JINSI PAKA ALIVYOMALIZA FAMILIA YETU SEHEMU YA 1

JINSI PAKA ALIVYOMALIZA FAMILIA YETU

       SEHEMU YA 1

   WHATSAPP 0655585220

              ZANZIBAR

Anza nayo......
Nilikua ni mwenye kusikia tu, kwamba duniani kuna wachawi, majini na mambo ya kurogana. Nilifikiri itakua ni imani tu wanazozijenga watu vichwani mwao na kuamua 'kujitisha'.
Safari yangu ya kuamini uwepo wa masuala haya ilianza takribani mwaka mmoja uliopita.
Kwa majina naitwa Naomi Salisala, ni msichana mwenye umri wa miaka ishirini sasa.
Mwishoni mwa mwaka juzi, tulipata likizo fupi baada ya masomo ya muhula mzima mimi pamoja na wadogo zangu wote.
Baba na mama waliamua watupeleke kijijini kwa bibi na babu maana ni muda mrefu ilikua hatujaonana nao.
Ilikua jumapili asubuhi, ndani ya basi lililojaa abiria wengi waliovaa Kanzu na mabaibui. Baba na mama baada ya kutusindikiza na kutufungashia "maporopocho" ya njiani, dakika chache tu Safari ya kuelekea Kwedizinga mkoani Tanga kwa bibi ilianza.
***
Ilichukua kama masaa matano hivi hadi sita tayari tulishafika kituo kimoja kinaitwa Michungwani kama konda alivyoelekezwa na baba atushushe.
Babu na bibi walikua wanatusubiri kituoni pale, kwa bashasha usoni mwao walitupokea na moja kwa moja tulielekea nyumbani, na kwakua hakukua mbali sana tulitembea tu kwa miguu.
Kwa kweli tulifuruhia sana likizo yetu, tulikula matunda ya kila aina hasa mafenesi, tuliwajua baba wadogo zetu, mashangazi na baadhi ya ndugu zetu wengine.
.......
Iliwadia siku ya kurejea nyumbani sasa, baada ya bibi kutufungashia mizigo na zawadi mbalimbali tuzilete nyumbani, Nilishangaa mdogo wangu kumlilia sana paka mmoja aliyekuwepo pale nyumbani kwa babu na bibi.
Alikua si mpenda paka kabisa hapo kabla, Na nilishangaa sana kung'ang'ania kwake kule.
"Muache bwana mtoto akapate wa kucheza cheza nae".
Baada ya bibi kuona nimekua mkataaji sana wa suala lile la mdogo wangu ikabidi amfanyie upendeleo kidogo.
Sikua na namna zaidi ya kukubali tu tumbebe, ila kwa kweli mimi na paka " Si wenye kuivana kabisa". Maana nawaogopa pia, Sijui kwanini nawaogopa ila nawaogopa sana labda itakua ni NAFSI YA KIKE tu..... Maana wanasemaga ujasiri huwa amepewa mwanaume kwa kiasi kikibwa.
***
Njia nzima kwenye basi ni "Ng'waau!!! Ng'wauuu!!!" kwa kweli siku ile dogo aliniboa sana!!!
Alikua amefungwa kwenye kiboksi na tukawa tumemuweka karibu yetu, basi ikisikika tu "Ng'waaau!!!", watu wote wanatugeukia sisi.
Nilishkuru sana baada ya kufika kituoni Ubungo maana kwa kero ile nilihisi kama ni safari ya mwaka mzima, baba na mama wote walikuja kutupokea.
Moja kwa moja tukaingia kwenye gari ya nyumbani aina ya Noah tuelekee nyumbani kwetu maeneo ya Tegeta, huku baba akituhoji hali ya huko na baadhi ya ndugu zake.
......
Kwa kua nilichoka sana, tangu saa kumi na moja jioni baada ya kufika nyumbani nililala kuja kushtuka tayari ni saa nne na nusu hivi usiku.
Kawaida nyumbani hata kama hujala, chakula chako kinakua kinahifadhiwa kwenye kabati ili muda wowote ule ukiwa tayari kula 'unajisevia'.
Moja kwa moja nikaelekea kabatini nikafungua mahotpot, " waaaaaooooh" kilipikwa chakula nikipendacho sana si kingine bali ni ndizi za nazi na samaki.
Ile na narudi nichukue sahani tu...
"Ng'waaaaauuuuuh!!!"
Nilishtuka sana, kumbe yule paka tayari baada ya kusikia harufu ya samaki alishafika miguu mwangu.
"Ssshhhhhiiiiiiiiiihhhhh"
..Nilimfukuza huku mwenyewe nikitetemeka sana, kwa woga wangu anaweza akanirukia hahahah!.
Naye ni muoga, huyooo akaenda zake! Nikachukua zangu sahani nikaanza kupakua. Nataka nimalizie kuweka kijiko cha tatu tu....
"Vuuuuuum!!!!!"... Umeme ukakatika.
Daaah, niliingia woga sana kwa kweli. Jenereta lipo nje ila kwenda kuwasha nikiwa mwenyewe niliogopa nikaamua niende kumuamsha dada wa kazi ili anisindikize.
Haraka haraka nikawahi chumbani, maana tulikua tunalala wote. Na yeye anavyolala kama mzigo yani, amsha na kuamsha haamki nahisi ni uchovu wa kazi za kutwa nzima.
Njaa kali niliyokua nayo ikashinda woga, ikabidi nipige moyo konde niende mwenyewe nikawashe.
Ile natoka tu mezani, naona mtu amevaa nguo nyeupe huku anakula chakula.
" Baba??!!"... Niliita.
Halikutoka jibu lolote usipokua ni ukimya tu.
Nikaita tena "Baba!!!!"
(Kimyaaaaaaaa!!!)
Sijui uliniingia ujasiri gani?!, ikabidi nisoge kwa karibu nihakikishe ni nani anayekula kwenye giza.
Tobaaaaaa!!! Ile nafika tu pale, yule mtu akaniiinulia uso wake, macho yake yanawaka ile mbaya, huku masharubu yamemjaa mashavuni. Alikua ni paka!!!!
JE UNAFAHAMU NINI KITAENDELEA KATIKA MKASA HUU??

Comments

Use [video]youtube-video-link[/video] to insert video in comment
Use [img]image-link[/img] to insert image in comment