Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 17

MTOTO WA MAAJABU: 17

Mariam akiwa amelala fofofo, akasikia mtu anamuamsha, moja kwa moja alihisi kuwa ni mama yake anamuamsha ila alivyoamka alishangaa sana kuona kuwa aliyekuwa akimuamsha ni mumewe Juma.
Hapo Mariam alishangaa sana na kuamka vizuri huku akimuuliza mumewe,
“Nimefikaje hapa?”
“Khaaaa Mariam mke wangu, kwani hujui?”
“Sijui ndio”
“Wewe si umekuja na kugonga mlango, nikakusema tabia ya kuja usiku ukasema una usingizi sana tutaongea kesho si ni wewe!!”
“Kama ni mimi, mbona muda huu umeniamsha?”
“Nimeona unakoroma sana Mariam na sio kawaida yako kukoroma ndiomana nikaamua kukuamsha ili uache kukoroma”
“Ila na wewe Juma nimeanza kutokukuamini”
“Kivipi sasa?”
“Sikia nikwambie, mimi nilikuwa kwetu na tumekubaliana na mama kuwa saa nane usiku ananiamsha ili tukafanye ile dawa, na muda huu nilijua ni yeye ndio ananiamsha”
“Kwahiyo unahisi mimi nimekubeba kichawi wakati umerudi mwenyewe jamani Mariam?”
“Kwani saa ngapi saa hizi?”
Juma akachukua saa na kuangalia mida, kisha akamwambia mkewe,
“Ni saa tisa usiku”
“Aaaarrgh yani mama atakuwa amechukia sana”
“Kwani hajakuona ulivyokuwa unaondoka?”
“Hivi wewe nakwambia nilikuwa nyumbani hunielewi au? Mimi sijarudi hapa, ni uchawi labda ndio umefanyika na hata sijui ni kwanini nafanyiwa hivi jamani khaaa”
Wakati wanaendelea kuongea Mariam alishikwa na usingizi mzito sana na kulala kwahiyo Juma na yeye aliamua kulala kwani hakuwa na wa kuongea nae muda huu.

Kulipokucha tu, Juma alimuamsha mke wake maana bado alikuwa na maswali naye, kwahiyo Mariam aliamka ila alikuwa amechoka sana,
“Jamani mimi nimechoka”
“Ila amka tuongee ni mambo ya muhimu Mariam, maana najua hata badae naweza kukukuta umelala”
Ikabidi Mariam aende kuoga kwanza ili aweze kuongea na mume wake, kwahiyo alipotoka kuoga ndio wakaanza kuongea ila Juma alienda nae kunywa chai kwanza kwani alijua wakiongea huku wanakula basi mkewe hatolala.
Walikaa kwenye kunywa chai sababu Anna alikuwa ameshaandaa, basi Mariam akasema,
“Khaaa huyu Anna jamani, ameshaandaa chapati!”
“Je unapenda chapati?”
“Sana, yani napenda chapati mimi balaa”
“Unaonaje siku nyingine uwe unaandaa mwenyewe”
“Khaaa siwezi, maana nitachoka sana”
Juma alitikisa kichwa, kisha akamuuliza mkewe,
“Ila kwanini jana uliamua kurudi usiku?”
“Wewe, si tulishaongea, mimi sijarudi hata mpaka sasa najishangaa nipo vipi hapa”
“Sikia Mariam, uliniomba ruhusa na mimi kama mumeo nikakuruhusu maana jambo ulilosema kuwa unaenda kulifanya ni jambo la maana, ila nikashangaa saa sita usiku jana unagonga mlango hata sikujua kama ni wewe, nikaja kufungua, nilishtuka kwakweli maana usiku ule ungekabwa je ingekuwaje? Uliingia na kusema una usingizi sana, ila ulipokuwa unakoroma sana ndio nikakushtua yani kwakweli Mariam sijapenda hii tabia kabisa”
“Unajua unasema lakini nakushangaa kabisa Juma, hata sijui unazungumzia kitu gani kwakweli. Mimi sijarudi hapa, hata mimi mwenyewe sijielewi”
“Kama ni hivyo mpigie simu mama yako tujue iko vipi hiyo”
“Halafu kweli, nilisahau kabisa swala la kumpigia simu mama, najua hata na wao wameshangaa sana kutoweka kwangu, mambo ya kishirikina haya sijapata kuona, yani hapa naongea kwa kujipa moyo tu ingawa kiukweli nahisi kama kuchanganyikiwa vile”
Mariam alienda kuchukua simu yake na kuja nayo halafu akapiga na kuweka sauti kubwa ambapo mama yake alipokea, moja kwa moja Mariam alimuuliza mama yake,
“Kwani mama jana imekuwaje? Mbona nipo huku kwangu tena!”
“Unauliza imekuwaje? Yani unathubutu kabisa kuuliza kuwa imekuwaje, mtoto mjinga kabisa wewe, kwanza unakera”
“Nimefanyeje kwani mama?”
“Wewe tumeshaongea vizuri na kupanga kila kitu, kilichokufanya uamke saa tano na kusema kuwa unaondoka!”
“Khaaa mama jamani”
“Hakuna cha mama jamani, hadi nakuuliza utapata usafiri gani muda huu maana gari za kuja kwetu huku tunazijua vizuri sana, kwakweli umenikera Mariam”
“Khaaa mama kwahiyo niliondoka?”
“Usiniulize ujinga mimi wakati upo kwako unakula muda huu, nasikia tu midomo ikitafuna cha urafi wewe”
Mama Mariam alikata ile simu, ni wazi alikuwa amechukia sana kuhusu lile swala.
Juma akamwambia mkewe,
“Unaona sasa, hata mama yako anasema jambo hilo hilo”
Mariam hakujibu muda huu ila alimalizia kunywa chai na kurudi chumbani, wakati huo Juma nae alirudi kujiandaa na kuondoka zake.

Kwakweli Mariam aliwaza sana na kujiuliza sana kuwa ni kitu gani kile, ila wazo lake lingine lilimwambia kuwa ni mtoto wake yule, akajisemea,
“Au badala ya mtoto nikazaa jini jamani! Hivi kitoto si kinaongea kile, ngoja nikakiulize leo”
Mariam alitoka ila mtoto alikuwa nje na Anna, basi Mariam alienda hadi pale nje na kumuangalia mtoto wake kisha akamuuliza,
“Wewe mtoto ni tabia gani hii ya mimi kwenda mahali halafu wewe unanirudisha kimazingara?”
Ila mtoto hakumjibu kwani aliendelea kucheza, basi Anna akamwambia Mariam,
“Ila dada, hivi akikujibu huyu mtoto hilo swali lako utaweza kuendelea kumuhoji?”
“Kwanini nisiweze? Kwa kifupi mimi nimemchoka huyu mtoto maana amenifanyia hivi sio mara moja, kila siku mtoto ananifanyia vituko tu, leo nijibu hivi kweli wewe ni mtu au nimezaa jini?”
Anna akamwambia tena,
“Hivi dada akisema yeye ni jini utafanyaje? Muache mtoto acheze bhana, muone huyu mtoto kama watoto wengine”
“Hujui tu jinsi gani huyu mtoto ambavyo simpendi, hata nachukia kuzaa kiumbe cha ajabu kiasi hiki aaargh”
Kisha Mariam alirudi chumbani na moja kwa moja alienda kulala maana alikuwa na mawazo mengi sana.

Juma akiwa ofisini akapata ujumbe toka kwa dada yake kuwa ataenda nyumbani kwao kuwatembelea, yani Juma alifurahi sana kwakweli na kumkaribisha,
“Nitakuja na mtoto wangu?”
“Aaaah yule Shamimu!”
“Eeeh ndio, huyo huyo amekua sana siku hizi, tena anaongea maneno yote”
“Hivi ana miaka mingapi kwasasa?”
“Ana miaka mitano, amekua kwasasa”
Basi Juma alimkaribisha sana dada yake ambaye alimwambia kuwa akifika atataka wakampokee stendi maana kule alienda siku nyingi sana, kwahiyo Juma alikubali na kumuuliza,
“Si Kesho eeeh dada!”
“Ndio ni kesho”
“Usijali, wifi yako atakupokea”
Wakaongea kidogo na kukata ile simu, kisha Juma aliendelea na mambo yake ila alifurahi sana kwa dada yake huyu mama Shamimu kusema kuwa anafika nyumbani kwake, hii ilikuwa ni furaha yake sana maana ilikuwa ni siku nyingi kidogo hawajaonana.
Juma alipomaliza kazi zake, alifatwa na Pendo leo maana hakuongea nae tena toka lile tukio liishe,
“Kwakweli Juma umeniangusha sana!”
“Pendo nisamehe tu ila kwakweli sikuweza kumsaliti mke wangu”
“Kheee mke wako ni mwanamke mwe nye bahati sana, ni wanaume wachache sana wenye uwezo wa kusema hivyo!”
Nasema hivyo sababu nampenda, hakuna mtu aliyenilazimisha mimi kumuoa yule mwanamke, bali nilimuoa kwa ridhaa yangu mwenyewe, sababu ya kumpenda sana, huwa namuona yeye ndio kila kitu katika maisha yangu”
“Kheee hongera kwake, ila kuna kipindi nilikuwa nakuona ona na makopo ya maziwa, vipi mna mtoto mdogo?”
“Ndio”
“Hongera sana, ni msiri wewe jamaa balaa. Anaitwa nani mtoto wenu?”
Yani Juma alifikiria kwa haraka haraka pale, aliwaza kuwa akimwambia kuwa mtoto hana jina itakuwa na mshangao yani mtoto asiwe na jina hadi leo! Basi akaropoka tu pale,
“Mwanangu anaitwa Pendo”
Pendo alitabasamu na kufurahi sana kisha akamwambia Juma,
“Ooooh hiyo ni nzuri sana, kumbe ni wajina! Sasa nimeelewa ni kwanini huwa unapenda sana kuongea na mimi kumbe nimefanana jina na mtoto wako!”
Juma akatabasamu tu na kujibu,
“Ndio”
“Eeeeh kwanini umemuita Pendo? Mimi wazazi wangu waliniita hivi sababu mimi nilikuwa kama ndio nimeingiza upendo kwenye familia yetu, maana ndugu zangu wote ni wa kiume, basi nilivyozaliwa mimi waliona upendo umezaliwa upya ndio nikaitwa Pendo, na wewe kwanini mwanao umemuita Pendo?”
“Mmmmh mwanangu mimi kabla hajazaliwa nilijua tu atazaliwa mtoto wa kike na nilisema kuwa nitampenda sana, kwahiyo nampenda sana mwanangu Pendo”
“Oooh nitakuja kumuona wajina, natamani sana kumuona. Nitamletea na zawadi”
Basi walikuwa wakitabasamu tu pale na kuongea ongea yani Juma alisema vile ili tu asiweke maswali mengine ingawa ni wazi kuwa mtoto wao hawakumpa jina.

Usiku wa leo wakati wa kulala, Juma alimueleza mke wake juu ya ujio wa dada yake kwani alitaka mkewe ndio aende kumpokea pindi dada yake akifika,
“Nadhani tumeelewa Mariam”
“Ila kwanini usiende wewe!”
“Sasa mimi nitaenda vipi Mariam? Kesho kuna kazi ya muhimu sana, sasa ushindani wa nini tena!” 
“Mmmh yule dada yako ana mdomo yule”
“Ila Mariam una nini jamani mke wangu, kumbuka kwenye familia yetu ni mama Shamimu ndio alikuwa wa kwanza kukukubali, haya huo mdomo wake ni mdomo gani?”
“Mmmh sisemi sana, tulale ila yule dada yako tutaona tu kama akikaa hapa siku mbili itakuwa kama amekaa mwaka mzima”
“Acha hayo maneno jamani Mariam”
Basi kwa muda huo waliamua tu kulala kwani Juma huwa anamjua mkewe vizuri na wakiongea sana wanaweza kugombana.
Asubuhi na mapema, Juma alijiandaa na kuondoka, leo hakunywa chai wala nini na alimuacha Mariam akiwa amelala tena fofofo.

Mariam alikuja kuamka kwenye mida ya saa nne asubuhi, basi alijiandaa vizuri na kwenda kunywa chai huku akiongea na Anna,
Mdogo wangu Anna, leo kuna mgeni kwahiyo kile chumba kingine kisafishe maana atalala”
“Nishakisafisha dada”
“Kheee muda gani tena?”
“Leo asubuhi nimekisafisha, nilikuwa naangalia angalia nikakiona ni kichafu basi nikaingia na kukisafisha na kupanga vitu”
Mariam alimshangaa Anna na kuzidi kumsifia kuwa ni mchapakazi, alipomaliza kunywa chai akainuka na kwenda kukiangalia hiko chumba, kwakweli alishangaa maana kilisafishwa vizuri sana, hakuna taka yoyote iliyoonekana kwenye chumba kile na kumfanya Mariam atabasamu.
Alivyorudi sebleni aliamua tu kujilaza kwenye kochi kwani alikuwa anaona uchovu balaa na alipojilaza ni alilala usingizi kabisa.
Ni Anna ndio alimshtua kwa kumpa simu yake,
“Dada, simu yako imeita sana”
Basi akaipokea maana mpigaji alikuwa ni Juma, basi aliongea nae kuwa mgeni wao ameshafika ikabidi Mariam aende kujiandaa, alivyoingia chumbani kwake alitabasamu kwakweli maana chumba kilikuwa ni kisafi sana hadi alikuwa akijisemea,
“Kweli panya na mende wanakaa sehemu chafu, kwa usafi wa chumba hiki unaweza pata panya au mende kweli? Hata mbu siku hizi hakuna, ila kuwa na mdada wa kazi ni raha sana maana kila kazi unafanyiwa hadi raha yani”
Alikuwa akitabasamu tu na kujiandaa halafu alienda stendi kumpokea huyo wifi yake.

Mariam alifika stendi na kumkuta kweli wifi yake yupo kumsubiri, ila alimuona na mzigo mkubwa basi akawaza moyoni,
“Kheee mzigo wote huo, anataka kuhamia au nini!”
Akamsogelea na kumkumbatia ila kiukweli ule mzigo ulimpa mashaka sana, wakabeba na moja kwa moja wakaanza kuongozana huku Mariam akimdadisi ajue wifi yake atakaa kwa muda gani,
“Vipi wifi, karibu sana ni siku nyingi sana. Basi hivyo umekuja leo kesho utaondoka wewe jamani!!”
“Hapana wifi, saivi nimekuja kuangalia angalia mazingira huku maana kule kwangu kumenichosha”
“Nini tena wifi?”
“Kuna wachawi nakwambia, jamani kuna wachawi hapafai kabisa”
“Sasa umemuacha nani wifi? Utakaa huku kwa muda gani wifi?”
“Nadhani nitakaa huku kwa muda wa mwezi mmoja, miwili hivi au mitatu”
“Duh!!”
“Nini wifi, hujapenda?”
“Hapana wifi napenda sana, hata ukikaa mwaka hakuna wtatizo, karibu sana wifi yangu”
Basi wakatabasamu na safari ya kuelekea nyumbani iliendelea.
Hadi walipofika na kuingia ndani, huku mtoto wa Mariam akiwa amekaa kwenye kochi akiwaangalia tu, basi moja kwa moja mama Shamimu alimsogelea mtoto wa Mariam na kumshika huku akimpongeza Mariam kwa kusifia kuhusu mtoto,
“Hongera Mariam, yani umezaa kifaa khaaa mtoto mzuri jamani, hongera sana”
Mariam alicheka kwa unafki tu kwani kiukweli hata mtoto hakumtaka,
“Asante wifi yangu”
“Dah! Kwakweli umezaa mtoto jamani, khaaaa sikujua kama umezaa mtoto mzuri kiasi hiki, hongera sana”
Mariam hakutaka balaa pale kwani alijua mtoto anaweza sababisha majanga mapema basi akamwambia wifi yake,
“Wifi twende kidogo chumbani ukabadili nguo, ukaoge na upate chakula, najua umechoka sana wifi yangu maana kule kwenu ni mbali”
Basi mama Shamimu akainuka na kumshika mwanae mkono halafu moja kwa moja aliongozana na Mariam hadi kwenye chumba ambacho Mariam alimuonyesha kisha Mariam ndio akatoka na kumwambia Anna,
“Anna, yule ni wifi yangu kabisa ni dada wa Juma yule toka nitoke”
“Aaaah kumbe, ila kafanana fanana nae”
“Ndio wamefanana na mama yao hawa, yani mama yao yupo hivi hivi nakwambia hata ukimuona utakubaliana na mimi. Waandalie chakula basi”
Kisha Mariam akaenda chumbani kwake wakati Anna akiandaa chakula.

Juma aliporudi leo alienda moja kwa moja kumsalimia dada yake ila sababu dada yake alikuwa ameshalala akaongea nae tu kidogo na kumwambia,
“Tutaongea vizuri kesho dada maana nitawahi kurudi”
“Sawa mdogo wangu maana nina mengi sana ya kuongea na wewe”
Basi wakaagana na muda huu Juma alienda moja kwa moja kula chakula cha usiku kwanza halafu ndio akaenda kulala.
Basi Juma alivyoingia tu kulala, Mariam alimuuliza mumewe,
“Huyo dadako uliyeenda kumsalimia hajakupa umbea?”
“Jamani Mariam, siku ya kwanza tu atanipa umbea gani?”
“Hivi unajua kama anakaa hapa mwaka mzima?”
“Kivipi?”
“Atakueleza mwenyewe kesho, kaja na furushi hilo, bonge la shangazi kaja hadi nikashangaa halafu na begi kumbe kapanga kukaa hapa mwaka mzima”
“Hata sikuelewi Mariam”
“Utaelewa tu hiyo kesho akikuelezea mwenyewe”
Basi Juma hakusema maneno zaidi zaidi alilala tu kwa muda huo.

Mapema kabisa kama kawaida, Juma alijiandaa na kwenda kwenye shughuli zake kama kawaida kwahiyo Mariam alibaki amelala kama kawaida.
Leo Mariam aliamka kwenye mida ya saa tatu asubuhi na kumkuta wifi yake amekaa akinywa chai, basi akasogea na kumsalimia ambapo na yeye alikaa kunywa chai, kisha wifi yake akaanza kumsema,
“Kheee Mariam bado tu unaendelea na tabia yako ya kuchelewa kuamka ilihali una mtoto?”
“Kwani mtoto kitu gani wifi? Mdada wa kazi yupo, anamlea na kumuhudumia mtoto sina tatizo mimi”
“Ila una raha sana wifi yangu maana Juma anakupenda kupita kiasi”
“Nalijua hilo wifi, kaka yako hazungushi hapa”
Basi mama Shamimu akaguna tu na kuendelea kunywa chai yani Mariam huwa hajali kabisa maana ana uhakika asilimia zote kuwa anapendwa sana na Juma.

Leo Juma kama alivyoahidi basi muda huu aliwaaga wenzie kuwa anaondoka, wakati anatoka akakutana na Pendo ambaye alimuuliza,
“Mbona mapema hivyo?”
“Aaaah narudi kwangu, dada yangu amekuja nataka nikaongee nae”
“Oooh wow, hiyo ni habari njema, naomba twende wote nikamuone wajina”
Basi Pendo alichukua mkoba tu na kuunganisha na Juma, hapo Juma hakujua hata jinsi ya kumkatalia na kuamua kuondoka nae tu kwenda nae nyumbani kwake.
Basi Juma na Pendo walivyofika tu, yule mtoto wa Juma na yeye alikuwa anatoka nje maana mlango ulikuwa wazi, basi Pendo akasema kwa furaha,
“Ndio yule nini mtoto wako katoka?”
“Ndio ni yeye”
Pendo akatabasamu na kumsogelea yule mtoto kisha akainama na kumwambia,
“Pendo, niamkie mtoto mzuri”
Pendo alishangaa yule mtoto akimnasa kibao cha nguvu.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni