MTOTO WA MAAJABU SEHEMU YA 01

MTOTO WA MAAJABU: 1

By, Atuganile Mwakalile.
Mariam alikuwa na mawazo sana kutokana na ile mimba aliyobeba kupitiliza muda wa kawaida wa kujifungua yaani miezi tisa kwani kwasasa mimba yake ilifikisha miezi ishirini na nne yani miaka miwili bila ya dalili zozote zile za kujifungua na kumfanya awe na mawazo zaidi, ukizingatia ameshajaribu njia nyingi ila imeshindikana na hakuwa kabisa na dalili ya kujifungua wala nini.
Mumewe alimuona mkewe jinsi ambavyo anakosa raha kila siku, mara kwa mara huwa anamuuliza ila leo aliamua kukaa nae na kuongea nae vizuri, alimuuliza
“Mke wangu tatizo ni nini?”
Ila Mariam hakujibu kitu kanakwamba hakusikia chochote, hii ni kutokana na mawazo ya mbali sana aliyokuwa nayo hadi mumewe ikabidi amuite kwa sauti,
“Wewe Mariam, wewe!!”
Ndipo Mariam alishtuka na kumuangalia mume wake kisha akamuuliza,
“Kumbe unaongea na mimi?”
“Ndio, unajua nakuona huna raha kabisa”
“Naitoa wapi raha mume wangu? Mimba gani hii jamani! Kwanini hii mimba inanieleleza hivi? Nimekosa nini mimi? Miaka miwili hii imepita na mwezi huo unakatika yani mimba imekaa miezi ishirini na tano kweli!! Hakuna dalili ya uchungu wala nini halafu hospitali wanasema nisubiri tu, kwakweli nimechoka”
“Halafu tumbo limekuwa kubwa sana mke wangu kupita kawaida!”
“Yani hadi kero mume wangu, nachukia hatari basi tu ila hii hali inanikera sana”
“Ngoja, kesho tutaenda tena hospitali ili kujua ni kwanini inakuwa hivi ili kama inawezekana hata operesheni wakufanyie”
“Kila tukienda wanazingua, mimi nimechoka kwakweli”
“Sawa, ila tutaenda hospitali nyingine lazima tupate suluhisho la hiyo mimba mke wangu. Mimi binafsi sijapenda”
“Bora iwe hivyo, kwakweli nimechoka tena nimechoka sana. Hata mimi sipendi kabisa hali hii, mtu unakaa na mimba kama unataka kuzaa tembo!! Ndio mambo gani haya!”
“Pole mke wangu”
Kwakweli Mariam hakuwa na raha kabisa kutokana na ile mimba, sababu ilimkosesha raha kabisa na alishindwa kufanya mambo yake mengi sana.
Kesho yake kama ambavyo walipanga na mumewe, walienda hospitali kwaajili ya kuangalia maendeleo ya ile mimba na kwanini ilipitiliza muda wake kiasi kile, waliamua kubadilisha hospitali kwani waliona labda hospitali ambayo huwa anaenda hawana ujuzi mzuri kwani alikuwa ameshachoka kuibeba ile mimba, moja kwa moja walikutana na daktari ambaye alikuwa ni mtaalamu wa mambo ya wanawake na kuongea nae na kuhusu swala zima la kupitiliza kwa ule ujauzito,
“Umesema imepita miaka miwili?”
“Ndio, tena sio miaka miwili tu maana na mwezi ushakatika sasa, imepitiliza miezi ishirini na tano. Kwakweli nimechoka, wakati watu hubeba mimba kwa miezi tisa tu!! Sasa kwanini mimi inakuwa hivi jamani!”
“Pole sana, ila ngoja kwanza tukakupige ultrasound halafu nijue ni kitu gani kinaendelea”
Walikubali na moja kwa moja walienda kwenye vipimo, majibu yalipotoka walienda kuongea na daktari,
“Kwanza hongera sana, inaonyesha umebeba mapacha wa kiume”
“Kheeeee mapacha tena!”
“Mbona unashangaa sasa? Hupendi mapacha au? Wanawake wengi sana hupenda kuzaa mapacha, kwani ni raha kuishi nao utapata shida kidogo tu kwenye malezi kama kipato chako kidogo ila mapacha ni watoto wazuri sana kwahiyo unatakiwa kufurahi”
“Haya tuachane na hizo habari dokta, nitajifungua lini maana nishachoka”
“Sijaona tatizo lolote kwenye mimba yako, utajifungua tu kawaida”
Basi mume wa Mariam akamwambia daktari,
“Hivi kwani hakuna uwezekano wa mke wangu kufanyiwa tu operesheni bila kusubiria huo uchungu?”
“Kwahiyo mnataka kwa operesheni sio!”
“Dokta, nimechoka mimi sijui kama umenielewa nilivyokwambia kuwa mimba hii imepitiliza miaka miwili nadhani kitoto kitakachotoka hadi kitakuwa kinatembea”
Dokta akacheka kidogo huku akitikisa kichwa na kusema,
“Sawa, ngoja niwapangie siku ya kuja kufanya hiyo operesheni”
Dokta akaangalia ratiba yake pale na kuwaambia kuwa waende kesho kutwa kwaajili ya kufanya hiyo operesheni.
Mariam alifurahi kwani alishachoka kwakweli, basi walimaliza pale na kuondoka zao kurudi nyumbani kwao.
Walipofika nyumbani waliongea kidogo ambapo mume wa Mariam alimuuliza mkewe,
“Nakumbuka mara ya mwisho tulipopiga ultrasound tuliambiwa ni mtoto mmoja, sasa leo imekuwaje tena ni mapacha?”
“Yani na wewe unashangaa tu habari za mapacha badala ya kushangaa swala la kukaa na mimba miaka miwili jamani!! Yani mimi nimechoka, hata wawe mapacha sijui vitu gani watoke tu, nimechoka kwakweli”
Kiukweli Mariam hakuwa na raha kabisa ukizingatia hii mimba ndio imesababisha hadi yeye na mumewe kwenda kuhamia sehemu ya mbali kwani akikumbuka watu wanaomfahamu walikuwa wakimshangaa sana kuwa bado hajajifungua! Na yeye ilikuwa inampa hasira sana wakimshangaa ndiomana na mumewe waliamua kuhamia mbali na kuishi wenyewe bila ya watu wanaowafahamu vizuri kuwa karibu.
Mumewe alimuuliza Mariam,
“Leo ungependa kula nini?”
“Kama kuna chakula cha kuleta uchungu basi mimi ndio nakitaka hiko chakula, sijui kama na wewe unanielewa kuwa nimechoka!”
Mumewe hakuongea sana kwani alikuwa akijua wazi muda mkewe njaa ikimshika basi huwahi kwenye majungu mwenyewe na kutafutiza chakula, ila muda huu sababu ana hasira ndiomana alijibu hivi.
Siku ilifika ambapo Mariam alitakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji, kwahiyo walijiandaa na vifaa pamoja na mumewe na kwenda hospitali, hawakuwaambia ndugu maana sio kwamba hii ni mara ya kwanza kuamua hivi hapana, ila ilishawahi kutokea na haikuwa na mafanikio.
Na ndivyo ilivyokuwa hata kwa siku hii, ilionekana presha ya Mariam ipo juu sana kiasi kwamba ilikuwa ngumu kwa yeye kufanyiwa upasuaji, kwakweli Mariam alichukia sana na kurudi na mumewe nyumbani.
“Jamani Juma, hali hii hadi lini mimi nimechoka”
“Pole mke wangu, ila mimi naamini tu kuwa mambo yatakuwa sawa”
“Kama hao mapacha si watoke tu, loh nimechoka sana”
Mariam aliamua kwenda kulala, wakati huo Juma alimpigia simu mama yake na kumueleza kile ambacho kimetokea,
“Kheeee mlienda tena hospitali halafu yametoka kama yale yale?”
“Ndio mama”
“Khaaaa, mimi nataka mjukuu jamani. Kuna mtu namsubiri kaniambia ataniletea dawa nyingine ya kieyeji”
“Unadhani hiyo itafanya kazi vizuri mama?”
“Ndio, aliyeniambia safari hii namuamini, hana mambo ya longolongo kabisa, kwahiyo hata msijali”
“Sawa mama”
Juma alienda kumpa hiyo habari Mariam na kumfanya Mariam afurahi sana,
“Kheeee afadhari yani, nimechoka sana loh!”
“Usijali, hata mimi nakuonea huruma”
“Ila isiwe kama ile midawa ya kipindi kile jamani, hakuna kitu kinafanyika wala nini!”
“Mama kasema kwasasa ni uhakika”
Basi Mariam alifurahi sana, na hapo hata kula siku hii alikula vizuri tu.
Siku hii, alifika mama mkwe wa Mariam na kumkaribisha pale kwao kwa furaha sana kwani Mariam alichokuwa anataka ni kupata dawa tu, basi yule mama alianza kuongea na Mariam pale kuhusu dawa aliyomletea,
“Kwanza pole mwanangu unajua ni nini, nimehangaika yani kuipata hii dawa balaa, unajua mwanzoni nilijua umechezewa yani umerogwa!”
“Ndio nimerogwa mama”
“Hamna Mariam, nasikia kuna kosa umefanya”
“Kheeee kosa gani sasa ambalo mimi silijui?”
“Mimi silijui pia, ila nasikia kuna kosa umefanya, kuna kitu ulikatazwa kufanya sijui kukila wakati una mimba halafu wewe ukakifanya na ndio kimekuletea matatizo hayo”
Mumewe akadakia,
“Inawezekana mama, maana wakati Mimba changa khaaa Mariam alikuwa anakula hovyo hovyo yani”
“Hata mimi nakumbuka, yani mimba za wenzie zikiwa changa huwa utakuta tunapatwa na vichefuchefu na kula kula hovyo hatuwezi mpaka mimba iongezeke kidogo ila Mariam khaaa ulizidi mkwe wangu jamani nakumbuka kuna siku nimekukuta unakula hadi mbegu za mapapai”
“Jamani mama, yani huwezi amini wakati mimba hii ilivyokuwa changa nilikuwa natamani kila kilichokuwa kinakuja mbele yangu na nilikuwa sishibi, nakumbuka kuna vyakula vingine vilikula hadi aibu kuvisema ila mbegu za mapapai ni dawa mama”
“Kweli ni dawa ila sio kwa mtindo ule ambao ulikuwa unakula wewe”
Mumewe akasema,
“Mimi nakumbuka, kuna siku Mariam ulikamata kindege kidogo ndani ukakinyonga na kukichoma halafu ukakila khaaa nilikushangaa sana, kwahiyo inawezekana kweli ulikula vitu vya ajabu”
“Na ndio nilivyoambiwa wanangu, tunaambiwa hakuna cha mchawi wala nini, inasemekana Mariam hakurogwa wala nini ila kuna kitu alikosea, ila nimepewa hii dawa itaenda kumsaidia”
Mariam hakutia neno kwa wakati huu kwani yeye cha msingi alitaka kusaidiwa tu maswala ya kula kula hovyo kwanza hakuona kuwa ni tatizo kwani wenye mimba wengi huwa wanatamani hata vitu visivyokuwepo, kwahiyo alikuwa akiwasapoti tu sababu alikuwa akitaka dawa tu kwa muda huo.
Mama mkwe wa Mariam alitoa dawa ambazo zilikuwa zimefungwa kwenye vifundo vitatu na kuanza kumuelekeza Mariam namna ya kutumia,
“Ni Hivi, hili fundo la kwanza utaoga siku ya kwanza yani unachanganya kwenye maji ya kuoga. Ukishaoga mwenyewe unajimwagia haya maji ya dawa, hili fundo la kwanza linabeba miezi yote kumi na mbili yani mwaka mmoja ambao mimba hiyo imepitilia, halafu siku ya pili utachanganya hili fundo la pili kwenye maji na lenyewe litabeba mwaka mzima, halafu hili fundo la tatu utachanganya kwenye maji siku ya tatu na kuoga, na lenyewe litabeba huo mwezi mmoja uliopitiliza, baada ya hapo utapata majibu yake mkwe wangu, lazima ujifungue, yani nitafurahije jamani! Nataka mjukuu mimi. Halafu siondoki hivyo, ndio nimekuja moja kwa moja kwani najua wiki hii hii mambo yatakuwa tayari”
“Ooooh asante mama, kwahiyo naanza kuoga leo?”
“Ndio, leo leo Mariam, hujalichoka hilo tumbo au?”
“Nimelichoka tena nimelichoka sana”
“Haya, itabidi uanze leo”
“Ngoja nikaianze sasa hivi”
Mariam alichukua ile dawa na kwenda nayo ndani huku akienda kujiandaa kuoga, basi mama mkwe wake alibaki na mwanae pale wakiwa wanaongea ongea kidogo.
“Kwakweli mama nakushukuru sana, nahitaji mke wangu awe mzima”
“Usijali, mbona huyu anapona kabisa, hakuna tatizo yule mzee niliyekutana nae unajua hajachukua hata mia yangu. Kasema kambo yakiwa mazuri basi nitaenda kumpa zawadi”
“Kheeee kweli huyo ni mganga mama”
“Ni mganga sana, ndiomana kasema ukweli kuwa Mariam hajarogwa wala nini ila kajiroga mwenyewe”
“Ila sijawahi kusikia mambo haya kabisa mama, yani nahisi kuna kitu kimejificha hatukijui mama yangu”
“Tutajua tu hata usijali”
Basi wakaendelea tu na maongezi pale ila Mariam hakurudi tena pale sebleni wala nini.

Mariam alipomaliza tu kuoga kwa ile dawa akaanza kujihisi tofauti tumboni, yani kama vile wale watoto wamefunga kamba tumboni wakiruka ruka.
Alikosa raha na amani kabisa, basi moja kwa moja akaenda kulala, mumewe akamfata kumuuliza,
“Vipi tena, unajihisi vipi Mariam?”
“Kheeee makubwa yapo hapa jamani, yani hawa watoto kamavile wanaruka kamba tumboni, yani hii mitoto itakuwa mikubwa kabisa, mbona kunieleleza hivi mimi jamani!”
“Pole mke wangu, ila hiyo ya watoto kuruka kamba tumboni, kweli ni kioja ngoja nikamwite mama”
Mume wa Mariam alimuita mama yake ambapo na yeye aliambiwa vile vile na Mariam, yule mama aliupumua kidogo tu na kumwambia Mariam,
“Usijali Mariam, vumilia tu kila kitu kitakuwa sawa. Naamini kuwa mambo yatakuwa sawa tu, vumilia Mariam”
“Asante mama”
Basi walimuacha Mariam pale aweze kupumzika huku wakiendelea na mambo mengine kama kumtayarishia chakula maana waliona hali yake sio nzuri kwa wakati huo ila sababu walitaka kuona ile dawa ikifanya kazi, ilibidi tu wawe wapole na wavumilie.
Usiku ule ndio Mariam alisema kuwa kidogo tumbo limetulia na aliweza kukaa na kula chakula kwasasa huku akiongea na mama mkwe wake,
“Siku hizi utaalamu mwingi, ushajua ni mtoto gani?”
“Mmmmh mama, kwasasa hata jinsia ya mtoto sio ya muhimu kwangu, cha muhimu ni kushusha huu mzigo tu”
Mumewe akasema,
“Ni mapacha mama, dokta kasema ni mapacha wa kiume”
“Ooooh hongera mtoto wangu, ndiomana kuna mambo ya ajabu yamefanyika hapa kumbe hawataki hii baraka ije kwetu khaaa!! Hongera sana mwanangu, umri wako umeenda ila kumbe utapata mwanamke na atakuzalia uzao wa kwanza midume miwili”
Mume wa Mariam aliangalia chini tu kiasi kwamba mama yake alimuuliza,
“Mbona hishangilii sasa?”
“Nishangilie nini mama ikiwa mke wangu anateseka kwa kiasi hiko? Sikujua kama mapacha ndio wanasumbua hivi yani, bora angezaa mmoja tu”
“Hamna bhana, huyu uzazi tu umemuendea vibaya, wala mapacha hawasumbui wala nini ila huyu uzazi umemsumbua tu huu, sio sababu ya kubeba mapacha tumboni wala nini!”
Mariam alikuwa kimya kabisa kwani alikuwa akitamani tu muda ufike aweze kujifungua basi na sio kuongelea kuhusu watoto aliowabeba tumboni kwa zaidi ya miaka miwili.
Siku ya pili, Mariam anaenda kuogea tena ile dawa kama ambavyo alipewa maelekezo na mama mkwe wake ila baada ya kuoga tu akamsikia mtoto tumboni kama akibinuka sarakasi na kumfanya Mariam achukie sana.
Akaenda kwa mama mkwe wake kumlalamikia,
“Mama, yani huyu mtoto kama anabinuka sarakasi tumboni”
“Khaaaa Mariam, si mapacha hao!! Watakuwa ndio wanajiandaa kutoka”
“Jamani mama hadi tumbo linaniuma”
“Pole sana”
Mariama akaondoka zake na kwenda kulala ila kiukweli leo hata kulala hakuweza maana tumbo lake lilikuwa linacheza cheza muda wote na kumkosha raha kabisa.
Basi alijigeuza hadi usiku ulifika na hata kula aligoma kwa siku hii kabisa, yani kwa jinsi alivyokuwa akijihisi tumboni ilimlazimu kuamua kwenda kuoga usiku ile dawa ya siku ya tatu kabla hata siku yenyewe haijafikia vizuri kwani alijihisi kukereka kwa yale maumivu ya mtoto kujibinua tumboni.
Sasa alipoanza kuoga na hii dawa akasikia sauti ya mtoto mdogo,
“Mama, ndio hutaki niendelee kubaki tumboni mwako?”
Mariam hakutaka kuifatiliza hii sauti wala nini bali alijimwagia tu ile dawa ila alirudi akiwa na maumivu makali sana,
“Jamani nakufa, jamani sijawahi kupatwa na maumivu kama haya, nakufa jamani”
Mama mkwe wake alimfata na alivyomsikiliza vizuri Mariam akajua tu ni uchungu umemuanza,
“Kheeee mbona mapema kabla hata hujamaliza dawa?”
Mariam hakumjibu kitu kwani kiukweli alishamaliza dawa, ule uchungu ulikuwa unamchanganya akili yake haswaa, yani alikuwa akijihisi vibaya sana.
Basi usiku ule ule mume wa Mariam ilibidi akatafute usafari ili waweze kuwahi hospitali ili aweze kujifungua kwa huduma nzuri.
Damu nazo zilianza kummwagika Mariam na kuonyesha kweli hapo mambo yameiva sasa, mama mkwe aliendelea tu kumpa moyo,
“Jikaze Mariam, ndio ukubwa huo”
“Mama nakufa mimi, sirudii tena mimi khaaaa ndio uchungu wenyewe upo hivi! Nakufa jamani, sio kwa maumivu haya loh!”
Mariam alikuwa akipiga kelel tu, basi usafiri ulivyofika moja kwa moja waliingia kwenye gari na kuelekea hospitali.
Walivyofika hospitali, moja kwa moja Mariam alipelekwa leba maana alionekana kuwa na hali mbaya tayari.
Daktari alimpiga pale na kusema,
“Khaaaa mtoto katanguliza miguu, hapa hakuna jinsi ni operesheni tu”
Basi wakaenda kuchukua karatasi za kusaini waweze kumpeleka Mariam kwenye operesheni ila muda ule ule wote walishangaa pale Mariam akijilaza kitandani na mtoto akitoka vile vile akiwa ametanguliza miguu, yani Mariam alijifungua kawaida kabisa ingawa mtoto alikuwa katanguliza miguu.
Kitu ambacho kilimshangaza Mariam, hakujifungua mapacha bali alijifungua mtoto mmoja, kitu kilichowashangaza pale leba wote ni kuwa mtoto wa Mariam baada ya kuzaliwa alikaa mwenyewe pale kitandani.
Itaendelea……!!!
Kwa mawasiliano 0714443433

DONATE VIA PAYPAL Help make a donation if the article feels useful. Your donation helps the Admin to be even more active in sharing quality blog templates. thanks.
Machapisho Mapya Machapisho Mapya Machapisho ya Zamani Machapisho ya Zamani

Machapisho mengine

Maoni

Chapisha Maoni