Featured Post

MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 06

MTOTO WA MAAJABU: 6


Kisha wakaingia ndani sasa na kusogea mezani, ila walishangaa sana kwani ugali wote ulishaliwa na samaki wote walishaliwa.
Yani kila mtu alibaki na mshangao wa hali ya juu, Dora na Mariam walitazamana wakati huo Juma aliuliza,
“Hiko chakula kiko wapi sasa?”
Mariam akamjibu,
“Hata sisi tunashangaa mume wangu ujue”
“Mnashangaa nini sasa?”
“Hivi huoni kama chakula kimeliwa hapa? Tena kilikuwa ni kitamu hicho balaa”
“Sasa kimeliwa na nani?”
“Hata sisi tunashangaa”
Mariam akamtazama Dora na kumuuliza,
“Eti jamani Dora, si tuliandaa chakula mezani hapa!”
“Ndio dada”
“Itakuwa nani amekula jamani!”
Juma aliwaacha pale na kwenda chumbani kwani moja kwa moja alihisi huyo mke wake Mariam na Dora wamefanya jambo, yani alihisi kuwa wamekula kile chakula maana hakuona kama ni kitu cha kawaida kabisa kile.
Aliamua tu kujilaza, ila alikuwa akihisi njaa sana maana tayari alishasema kuwa siku hii angekuja kula nyumbani kwake.

Dora na Mariam wanaulizana tena kwa muda ila Dora anahisi kitu kuwa huenda Mariam kamvizia wakati yuko nje na amekula kile chakula ila hakusema kwa muda huo, basi Mariam akamwambia Dora,
“Hebu Dora tufanye hivi, songa ugali mwingine niende hapo gengeni nikanunue hata tembele uje upike tule”
“Dah!! Njaa inauma sana dada”
“Hata mimi njaa inaniuma ila sijui ni kitu gani kimetokea jamani”
Basi Mariam akaondoka na kumuacha Dora akisonga ugali mwingine huku akijiuliza mambo mengi sana, kisha Mariam alirudi na mboga ambapo Dora aliipika na Mariam akamuita mumewe wakala kile chakula ila Juma hakuwa na furaha kabisa kwani alihisi ni mchezo mchafu kafanyiwa na mke wake ukizingatia mke wake ni mvivu sana.
Waliposhiba, moja kwa moja Mariam alienda kulala maana alikuwa akishiba basi anashikwa na usingizi sana, muda huo Dora alikuwa nje akiosha vyombo, Juma aliamua kwenda kumuuliza Dora,
“Samahani Dora, hivi dada yako kweli alipika chakula leo?”
“Kupika ni kweli alipika”
“Niambie ukweli Dora maana mke wangu kwa uvivu namjua vizuri sana, ni mvivu sana huyu mwanamke. Alipika kweli?”
“Hapo nakwambia ukweli shemeji, kupika alipika ingawa wakati anapika anatuma huyo kama muhindi, utasikia, nisogezee maji, hebu koroga hapo, nisogezee mwiko, hebu nikatie kitunguu yani yeye akikaa mahali basi habanduki ndio hapo hapo ila kupika alipika shemeji”
“Sasa chakula kimeenda wapi?”
“Hapo hata mimi nashangaa kwakweli, chakula kimeenda wapi? Tena alipika vizuri hadi mimi nikawa natamani na kuamua kutoka nje kukusubiri maana alisema tukusubiri kwanza ndio tuweze kula kile chakula, nilipokuona unakuja nilimuita na ndiomana na yeye alitoka nje kukuangalia kama unakuja kweli, ila sasa aliyekula kile chakula ndani hata sijui shemeji”
“Mmmmh!! Sawa, nitajua cha kufanya”
Basi Juma akaondoka zake na kumuacha Dora pale akimalizia kuosha vyombo.

Usiku ule wakiwa sebleni waliweza kujadiliana sasa kuhusu mtoto maana alionekana muda wote kuwa ameshiba sana,
“Yani leo mtoto kanywa maziwa kidogo sana”
Juma akauliza,
“Au anaumwa?”
Mariam akasema,
“Sidhani kama anaumwa ila labda kabadili tu kipindi maana kuna kipindi watoto huwa wanakula sana na kuna kipindi huwa hawali sana”
Basi Dora akasema tena,
“Ila mbona analala sana?”
Juma hakutaka yale majadiliano zaidi kwani aliinuka na kumbeba mtoto halafu akampeleka chumbani na kumlaza, kisha yeye alibaki nae chumbani huku Dora na Mariam wakiwa pale wanajadiliana.
“Ila dada mbona mtoto analala sana leo?”
“Mmmmh Dora, mambo ya mtoto huyu yaache tu, yatakuumiza kichwa, fanya tu kazi zako maana ukifikiria ya huyu mtoto unaweza kuwa kichaa”
Kisha Mariam aliinuka na kwenda kulala pia, ila kiukweli Dora alikosa amani kabisa ya kuishi mule ndani kwanza alianza hata kupatwa na uoga flani hivi.

Asubuhi na mapema, Dora aliamka na kuandaa chai kwanza na vitafunwa kisha akaiweka mezani na kwenda kufanya sasa kazi zingine, alisafisha ndani, alienda kuosha vyombo, kufagia nje na kujaza maji, aliingia tena ndani kwenye mida ya saa tatu asubuhi wakati huo Mariam nae alikuwa ndio anaamka, basi akamsalimia na kitu cha kwanza kabisa Mariam aliangalia mezani na kushangaa kuona Dora alishatenga chai,
“Kheee leo mapema ushatenga chai?”
“Ndio dada, nimepika mapema kabisa”
“Sema leo sijaamka na njaa kabisa, sina njaa wala nini. Ngoja nikae kae kwanza, au ngoja nikaoge kwanza”
Basi Mariam alienda kuoga, wakati huo Dora na yeye alitoka nje, shida ya Dora ni kuona kama ile chai iliyoandaliwa itanywewa au ni vipi maana bado hakuelewa kuhusu chakula cha jana.
Ila hadi badae anarudi ndani, na Mariam anakuja na kunywa ile chai hawakukuta imenywewa hata kidogo.
Walipomaliza ndipo mtoto alipoanza kulia njaa ambapo Dora alienda kumuandalia maziwa na kumpatia yale maziwa, kisha yule mtoto aliyanywa na kulala, muda huu Dora aliendelea na mambo mengine ila bado alikuwa akijiuliza kuwa chakula kililiwa na nani.

Muda huu wakiwa wamekaa pamoja, Dora aliamua kumuuliza swali Mariam kwani kuna kitu kilikuwa kinamshangaza sana toka amefika mahali hapa,
“Dada, toka nimefika ni siku nyingi zishapita ila mbona sijawahi kuona huyu mtoto akijisaidia haja kubwa?”
“Kheee unapenda kufua nguo za haja eeeh!”
“Hapana sio hivyo ila kujisaidia haja kubwa ndio uhai wenyewe huo, mtu yoyote lazima ujisaidie, kumbuka mtu unakula chakula, je kinaenda wapi kama mtu hujisaidii? Sasa huyu mtoto toka nimefika sijakusikia hata mara moja kuwa amejisaidia haja kubwa”
“Mmmmh Dora, acha tu habari za huyu mtoto nakwambia, wala hata usizifatilie ukitaka kuishi kwa amani”
“Halafu mbona anaonekana ni mtoto mkubwa tu ila muda wote huwa unamlaza kwenye kochi? Kwani haiwezekani akakaa huyu mtoto dada?”
“Wewe unavyomuona huyo mtoto unaweza kumkadilia kwenye umri gani?”
“Yani anaonekana ni mtoto mwenye mwaka na kitu hivi”
Mariam alimuangalia mtoto wake kisha alimuangalia Dora na kumuuliza,
“Hivi umeshapika chakula cha mchana?”
“Bado sijapika”
“Basi nenda kapike kwanza tuje kula maana sidhani kama nina majibu ya maswali yako”
Dora hakuwa na jinsi zaidi zaidi ya kwenda kupika tu chakula cha mchana.
Muda huu Mariam aliinuka na kwenda kulala chumbani kwani alikuwa akijihisi uvivu sana kuendelea kukaa pale sebleni.

Dora alipomaliza kupika, aliandaa chakula mezani na kukiacha hapo halafu yeye alitoka nje kwani alitaka kusona kama na siku hiyo hiko chakula kitaliwa au la, basi akakaa nje kwa muda sana hadi pale alipoitwa na Mariam,
“Wewe Dora, kumbe umemaliza kupika hata husemi jamani!”
“Samahani dada, nilitoka kupunga upepo nje”
“Haya basi, njoo tule”
Walienda na kukaa kula, ila chakula kilikuwa vile vile, yani hakikuliwa wala nini kilikuwa vile vile kama ambavyo Dora alikiandaa.
Basi walikula pale huku wakiongea mambo mbalimbali tu kwa wakati huo.
Walipomaliza tu, Dora alitoka kwenda kuosha vyombo ila kabla hajaanza kuosha yule mtoto alijisaidia maana huwa akijisaidia ni harufu nyumba nzima, Mariam alimuita Dora,
“Wewe Dora, hebu njoo. Msafishe mtoto hapo amejisaidia”
“Mmmmh dada!!”
“Unaguna nini sasa?”
Dora hakujibu ila alienda kumchukua mtoto ili akamsafishe, kwakweli hata yeye alishangaa na kumwambia Mariam,
“Dada, mbona anajisaidia kama kinyesi cha mbuzi?”
“Aaah ni sababu ya kutokujisaidia kwa siku nyingi”
“Hapana dada, hii ni tatizo. Kikwetu nakumbuka kuna dawa tulikuwa tukimpa mtoto kama akitoa haja inayofanana na mbuzi, ila huyu ni kama ya mbuzi kabisa”
“Dawa gani”
“Inapatikana polini, unataka nikamtafutie na huyu?”
“Ndio, itakuwa vizuri ukifanya hivyo”
“Sawa basi, kesho nitaenda kuiangalia kwenye kale kapori”
“Sawa mdogo wangu, ila utaenda muda gani?”
“Itabidi niende jioni dada maana hiyo dawa itabidi tumpatie asubuhi”
“Aaaah!! Basi sawa, hakuna tatizo mdogo wangu”
Wakajadiliana pale na kuendelea na mambo mengine.

Usiku ule Mariam anamwambia mumewe kuhusu dawa ambayo Dora ameisema, na Juma anakubaliana na hiyo dawa,
“Kama dawa ipo basi ni vizuri sana, mtoto apatiwe maana sio jambo la kawaida hata mliponiambia kuwa mtoto anajisaidia kinyesi kama cha mbuzi nilishangaa sana, ila kama kuna dawa ni vyema mtoto akapatiwa”
“Sawa, kasema kuwa ataenda kuitafuta kesho jioni”
“Sasa mke wangu, itabidi chakula cha usiku upike wewe au unaonaje hapo?”
“Kweli itabidi nipike mimi ila na wewe uwahi kurudi, ili Dora akienda huko basi wewe uwepo hapa nyumbani na mimi”
“Ila umpate mtu wa kumtuma muda wa kupika eeeh!”
“Aaah jamani mume wangu, unaniona mimi ni mvivu hatari. Sikia, kesho nitapika pilau, kwahiyo nitakachokifanya ni kila kitu tutaandaa na Dora, yani ataondoka hapa wakati mimi ndio naanza kupika. Hapo atakuwa kanisaidia”
“Ila mke wangu huwa unaonaje kitu kama hiko ukikifanya mwenyewe?”
“Jamani huwa naona uvivu hatari, mara nyingine sio kwamba sitaki kufanya kazi ila naona uvivu”
“Punguza huo mwili mke wangu”
“Umeanza sasa, uvivu wangu na mwili vinauhusiano gani? Mbona kuna watu wembamba wavivu? Na kuna watu wanene wavivu pia. Kwanza mimi uvivu nimeanza zamani kabla hata sijanenepa, umesahau kuwa hii mimba ndio ilifanya ninenepe hivi? Umesahau kipindi unanioa Juma?”
“Kweli, kipindi kile hukuwa mnene hivyo”
“Ndio hivyo, wale wenye miili yao ya asili wanaweza kuendelea na kazi ila wengine sio asili yetu, ukijumlisha na uvivu wa siku zote basi ndio balaa. Ila nitapika hiyo kesho maana hata mimi nataka hiyo dawa ya kumpa mtoto aache kutoa haja ya mbuzi, halafu inanuka hiyo hatari”
Walijikuta wakiongelea hilo swala la dawa ya mtoto sasa, walijadiliana kwa muda kisha ndio waliamua kulala kwa muda huo.

Mapema kabisa leo, Dora alifanya vile vile kwa kuandaa chai na mkate, kisha akaweka mezani na kwenda kuendelea na shubhuli zingine, ila hadi anarudi hakuna ambacho kilikuwa kimeliwa wala nini yani kila kitu kilikuwa vile vile hadi muda ambao yeye na Mariam walikaa na kunywa chai, yani bado Dora alikuwa akijiuliza sana kuwa ni kitu gani kinafanyika mule ndani? Mbona akiweka chakula hakiliwi kama ambavyo wanakuta chakula kilichotengwa na Mariam? Hapo hakuelewa kwakweli.
Basi alifanya kazi zake na muda huu alikuwa amekaa na dada yake Mariam na kuanza kuongea,
“Badae ndio nitaenda kuchuma ile dawa”
“Aaaah tena umenikumbusha, jioni napika pilau. Haya kalete vitunguu swaumu umenye na utwange”
“Kheeee dada sio tumenye?”
“Sasa vitunguu tu navyo tumenye wote jamani!! Kheeee Dora upoje wewe, kutaka kushindana na mama mwenye nyumba!”
Hapo Dora hakuongea zaidi, basi akenda kuleta vile vitunguu na kumenya huku Mariam akimwambia,
“Tena andaa kila kitu unachojua kinapaswa kupikwa kwenye pilau, yani mimi nataka nikianza kupika basi nipike moja kwa moja, kusiwe na kingine cha kufata. Niwekee kabisa”
Basi Dora alifanya kazi ya kuchambua kila kitu na kumuwekea jikoni Mariam ili akianza kupika kila kitu kiwe tayari,
“Hivi na ile nyama imeiva eeeh Dora?”
“Ndio dada, nimeshaiepua”
“Sawa umefanya vizuri mdogo wangu ila msubirie shemeji yako arudi ndio uende huko porini kuchuma hiyo dawa”
Dora aliitikia pale na kuendelea na mambo mengine pale.

Kweli Juma aliwahi kurudi na alipofika tu, Dora alijiandaa kwaajili ya kwenda kuchuma dawa kwahiyo pale alimuacha Mariam na mume wake.
Dora alienda kwenye pori ambalo halikuwa mbali sana na pale kuangalia ile dawa ya kwao ambayo huwa wanawapa watoto wadogo ila akiwa kule alijiuliza sana,
“Mbona yule mtoto anaonekana mkubwa ila ananyweshwa maziwa tu! Yule mtoto alitakiwa kupata na vyakula vingine, kwanini anapewa maziwa tupu? Nitamuuliza yule dada leo”
Basi akatafuta tafuta ile dawa na kuiona, hivyo basi akaichuma ya kutosha tu na kuanza kurudi zake nyumbani kwao.
Akiwa njiani kurudi kuna mdada alimuita Dora,
“Dora, Dora”
Dora aligeuka na kumuangalia aliyemuita, ila sura ya yule mdada ilikuwa ni ngeni kabisa machoni mwake, hata alishangaa imekuwaje yule mdada kumfahamu yeye, ila yule mdada alitabasamu na kumsogelea Dora kisha alimsalimia,
“Za siku Dora”
Yani Dora alikuwa akimjibu kinyonge maana hakumkumbuka kabisa,
“Mbona unajibu kinyonge hivyo?”
“Unajua sikukumbuki kabisa, samahani. Kwani wewe nani? Mimi na wewe tunafahamiana vipi?”
“Najua ni zamani sana, kunikumbuka itakuwa shida. Ila Dora hubadiliki kabisa wewe, sura yako ipo vile vile jamani. Vipi hayo majani unayapeleka wapi?”
“Ni dawa, nampelekea mtoto wa dada yangu”
“Kafanyaje kwani?”
“Aaaah ni dawa tu ya kumsaidia tumbo”
“Hivi unamjua vizuri mtoto unayemlea Dora?”
“Kumjua kivipi? Na wewe umenijuaje?”
“Mimi nakujua, na huyo mtoto unayemlea namjua pia, nakuonea huruma sana”
“Jionee huruma na wewe, mimi nipo kazini sijui mwenzangu unataka nini?”
“Ni bora nibaki sina kazi kuliko kufanya hiyo kazi unayoifanya wewe, mama mwenye nyumba ni mvivu haijapata kutokea, katoto kajabu hakuna mfano halafu wewe umetulia tu”
Dora aliamua kuondoka zake, kwani kitu ambacho alikuwa hakipendi kwneye maisha yake ni kuongea mambo ya wengine, alikuwa anaona ni vyema awaambie wahusika lakini sio kuongea na yasiyomuhusu.

Dora alifika na kukuta chakula kinanukia hatari, yani kile chakula kilikuwa kinavutia sana, wakakipakua na kuweka mezani kwaajili ya kula, hapo Mariam aliandaa na kachumbari nzuri kabisa ila Juma akasema,
“Jamani, bila pilipili kweli! Chakula kitamu hivi kikose pilipili! Ngoja nikachukue pilipili kwanza tuje kula”
Basi Juma alienda kununua pilipili wakati huo Mariam na Dora waliandaa chakula mezani, kisha Dora alienda kuweka ile dawa vizuri halafu Mariam alienda kuoga kwanza.
Muda kidogo Juma aliwaita maana alikuwa amesharudi, basi Mariam na Dora walifika,
“Khaaaa jamani, mmeshindwa kunisubiri kweli nimeenda kuchukua pilipili tu hapo”
“Kwani vipi?”
“Vipi nini? Huoni hapo mezani mlichokifanya”
Mariama aliangalia vizuri na kukuta chakula chote cha mezani kimeliwa, ile kachumbari pia imeliwa,
“Khaaaa jamani, mambo gani haya?”
“Haya mambo ni ya ajabu sana jamani, kwahiyo na leo chakula kimeliwa?”
Walijikuta wakijadiliana bila kupata jibu, na kwenye sufuria kilibaki chakula kidogo tu, ikabidi wakakichukue kile wale, wapike na chai wanywe pamoja na mkate huku wakilalamika mwanzo mwisho kwa hiko kilichotokea.
Yani siku hii hadi wanaenda kulala walikuwa wakilalamika tu hakuna mfano yani, kila mmoja alikuwa akilalamika kivyake.

Asubuhi na mapema, Juma aliondoka zake basi Dora alimuamsha Mariam kisha walisaidiana kumpa yule mtoto ile dawa ambapo alikunywa tu vizuri.
Ila baada ya kunywa ile dawa Dora alimuuliza Mariam,
“Hivi dada, ni nani anayeweza kuwa anatufanyia ujinga wa kula chakula humu ndani?”
“Hata sijui kwakweli”
Basi Dora akafikiria kitu na kumwambia Mariam,
“Dada, leo naomba ukapike chai halafu tuitenge mezani, ili tuone huyo anayekula ni nani?”
“Kwanini nipike mimi?”
“Anayekula anaonekana anapenda kula chakula unachopika wewe”
“Haya tutamjuaje sasa?”
“Tutaweka sumu ya panya kwenye hiko chakula, halafu tutatulia tuone matokeo yake”
“Kwahiyo tutagunduaje huyo anayekula?”
“Sababu atakufa akila”
Mara mtoto alikohoa kidogo na kufanya wote wageuke kumuangalia, kisha yule mtoto akawaambia,
“Hata msijisumbue kuweka sumu ya panya maana anayekula chakula ni mimi, napenda sana kula chakula anachopika mama yangu”
Mariam na Dora walijikuta wameganda kama vile wamechomwa sindano za kuwagandisha yani hawawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma.

Itaendelea…..!!!

By, Atuganile Mwakalile.
Leo MWANAUME WA DAR itaendelea humu pia, 
DONASI VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Donations will be used to renew the domain https://www.bongolives.com/. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni