MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 12

MTOTO WA MAAJABU: 12

Basi Juma alikaa kwanza ila leo alimshangaa mtoto wao kuwa anakaa maana hakuwahi kumuona akikaa, akauliza
“Kumbe mtoto wetu anakaa?”
Ila akashtuka sana baada ya kuona mtoto wao akishuka kwenye kiti na kumfata kwa kutembea.
Juma alijikuta akisema kwa nguvu tena kwa hali ya uoga,
“Kheeee kumbe na kutembea anatembea!!”
Akatokea Anna pale na kusema,
“Ndio anatembea shemeji, unajua huyu mtoto ni mkubwa kama hivyo mnavyosema kuwa amekaa tumboni miaka miwili, kwahiyo ni mkubwa wa kutosha tu yani huyu ilitakiwa afanye hatua kwa haraka sana hata hivi amechelewa kutokana na chakula mlichokuwa mnampa ila mimi nimeanza kumpa chakula kinachotakiwa basi anakula vizuri na kuendelea na hatua zake na ndio mpaka sasa anatembea”
Juma akapumua kidogo na kuuliza,
“Kwahiyo siku hizi hanywi maziwa?”
“Maziwa anakunywa mara moja moja ila anakula zaidi chakula ambacho tunakula sisi, huyu sio mtoto mdogo shemeji”
Juma alimuangalia mke wake ambaye alikuwa amekaa kimya tu, basi akamuuliza,
“Ulikuwa unajua kama mwanetu anatembea?”
Mariam akajibu,
“Nijue wapi na muda wote nimechoka na kujisikia kulala tu. Yani na mimi nimemuona leo kama ambavyo wewe umemuona”
“Mbona hujashtuka?”
“Sasa unafikiri huko kutembea kunashtua sana? Ngoja siku akuongeleshe ndio utashtuka zaidi na kuamini maneno yangu”
Juma akauliza vizuri kamavile hajawahi kuambiwa swala hili, basi akauliza,
“Kwani anaongea?”
Hapo Anna akamwambia Juma,
“Shemeji, ni vyema uende kula halafu hayo mengine mtajadiliana badae”
Mariam nae akadakia,
“Kweli twende kula, yani nina njaa mimi balaa’
Mariam aliinuka pale, Juma nae alimfata mezani kwenda kula.

Wakati wanakula, Juma akamuuliza Mariam 
“Unaonaje ladha ya chakula?”
“Ni kitamu sana”
“Yani mke wangu hiki chakula ni kama umepika wewe”
Mariam ndio kwanza akaanza kumpongeza Anna,
“Mambo ya Anna hayo, huyu mtoto ni hatari kwenye maposhi. Wasichana wangu wa kazi waliopita wote sikuwapenda ila huyu nampenda sana”
“Mmmh, haya bhana”
Yani Juma alimuona mke wake kutokugundua chochote kile, basi moja kwa moja walipomaliza kula aliamua kwenda kulala pamoja na mke wake ila kama kawaida ya Mariam ni kulalamika kuwa amechoka mwanzo mwisho, hadi Juma alitamani kumwambia ukweli kuwa yule msichana wao wa kazi sio mzuri na anamtumikisha ila tu alijikuta akishindwa kumwambia kwanza.
Kwahiyo walilala, na walipoamka asubuhi tu, Juma alijiandaa na kwenda sebleni ambapo chai ilishaandaliwa na leo ziliandaliwa chapati pale mezani pamoja na chai, Juma alikaa na kunywa ile chai ni kweli chapati zilikuwa ni nzuri sana ila bado Juma aliumia kwani aliona wazi kuwa mkewe ndiye ambaye anafanya kazi mule ndani kwa namna ya kutokujijua wala kugundua chochote.
Juma alikunywa chai na kurudi kumuaga mkewe,
“Ila na wewe Mariam punguza kulala basi mke wangu”
“Nachoka sana yani, nitapunguzaje kulala”
“Kwa stahili hiyo sidhani kama tutaweza kumtafuta mdogo wa mtoto wetu”
“Nikiwa sijachoka tutamtafuta tu, usijali mume wangu ila kwa kipindi hiki niache”
“Unajua umekuwa wa ajabu sana! Ni kweli huwa unachelewa kuamka ila siku hizi Mariam unachelewa sana mke wangu”
“Niache nilale bwana, kazi njema”
Juma hakuwa na namna zaidi ya kuondoka zake kwenda kazini.

Muda huu Mariam aliamka na yeye kuoga na kunywa ile chai aliyoandaliwa huku akiendelea kusifia upishi wa Anna kuwa ni wa kiwango kikubwa sana, kisha alikaa kwanza na kuanza kuongea nae,
“Anna mdogo wangu, una mchumba wewe?”
“Mchumba! Hapana dada mimi sina mchumba”
“Mpenzi je?”
“Hapana dada, hayo maswala ya mapenzi siyawezi nimejitenga nayo kabisa, wakati wa udogo wangu nimeshuhudia mambo mengi sana kwahiyo hata sina hamu na mapenzi”
“Umeshuhudia mambo gani?”
“Nina dada yangu, kipindi hiko alikuwa na mwanaume wake na walikuwa wakipendana sana ila kitu ambacho dada hakukijua ni kuwa yule mwanaume alikuwa akimtumia tu yeye, yani hakuwa na upendo wa dhati. Yule mwanaume alionekana kumpenda sana dada sababu kwetu kulikuwa na hela kwahiyo shilingi mbili tatu hazikumpiga chenga dada yangu na kujikuta akijitoa na kumuhudumia yule mwanaume vilivyo, kumbe yule mwanaume ana mwanamke wake, halafu kibaya zaidi mwanamke wa yule mwanaume akaja kuchanganya kaka zangu wawili kimapenzi, toka hapo nikasema mimi kwangu mapenzi hayana nafasi, ni uongo uongo mtupu, kumjua mtu anayekupenda ni kazi sana”
“Ila umesema ukweli mdogo wangu, kumjua mtu anayekupenda ni kazi sana. Halafu unaweza kumpenda mtu ila yeye asikupende na unaweza kupendwa na mtu ila wewe usimpende ndiomana mimi nilivyoona umri unaenda nikawa sina namna tena ni kuolewa tu na yeyote anayeonyesha kunipenda sana, uwiiiii huyu Juma hadi alikuwa analia sababu ya kunipenda mimi yani, ikabidi tu nimkubalie na kuamua kuishi nae. Ila sikumpenda wala nini, nimejifunza kumpenda ndani ya ndoa”
“Kwahiyo siku hizi unampenda?”
Mariam akatabasamu na kusema,
“Siku hizi nampenda maana hapo mwanzoni nilikuwa naona ni kitu gani tena hiki jamani! Kiukweli mwanzoni sikutulia ila saivi nimetulia na ninampenda tu mume wangu. Kwahiyo wewe Anna hutokuja kuolewa?”
“Sijui kama nitaolewa dada, leo hujachoka dada?”
“Kwanini?”
“Hadi muda huu hujaenda kulala?”
“Tena umenikumbusha mdogo wangu, ila leo ngoja nilale hapa hapa sebleni maana nikilala chumbani nalala sana hadi najisahau”
Na kweli kwa muda huo huo Mariam alivuta mto na kulala pale pale sebleni.

Juma akiwa anatoka kwenye shughuli zake alikutana na yule binti ambaye huwa anakutana nae mara kwa mara, yule binti akamsalimia Juma,
“Habari yako baba Mishi”
“Hivi una matatizo gani wewe! Mwanangu hawezi kuitwa Mishi hata iweje”
“Haya, hongera kwa kupata mdada wa kazi”
“Hivi wewe ni mchawi au ni kitu gani? Umejuaje kuwa nimepata mdada wa kazi?”
“Kwa uvivu ule wa mke wako? Mbona ni lazima mpate msaidizi pale kwenu, hongera sana”
“Wewe unajuaje kama mke wangu ni mvivu?”
“Asiyejua kama mkeo ni mvivu ni nani? Mkeo ni mvivu na jamii yote inamfahamu, nilitamani niwe mimi nafanya kazi kwako ila hata yule uleyemuweka nimemfurahia sana, atamnyoosha mke wako”
“Unamaana gani sasa?”
“Huelewi tu nina maana gani? Siku moja usiende kazini halafu utajua kuwa nina maana gani ila hakikisha mkeo unamuamsha mapema sana hata nenda nae nje ukafanye nae zoezi, hata akatae jitahidi umuweze kwa siku hiyo halafu ndio utajua kitu gani namaanisha”
“Mmmmmh au yule binti anamtumikisha mke wangu?”
“Usiniulize hivyo mimi ila nenda mwenyewe kafanye utafiti, mimi yangu nimemaliza sina mambo ya ziada hapa”
“Poa nimekuelewa”
“Haya kwaheri baba Mishi”
“Tena ukome, mimi sio baba Mishi”
Yule binti alicheka na kusema,
“Yani jina atakalokutajia mwanao utaona bora hata ya jina ninalolitaja mimi, utalia nakwambia”
Huyu binti aligeuka na kuondoka zake, yani Juma alimuangalia kwa hasira kidogo kisha na yeye akaondoka zake kurudi nyumbani kwake huku akiwaza kuwa ikiwezekana kesho ndio asiende kwenye shughuli zake ili aweze kubaki nyumbani kwaajili ya kumuangalia mke wake.

Usiku wa leo, Juma aliongea na Mariam kuwa kesho hatoenda kwenye shughuli zake ambapo Mariam alimuuliza,
“Kwanini huendi sasa?”
“Aaaah si nimeamua kupumzika tu”
“Kwanini upumzike kesho?”
“Jamani, kwani kupumzika kuna tatizo Mariam? Kupumzika ni kuamua tu”
“Mimi kesho kuna kitu nataka nikuagize, sasa ukibaki nyumbani ni nani ataenda kuniletea ninachokitaka?”
“Kwani unataka nini?”
“Yani unavyoniona jamani leo kutwa nzima nimejikuta nikitamani kula tende balaa, kwahiyo kesho nenda zako tu mjini ukaninunulie”
“Khaaaa Mariam jamani!”
“Ndio, fanya hivyo”
Juma hakusema kitu na waliamua kulala muda ule ila kama alivyoambiwa kuwa amuamshe mapema alijikuta akichelewa kuamka kwa siku hiyo, basi alipoamka tu aliamua kujiandaa kwaajili ya kwenda kwenye shughuli zake kwahiyo akamwambia tu,
“Nitakuletea hizo tende, niagize chochote kingine unachotaka Mariam”
“Mmmmh sijui na kitu gani kingine, ila niletee hizo hizo tu”
Basi Juma siku hii hata kunywa chai hakujisikia kwakweli, kwahiyo aliondoka zake na kwenda kwenye shughuli zake.

Mariam alipoamka, moja kwa moja alienda kunywa chai kama kawaida yake ila Anna akamwambia,
“Dada ukimaliza kunywa chai naomba twende nje kidogo”
“Sawa, hakuna tatizo”
Kwahiyo Mariam alipomaliza tu kunywa chai, moja kwa moja alitoka nje na Anna ambapo Anna alienda kumuonyesha pale alipokuwa akipanda mahindi kuwa yameanza kutokeza,
“Dada umeona mahindi yalivyoanza kutokeza! Kila kitu ni maamuzi katika maisha”
“Hongera sana Anna kwakweli”
“Na wewe hongera dada”
“Mimi hata sistahili kupewa hongera maana hata wazo hili sikuwa nalo, halafu hata kulima kidogo sijajishughulisha kabisa, kwahiyo mimi hata sistahili kupongezwa”
“Unastahili dada maana wewe ni mwenye nyumba, mahindi yakikua utaanza kula wewe dada”
Mariam alitabasamu na kusema,
“Na ninavyopenda kula yani, hapo hunibandui mbona, nitaanza kula hayo mahindi kama hata kushika jembe najua vile”
Anna na yeye alikuwa akicheka, kwahiyo walijikuta wakiongea na kufurahi kwa muda, kisha Mariam ndio akarudi ndani na kwenda kulala kama kawaida yake ya siku zote.

Juma akiwa antoka kwenye shughuli zake na leo alikutana tena na yule binti ambaye huwa anakutana nae mara kwa mara halafu yule binti akamwambia,
“Unajua nilijua leo ndio ungefanya nilichokwambia ili ujue ukweli”
“Yani leo nimeshindwa kwanza kabisa nimechelewa kuamka halafu mke wangu kaniagiza tende”
“Ulidhani utaweza? Mkeo akikuagiza kitu lazima umpelekee kwani? Mkeo ni mjamzito kusema akikosa atajihisi vibaya? Si anatamani tu, atakula hata siku nyingine. Sikia Juma, nilijua jana ungeomba usaidizi ila wewe ni hamna kitu kwakweli, tena hamna kitu kabisa”
“Kwahiyo ulitaka nikuombe wewe usaidizi? Wewe ni mganga au ni kitu gani?”
Kisha yule binti alitoa mbegu mbili na kumkabidhi Juma huku akimwambia,
“Leo mkienda kulala, weka hizi mbegu mbili chini ya mito yenu kitandani halafu utapata jibu”
“Mmmmh hizi mbegu umenipa mbona ni njegere na mbaazi?”
“Ndio, ni njegere na mbaazi ila kwangu vina maana kubwa sana”
“Maana yake ni nini?”
“Wewe nenda kaweke kama ninavyokwambia halafu ndio utapata jibu, nimetumia tu hizi mbegu ila nina maana kubwa zaidi ya hizi mbegu”
Juma alichukua zile mbegu na kuziweka mfukoni kisha huyu binti akaondoka na kumuacha Juma akimuangalia tu pale mpaka alipoishia ndipo Juma alipoondoka kwenda nyumbani kwake.

Muda wa chakula cha usiku Juma alikuwepo mezani pamoja na Mariam, na Anna wakila chakula cha usiku kwa pamoja huku wakiongea ongea baadhi ya mambo ambapo Anna aliwauliza,
“Jamani hapa hamna mazoea na majirani?”
Mariam akajibu,
“Majirani wa kazi gani? Kazi yao umbea umbea tu”
“Siku ukipatwa na matatizo je mtakimbilia wapi?”
“Tuna ndugu wa kutosha Anna, hatuna haja ya majirani au unasemaje mume wangu?”
Juma akajibu,
“Mimi sina usemi, ila mimi siwezi kufata fata majirani na kuweka ukaribu nao wakati mke wangu hafanyi hivyo, yeye ndiye anayeweza kuwa karibu na majirani, mimi ni mwanaume na yeye ni mwanamke”
Kisha Anna akasema sasa,
“Ila majirani nao mara nyingine hata sio wazuri, mambo yao ni umbea umbea tu kwenye majumba ya watu. Kuangalia watu wanaishi vipi, wanakula nini, kiukweli hata mimi majirani siwapendi, kwanza hawafai kabisa hao majirani jamani”
Mariam hapo ndio alipapenda zaidi na kusema,
“Ndiomana mimi nakupenda sana Anna, wewe mtoto huna mambo ya Kiswahili kabisa. Mimi nafurahi sana wewe umekuja kwetu”
Walitabasamu pale na kuendelea kula.

Wakati wa kulala, Juma alifanya kamavile ambavyo aliongea na yule binti kwani aliweka zile mbegu kwenye godoro lao na kisha kulala na mke wake.
Ila kiukweli ilikuwa ni tofauti sana leo kwani walifanya kazi ya kujigeuza tu na hakuna hata mmoja aliyelala kwa muda ule zaidi ya kujigeuza hadi mwisho wa siku waliamua kuamka na kuanza kuongea,
“Kheeee jamani kuna nini leo mbona siwezi kulala?”
“Hata mimi nashangaa mke wangu, yani kulala nimeshindwa kabisa, hakuna usingizi kabisa hapa”
Walijikuta wakiongea hadi saa kumi na moja alfajiri, basi Juma akamwambia mke wake,
“Unaonaje tukaenda nje kufanya zoezi labda tutaweza kuja kulala”
“Zoezi gani?”
“Twende tukakimbie kimbie mke wangu”
Kiukweli Mariam alichukia sana kwa yeye kushindwa kupata usingizi, kwahiyo alikubali na kwenda nje kufanya zoezi la kukimbia kimbia nje, yani walikuwa wakikimbia taratibu, Juma alifanya vile sababu hakutaka kumchosha sana mke wake.
Waliporudi ndani, walikuwa wamechoka kwahiyo moja kwa moja walienda kuoga ambapo Mariam alisema wakanuwe chai kwanza na ndio waende kulala tena.
Ila ilikuwa tofauti leo kwani walipofika sebleni walikuta Anna hajaandaa chai wala nini mpaka Mariam alimuuliza,
“Anna vipi leo? Hujaandaa chai halafu na usafi bado hujafanya?”
“Yani dada leo sipo vizuri sana, ngoja nikawaandalie chai”
Anna aliwaandalia chai na kuwatengea ila chai ya leo haikuwa na ladha kama chai wanayokunywaga siku zote.
Basi Juma alimuuliza mke wake,
“Unaionaje chai ya leo?”
Mariam akajibu,
“Sio nzuri kama ya siku zote ila nadhani ni sababu Anna anaumwa”
Basi Juma hakusema sana, yani alichotaka Juma ni mkewe kugundua mwenyewe kuwa huwa anatumikishwa na Anna.

Mariam alipotaka kulala sebleni, Juma alimlazimisha kwenda chumbani ili waongee asilale, ila walipokaa kitandani tu ni kweli usingizi wa Mariam ulikata kabisa kwahiyo hakuweza kulala hadi mchana ulifika wakiongea tu, wakatoka kwenda kula na wakakuta ndio Anna anaandaa chakula ila hadi Mariam alisikitika kwa kile chakula kwakweli na kumsema Anna,
“Jamani mdogo wangu, hata huu ugali haujaiva kwakweli”
“Dada, sipo vizuri hata chakula cha jioni itabidi unisaidie tu”
“Mmmmh mimi huyo na uvivu huu!! Hapana kwakweli, siwezi kupika Anna, jitahidi tu”
Juma akasema,
“Tena jioni naomba mniandalie pilau”
Mariam akamwangalia Anna na kumwambia,
“Umesikia ambacho baba amesema eeeh!!”
Anna akaitikia tu yani hakuwa na namna yoyote ile.

Jioni ilipofika, Juma alikuwa chumbani na mke wake alishangaa tu akipigiwa simu na mtu ambaye wanafahamiana sana, mtu yule alisema kuwa yupo stendi anataka kufika nyumbani kwao,
“Basi nakuja kukufata, nisubiri tu hapo hapo stendi”
Ikabidi Juma amuage mke wake na atoke kwa muda huo ila alitoka akiwa na mashaka sana.
Juma alifika stendi ila hakumuona yule mtu wala nini, alimpigia simu ila hakumpata hewani ikabidi tu aamue kurudi nyumbani ila alipofika tu nyumbani ni moja kwa moja alienda jikoni kwani alikuwa na mashaka sana, alishangaa sana kufika jikoni kumkuta mkewe wake akiendelea na mapishi ya chakula cha usiku.

Itaendelea…..!!!
Kwa mawasiliano 0714443433
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni
close