Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 11

MTOTO WA MAAJABU: 11

Basi Juma aliamua kutoka nje ili kumuangalia Anna, alipozunguka kule nyuma karibu na lile eneo lililolimwa alishangaa kumuona mkewe akiwa yupo kupanda mahindi.
Juma alishangaa sana ukizingatia mkewe alimuona chumbani tena akiwa hoi kabisa, basi Juma akaita,
“Mariam, Mariam…”
Na muda huo yule mke wake aligeuka ila akashangaa kuona kuwa ni Anna ndio aliyekuwa akipanda mahindi, yani Juma hakuelewa alifikicha macho yake sana ila hakuelewa kitu na hakusema kitu badala yake alirudi ndani na moja kwa moja alienda tena chumbani, nia yake ilikuwa ni kumuamsha Mariam ili aongee nae ila badala ya kumuamsha Mariam alijikuta na yeye akiwa amelala.
Juma akiwa kwenye usingizi alimuona mtoto wake akiwa anatembea ndani ya ndoto halafu yule mtoto wake alimwambia Juma,
“Mimi nakupenda sana wewe baba sababu unanipenda sana, hakuna kibaya cha kukupata wewe, ila huyu mama muache akome tu”
Juma alishtuka sana toka kwenye ile ndoto aliyoiota na kumuangalia mke wake ambaye alikuwa hoi ila baada ya muda mfupi na yeye alishtuka na alianza kulalamika kuchoka kama kawaida yake kwa kipindi hiki kulalamika kuwa amechoka sana,
“Nimechoka jamani, viungo vyote vinaniuma mimi jamani!”
“Pole mke wangu”
Ikawa ndio kama Mariam kashtuka vizuri maana mwanzoni hata hakujua kama mume yupo ndani, basi akamuangalia na kumuuliza,
“Umerudi muda gani Juma?”
“Nimerudi muda sio mrefu ila nimekukuta umelala hoi”
“Aaaah kumbe! Yani nachoka jamani siku hizi, nachoka sana au nina mimba tena!”
“Hiyo mimba tena uitoe wapi Mariam? Kumbuka kuwa ulikuwa ukinipa sababu ya mtoto kila siku kipindi kile tunalala na mtoto halafu kipindi hiki kila siku unadai kuwa umechoka haya hiyo mimba itatokea wapi?”
Mariam alitulia na kuona ni kweli hawezi kuwa na mimba nyingine ukizingatia hajashirikiana na mume wake toka alipojifungua huyo mtoto wake na amekuwa na sababu kila siku za kutokushirikiana nae, ila sababu tu Juma anampenda ndiomana alikuwa hamlazimishi.

Usiku wa siku ile, walienda tu kula na moja kwa moja kurudi kulala ila kwakweli Juma alikuwa na maswali sana katika akili yake hata hakujua ni wapi aanzie na majibu ya maswali yake ila aliamua tu kulala kwa usiku huo.
Kulipokucha tu, Juma alipoamka alikuta chai imeshaandaliwa mezani yani kwa kipindi hiki ilimbidi Juma awe anakunywa chai nyumbani kwake kabla hata ya kwenda kwenye mizunguko yake,basi alimuasha mkewe ili waweze kunywa chai pamoja,
“Twende tukanywe chai kwanza Mariam”
“Mmmmh niache nilale kwanza, nikiamka ndio nitakunywa chai”
Juma hakuwa na namna zaidi ya kumuacha alale halafu yeye kwenda kunywa chai na kumuaga Anna, 
“Badae Anna”
“Na leo utawahi kurudi shemeji kama jana?”
“Mmmmh sijui lakini naweza kuwahi kurudi”
“Haya sawa”
Basi Juma akaondoka zake huku Anna akirudi kukaa sebleni na mtoto.

Kwenye mida ya saa nne asubuhi ndipo Mariam alipoamka tena alikuwa amechoka sana, yani alikuwa ajinyoosha tu na kupiga miyayo ya ucbhovu muda wote, basi alienda kuoga na kutoka sebleni huku akimwambia Anna,
“Umeshaandaa chai Anna?”
“Ndio dada, tena muda mrefu tu”
“Aaaah wewe ni binti mzuri sana, wewe ni mchapakazi sana yani mimi siwezi mwenzenu”
“Ila dada kila kiru ni maamuzi, hata wewe ukiamua unaweza”
“Hapana, mimi siwezi, yani mimi ni mvivu sana kufanya kazi”
Basi moja kwa moja alienda mezani na kuanza kunywa chai, huku akimuongelesha Anna,
“Halafu sikukuuliza, hivi ulishamaliza kulima na kupanda?”
“Ndio dada, yani hapa tunangoja mazao tu, tutakula sana mahindi. Kazi iliyobakki hapa ni kupalilia tu”
“Jamani haya mambo mwenzenu ndio siwezi kabisa, wanayaweza watu wa vijijini”
“Hivi dada unajua mimi sio wa kijijini”
“Sasa umewezaje kulima Anna?”
“Kila kitu ni kuamua dada yangu, kulima unashika jembe na kuliinua juu na kulishusha kwenye ardhi, yani ukiamua unaweza”
“Kwahiyo wewe Anna ni umekulia mjini kabisa?”
“Yani dada nikikuelezea historia ya maisha yangu unaweza kulia, maisha yanabadilika sana sio kama tunavyoyategemea. Maisha hayaeleweki”
Mariam alijikuta akitamani sana kujua historia ya Anna hivyobasi alikunywa chai kwa haraka na kwenda kukaa karibu na Anna ili Anna amuelezee historia ya maisha yake,
“Eeeeh niambie mdogo wangu”
“Ila nitakueleza kwa kifupi tu!”
“Ndio nielezee mdogo wangu”
“Yani dada, mimi nilizaliwa kwenye familia ya watoto wanne na mimi ndio nilikuwa kitinda mimba kwa mama yangu, ila wale wenzangu niliachangia nao mama tu, mimi baba yangu yupo. Sasa mama yetu alikufa, tena aliuwawa tu kikatili, yani unamuona mama yako muda huu halafu saa moja badae anauwawa kikatili, unapewa tu taarifa kuwa amekufa. Mimi wakati mdogo nimeishi maisha ya kitajiri sana, nilikuwa sifanyi kazi yoyote, mama alinidekeza na kunipenda sana, alinipa kila nilichokitaka ila tangu amekufa ndio mambo yalipobadilika kwangu. Baba yangu karogwa na mwanamke huko hanitaki na wale ndugu zangu wamechukua kila kitu hawataki kuishi na mimi wanasema niende kwa baba yangu, nimeishi kwa shida sana baada ya hapo, nikawa nahangaika tu, hakuna cha kusoma wala hakuna cha nini na ndio nahangaika tu na kazi za ndani, nashukuru hata nimefika hapa mmenipokea”
“Kheee pole sana, huyo mwanamke aliyemchanganya baba yako akili ataalaaniwa kabisa. Kwahiyo baba yako ana hela tu!”
“Ndio, baba yangu ana hela najua siku akili ikimrudia ndio atanikumbuka mtoto wake ila kwasasa hanitaki kabisa wala hata hanikumbuki”
“Pole sana, hao ndugu zako nao Mungu atawalaani mdogo wangu, yani kweli wakuache uhangaike wakati wenyewe wapo?”
“Yani dada angalia tu watu hivi hivi ila unathaminika ukiwa nacho, mimi walinipenda kumbe sababu ya mama ila kwasasa mama hayupo hawanipendi tena, hawanitaki tena yani mimi nipo tu kuhangaika na maisha”
“Pole sana mdogo wangu, kuanzia sasa jihesabie kuwa umempata ndugu yako maana mimi nitakupenda na kukuthamini, nitakuwa na wewe bega kwa bega yani mimi huwa roho inaniuma sana nikisikia kuwa kuna mtu ndugu zake wamemtenga, usijali Anna, kuanzia sasa mimi ndio ndugu yako”
Basi Anna alienda kumkumbatia Mariam huku akimwambia,
“Asante sana dada”
Mariam alizidi kumsisitiza Anna kuwa atamsaidia na atakuwa nae bega kwa bega ukizingatia ule ufanyaji kazi wa Anna ndio ulimfanya Mariam azidi kuvutiwa na Anna.
Basi baada ya kuongea ongea pale alijikuta akilala pale pale sebleni.

Mariam alipokuja kushtuka muda huu ilikuwa ni tayari mchana, basi akamuuliza Anna pale,
“Kwahiyo nililala hapa hapa”
“Ndio dada”
“Ila leo sijachoka sana wala nini, bado nina nguvu zangu ila siku hizi naamka asubuhi nikiwa nimechoka sana”
“Dada, unaonaje kila asubuhi tukianza zoezi la kukimbia!”
“Weeee, mimi hata mazoezi siwezi jamani, kujichosha tu. Siwezi kabisa”
Basi aliinuka na kwenda kula, ambapo Anna nae alienda kula basi Mariam akawa anakula na kumwambia Anna,
“Unajitahidi kusonga ugali mlaini sana”
“Sababu na mtoto nae anapenda ugali mlaini”
“Kwahiyo huwa anakula?”
“Ndio, huwa anakula. Anapenda sana, ila dada acha kumuogopa mtoto wako nahisi kuwa huwa unamuogopa maana hata siku moja hukai nae”
“Yani Anna mdogo wangu acha tu, ila kwasasa mimi na wewe tumekuwa kama ni ndugu, ngoja nikwambie kuhusu huyu mtoto”
“Eeeeh niambie”
Basi Mariam akamueleza Anna jinsi alivyohangaika na ile mimba kwa miaka miwili na jinsi mama mkwe wake alivyomletea dawa na jinsi alivyoitumia na yale aliyokutana nayo hospitali na jinsi mtoto walivyogoma kumuhudumia na jinsi ambavyo huwa akiongea, basi Mariam akamalizia kwa kumwambia Anna,
“Kiubinadamu lazima mtu uogope kwakweli, ndiomana mimi nimejikuta namuogopa sana mtoto ingawa ni mtoto wangu”
“Sasa unahisi kwanini mimi simuogopi?”
“Sijui, pengine sababu hujaona mambo yake ya ajabu”
“Sikia dada, mambo mengine ya ajabu ya huyu mtoto umeyataka mwenyewe dada yangu. Haya ulipewa dawa uoge kwa siku tatu, ni kitu gani ulichokuwa unakimbilia ukaoga kwa siku mbili? Ni kitu gani kimekushangaza kwa mtoto kutoka na meno, sasa mtoto akae tumboni kwa miaka miwili, akitoka si ameshakuwa mkubwa huyo! Hata kulia tena kitoto hawezi, na ndio kitu kilichotokea hapa, ilitakiwa ukubaliane na hali halisi, kwanza mmeyataka wenyewe, ulishaona mazingira ya mimba yamekuwa ya ajabu, ungevumilia tu na kujifungua nyumbani kisha ungemuhudumia vizuri mtoto wako na baada ya siku kadhaa ungempeleka hospitali na angepata huduma zote ila kule hospitali lazima waogope maana ni mtoto gani anazaliwa anatanguliza miguu? Kwa kawaida huwa mtoto anatanguliza kichwa, ila mtoto akitanguliza miguu basi huyo huwezi ukasema tena kuwa ni wa kawaida, lazima kuna uwalakini hapo, lazima hospitali waogope. Yani wewe mtoto umemnywea midawa kama yote halafu unashangaa kutokea na mambo ya ajabu jamani, sasa unashangaa nini?”
“Ila dawa nilikunywa baada ya kuona mimba imepitiliza?”
“Hivi hujawahi kunywa dawa kwa mganga wakati mimba changa wewe! Usije ukafikiri mimi ni mtabiri dada yangu, kuna vitu tu mimi huwa nikiviona nagundua mambo mengi. Jifikirie kuhusu hili nililolisema halafu utakuja kunipa jibu”
Mariam kidogo alikaa kimya na kumwambia Anna,
“Hebu niambie unachoelewa Anna?”
“Hapana dada, tuendelee tu na mambo mengine”
Basi waliendelea kula na baada ya kula sasa ndio Mariam alienda kulala ndani kabisa wala hakutaka kupata muda wa kutafakari wala nini.

Usiku huu Mariam akiwa anaongea na mume wake alikumbuka pia swala aliloongea na Anna mchana kuwa pengine aliwahi kunywa dawa kwa mganga, basi akamuuliza mume wake,
“Hivi kwenye kumbukumbu zako, wakati nina mimba changa nimewahi kwenda kwa mganga?”
“Kivipi mke wangu?”
“Sababu Anna kaniambia kuwa vitu vingine kwa mtoto wangu nimevisababisha mwenyewe”
“Kama vitu gani?”
Mariam alijikuta akiachana na hii habari na kuanza kumuelezea mumewe habari ya Anna,
“Halafu Juma, kumbe Anna ana shida sana usimuone hivyo”
“Kivipi?”
“Yani kumbe ni yatima halafu ndugu zake wamemfukuza na wamegawana mali zote, mama yake alikuwa na mali nyingi sana, tena mama yake alikuwa ni tajiri ila ndugu zake wamegawana kila kitu na kumuacha Anna patupu”
“Dah masikini, lakini ndio binadamu walivyo yani wanaonea sana watoto yatima”
“Yani nimemuhurumia Anna jamani, acha tu nikae nae hapa kama mdogo wangu, nitampenda na nitamtunza”
Juma aliitikia tu, na wote waliachana na kujadiliana habari ya mtoto tena kwani walijikuta wakijadiliana kuhusu Anna tu kwa wakati huo hadi muda wa kulala.

Kulipokucha tu kama kawaida Juma alijiandaa ila alipita kwanza kunywa chai maana ilishaandaliwa tayari ila kiukweli vingi vilivyokuwa vikipikwa alihisi kama ladha ya chakula ambacho mkewe huwa anapika akiamua kupika ila hakusema neno badala yake alimaliza na kuondoka zake kwenda kwenye shughuli zake, ila kabla ya kuondoka Anna alimuuliza tena na leo,
“Shemeji na leo utawahi kurudi?”
“Sijui inategemea, unataka kuniagiza nini?”
“Hamna kitu shemeji nilikuwa nakuuliza tu shemeji yangu”
“Sawa”
Ila kabla hajaondoka vizuri Anna alimwambia tena,
“Shemeji subiri kidogo”
Kisha Anna alikuja na mwamvuli na kumkabidhi Juma huku akimwambia,
“Hali ya hewa ya leo sio nzuri, uwezekano wa mvua kunyesha ni mkubwa sana, bora uende na mwamvuli shemeji”
“Sawa asante”
Juma alibeba ule mwamvuli na kuondoka zake kwenda kwenye shughuli zake.

Juma akiwa ametoka kwenye kazi zake, alifika muda huu nyumbani kwake na kukuta kila kitu kama kawaida kimeshaandaliwa mezani, sasa alienda chumbani na huko alishangaa sana kwani alikuta mkewe akiwa amelala chini halafu miguu yake ikiwa na tope, alishangaa sana ingawa mvua ilinyesha sana siku ile ila ni ngumu kwa mke wake kuwa na tope na ukizingatia huwa hafanyi kazi yoyote, sasa lile tope alitoe wapi? Basi akamshtua Mariam pale chini ila kabla hajamaliza kumshtua alimsikia Anna alimuita,
“Shemeji, shemeji”
Juma akahisi ni shida ya mtoto, hivyobasi alitoka kwa haraka na kwenda kusikiliza kuwa tatizo ni nini, alipofika sebleni alimuuliza Anna,
“Kwani kuna tatizo gani?”
“Hamna tatizo shemeji ila nilikuwa nakuuliza hivi samaki wa mchuzi unakula kweli wewe?”
“Ndio nakula, kwanini umeuliza?”
“Unajua leo tumepika tu samaki wa mchuzi bila mboga nyingine ndiomana nimekuuliza ili kama huli nikupikie mboga nyingine”
“Aaaah sawa, nakula”
Basi Juma aliachana nae na kurudi chumbani ila hakuona umuhimu wa yeye kuitwa na Anna sababu swali lile angemuuliza tu mke wake ambaye anajua kama anakula au hali, basi Juma aliingia chumbani na muda huu alimkuta mkewe amekaa moja kwa moja alimuangalia miguuni kama kuna matope ila alishangaa sana kuona miguu haina matope tena wala nini ila tu Mariam kama kawaida alikuwa akilalamika kuchoka yani hii hali ilianza kumtia mashaka Juma kwakweli, akaona ni vyema apange siku aende kumuuliza mama yake kwani huwa anamuona mama yake kuwa na uelewa wa mambo mengi sana.

Leo Juma alitoka mapema kwenye shughuli zake na moja kwa moja alienda kwao ili kwenda kuzungumza na mama yake kutokana na yale anayoyahisi yeye kwani alianza kumuhisi vibaya Anna, na lile swala la mkewe kuchoka muda wote ndio lililompa mashaka sana. 
Basi alifika na kumkuta mama yake yupo kwake kama kawaida, basi alimsalimia na kuanza kuongea nae ambapo swali la kwanza kabisa yule mama alimuuliza Juma,
“Kwanza meshapata mdada wa kazi?”
“Ndio tumepata mama, na hiki ndio kilichofanya nije kwako mama”
“Vipi tena? Na huyo mdada wa kazi kaondoka?”
“Hapana hajaondoka ila kuna mambo sielewi toka yule mdada afike, kwanza yule mdada ni mchapakazi hatari yani anafanya kazi hadi raha, tatizo lipo sehemu moja tu”
“Sehemu gani hiyo tena?”
“Ni hivi, toka aje yule mdada basi mke wangu anachoka sana, mke wangu analalamika kuchoka usiku na mchana, kuna siku mke wangu alikuwa kama amelala ila badae nikamuona analima nje ila badae akageuka na kuwa yule mdada, sasa nahisi huenda yule mdada ni mchawi kwahiyo anamtumikisha mke wangu kwenye kazi za mule ndani”
Kwanza kabisa mama yake Juma akacheka sana na kumuuliza Juma 
“Sasa unatakaje?’
“Ndio nimekuja kuomba ushauri kwako mama kuwa nimfukuze yule mdada au nifanye kitu gani, na kama nikimfukuza basi niandalie mdada wa kazi mwingine mama yangu”
Huyu mama alimuangalia kwa makini Juma na kumwambia,
“Hivi akili zako ni nzima kweli Juma? Kama huyo mdada anamtumikisha mkeo basi ni vizuri sana maana mkeo amezidi uvivu jamani, mwanamke gani mvivu kiasi kile? Muache tu akomeshwe, tena huyo mdada usimfukuze wala nini hata usiwaze kumfukuza, nilidhani anakutumikisha wewe kumbe anamtumikisha mke wako, acha tu mke wako atumikishwe maana amezidi sana, mtu gani hata hajielewi yule”
“Kwahiyo mama unaona ni sawa?”
“Kwanza huna ushahidi kama anamtumikisha kweli maana kusema amechoka sio ishara kuwa anatumikishwa na hata kama una ushahidi muache kwanza mkeo apate adabu jamani maana kazidi sana, tena mimi nikija namletea na huyo mdada wenu wa kazi zawadi kabisa, khaaa Mariam anachosha akili na uvivu wake jamani mtu kila kazi afanyiwe, kipindi kile eti sababu katoka kujifungua basi hadi akila vyombo nitoe mimi khaaaa muache tu afundishwe adabu kwanza.”
Juma akaona hakuna sapoti kwa mama yake kabisa ikabidi tu amuage ila mama yake alimkumbusha kitu,
“Hivi mmeshampa mtoto jina?”
“Bado mama”
“Maana jina langu la Ashura mmelikataa, haya mtampa jina gani siku zimeenda”
“Hata sijui tumpe jina gani mama?”
“Nakupa kazi mkajadiliane na mkeo mpate jina la kumpa huyo mtoto wenu”
“Sawa mama nimekuelewa”
Basi kwa muda huu ndio Juma akaondoka zake kuelekea nyumbani kwake.

Juma alivyofika tu nyumbani kwake, kama kawaida alimkuta mkewe akilalamika kuwa amechoka sana tena bila hata ya salamu yani kitu cha kwanza alichokisema Mariam ni kuwa amechoka sana.
Basi Juma alikaa kwanza ila leo alimshangaa mtoto wao kuwa anakaa maana hakuwahi kumuona akikaa, akauliza
“Kumbe mtoto wetu anakaa?”
Ila akashtuka sana baada ya kuona mtoto wao akishuka kwenye kiti na kumfata kwa kutembea.

Itaendelea.....!!!
Kwa mawasiliano 0714443433 au 0765692210.
By, Atuganile Mwakalile.

Leo story ya MWANAUME WA DAR inaendelea.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni