asimpe jina mtoto ndipo mama Shamimu aliposema,
“Kheee Mariam, bado roho mbaya hujaacha tu hadi leo jamani! Mimi ni shangazi wa huyu mtoto, nampa jina sasa tuone mtafanyaje, kuanzia sasa huyu mtoto ataitwa Khadija”
Hapo hadi Juma aliogopa maana yule mtoto alikunja sura sana akionyesha kuwa amekasirishwa, na alikuwa amekaa kwenye kochi ila akashuka chini.

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
Story ya MWANAUME WA DAR inaendelea leo.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni