Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 10

MTOTO WA MAAJABU: 10

Kisha alianza kujinyoosha nyoosha viungo vyake na kulalamika,
“Jamani nimechoka mimi, nimechoka sana. Viungo vyote vinauma jamani!”
Ila alishangaa kumuona kama mwanae akitabasamu kisha huyu mtoto akamwambia mama yake,
“Umepatikana sasa na uvivu wako”
Mariam alimuangalia huyu mtoto kwa makini sana leo kisha akasema,
“Jamani huyu sio mtoto wangu”
kisha yule mtoto akasema,
“Wakati unanizaa kuna mwingine alikuwa anazaa zaidi yako?”
Mariam akaogopa kujibishana na huyu mtoto basi akainuka na kwenda chumbani kwake ambapo alichukua nauli tu na kutoka ila mlango wa nje alikutana na Anna ambaye alimuuliza,
“Dada unaenda wapi?”
Mariam hakuwa na jibu la haraka haraka kwani safari ya leo hakujipanga nayo vizuri, kisha Anna akamwambia,
“Yani dada unataka kumtoroka mtoto wako?Hivi unajua kwenye maisha ya tu basi mama ana nafasi kubwa sana, kwanza anabeba mimba, pili anateseka na ile mimba na tatu anazaa kwa uchungu sana, yani mama ndiye anayejua mateso anayoyapata ili kumpata mtoto ndiomana wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi, sasa wewe ni mama gani usiyeujua uchungu wa mwanao? Yani bila ya aibu unataka kumtoroka mwanao?”
Mariam alimuangalia Anna kisha hakusema chochote na kuondoka zake ila Anna alimuangalia tu na kucheka.

Mariam alienda hadi stendi na alikuwa amechoka sana, alisubiria daladala na kuona zinachelewa hivyobasi akaamua kukaa pale stendi na kujikuta akilala pale pale yani hakuwa na habari tena ya kitu gani kinaendelea kwake.
Muda huu Mariam alisikia mtu akimuamsha,
“Weee Mariam, weee Mariam weee”
Alipoamka alikutana macho na mumewe na kushangaa ila alikuwa chumbani basi mume wake akamwambia,
“Nimekuamsha ili nikuage kuwa ndio natoka muda huu”
Mariam alimshika mkono mume wake na kumuuliza,
“Umerudi muda gani na umenikuta wapi?”
“Jana nimechelewa kidogo kurudi ila nimekukuta umelala hoi basi ikabidi nisikusumbue, ndio asubuhi hii nimekuamsha ili nikuage inaonekana umechoka sana”
“Na kweli nimechoka sana mume wangu, ila ngoja niamke nikaoge ninywe chai ila kuna kitu sielewi jamani”
“Kitu gani tena?”
“Aaarrgh sijui kwanini imekuwa hivi, sielewi mimi”
“Huelewi nini mke wangu Mariam?”
Mariam aliinuka na kwenda kuoga, ila Juma alimsubiria hadi Mariam alipotoka kuoga na kumwambia,
“Mke wangu, kuna nguo zangu chafu nyingi sababu ya kazi ya jana, naomba unifulie basi”
“Kheee umeanza kuwa na wazimu wewe mwanaume? Toka lini mimi nikafua! Nitamwambia huyo Anna akazifue”
“Sawa hakuna tatizo, mimi nimekwambia tu wewe sababu wewe ni mke wangu”
Muda huo Juma aliondoka zake na kumuacha Mariam akiendelea kuvaa.

Mariam alipotoka chumbani, alikuta chai imeshatengwa mezani huku Anna akiwa sebleni akicheza na mtoto tu, alimsalimia pale halafu Anna alimkaribisha mezani kisha Mariam alimuuliza Anna,
“Hivi Anna kuna kitu chochote mimi na wewe tumeongea jana?”
“Kitu gani dada?”
“Sijui uliniambia kuwa namtoroka mwanangu?”
“Unamtoroka mwanao? Kivipi?”
Mariam akaona kamavile Anna hamuelewi basi alienda kukaa mezani na kumimina chai huku akifunua vitafunwa ila alishangaa sana,
“Kheee hivi vyote umepika wewe Anna?”
“Ndio dada”
“Jamani, umejuaje kama napenda hivi jama ni Anna! Wewe ni binti mzuri sana, yani bagia na sambusa huwa napenda sana”
Anna alitabasamu tu huku Mariam akianza kula na kusifia kuwa ni nzuri sana huku akimpongeza Anna kwa kupika vizuri ila alivyomaliza kula alirudi kukaa kidogo kisha akajikuta akilala pale kwenye kochi kwa muda kidogo aliposhtuka alimkuta Anna akiwa bado anacheza na mtoto alimuuliza,
“Anna, umesafisha chumbani kwangu?”
“Ndio dada, nimeshasafisha”
“Aaaah upo vizuri sana wewe, na nguo za shemeji yako zile umeenda kuzifua?”
“Nimeziloweka dada, nitazifua muda sio mrefu”
“Na zile nguo zangu?”
“Zote nimeloweka dada, nataka nikianza kufua basi zitakate kabisa”
“Dah ndiomana nakupenda Anna, wewe ni binti mchapakazi sana. Hongera, ngoja mimi nikapumzike kidogo maana nimechoka sana”
“Sawa dada”
Mariam muda huu alienda zake chumbani na kweli alikuta kumesafishwa vizuri sana hadi alipenda na zile nguo chafu zote zilikuwa zimetolewa, basi alijikuta akisema,
“Kwakweli huyu binti ndio mdada wa kazi niliyekuwa nahitaji, sio jitu unaliambia kasafishe chumba linaanza kusema oooh kazi zingimne ufanye mwenyewe dada wakati kumlipa namlipa vizuri aaarggh walikuwa wananikera wale basi tu, ila huyu ndio nimepata kwakweli, nadhani nitadumu nae”
Kisha kwa muda huu alilala sasa.

Mariam aliposhtuka alikuwa amechoka sana na kugundua kuwa hata chakula cha mchana kwa siku hiyo hakula wala nini, basi moja kwa moja alienda sebleni na kumkuta Anna akicheza na mtoto tu,
“Jamani Anna hata kunikumbusha kuhusu kula chakula cha mchana jamani!”
“Samahani dada nilijua ukilala hupendi kusumbuliwa”
“Yani mimi kwenye swala la kula uwe unaniamsha tu maana napenda sana kula na kulala”
“Sawa dada, nitakuwa nakuamsha”
“Yani kama saa hizi njaa inaniuma ile mbaya”
“Usijali dada, chakula tayari”
Anna alienda kupakua chakula na kuweka mezani ambapo Mariam alianza halafu Anna alipakua chakula kingine na kuanza kumlisha mtoto, hapo Mariam alishangaa sana na kuuliza,
“Mbona unamlisha mtoto chakula cha kikubwa?”
“Hata yeye ni mkubwa dada, sio mdogo huyu, kuna mambo kachelewa tu ila ni mkubwa?”
“Unajua ana umri gani huyo?”
“Ana miaka miwili”
“Miaka miwili ya wapi? Ni kweli mimba yake nimekaa nayo kwa miaka miwili ila yeye hana miaka miwili”
“Ila dada, chakula cha hivi ndio anapenda na anajisaidia choo kizuri sana tofauti na kule chakula chako cha kumchanganyia maziwa ya unga na ya ng’ombe”
“Kwani sababu ya maziwa ndio iliyopelekea kujisaidia choo cha aina ile?”
“Hapana sio sababu ya maziwa, ila kuna kitu kipo kwa mwanao halafu ulivyokuwa ukimpa maziwa yale ndio ulikuwa ukimuharibu huyu mtoto, kuna kitu ulikuwa hujagundua kuhusu huyu mtoto ila huyu ni mtoto mzuri sana. Si unaona anavyokula vizuri sana kwa muda huu”
Anna alimlisha mtoto na alipomaliza, Mariam nae alikuwa kamaliza kula huku bado akishangaa sana jinsi ambavyo Anna alionekana kumzoea yule mtoto tofauti na yeye ambaye amemzaa. Mariam akainuka kwanza ili arudi chumbani ila alimuuliza Anna,
“Vipi ulifua zile nguo?”
“Ndio dada, bado kuzianua tu”
“Vizuri sana Anna, ukizianua njoo nazo chumbani na uzipange vizuri kabatini”
“Sawa dada”
Basi Mariam akaingia chumbani kwake ila muda huu hakutaka kulala wala nini, alichukua simu ili ampigie mama yake na amueleze juu ya mdada wa kazi aliyempata ila alijikuta akilala huku ameshika ile simu mkononi.

Juma aliporudi leo nyumbani kwake, aliingia na kumkuta Anna akiwa ametoka kumlaza mtoto chumbani kwahiyo alimuuliza tu,
“Dada yako yuko wapi?”
“Amelala”
“Ooooh anawahi kulala sana siku hizi jamani”
“Anawahi kweli kulala”
Basi Juma aliingia chumbani kwao na alipenda kweli mpangilio wa chumba chao alioukuta, alikuta chumba kimesafishwa vizuri sana, nguo zimepangwa vizuri na alichopenda zaidi ni pale alipofungua kabati na kukuta nguo zimepangwa vizuri sana kabatini, akatabasamu na kumuamsha mke wake, Mariam aliamka huku Juma akitabasamu na kumwambia.
“Asante mke wangu?”
“Asante ya nini?”
“Najua hii ni kazi yako humu chumbani?”
“Kivipi? Ni Anna ndio nilimpa kazi ya kusafisha”
“Hata kama ila kafanya kwasababu yako, nashukuru mke wangu maana humu chumbani kulikuwa kunasafishwa juu juu tu ila leo ni kumesafishwa hadi raha jamani. Nafurahi sana mke wangu”
“Yani huyu Anna ni mchapakazi jamani mume wangu, hadi raha”
“Kweli ni raha, twende basi tukale”
“Mimi tayari nimeshakula, kwahiyo labda ukale wewe tu hata hivyo nimechoka jamani mume wangu nimechoka sana”
Yani Juma alikuwa akimshangaa mke wake kwa kauli ya kuchoka balaa ukizingatia kazi zote zilikuwa zinafanywa na mdada wa kazi, sasa yeye ni kitu gani kinachomfanya achoke kwa namna ambayo anailalamikia kila siku? Yani Juma alikuwa anachukia, ni basi tu alimpenda mke wake.
Juma alienda zake kula na kurudi zake kulala, mpaka asubuhi Mariam alikuwa amelala tu na muda wote alikuwa akilalamika kuwa amechoka sana.

Leo Juma kabla ya kuondoka kwenda kwenye shughuli zake, aliweza kukaa na mke wake kuwa chai kwa pamoja ambapo ilikuwa ni chai na chapati, basi Juma akamtania tu Mariam,
“Kheee huyu Anna anapika chapati kama wewe”
Mariama akatabasamu tu na kusema,
“Ila huyu anajua zaidi kupika”
“Hata wewe mke wangu kupika unajua sema tu ni mvivu, siku ukiacha uvivu wako mbona humu ndani tutakuwa tunajing’ata vidole kwa mapishi yako”
Mariam akatabasamu tu kisha akamwambia tena mumewe,
“Ila siku hizi ni tofauti na wale wasichana waliopita, kila chakula unachokula unakisifia mume wangu”
“Ni kweli, huyu binti naona huwa unamuelekeza kupika maana huwa chakula chake kama umepika wewe vile, kinanoga hatari. Ona kama hizi chapati, kwakweli leo nimefurahi sana mke wangu”
Juma alimaliza pale kunywa chai na kumuaga sasa Mariam kuwa anenda kwenye shughuli zake kwahiyo aliondoka zake.
Muda huu Mariam alienda kuongea kidogo na Anna kwani huwa hata hakai nae kuongea nae sababu ya kulala,
“Hebu Anna mdogo wangu nisaidie kitu, hivi ni kwanini nachoka sana ikiwa sifanyi kazi yoyote?”
“Kulala nako ni kazi dada, mtu gani muda wote unalala jamani! Lazima uchoke”
“Sasa mimi kama hivi nimemaliza kunywa chai najihisi usingizi balaa”
“Sasa huo usingizi ndio unakuchosha”
“Sasa nikae nifanye nini?”
“Unaweza hata ukaenda kulima lima pale nje, unajua dada una eneo zuri sana”
“Kheeee, na wewe usitake kuniudhi sasa, hivi kweli kabisa mimi niende kulima mimi? Kabisa mimi niinamishe mgongo kulima, nimepungukiwa na nini?”
“Kwani wanaolima dada wamepungukiwa na nini?”
“Ni umasikini ndio unaowafanya walime”
“Kheee dada, wakulima ni matajiri sana ujue, yani kilimo kina hera ni sababu tu unakidharau”
“Ila mimi siwezi kulima”
“Sawa dada, sijasema kuwa unaweza. Ni kweli nakuona huwezi kulima maana hata mikono yako ni laini sana dada yangu, ila mimi naweza leo nikalima lima kidogo pale ingawa kulima sio fani yangu pia”
“Bora ufanye wewe, upo vizuri sana wewe mtoto”
Kisha Mariam aliinuka na kwenda kulala ila kabla ya kulala leo alipigiwa simu na mama yake na kuanza kuongea nayo,
“Tena nilitaka kukupigia mama?”
“Mbona hukupiga?”
“Si nikapitiwa na usingizi”
“Yani wewe na huo usingizi umekuwa kama mjinga hadi unakera, haya mbona hukuja tena?”
“Mmmmh mama, wewe acha tu. Kuna makubwa yalinipata”
“Yapi tena hayo?”
“Acha tu mama yangu ila tumepata mdada wa kazi mzuri sana”
“Huyo atavumilia vituko vyenu humo ndani? Na yeye ataondoka tu”
“Hapana mama, yeye kampenda hadi mtoto wetu, anaishi nae vizuri sana halafu ni mchapakazi hatari”
“Ila mwanangu……”
Kabla hajaendelea simu ilikuwa imekatika, Mariam aliijaribisha lakini haikupatikana, basi Mariam aliiweka pembeni na muda huo akaamua kulala tu ingawa mama yake naye ameshamsema kuhusu swala la kupenda kulala kila wakati.

Mariam alipoamka muda huu, alijihisi kuchoka zaidi ya mwanzoni, alitoka kwenda kula na kukuta chakula kimeshawekwa mezani kwahiyo alifikia tu na kuanza kula huku akimsemesha Anna,
“Hivi wewe umeshakula?”
“Tayari dada, nimeshaanza hata kulima huko nje”
“Ooooh kazi nzuri sana, upo vizuri sana Anna. Wewe mtoto nikipata zawadi nitakuletea jamani zawadi yako”
“Asante sana dada, unataka tupande nini?”
“Sijui, kwani tupande nini?”
“Tupande mahindi na maharage”
“Inawezekana eeeh!!”
“Ndio dada, inawezekana. Shemeji akirudi mwagize hizo mbegu ili tuweze kupanda”
“Aaaah ngoja nimpigie simu tu aje nazo, halafu kesho upande hizo mbegu”
Mariam alipomaliza kula, moja kwa moja alichukua simu yake na kumpigia simu mumewe ambapo alimuagiza hizo mbegu za mahindi na maharage halafu alipomaliza hapo alienda kulala.

Juma aliporudi alimkuta mkewe kalala kwahiyo zile mbegu aliziacha sebleni na alimuona mkewe amechoka sana kwahiyo yeye alienda tu kula na kwenda kulala pia.
Kulipokucha tu Juma alianza kuongea na mke wake,
“Hongera mke wangu, hiyo ndio akili sasa tuna eneo kubwa ila hatujawahi kuwaza hata kupanda mahindi ya kula, hongera sana”
“Unafikiri ni wazo langu basi! Ni Anna huyo ndio kashauri hivyo”
“Ila kulima si unamsaidia?”
“Nani amsaidie bhana, mimi na kulima wapi na wapi Juma? Analima mwenyewe tu, halafu kulima anapenda yule mtoto”
“Basi twende tukaangalie alivyolima”
“Aaaah nimejichokea haswa, siwezi kwakweli”
Basi Juma alitoka nje na kuangalia palipolimwa ni kweli palilimwa sehemu kubwa sana na hata yeye alijisemea kuwa Anna ni binti ambaye anajiweza sana sababu kulima eneo kubwa vile sio mchezo.

Mariam hakutoka hata kula chakula cha asubuhi alitoka mchana tu ambapo alikula kidogo sana na kudai kuwa anaenda tena kulala, basi Anna alikuwa akimuangalia tu huku akitabasamu hadi Mariam alimuuliza,
“Mbona unatabasamu tu?”
“Hapana dada, yani swala lako la kulala kila wakati ndio ambalo linanifanya nibakiwe na tabasamu”
“Kwahiyo nakuchekesha eeeh ambavyo nasema kuwa naenda kulala kila muda? Nakushangaza eeeh!”
“Hapana, ila ndio maisha ambayo umeyachagua”
“Sawa, badae niamshe nile vizuri”
“Sawa dada”
Basi Mariam moja kwa moja alienda chumbani kwake na kulala, tena muda huu alijikuta akilala usingizi mzito sana.

Leo Juma aliwahi kurudi kutoka kwenye shughuli zake, alivyofika tu nyumbani moja kwa moja aliingia chumbani kwake na kumuona mke wake akiwa amelala na hajitambui kabisa.
Basi Juma aliamua kutoka nje ili kumuangalia Anna, alipozunguka kule nyuma karibu na lile eneo lililolimwa alishangaa kumuona mkewe akiwa yupo kupanda mahindi.

Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433
By, Atuganile Mwakalile.
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni