Iklan Billboard 970x250

PENZI KABLA YA KIFO SEHEMU YA PILI (02)

PENZI KABLA YA KIFO SEHEMU YA PILI (02)

PENZI KABLA YA KIFO.

Sehemu ya Pili.


Watu waliokuwa wakiendelea na shughulia zao, wakaziacha na kisha kumsogelea Elizabeth na kutaka kupiga naye picha tu. Ilionekana kuwa usumbufu, japokuwa alikuwa amefika dukani hapo kwa ajili ya kufanya manunuzi yake binafsi, uwepo wa watu wengi waliokuwa wakimfuata kila alipokwenda, ulimkera.
Hakujali wala hakuringa, kila aliyetaka kupiga naye picha, akafanya hivyo, baadaye kabisa, akaingia ndani ya duka kubwa la nguo na kisha kununua nguo kadhaa na kuondoka mahali hapo huku akifuatwa na kundi la watu nyuma yake.
“Candy!”
“Abee!”
“Mwanaume mwenyewe yule pale amesimama nje ya gari lake,” alisema Elizabeth huku akimwangalia mwanaume yule aliyeonekana nadhifu mno, alikuwa akizungumza kwenye simu huku akiwa ameliegemea gari lake la gharama, Hammer nyekundu.
“Ngoja nimfuate nikazungumze naye.”
“Elizabeth, huoni watu wanavyokuangalia?”
“Hata kama, siogopi chochote kile, acha nimfuate,” alisema Elizabeth,
Hakutaka kuvumilia, moyo wake ulikwishakufa na kuoza kwa mwanaume huyo ambaye alimuona mara moja tu na kumpenda, akaanza kumsogelea, mapigo ya moyo yaliongezeka, alitaka kumwambia ukweli, hakutaka kuvumilia kuona akiteseka, alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni mapenzi kutoka kwa mwanaume huyo.
Japokuwa alikuwa amezunguka kwa wanaume wengi pasipo kupata mtoto yeyote yule, akashindwa kujizuia, alipokuwa akimwangalia mwanaume huyo, moyo wake ulimwambia kwamba angeweza kupata mtoto kupitia huyo, hivyo alitaka kuhakikisha anamwambia ukweli kwamba anampenda, hata kama angemkataa, lakini alitaka kumwambia ukweli ili awe huru.
Wakati akiendelea kumsogelea huku watu wengi wakimfuata, akiwa amebakiza hatua ishirini kabla hajamfikia, mara mlango wa gari aliloegemea mwanaume yule ukafunguliwa, mwanamke mmoja akateremka, alikuwa mzuri wa sura, alivutia, alimbeba mtoto wake mdogo, akamfuata mwanaume yule na kusimama pembeni yake, akazungumza naye kidogo, wakaingia garini.
Hakukuwa na siku Elizabeth aliyoumia kama siku hiyo, hakujua kama yule mwanamke aliyeteremka kutoka garini alikuwa mke wa yule mwanaume au rafiki yake. Akahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, akabaki amesimama huku akiliangalia lile gari ambalo liliwashwa na kuondoka mahali hapo.
“Haiwezekani!” alisema Elizabeth, hapohapo akalifuata gari lake la kifahari, akaufungua mlango na kuingia ndani.
“Vipi Elizabeth!”
“Mwanaume yule anafaa kuwa mume wangu! Sitaki mwanaume mwingine zaidi ya yule,” alisema Elizabeth huku akionekana kuchanganyikiwa, hapohapo akawasha gari na kisha kuanza kulifuata gari lile, akili yake kwa wakati huo ilichanganyikiwa mno. Donge kubwa la mapenzi likaung’ang’ania moyo wake.
Elizabeth hakukubali, moyo wake ulikufa na kuoza, hakutaka kuona mwanaume mzuri kama yule akimkosa, alitaka kumpata, awe mume wake wa dhati kwa kuamini kwamba ingewezekana hata kupata mtoto kwa mwanaume huyo.
Aliendesha gari kwa kasi kidogo kuelekea Mwenge kupitia kwenye Barabara ya Sam Nujoma, walikuwa wakiendelea kulifuatilia gari lile ambalo liliendeshwa kwa mwendo wa kasi kuelekea Mwenge. Hawakutaka kulipita, waliendelea kulifuatilia mpaka lilipochukua Barabara ya Bagamoyo kuelekea Mbezi Beach.
Kilichomuuma ni uwepo wa mwanamke yule garini mule, hakujua kama alikuwa mkewe au dada yake, moyo wake uliumia mno mpaka yeye mwenyewe kujishangaa.
Siku ya kwanza tu kumuona mwanaume yule, akatokea kumpenda na hata alipomuona na mwanamke mwingine, akahisi kuwa na wivu mkali moyoni mwake.
“Candy!”
“Abeee!”
“Hivi yule mwanamke ni nani?”
“Sijui! Labda mkewe,” alisema Candy pasipo kujua ni kwa namna gani jibu lake lilivyomuumiza Elizabeth.
“Haiwezekani! Hawezi kuwa na mume mzuri kiasi kile, yule anatakiwa kuwa na mwanamke mzuri kama mimi,” alisema Elizabeth.
“Ndiyo! Ila utafanya nini kama utagundua kwamba yule ni mkewe?”
“Tutaona, chochote nitaweza kufanya, hata kama kutumia utajiri wangu wote! Nipo radhi, ili mradi nimpate tu” alisema Elizabeth.
Alimaanisha alichokisema, hakuwa na utani hata kidogo. Kila alipomfikiria mwanaume yule, moyo wake ulimpenda mno. Waliendelea kulifuatilia gari lile, lilipofika Afrikana, gari likakata kona na kuchukua barabara ya upande wa kulia. Nao walikuwa nyuma kama kawaida.
Alichohitaji kujua ni mahali alipoishi mwanaume yule, alikuwa makini barabarani, kila walipopita, kwa kuwa gari lake lilikuwa la kifahari na lilijulikana sehemu nyingi, watu walikuwa wakilipiga picha tu.
Mbele wakakutana na makutano ya barabara, gari halikuchukua barabara nyingine zaidi ya kusonga mbele, lilipofika lilipokuwa likielekea, taa zikaanza kuwaka kuashiria kwamba lilitakiwa kuingia katika jumba moja kubwa la kifahari. Dereva akaanza kupiga honi.
Hicho ndicho alichotaka kuona, alipoona hivyo, akaridhika na hivyo kugeuza gari, kwa sababu alijua mahali alipokuwa akiishi mwanaume yule, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo.
“Tuondoke, nishapafahamu! Nitarudi siku nyingine,” alisema Elizabeth na kisha kuondoka mahali hapo.
Siku hiyo ilikuwa ni ya kumfikiria mwanaume yule tu, hakuwa akimfahamu lakini alijihisi kuwa na mapenzi mazito juu yake. Kitandani, hakulala kama siku nyingine, alipofumba macho, taswira ya mwanaume yule ilimjia kichwani mwake kitu kilichompa wakati mgumu kupatwa na usingizi.
Alikuja kupatwa na usingizi saa saba usiku, muda wote huo alikuwa akiendelea kumfikiria tu. Alipoamka saa tatu asubuhi, kitu cha kwanza kabisa ni kumpigia simu Candy na kumtaka kufika nyumbani kwake.
“Ninataka unisindikize sehemu,” alimwambia rafiki yake huyo.
“Wapi tena?”
“Kule kwa jana, ninataka kuonana na yule mwanaume leo hiihii,” alisema Elizabeth.
“Mmh!”
“Mbona unaguna.”
“Tutamuona vipi?”
“Wewe twende tu,” alisema Elizabeth.
Alikuwa rafiki yake mkubwa ambaye kwa kifupi ungeweza kusema kwamba ndiye aliyemuweka mjini, Candy hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na hatimaye safari ya kuelekea Afrikana kuanza.
Hawakutaka kutumia gari walilotumia jana yake, wakabadilisha gari kwani lile lilijulikana mno kwa kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa akiendesha gari la thamani nchini Tanzania zaidi yake, gari lile likawa nembo, kila lilipoonekana, watu walijua kwamba mahali hapo kulikuwa na Elizabeth.
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika walipokuwa wakienda. Alichokifanya Elizabeth ni kuteremka na kisha kuwafuata wanaume kadhaa waliokuwa pembezoni mwa bahari ili kuwauliza.
“Za saa hizi!” aliwasalimia.
“Aaah! Elizabeth!”
“Ndiyo mimi! Samahanini kama nitawapotezea muda wenu.”
“Hakuna tatizo mrembo!”
“Ninauliza ni nani anaishi nyumba ile pale,” alisema Elizabeth huku akiinyooshea kidole nyumba ile.
“Kuna jamaa fulani hivi anaitwa Edson, mmiliki wa ile hoteli kubwa ya Amazon Five ya kule Upanga, yeye ndiye anaishi mule.”
“Ana mke?”
“Ndiyo, tena na mtoto mmoja.”
“Sawa. Ofisi yake ipo wapi?”
“Ipo pale kwenye Jengo la Ubungo Plaza, pia ni meneja wa Kampuni ya Ndege ya Flying 15, ukifika hapo, ukimuulizia, utaambiwa alipo,” alisema kijana mmoja.
“Umesema anaitwa Edson?”
“Ndiyo! Edson Gwamanya.”
“Nashukuru!”
Hakutaka kuwaacha vijana wale hivihivi kwani walionekana kuwa msaada mkubwa mno kwake, hivyo akawapa fedha ili wagawane. Hiyo haikutosha, walichokiomba ni kupiganaye picha, hilo wala halikuwa tatizo, akapiga nao picha na kuondoka huku akiwaacha wakiwa na furaha mno.
Kidogo moyo wake ukaridhika, kitendo cha kuambiwa mahali alipokuwa akifanyia kazi Edson kidogo ilimridhisha, hakutaka kulaza damu, alichokifanya ni kuelekea huko huku akiwa na furaha mno.
Walitumia dakika arobaini mpaka kufika katika jengo refu la Ubungo Plaza ambapo wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Kila mtu aliyemuona Elizabeth, alibaki akimkodolea macho, msichana huyo alikuwa na mvuto mkubwa mno, kila alipopita, watu walikuwa bize kumwangalia tu.
“Samahani! Ninamuulizia Edson Gwamanya,” alisema Elizabeth, alikuwa akizungumza na msichana mmoja ndani ya jengo hilo.
“Yupo ghorofa ya saba,” alisema msichana yule na kumpa maelekezo zaidi ya kufika huko.
Hawakutaka kupoteza muda, wakaelekea sehemu ya kupanda lifti na kusubiri kwa nje. Watu hawakuchoka kumwangalia, kila aliyemuona, alibaki akimkodolea macho huku wengine wakishindwa kuvumilia na kujikuta wakimsalimia huku nyuso zao zikitawaliwa na tabasamu pana.
Lifti ilipofika chini, ikafunguka, wakapanda na kuanza kupanda juu. Moyo wa Elizabeth ukaanza kudunda kwa nguvu, hakujiamini kabisa, alijikuta akianza kutetemeka kwani kukutana na mwanaume huyo kwa mara ya pili kulimtia hofu moyoni mwake.
Lifti ilipofika ghorofa ya saba, ikasimama na kisha kuteremka. Macho yao yakatua katika mlango ulioandikwa Flying 15, wakaanza kupiga hatua kuufuata mlango huo, muda wote huo mapigo ya moyo wa Elizabeth yalizidi kudunda zaidi, hakuonekana kujiamini hata mara moja.
“Subiri kwanza,” alisema Elizabeth, alimsimamisha Candy.
“Kuna nini?”
“Mbona nahofia hivi?”
“Jamani! Hebu jipe nguvu, tuumalizie huu mkia, tushamla ng’ombe mzima,” alisema Candy, Elizabeth akashusha pumzi nzito.
Wakapiga hatua mpaka walipoufikia mlango ule na kisha kuufungua, mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa sekretari ambaye walimsalimia na kisha kukaa katika viti vilivyokuwa mahali hapo.
Kipindi chote sekretari yule alibaki akimwangalia Elizabeth, alikutana na msichana aliyekuwa supastaa, aliyependwa na wanawake wengi, kila alipomtazama, alijisikia raha moyoni mwake.
“Karibuni sana,” alisema sekretari huku akitoa tabasamu pana.
“Ahsante. Tunaweza kumuona meneja?”
“Hakuna tatizo.”
Alichokifanya sekretari ni kuchukua ile simu ya mezani na kisha kumpigia meneja wake, wala simu haikuita kwa kipidi kirefu, ikapokelewa na Edson ambapo akamwambia kwamba awaruhusu wageni hao waingie ndani.
Waliporuhusiwa, wakaanza kuufuata mlango wa kuingia ndani ya ofisi ile. Candy alikuwa mbele huku Elizabeth ambaye ndiye aliyekuwa na shida ya kuonana na mwanaume huyo akiwa nyuma.
Walipoingia tu, kitendo cha Elizabeth kumuona Edson, mapigo ya moyo wake yakaongeza kasi ya kudunda, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kila alipomwangalia Edson ambaye uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, uzuri aliokuwa nao ukazidi kuongezeka huku Elizabeth akahisi kama yupo ndotoni, kukukutana na mwanaume mzuri kama alivyokuwa Edson ilikuwa moja ya tukio lisiloaminika machoni mwake.
“Karibu,” aliwakaribisha Edson, kitendo cha Elizabeth kuisikia sauti ya Edson tu, akahisi ngoma za masikio yake zikianza kucheza. Alifarijika kupita kawaida.
Alimini kwamba duniani kulikuwa na wanaume wengi, ila hakukuwa na mwanaume aliyemzidi uzuri yule aliyekuwa mbele yake, yule aliyeonyesha tabasamu huku akionekana kuwa mtu mchangamfu mno, Edson.
Kila alipomwangalia, alihisi akimpenda zaidi ya alivyokuwa akimpenda kabla, sura yake ilimvutia na kila alipoendelea kumwangalia, aliamini kwamba hakukuwa na mwanamke yeyote aliyestahili kuwa na mwanaume huyo zaidi yake.
Alitamani kupata nafasi zaidi ya kuzungumza naye, amwambie ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia, hata kama atakataliwa, ajue lakini si kuona mwanaume huyo akipita huku mwanamke mwingine ambaye kwake alionekana kutokuwa na hadhi ya kutembea naye akiwa ameolewa na kuwekwa ndani kabisa.
“Huyu namfahamu, anaitwa Elizabeth! Sijui wewe unaitwa nani?’ aliuliza Edson, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.
“Naitwa Candy!”
“Ok! Karibu sana!”
“Ahsante. “

Je, nini kitaendelea?
Related Posts
SHARE
Subscribe to get free updates

Related Posts

Chapisha Maoni

Post Central Advertising