Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 09

MTOTO WA MAAJABU: 9

Ila badae alijipa ujasiri na kwenda kumnawisha kisha kumrudisha na kumvisha nguo vizuri halafu akajisemea sasa,
“Kwakweli hii nyumba itanishinda, mtoto anatoa kinyesi kinanuka hivi na kinafanana na kinyesi cha mbuzi halafu mama yake ni mvivu sijawahi ona dunia nzima. Mimi siwezi kuendelea kuishi hapa”
Mara yule mtoto akamwambia Lulu,
“Ulidhani kuwa utaweza?”
Lulu alijikuta akitetemeka mahali pale nakuanguka chini.
Kwakweli Lulu hakujitambua kabisa yani ila alimsikia yule mtoto akiendelea kuongea pale pale,
“Hapa hapakufai Lulu, wewe hufai kukaa na mama yangu nilijua tu kuwa lazima pa kushinde hapa, unatakiwa kuondoka. Tena hata usiage, wewe ondoka tu waache na maisha yao humu ndani, hupawezi”
Yani Lulu alizidi kuogopa pale chini na kujikuta akizimia tu pale pale kwa uoga aliokuwa nao.

Juma na Mariam waliingia ndani na kumkuta Lulu akiwa chini, basi Juma akainama kumuinua ambapo lulu aliinuka bila hata ya kuongea kitu chochote kile kwani moja kwa moja alienda chumbani kwake, yani Mariam na Juma walijikuta wakiangaliana huku wakikaa pale sebleni na kujiuliza kuwa tatizo ni kitu gani mpaka imekuwa vile? Mbapo Juma alimuuliza mke wake,
“Unadhani ni kitu gani kimemsababisha kuwa vile alivyokuwa?”
“Mmmmh sijui ni kitu gani kwakweli maana kumbuka kuwa wote hatukuwepo hapa nyumbani”
“Haya tuachane na hayo, na wewe kwanini umeaniacha hospitali mwenyewe?”
“Aaaah kuna makubwa sana hapa, yani kila nikijitahidi nagonga mwamba”
“Kivipi?”
“Mama ameniambia kuwa mtoto wetu amerogwa, nikaongea nae na tulipatana nae kuwa leo niende nyumbani ili kwenda kuongea nae vizuri swala hilo, nikajua wazi kuwa nikikuomba ruhusa basi huwezi kukubali ndiomana nikaamua kutoroka pale hospitali”
“Khaaaa kumbe! Mbona mambo ya kawaida tu hayo, ungeniambia ningekataa vipi wakati ni kwaajili ya mtoto wetu Mariam? Haya, ila mbona badae umeamua kurudi nyumbani sasa? Na viatu viko wapi Mariam?”
“Kuwe na viatu wakati umetuma kibaka aje kuniibia hadi nauli yangu? Yani mambo vuluvulu, hapa nilipo sielewi kitu, nakuitikia tu. Ngoja na mimi niende nikapumzike kama Lulu labda akili itanikaa sawa maana naona kuwa akili haipo sawa kabisa”
Mariam aliinuka na kwenda chumbani kwao kwahiyo pale sebleni alibaki Juma na mtoto tu.

Juma alitikisa kichwa chake na kuamua kwenda kuangalia jikoni ila alikuta hakuna kitu chochote kilichopikwa ukizingatia huyu mdada wa kazi nae wamemkuta yupo chini na wamemshtua ila hajawajibu kitu zaidi ya kuinuka tu, basi Juma akajisemea,
“Au yule Lulu anajihisi vibaya kwa uvivu wa mke wangu? Maana mke wangu na yeye jamani ni shida sana”
Basi Juma aliamua yeye mwenyewe kuingia jikoni na kuanza kupika chakula cha kula usiku huo.
Juma alipomaliza kupika, alienda kumuamsha mke wake ambaye aliamka na moja kwa moja alianza kula, kisha Juma alienda kumuita Lulu, akamgongea mlango na kumwambia,
“Njoo ule Lulu”
“Hapana shemeji nimeshiba, asante”
“Mmmmh umekula nini?”
Mariam akadakia,
“Sasa na wewe mtu kakwambia ameshiba, mambo ya umekula nini yanatoka wapi? Alichokula anakijua mwenyewe ndiomana kakwambia kuwa ameshiba, muache tu.”
Juma akarudi zake kula na mke wake huku akimwambia,
“Ila mke wangu Mariam, mtu akikataa kula kama hivyo lazima ujue sababu”
“Sasa unataka kujua sababu ili iweje jamani? Mtu kakwambia ameshiba, sasa unataka sababu ya kushiba kwake ili ufanyeje? Halafu hayo maswala ya baba mwenye nyumba kumfatilia fatilia mdada wa kazi yameanza lini? Mkiambiwa mnatembea na wasichana wa kazi mnakataa”
“Jamani Mariam, kipindi chote hiko tumeishi pamoja sijawahi kutembea na msichana wa kazi, ndio iwe leo jamani! Hakuna kitu cha namna hiyo ila mimi ni baba kwahiyo lazima nijali hali ya watu wa kwenye familia yangu”
“Haya unatakiwa kuanza kunijali mimi kwanza”
“Nimekuelewa mke wangu”
Juma hakutaka mabisahano sana kwani aliendelea tu kula pale na mkewe na walipomaliza walimchukua mtoto wao na kwenda kupumzika ndani kwao, ila kama kawaida Mariam hakutaka kabisa kuwekwa karibu na mtoto huyo, hadi Juma aliamua kumuuliza leo,
“Sasa mke wangu ni lini utakubali kulala na mtoto wako?”
“Mimi!! Hapana kwakweli, siwezi kukubali yani ingekuwa inawezekana hata Lulu angekubali basi huyu mtoto angekuwa analala chumbani kwake”
“Kwahiyo wewe unaona ni vyema mtoto alale kwa mdada wa kazi kuliko kulala na wewe?”
“Ndio, tena ingekuwa vyema sana. Itabidi kesho nimebembeleze kama atakubali”
Juma hakusema neno zaidi na kuamua tu kulala kwa wakati huo kwani kuna muda alishindwa kabisa kumuelewa huyu mke wake.

Usiku ule ule, Lulu alipanga nguo zake vizuri yani hakutaka hata kupata mshahara wake wala nini kwani ilipofika saa kumi alfajiri aliamua kuondoka, na hakuona umuhimu wa yeye kuendelea kuwepo mahali hapo.
Lulu aliondoka zake kwa usiku ule hadi stendi huku akiwaza kama atapata usafiri au la, akiwa stendi kuna mdada alikutana nae na kusalimiana nae maana walikutana wawili tu stendi, yule mdada alimuuliza Lulu,
“Unatokea wapi?”
“Kuna nyumba huko nilikuwa nafanya kazi, ila kwakweli nimeshindwa kuendelea kuishi kwenye ile nyumba maana kuna mambo ya ajabu sijapata kuona”
“Mambo gani hayo?”
“Kwanza mama mwenye nyumba ni mvivu huyo balaa, anataka kila kitu afanyiwe”
“Ila unaelewa maana ya mdada wa kazi wewe?”
“Naelewa ndio, mdada wa kazi ni msaidizi wa kazi za nyumbani na msaidizi si kwamba ndio anatakiwa kufanya kazi zote peke yake, kuna kazi zingine zinatakiwa kufanywa na mwenye nyumba”
“Kama kazi gani?”
“Mfano, yule dada kaolewa ila anataka mimi ndio niwe namtandikia kitanda, mimi ndio niwe nasafisha chumba anacholala yeye na mumewe, mimi ndio niwafulie nguo zao za ndani yani yeye hafanyi kazi yoyote ile”
“Huyo dada ana ulemavu wowote?”
“Hamna, ni mzima kabisa yani. Hana ulemavu hata kwa mbali”
“Mmmmh unanishangaza maana walemavu wenyewe huwa kuna kazi wanafanya ila huyo nadhani ni zaidi hata ya walemavu, ila kuna ulemavu wa aina nyingi, na huyo ana ulemavu wa akili. Haiwezekani kabisa mtu mwenye akili timamu kuwa mvivu kiasi hiko! Hatukatai kusaidia, basi mtu uwe unafanya mara moja moja, ndio kila siku kweli?”
“Ndio yani kila siku ndio kazi zangu hizo, hata siku moja humkuti hata akisema leo namlisha mtoto yani”
“Sasa huwa anafanya nini kwasana?”
“Yeye anapenda kulala muda wote, yani akishiba tu basi analala”
“Pole sana, kingine kilichokuondoa hapo tofauti na huo uvivu wa mwenye nyumba?”
“Ni mtoto wa yule dada, ana maajabu sana, ana jisaidia kinyesi cha mbuzi halafu anaongea”
Huyu mdada mwingine akatabasamu na kumwambia Lulu,
“Naomba nipeleke huko tafadhari”
Lulu alimshangaa na kumwambia,
“Ila mimi nimetoroka na sitaki wanione”
“Hawatakuona, wewe nionyeshe tu kuwa nyumba yenyewe ndio hiyo hapo halafu mimi najua cha kufanya maana hata mimi nahitaji kazi za ndani”
“Ila hapo mbona utakimbia”
“Hapana, mimi siwezi kukimbia labda wakimbie wenye nyumba”
Huyu dada alikuwa akicheka tu huku akiongea hayo, basi Lulu aliongozana nae hadi kwenye nyumba ya wakina Mariam na kumuonyesha kuwa nyumba yenyewe ni hiyo hapo kisha Lulu aliondoka sasa na kurudi stendi ambapo alipanda gari na kuondoka zake.

Kulipokucha, wakati Juma amemaliza kujiandaa na kutaka kutoka, Mariam alimzuia kwanza na kumwambia,
“Ngoja kwanza, tuongee na Lulu kabisa kuhusu kulala na mtoto wetu”
“Khaaaa yani umedhamilia kabisa?”
“Ndio, kwa kifupi nimechoka kulala na huyu mtoto chumbani kwetu”
“Haya”
Basi Mariam alimuita Lulu ila Lulu hakuitika, alienda kuangalia chumbani kwa Lulu na kukutana na ujumbe tu, ambao alitoka nao na kumsomea mume wake,
“Dada na shemeji, mimi nimeamua kuondoka. Kazi hapo nyumbani kwenu sitaki tena, kila siku dada huwa unaniambia kama kuondoka na niondoke tu, unaniambia kuwa nisikusumbue wala kukubabaisha kuwa kazi ni nyingi. Kwakweli nimechoka yani dada unatuma kama muhindi vile! Nimechoka sana, na kikubwa ni mtoto wenu ameniogopesha sababu anaongea, kwaherini”
Juma na Mariam walitazamana basi Juma akamwambia mke wake,
“Ila nilikwambia Mariam, uvivu wako huo tutapoteza wafanyakazi wengi sana, kumbuka hata kipindi huna mimba ni wadada wangapi wa kazi walioondoka kwetu? Haya saivi una mtoto ndio mambo yamekuwa yale, yale. Mimi nilikwambia Mariam yakitokea haya usinizuie tena kwenda kazini”
“Kheee unadhani utaondoka uniache hapa peke yangu na huyu mtoto? Kwahiyo wewe unaona uovu wangu tu wa uvivu ila uovu wa mwanao anayeongea huuoni wala nini! Yani wewe huoni hata kama huyu mtoto ndio anayefanya wadada wa kazi waondoke humu!”
“Hata kama, ila sababu kubwa ni uvivu wako wewe, tena usikute hata huyu mtoto karogwa sababu ya uvivu wako, sijui ni mwanamke wa aina gani wewe!”
“Si unipe talaka yangu, kwanini unateseka sasa?”
“Talaka sikupi sababu nakupenda sana ila jirekebishe Mariam”
Juma akataka kutoka ila Mariam akamzuia kwa madai kuwa hawezi kubaki mwenyewe, Juma hakuwa na namna zaidi ya kuanza kupiga simu kuomba msaada wa kupata mdada wa kazi, kwanza Juma alimpigia mama yake simu ambapo alipomwambia tu mama yake alishangaa sana,
“Kheee huyo Lulu ni binti mstaarabu sana, mpole na mchapakazi, amewashinda huyo niwatafutie nani sasa?”
“Tusaidie mama yangu?”
“Kwakweli msitegemee kwangu maana sina msaada wowote”
Simu ilipokatika ilibidi Juma ampigie simu mama yake na Mariam ili amuombe msichana wa kazi pia, ambapo huyu mama alimwambia Juma,
“Mtoto wako ndio kikwazo hapo, hakuna msichana wa kazi atakayekubali kuishi na mtoto wa ajabu kiasi hiko”
“Ila mama sio mtoto tu ila wadada wengi wanaondoka kwasababu ya uvivu wa Mariam”
“Ila na wewe wakati unamuoa Mariam si nilikwambia lakini? Si nilikwambia kuwa mtoto wangu ni mvivu, kwani nilikuficha hilo jambo? Nilikuweka wazi kabisa kuwa Mariam wangu namjua mwenyewe, ya kwamba ni mvivu sana na siku zote alikuwa anatamani kuolewa ili aondoke nyumbani na kuachana na kazi za nyumbani, si nilikwambia wewe! Unalalamika nini sasa?”
“Basi mama yameisha, ila nahitaji mdada wa kazi”
“Tafuteni tu huko huko maana huku siwezi tena, Dora kashawatangazia sifa mbaya sana, siwezi kwakweli”
Mama Mariam akakata simu, kisha Juma akamuangalia Mariam na kumwambia,
“Unaona sasa Mariam, uvivu wako huo umefanya hadi tuwe na sifa mbaya”
“Uvivu wangu wapi, unadhani sijamsikia mama anachosema hapo? Ni mtoto ndio kafanya tuwe na sifa mbaya na sio uvivu wangu”
“Kwahiyo leo sitatoka?”
“Ndio, hakuna kutoka hadi tupate msichana wa kazi wa kuishi na mimi hapa”
Yani Juma alichukia sana, kwa mara ya kwanza alijikuta akijuta kumuoa huyu mwanamke kabisa.
Ila muda huo huo wakasikia mtu akibisha hodi, ikabidi Juma aende kufungua maana Mariam mara nyingi huwa na uvivu sana.
Akaingia binti ambaye kwa kumkadilia alikuwa kwenye miaka kumi na nane, basi aliwasalimia pale na kuwaambia,
“Samahanini naomba mnisaidie”
“Tukusaidie nini?”
“Natafuta kazi, kwahiyo kama kuna vikazi vya kufanya hapa mnaweza kunipatia au kama kuna mtu anahitaji msichana wa kazi mnaweza kunielekeza niende”
Mariam alimuangalia na kupumua kisha akasema,
“Yani mara nyingine ni kama bahati vile, sikia binti mimi na mume wangu hapa tulikuwa tukihitaji sana msichana wa kazi kwahiyo kuja kwako wewe imekuwa kama bahati”
“Jamani asanteni sana, nawashukuru sana”
Huyu binti alipiga magoti kama ishara ya kuwashukuru kwa hiki ambacho wamefanya kwake.
Hapo ndipo walipoanza kumuuliza maswali,
“Unaitwa nani kwani?”
“Naitwa Anna”
“Oooh Anna, karibu sana. Mimi dada yako naitwa Mariam, na huyu shemeji yako anaitwa Juma”
“Nashukuru sana kuwafahamu”
“Na sisi tunashukuru pia, karibu sana Anna”
“Asante”
Basi walimkaribisha pale Anna kuwa ni msichana wao wa kazi, na muda huo huo Juma aliweza sasa kumalizia kujiandaa na kuondoka zake kwenda kwenye shughuli zake.
Mariam alifurahi sana na kuanza kumuelekeza yule Anna baadhi ya mambo na kazi za pale nyumbani ikiwemo na kazi ya kumuhudumia mtoto wao, pia alitumia mwanya huo kumwambia Anna kuwa mtoto atakuwa analala na yeye sababu mtoto huyu huwa analala na wadada wa kazi.
“Aaaah kwahiyo halali na wazazi wake huyu?”
“Ndio, kashazoea kulala na mdada wa kazi huyu”
“Sawa mama hakuna tatizo”
“Nimefurahi sana Anna kuja kwenye maisha yetu”
Yani Mariam alikuwa na furaha kubwa sana kwa siku hii ya leo.

Kwa siku hii hii moja tu, Mariam alipenda kweli utendaji kazi wa Anna kwani alionekana ni msichana aliyekuwa anajishughulisha sana, basi Juma aliporudi wakati wa kulala alimuuliza kwanza mke wake,
“Mtoto je?”
“Kashachukuliwa na Anna huko amelala chumbani kwake”
“Duh!! Mke wangu, yani ushamwambia huyo binti alale na mtoto ikiwa huyo binti humjui vizuri wala nini”
“Sasa wewe unadhani kuwa huyo binti atamla mtoto wetu au ni kitu gani?”
“Hapana, mimi nimesemea tu. Vipi utendaji wake wa kazi?”
“Kwa leo tu nimempenda ila ngoja niendelee kumuangalia nitakupa jibu zuri mume wangu kadri atakavyoendelea kunifurahisha”
“Sawa, ila mimi binafsi sijapenda kwa mtoto kulala na msichana wa kazi”
“Ila mimi nimependa tena nimependa sana kwani yule mtoto alikuwa akizuia mambo yetu mengi sana”
“Lakini ni mtoto wetu”
“Hata kama ni mtoto wetu ila si haki yake kutufanya tusiwe na furaha, maisha yenyewe mafupi haya, tunatakiwa kufurahi, kweli tukawaze vioja vya mtoto kila siku! Kwanza nashukuru sana alivyopatikana huyu mdada wa kazi ambaye analala na mtoto wetu”
“Haya siongei zaidi”
Juma alikuwa sio mtu wa kubishana sana kwahiyo mara nyingi alimuachia ushindi tu mke wake ili mke wake afurahi ingawa ukweli hakupenda pia kuona kile ambacho kinaendelea pale nyumbani kwao.
Kulivyokucha tu, mapema kabisa akajiandaa na kwenda zake kwenye shughuli zake.

Kwakweli Mariam alipenda utendaji wa kazi wa Anna na alionekana kuwa ni mchapakazi sana hadi Mariam alimsifia Anna kwa mumewe Juma,
“Yani kwa siku hizi mbili tu, kwakweli nimempenda huyu binti hatari, unajua anafanya kazi sana tena sana”
“Basi cha uvivu umefurahi sana mke wangu kwa hilo”
“Kweli nimefurahi, unajua nakaa tu siku hizi na hiki ndio ninachokitaka. Yani mimi maswala ya kufanya fanya kazi kama mtumwa akuuu siyataki”
“Kwahiyo mtoto humuogopi tena?”
“Nitamuogopa wapi na muda wote huyo Anna ndio anashinda na mtoto! Yani anamuhudumia, anampenda hadi raha kama sio yule mtoto aliyekuwa akiniongelesha jamani, kwa Anna anatulia balaa”
“Basi ni vizuri kusikia hivyo mke wangu”
Juma alimjua mkewe kuwa ni mvivu kwahiyo alivyosikia yule msichana ni mchapakazi aliona ni jambo la kheri sana, basi kwa kipindi hiki walikuwa wakilala kwa furaha sana.

Leo Mariam alivyoamka alikuwa amechoka hatari, muda huu Anna alikuwa ameenda kumlaza mtoto chumbani kwake anapolala nae.
Basi Mariam alitoka sebleni na kumkuta Anna ndio anatoka chumbani pia,
“Hivi Anna ulifua na zile nguo za baba?”
“Ndio mama, na za kwako pia nimeshazifua”
“Oooh wewe ni binti makini sana Anna, ila leo nimechoka jamani, mgongo wote unauma”
“Pole sana dada”
“Naomba tu niletee chai niweze kunywa”
Anna akamuandalia Mariam ile chai ambapo Mariam alishangaa kwa vile vitafunwa alivyoweka Anna sababu alijua kutakuwa na mkate tu ila alishangaa kuona chapati,
“Kheee hizi chapati Anna umeenda kununua?”
“Hapana dada nimezipika”
“Kheee kweli wewe ni noma Anna, sasa chapati umepika saa ngapi? Nguo nazo umefua saa ngapi?”
“Unashangaa hilo tu dada, na maji nimejaza kila chombo”
“Kheee kwakweli nashukuru umekuja kwenye maisha yangu, hapa tu nimeamka na uchovu. Unajua kuchoka, yani nimechoka balaa”
Basi Mariam alikunywa ile chai huku akimsifia Anna kuwa anapika chapati vizuri sana.

Mariam alipitiwa na usingizi pale sebleni, alipokuja kushtuka alijikuta amechoka kushinda hata ya alivyokuwa amechoka asubuhi, alipotazama kwenye kochi aliona mtoto wake amekaa kwenye kochi pale, alishangaa sana na kujikuta akisema,
“Kheeee kumbe saivi wewe mtoto unakaa!”
Kisha alianza kujinyoosha nyoosha viungo vyake na kulalamika,
“Jamani nimechoka mimi, nimechoka sana. Viungo vyote vinauma jamani!”
Ila alishangaa kumuona kama mwanae akitabasamu kisha huyu mtoto akamwambia mama yake,
“Umepatikana sasa na uvivu wako” 

Itaendelea…..!!!
Ka mawasiliano 0714443433
By, Atuganile Mwakalile.

DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni