PENZI KABLA YA KIFO SEHEMU YA NNE (04)

PENZI KABLA YA KIFO

Sehemu ya Nne.


“Kuna mzigo wako bosi.”
“Kutoka wapi?”
“Kwa Elizabeth!”
“Waoo! Yaani kashamaliza kushona?”
“Sijui!”
Alichokifanya sekretari yule ni kuchukua ule fuko uliokuwa na urembo mwingi kisha kumpa bosi wake. Edson akauchukua na kuanza kuelekea nao ndani. Alichokijua yeye ni kwamba mule ndani kulikuwa na nguo aliyomwambia Elizabeth amshonee kwa ajili ya mkewe.
Alipofika ofisini, akaufungua mfuko ule na kuanza kutoa vitu vilivyopo ndani. Kwanza akashtuka, hakuamini kile alichokiona kwa mara ya kwanza, kitu ambacho kilikuwa cha kwanza kutoka ndani ya mfuko ule yalikuwa ni maua mekundu mawili.
Akashtuka, akayaangalia maua yale vizuri, alionekana kama mtu aliyeshangazwa na hali ile, hakuishia hapo, akatoa vitu vingine, akakutana na kadi, alipoifungua tu, akasoma ujumbe uliokuwepo, ulikuwa ni wa kimapenzi.
“Mungu wangu!”
Kitu cha kingine kukitoa kilikuwa ni kipande cha karatasi, akakichukua na kisha kukifungua ndani. Kilikuwa na ujumbe mfupi ulioandikwa kwa mwandiko mzuri wa kike, maneno yaliyopangiliwa, machache na yaliyokuwa na ujumbe mfupi tu yaliyosomeka.
Edson....
CD imejieleza kila kitu.
Elizabeth.
Hapo ndipo alipoingiza mkono wake ndani ya mfuko ule, akakutana na cd moja ambayo akaichukua na kisha kuichomeka katika mlango wa laptop yake na kisha kuchukua hedifoni na kuanza kusikiliza.
Cd ile ilikuwa na nyimbo kadhaa zilizoimbwa na waimbaji wengi wa Kimarekani, kulikuwa na Wimbo wa Fly Without Wings wa West Life, Just Go wa Lionel Rich na Never Let You Go wa Justin Bieber.
Edson alizisikiliza nyimbo zile zote ambazo aliambiwa kwamba zilikuwa na ujumbe kuhusu kile alichokuwa akikihisi moyoni mwake juu yake. Nyimbo zote hizo zilikuwa na ujumbe mkali wa mapenzi, alipozisikiliza, alihisi kitu cha tofauti moyoni mwake.
Hakikuwa mapenzi,ilikuwa ni chuki kubwa kwa msichana huyo, kwa kile alichokifanya, aliona kama alivuka mipaka kwani hakutegemea msichana kama Elizabeth kufanya jambo hilo ambalo aliliona kama kuingiliwa katika maisha yake na wakati alikuwa na mke aliyempenda kuliko wanawake wote.
“Hebu subiri kwanza, kumbe hanijui,” alisema Edson kwa hasira.
Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akachukua simu yake, moyo wake uliwaka kwa hasira, alijiona ghafla akimchukia Elizabeth, japokuwa alikuwa msichana maarufu, mwenye fedha na mrembo mno lakini hiyo haikuwa sababu ya kumfanya kumsaliti mke wake.
Simu ikaanza kuita, akawa na hamu ya kuisikia sauti ya msichana huyo, alitaka amtukane na kumuonya kwa kile alichokuwa amekifanya. Hakupendezwa nacho hata kidogo. Simu iliita na kuita lakini haikupokelewa, akakunja uso wake kwa hasira.
Simu ile ikaita mpaka ikakata, hasira zikampanda zaidi. Alichokifanya ni kutoka ofisini kwake, hakutaka kukaa, kazi zisingefanyika hata mara moja, alichokitaka ni kumfuata msichana huyo nyumbani kwake, hata kama hakutaka kupokea simu, aliamini kwamba endapo angekwenda nyumbani basi angeweza kumkuta, hicho ndicho alichokifanya.
“Kumbe huyu hanijui, sasa subiri....” alisema Edson huku akiwa na hasira kali kama mbogo. Akawasha gari na kuanza kuelekea nyumbani kwa Elizabeth aliyekuwa akiishi hukohuko Mbezi Beach.
***
Simu ya Edson ilipokuwa ikiita, aliiona sana, alikuwa akiiangalia simu yake tu pasipo kuipokea. Moyo wake ulijawa na hofu kubwa, hakujua kama upigaji wa simu ile ulikuwa ni wa amani au kulikuwa na tatizo.
Kila alipotaka kuipokea, mapigo yake ya moyo yalimdunda mno, alitetemeka mwili huku uso wake ukionekana kama mtu aliyekosa amani, akabaki akiiangalia mpaka simu hiyo ilipokatika.
Alikwishajua kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata kile alichomwachia sekretari, hakujua kama alifurahia au alichukia, hakujua maana ya kumpigia simu wakati ule, akabaki akitetemeka tu.
“Vipi tena?” aliuliza Candy aliyekuwa amefika nyumbani hapo asubuhiasubuhi.
“Hakuna kitu.”
“Nani anakupigia simu?”
“Edson!”
“Sasa mbona hupokei?”
“Naogopa!”
“Kwa nini?”
“Mmmh! Wewe acha tu!’
Walibaki wakizungumza mengi, bado Elizabeth aliendelea kumwambia Candy juu ya hisia zake za kimapenzi kwa Edson kwamba alikuwa hali, halali, alichokuwa akikihitaji ni penzi la dhati kutoka kwa mwanaume huyo tu.
“Candy! Nikwambie kitu?”
“Niambie.”
“Nilikwenda ofisini kwa Edson!”
“Lini?”
“Leo hiihii.”
“Kufanya nini?”
“Nilimpelekea vitu ambavyo vilionyesha ni kwa namna gani ninampenda, jamaniiii, hivi yule mwanaume kaniwekea dawa gani? Mbona nimedata hivi?” aliuliza Elizabeth huku tabasamu pana likionekana usoni mwake.
Wakati wanazungumza mengi kuhusu Edson, mara wakasikia mlio wa honi kutoka nje ya nyumba hiyo, kitu cha kwanza alichokifanya Elizabeth ni kuchungulia dirishani, mlinzi alikwenda na kufungua geti, hakufungua geti kubwa, akafungua dogo.
“Candy!” aliita Elizabeth kwa mshtuko.
“Nini?”
“Edson!” alijibu Elizabeth huku akionekana kuwa na wasiwasi mahali hapo.
Edson hakutaka kuzungumza chochote na mlinzi, ndiyo kwanza akamsukumia pembeni na kisha kuelekea ndani ya nyumba hiyo ya kifahari. Alipoufikia mlango, akakishika kitasa na kukifungua, akaingia ndani, macho yake yakatua kwa wasichana wawili, Elizabeth na Candy.
Alichokifanya ni kumtupia Elizabeth ule mfuko aliokuwa amemletea ambao ndani yake ulikuwa na vile vitu alivyokuwa amempa. Alipofanya hivyo, akageuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje, alipoufikia mlango wa sebule hiyo, hata kabla hajaufungua akageuka nyuma.
“Nisikilize wewe malaya!” alisema Edson, alionekana kufura kwa hasira, Elizabeth akawa anatetemeka tu.
“Kuanzia leo, sitaki unizoee kabisa, yaani sitaki unizoee hata mara moja. Siyo unajiona wewe ni malaya basi unafikiri dunia nzima wapo kama wewe. Ukinifuatilia tena, nitakupiga risasi mpumbavu weeee...” alisema Edson huku akionekana kuwa na hasira mno, alipomaliza, akaufungua mlango na kuondoka zake.
Elizabeth alibaki akiwa amesimama kama nguzo ya umeme, hakuamini kile kilichotokea, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, hakutingishika, alibaki vilevile na ghafla machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Hakutegemea kama kweli mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati angeweza kumfanyia kitendo kama kile. Alitamani hilo liwe moja ya tukio lililotokea ndotoni, alitamani kusikia rafiki yake Candy akimwamsha na kumwambia kwamba asubuhi ilikwishafika na hivyo walitakiwa kuendelea na ratiba nyingine kama kawaida.
Kile kilichotokea, hakikuwa ndoto, ni kweli mwanaume aliyekuwa akimpenda, Edson alikuwa amefika nyumbani hapo na kumtupia mfuko uliokuwa na vitu vya mapenzi alivyompelekea kama kumuonyeshea ni jinsi gani alimpenda, ni kweli alimwambia maneno machache kwamba asidiriki kumtafuta hata mara moja.
Elizabeth hakuamini hata kidogo, akajikuta akilisogelea kochi na kisha kutulia, sauti ya kilio kilichotoka mahali hapo kilikuwa kikubwa kilichomfanya hata Candy mwenyewe kushtuka. Ni kweli alikwishawahi kumsikia rafiki yake huyo akilia, lakini sauti ya kilio alichokitoa siku hiyo ilikuwa ni ya juu mno.
“Nyamaza Elizabeth....” alisema Candy huku akijaribu kumbembeleza.
Elizabeth hakunyamaza, aliendelea kulia, alipoona anabembelezwa sana huku moyo wake ukiendelea kuumia zaidi, akasimama na kuelekea chumbani kwake ambapo huko akajilaza kitandani na kuendelea kulia.
Hakukuwa na siku ambayo moyo wake uliumia kama siku hiyo, alipoona kwamba mapenzi aliyokuwa nayo juu ya Edson yalikuwa makubwa mno, akajilazimisha kuiingiza chuki moyoni mwake lakini jambo hilo halikuwezakana kabisa, bado aliona kuwa na mapenzi mazito kwa mwanaume huyo.
Siku hiyo hakutaka kutoka, hakutaka kuufungua mlango wa chumbani kwake. Japokuwa Candy alipiga sana hodi huku akimsisitizia aufungue mlango lakini hakufanya hivyo, aliendelea kubaki chumbani humo huku akilia.
Usiku, hakulala, alikesha huku mawazo yake yakiwa kwa Edson tu. Kila wakati aliishika simu ile na kuiangalia namba ya Edson, alitamani kumpigia na kuzungumza naye, japokuwa alikuwa ametukanwa lakini hilo wala halikuwa tatizo, vitisho vyote alivyokuwa amepewa kwake havikumuogopesha.
Hakutaka kujiuliza mara mbilimbili, hapohapo akampigia simu Edson huku saa yake ikimwambia kwamba tayari ilikuwa ni saa tano usiku. Simu ile ikaanza kuita, haikupokelewa, iliita na kuita mpaka ikakata.
Hakutaka kuacha, alichokifanya ni kupiga tena, yote hayo, alikuwa akitaka kuzungumza na Edson tu kwani bado moyo wake ulikataa kabisa kumtoa mwanaume huyo. Mara ya pili wala simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya Edson kusikika.
“Hallo!” iliita.
“Hallo Edson.”
“Wewe Elizabeth! Nilikwambiaje?”
“Nimeshindwa kuvumilia, kama unataka kuniua njoo uniue tu, siwezi kuona nikikukosa, nakupenda sana,” alisema Elizabeth huku akianza kulia.
“Nimekwambia hivi....”
“Ninakupenda Edson, ninahitaji uwe mpenzi wangu!”
“Hivi wewe mwanamke umechanganyikiwa?”
“Ndiyo! Nimechanganyikiwa kwa mapenzi yako, naomba unihurumie Edson....” alisema Elizabeth huku akiendelea kulia.
Huku akiendelea kuishikilia simu, akahisi kulikuwa na mtu alimpokonya mwanaume huyo simu ile, wakati akikaa kusikilizia, mara akasikia sauti ya mwanamke ikianza kuita kwenye simu. Hakutaka kujiuliza, alijua kwamba huyo alikuwa mkewe Edson, hakukata simu, alitaka kusikiliza angesemaje.
“Mbona unatusumbua sana Elizabeth! Hivi haukumuelewa Edson?” aliuliza mke kwa sauti iliyosikika kama mtu mwenye wivu mkali.
“Ninajua! Ila ninampenda mumeo!”
“Unasemaje?”
“Ninampenda mumeo! Ni mwanaume wangu wa ndoto, sipendi kulificha hili, mwambie kwamba ninampenda sana,” alisema Elizabeth huku kilio cha kwikwi kikisikika, hakuongea sana, akakata simu hiyo na kuanza kulia kwa sauti kubwa iliyozuiliwa na mto alioulalia kwa staili ya kuufunika uso wake.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Alhamisi hapahapa.

Comments

Use [video]youtube-video-link[/video] to insert video in comment
Use [img]image-link[/img] to insert image in comment