Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 16

MTOTO WA MAAJABU: 16

Juma moja kwa moja alienda kwenye chumba alichoonyeshwa, akaingia hapo na kumkuta mwanamke kalala huku mgongo ndio ukiwa juu, akamsogelea na kumpapasa mgongoni ila gafla akasikia sauti ya mtoto wake.
“Yani baba unataka kumsaliti mama?”
Juma alishtuka na kuangalia huku na kule bila kuona yoyote ila alimuacha yule mwanamke na kutoka nje hata Pendo alimshangaa kwani Juma aliondoka kwa upesi sana.
Hakupita tena kwenye shughuli zake kwani moja kwa moja alikuwa akielekea nyumbani kwake huku akiwa na mawazo sana, alijisemea,
“Hivi yule mtoto wangu ni mtoto kweli au kuna namna hapa katikati? Hivi Mariam nilimpa kweli mimba au alikuwa akidanga nje? Yani nina mashaka na yule mwanamke aaarrgh basi tu ninampenda sina cha kufanya”
Juma alirudi hadi nyumbani kwake ambapo kwa muda huu aliwakuta wote mezani wakiwa wanakula huku Anna akila yeye na kumlisha mtoto, basi Juma aliwasalimia na kutaka kupitiliza chumbani ila mtoto akamwambia,
“Njoo tule baba, najua una njaa”
Juma alimuangalia huyu mtoto wake bila kummaliza kwakweli, akitaka kumfanya ni kiumbe cha ajabu anashindwa maana huyu mtoto anaongea kawaida tena kwa sauti ya kitoto, na pia ana muonekano wa kawaida ila jinsi anavyofanya mara aongee mara nini ndio vitu vinavyowaogopesha mule ndani.
Juma hakusema kitu, ila alikaa na kuanza kula, wakati anakula aliuliza,
“Chakula kapika nani?”
Alikuwa akiuliza huku akimuangalia Mariam ambapo Mariam alijibu,
“Kapika Anna, si ndio mpishi wa humu ndani! Kwani unaona kapika nani?”
Juma akaguna na kusema,
“Naona kama umepika wewe, maana ladha ya hiki chakula ni kama umepika wewe!”
Muda ule ule mtoto wao akajibu,
“Ndio amepika mama, ndiomana na mimi nakula”
Yani humu ndani huwa akiongea huyu mtoto inakuwa kama ni ajabu sana kwahiyo huwa hakuna hata mtu mmoja anayejibu pale mtoto huyu akiongea, huwa hakuna anayejibu, hakuna anayeuliza swali wala hakuna anayehoji. Kwahiyo wote walikaa kimya na kuendelea kula tu kwa muda huo.

Juma alipomaliza kula, aliamua kwenda chumbani kwani alikuwa na mawazo mengi sana haswa ni mawazo ya juu ya kilichotokea, muda kidogo Mariam na yeye akaenda chumbani kwa mume wake na kuanza kuongea nae,
“Mbona leo mapema maana siku hizi hata sijui umeanza mpango gani huo wa kurudi usiku wa manane”
“Dah!! Mariam wewe acha tu”
“Niache tu kitu gani? Nisipokuuliza naonekana sio mke mwema, halafu nakuuliza napo napewa jibu la niache tu ndiomana mimi huwa siulizi wala nini”
“Ni nani kakwambia kuwa usipouliza unaonekana sio mke mwema?”
“Ni hako kabinti Anna, yani kila siku ambavyo huli chakula ananilazimisha nije kukuuliza kuwa kwanini huli, sijui jambo kidogo tu nikuulize, mara anasema nikuletee chakula chumbani, sasa mapemzi ya hivyo kwetu yatoke wapi? Kwani mimi sina kawaida ya kuwa na mapenzi ya kijinga kiasi hiko”
“Kwani kumuuliza mumeo ni ujinga?”
“Ni ujinga ndio, kama jibu lenyewe ndio hili etu Mariam acha tu, ni ujinga na mimi sikuulizi tena”
Juma hakusema neno, badala yake aliamua tu kujilaza maana angesema angeweza kuongea yasiyofaa.

Usiku wa leo wakati wamelala, kuna muda Mariam alishtuka na kilichomshtua ni simu yake maana leo hakuizima wala nini, kwahiyo aliichukua na kuiangalia, akashangaa sana kuona mama yake amempigia kwa muda ule, ila alipokea na kumsikiliza,
“Mama, mbona usiku sana?”
“Ndio ni usiku sababu na mambo yenyewe ni ya usiku usiku”
“Kivipi mama?”
“Mariam, leo nimekutana na mtu yani karopoka mengi sana kuhusu wewe”
“Yapi hayo mama yangu?”
“Unajua kaanza kunieleza toka kipindi wewe upo na mimba ya mtoto wako huyo hadi kipindi umejifungua, kumbe mama mkwe wako ndio alikuletea dawa ya wewe kuweza kujifungua?”
“Ndio mama”
“Ila yule mama huwa hakupendi, unajua nilimshangaa kipindi umejifungua alivyojifanya anakupenda hadi anafanya kazi zote humo ndani kwenu, anafua anapika yani kama sio mkwe wakati kwa kawaida huwa hakupendi”
“hata mimi naelewa hilo mama ila mimba ilivyokaa muda mrefu ndio ilinipatanisha nae, na mara nyingi alikuwa akijaribu kuniletea dawa mbalimbali. Huyo mtu kasemaje”
“Unatakiwa kuja huku nyumbani mwanangu, halafu kwenye mida ya saa nane usiku kuna sehemu tutaenda kwaajili ya tiba”
“Mmmmh mama ni wapi huko? Mbona usiku sana?”
“Unahitaji kupona au la? Unajua mimi naumia kiasi gani kama mama yako? Hata muda huu nimekupigia simu sababu naumia sana, jitahidi uje kesho”
“Sawa mama, nimekuelewa”
Basi Mariam akaagana na mama yake na kwa muda huo sasa, ndio Mariam aliweza kulala vizuri kabisa.

Leo Mariam alichelewa kuamka maana siku nyingine huwa anawahi ila leo alichelewa sana hadi alijishtukia na kujiona kuwa hayupo sawa baada ya kuangalia muda na kuona kuwa ni saa tano na nusu.
Aliamka na kujinyoosha maana alikuwa amechoka sana, alienda kuoga kwanza halafu ndio akatoka, ila muda huu alikuta Anna na mtoto wake wapo nje kabisa ikabidi atoke kwenda kuwasalimia,
“Jamani Anna mbona nimelala sana!”
“Pole sana dada, nilikuwa kupalilia”
Mariam aliangalia lile shamba lao dogo na kuona limepaliliwa kabisa hata jani hakuna basi alimpongeza Anna,
“Hongera sana mdogo wangu Anna”
Yule mtoto wao akadakia,
“Hongera na wewe mama”
Mariam hapa tu ndio palimmaliza nguvu kabisa kwani aliondoka na hakutaka hata kuendelea kuisikiliza ile hongera ya katoto chao.
Aliporudi ndani moja kwa moja alienda kunywa chai, ila alikuwa na mawazo sana na vilevile alikuwa na uchovu sana siku hiyo.
Alipomaliza kunywa chai alirudi chumbani na moja kwa moja alichukua simu yake na kumpigia mama yake maana alijiona ni wazi kuwa hatoweza kwenda kwao,
“Mama, samahani, sitaweza kuja leo yani nimechoka hapa balaa nahitaji tu kulala”
“Khaaa Mariam, yani unafanya uvivu hata kwa mambo yanayokuhusu jamani!”
“Sio uvivu mama, nimechoka sana”
“Umechoka umefanya nini kwani mwanangu? Najua kama kazi za nyumbani hufanyi, sasa huko kuchoka kumekuwaje tena?”
“Yani mama hata sijui jinsi ya kukuelezea, ni kweli sifanyi chochote ila nimechoka balaa naomba nije kesho mama”
“Nimekumbuka kitu mwanangu, naomba usishiriki na mumeo tendo la ndoa mpaka tutakapomaliza haya”
“Usijali mama kwanza hata hamu ya kushiriki sina wala nini, hata usijali kuhusu hilo”
Basi Mariam akaongea na mama yake na kupatana nae kuonana nae kesho yake.

Juma akiwa njiani kurudi nyumbani kwake, alipita ile njia ambayo huwa anakutana na yule binti na alivyopita tu alisimama mahali pale akiangalia angalia ila baada ya muda kidogo yule binti na yeye alisogea eneo lile na kumsalimia Juma, kisha Juma aliongea nae,
“Kuna kitu sielewi kuhusu mtoto wangu”
“Kitu gani huelewi?”
“Yule mtoto anaongea, ni jambo la ajabu sana”
“Sio jambo la ajabu, ulitaka mtoto wako awe bubu? Mbona wanadamu hamna shukrani lakini, asingekuwa anaongea napo ungesema ni mtoto gani huyu! Kaongea mapema napo unasema”
“Sina maana hiyo, hebu fikiria kuna siku nilipata mwanamke halafu nikasikia sauti ya yule mtoto eti baba unataka kumsaliti mama!”
“Ila kwanini unataka kumsaliti mkeo?”
“Jamani mimi ni mwanaume, ni mwanadamu mimi ambaye nimekamilika kabisa, na mimi nina uhitaji ila mke wangu hataki”
Huyu binti alimuangalia Juma kisha kuna maua Fulani akayachuma na kumwambia Juma,
“Nenda kamnusishe haya maua mkeo halafu utapata wasaa wa kufurahia nae tendo”
“Kwahiyo nisimwambie eeeh!”
“Ndio, usimwambie chochote, hata usimwambie kuwa unahitaji, yani utamnusisha tu hayo maua na kisha utalala nae utakavyo. Nimekupa tiba leo Juma, nadhani utaifurahia ndoa yako”
“Asante sana, maana yule mwanamke kila siku analalamika kuwa amechoka jamani, ananikosesha raha kabisa”
Basi Juma alichukua yale majani na kuweka vizuri mfukoni halafu aliagana na yule binti na kuondoka zake kwenda nyumbani kwake.

Juma alifika muda ambao walikuwa wanakula mule ndani kwake, kwahiyo na yeye alienda kujumuika nao kupata kile chakula kwa pamoja, basi walimaliza kula ndipo alipoenda ndani kuoga na kumsubiri mke wake sasa, muda kidogo ndipo Mariam na yeye alipoingia chumbani huku akilalamika kama kawaida yake,
“Jamani leo, nimechoka yani nimechoka sana leo”
“Pole mke wangu”
“Asante, hata sitaki tuongee sana. Tulale tu muda huu”
“Sawa, tulale”
Mariam alipanda kitandani na kujilaza, basi hapo hapo Juma alitoa yale maua na kumnusisha Mariam ambapo Mariam aliinuka mwenyewe kitandani na kumkumbatia Juma na hapo Juma alibahatika kulala na mkewe toka kipindi ambacho Mariam alijifungua.
Juma alikuwa na furaha sana leo, alijikuta tu akishukuru vile ambavyo yule binti amemsaidia ile dawa.
Basi wakalala hadi asubuhi, Mariam alikuwa wa kwanza kuamka na kumuuliza mume wake,
“Tumefanya nini sasa Juma”
“Kwani tatizo liko wapi mke wangu?”
“Sio tatizo liko wapi? Nakuuliza tumefanya nini?”
“Ngoja nikuonyeshe tulichofanya”
Juma alichukua yale maua yaliyobaki na kumwambia mkewe,
“Hebu nusa haya maua uone”
Mariam alinusa yale maua, na muda ule ule Mariam alilegea na kuanza kumkumbatia Juma bila kutaka kumuachia basi Juma alifurahi sana na kupata wasaa mwingine wa kulala na mke wake, baada ya hapo ndio akajiandaa na kuondoka zake, kwahiyo alimucha tu Mariam akiwa amelala.

Juma leo alikuwa na furaha sana hata alikuwa anawaza kuwa akikutana tena na yule binti atamuomba ampatie maua ya kutosha ili aendelee kufurahi na mke wake,
“Dah!! Sikujua kama kuna kitu chepesi vile katika kumpata mke wangu mbishi, kumbe kuna yale maua dah!! Akiyanusa tu kwisha habari yake, analegea na kuwa mpole mwenyewe. Yani natamani hata nipewe mbegu kabisa nikapande nyumbani kwangu”
Alikuwa akitabasamu tu mwenyewe, muda huo rafiki yake Hakim alifika na kumuuliza,
“Vipi Juma, unaonekana kuwa na furaha sana”
“Ni kweli nina furaha, acha tu”
“Dah! Haya ila hapa kuna habari zimesambaa kuhusu wewe hata sielewi ni kwanini imekuwa hivi”
“Habari gani?”
“Nasikia Pendo alikutafutia mwanamke ila hujafanya chochote nasikia una matatizo ya nguvu za kiume ndugu yangu”
“Dah!! Waache tu waseme hivyo, ila mimi sina tatizo lolote lile. Ilimradi nafurahia maisha na mke wangu basi inatosha”
“Sasa mbona ulihitaji mwanamke?”
“Sababu nilikuwa na mawazo, ila kwasasa sina mawazo tena, nipo na furaha tu moyoni mwangu”
“Haya, hongera”
Hakim hakuongea sana kwani hakuwa na kingine cha kumshawishi Juma sababu Juma alionekana kuwa na furaha sana.

Kwakweli Mariam leo alichukia sana hadi alijiuliza kuwa ameanza vipi kushiriki tendo la ndoa na mumewe wakati kashapanga mipango na mama yake? Hakuelewa kabisa, basi muda huu alikaa sebleni akiwa na mawazo sana hadi Anna alimuuliza,
“Mbona hivyo dada?”
“Aaarggh huyu mwanaume ni mpuuzi sana”
“Kwani kafanyaje?”
“Unajua leo ameshiriki tendo la ndoa bila ridhaa yangu, kwahiyo kanibaka yani”
“Kheee dada, kwani kwenye ndoa kuna kubakana?”
“Ndio, kama mtu hajataka basi ni kumbaka”
“Ila dada, ni halali yake maana hilo linaitwa tendo la ndoa kwahiyo kwa wanandoa ni halali dada yangu”
“Hata kama ni halali, alitakiwa kuniambia kwanza mimi nikubali”
“Hivi dada si uliniambia kuwa hujashiriki na mumeo toka umejifungua? Ulitaka afanyaje sasa jamani? Hata simlaumu kwa hilo, halafu ngoja nikuulize kwani kakupiga muda wa kushiriki? Kakulewesha pombe hadi useme kakubaka?”
“Sijui ni nini kilitokea ila ninachojua ni kuwa amenibaka, kwakweli kanikera sana maana kaharibu mambo yangu yote niliyopanga”
“Ilikuwaje kwani?”
“Wewe bado mdogo sana Anna, nisikukuze.”
Kisha Mariam aliinuka na kwenda chumbani ambapo alimpigia simu mama yake na kumweleza kilichotokea,
“Aaaah hapo haifai mwanangu, itabidi uje kesho basi, jitahidi usifanye nae chochote”
“Yani mama, leo nalala na nguo hata kumi, sifanyi nae chochote kile, ila mama inamaana dawa itaharibika eeeh!!”
“Ndio, hii dawa hairuhusiwi kushikwa na mtu aliyetoka kufanya tendo la ndoa ndiomana nimekutahadharisha mwanangu. Nakuomba sana uwe mwangalifu na usifanye nae kitu”
“Sawa mama yangu”
Mariam alikubaliana na mama yake pale kuwa ataenda kesho yake ila alikuwa na hasira sana, alichukia sana kwa kile kitendo kilichofanyw ana mumewe.

Usiku wa leo, Mariam alikaa na Juma na kuongea nae maana aliona ni vyema kumueleza ukweli ili asimfanyie tena kama vile,
“Mume wangu sikia, nakuomba sana tusishiriki tendo la ndoa kwasasa sababu kesho nataka kwenda kwa mama, kuna dawa tunatakiwa kufanya kwaajili ya mtoto wetu”
“Hebu nieleweshe vizuri Mariam”
basi Mariam alianza kumueleza mumewe vile ambavyo alielezwa na mama yake kuhusu hiyo dawa ili Juma asijekufanya tena akashindwa kwenda kutekeleza hiyo dawa,
“Aaaah hapo nimekuelewa, ila uwe unaongea kama hivyo mke wangu”
“Ndio hivi nimekwambia, ila umenibaka Juma sijapenda wala nini”
“Mariam, hebu rudisha kumbukumbu zako vizuri, nimekubaka mimi? Si wewe mwenyewe ndio ulikuja kunikumbatia huku ukisema kuwa unahitaji!”
Mariam aliinama chini na kusema,
“Hata sijui ni nini, sijui ni akili za ndoto au kitu gani, na ile asubuhi je nayo sielewi ilikuwaje ila tulilala wote”
“Ilikuwa vile vile Mariam, ila subuhi inanoga mke wangu jamani, natamani hata iwe kila siku”
“Nenda zako huko, usitake kuniharibia dawa zangu, unanikera tu muda huu”
Ila walielewana kwa muda ule sababu hata Juma alihitaji kwa sana ukombozi wa mtoto wake, kwahiyo alimpatia mkewe nauli na hela ya kumsaidia.
Kulipokucha tu, Juma alimuuliza mke wake,
“Kwahiyo leo utalala huko huko?”
“Ndio, itabidi iwe hivyo maana dawa yenyewe inafanyika saa nane usiku”
“Aaaah, basi sawa”
Juma alijiandaa na kuondoka zake, kwenda kwenye shughuli zake.

Muda huu Mariam na yeye alijiandaa kwaajili ya kwenda kwao, kwahiyo alimuaga tu Anna pale kuwa atarudi kesho yake,
“Kheee dada, kwahiyo leo hurudi?”
“Ndio, nitarudi kesho”
“Sasa dada, shemeji akinifukuza je?”
“Anaanzia wapi kukufukuza? Hakuna kitu kama hiko”
“Ila dada, mfano ukaenda huko na mimi pamoja na mtoto itakuwaje?”
“Hapana haiwezekani sababu hapa nyumbani panahitaji mtu wa kuangalia mazingira”
Basi Mariam akaondoka zake, leo hakuwa na tatizo la kugeuza viatu kwani aliona wazi kuwa hajaondoka kwa kutoroka ila alikuwa akitembea huku akiwa na mashaka tu ya kujikuta kwake tena.
Alifika hadi nyumbani kwao, na kuingia ndani ambapo mama yake alimkaribisha na kuongea nae kidogo,
“Bora umekuja Mariam ili tufanye hii dawa vizuri”
“Ndio mama, nipo hapa”
“Sawa, badae tutapanga vizuri ngoja kwanza nimalizane na wale ndugu zako wengine”
Mariam alimuitikia mama yake, kiukweli alikuwa na furaha sana kufika nyumbani kwao kwa siku ya leo.

Kwa muda huu sasa, Mariam alikuwa na mama yake, na waliweza kupanga mambo vizuri kabisa kisha mama yake akamwambia,
“Mwanangu, saa nane nitakuamsha halafu ndio twende kule tulikopanga”
“Sawa maam, itakuwa vizuri”
Basi usiku ule Mariam alilala tu kwenye chumba chake ambacho alikuwa akilala nyumbani kwao.
Mariam akiwa amelala fofofo, akasikia mtu anamuamsha, moja kwa moja alihisi kuwa ni mama yake anamuamsha ila alivyoamka alishangaa sana kuona kuwa aliyekuwa akimuamsha ni mumewe Juma.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni